Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Acinipo Jiji la Kale Lililosahauliwa

Acinipo Jiji la Kale Lililosahauliwa

Acinipo Jiji la Kale Lililosahauliwa

Na mwandishi wa Amkeni! nchini Hispania

TULIFURAHI kutembelea mahali ambapo Waiberia na Waroma walitembea zaidi ya miaka elfu mbili iliyopita. Mimi na mwenzangu tulikuwa tumesafiri kwa gari kutoka mji wa San Pedro de Alcántara, kwenye pwani ya Málaga, kusini mwa Hispania, ili kutembelea baadhi ya pueblos blancos (miji myeupe) ya Andalusia. Kisha tulisafiri kaskazini katika barabara ya mlima, tukapita Sierra de las Nieves upande wa kulia, na mwinuko wake wa Pico Torrecilla, wenye urefu wa meta 1,900. Hatukutarajia kuona mandhari hiyo yenye kupendeza tulipoteremka hadi jiji la kihistoria la Ronda lililozungukwa na kuta. Maelfu ya miaka iliyopita, jiji hilo maridadi lilikaliwa na Waselti (ambao waliliita Arunda), Wagiriki, Wafoinike, Waroma, Wavandali, na Waarabu walioshinda Wavisigothi katika karne ya nane W.K.

Tulitaka hasa kutembelea jiji la Ronda la Vieja, yaani, Ronda la Kale, lililoitwa Acinipo (linalotamkwa Athinipo). Ensaiklopidia ya Hispania inasema kwamba jina hilo la Kisidonia, lilitokana na wafanyabiashara Wafoinike walioishi huko baada ya kutoka Sidoni, mji wa Lebanoni leo. Jina hilo linahusiana na maneno ya Kigiriki na ya Kilatini cha kale yanayomaanisha zabibu. Sarafu za kale zina jina Acinipo na masuke ya ngano upande mmoja na upande mwingine una kichala cha zabibu. Inaonekana watu wengi walikuwa wakulima na watengenezaji wa divai. Kitabu kimoja kinasema kwamba Acinipo, “lilisitawi na kuwa jiji kubwa lililotengeneza sarafu na baadaye wakazi wake wakawa na haki sawa na raia wa Milki ya Roma   . . . , kwa sababu ya mahali lilipokuwa.”

Kutokana na kitabu chetu cha mwongozo na ramani, tulijua Acinipo liko kilometa kadhaa kaskazini-magharibi ya Ronda. Rafiki yangu Mmarekani alifurahi sana. Ilikuwa mara yake ya kwanza kutembelea Ulaya na kuona magofu ya Milki ya Roma.

Tulipopita kijia chembamba cha mashambani tuligundua kwamba haikuwa rahisi kupata magofu hayo. Tulimwomba mchungaji aliyekuwa akilisha kondoo atuonyeshe njia. Alituhakikishia kwamba tungeona mji wa Ronda la Vieja baada ya kilometa kadhaa. Baada ya muda tuliona genge refu mbele yetu lililokuwa kama ngome. Tulipofika kwenye lango la kituo cha kutazama vitu vya kale, tuliona kilima na magofu ya vitu vya kale kila upande. Hayo yalikuwa makao ya kale, labda ya enzi za Waroma. Inaonekana watu wengi waliishi hapo wakati fulani. Juu kilimani, karibu umbali wa kilometa moja, tuliona jiwe linalofanana na ukuta. Tulivutiwa nalo. Ni magofu gani yaliyo hapo?

Kwa Nini Walijenga Jiji Hapo?

Kwa nini Waroma waliamua kujenga jiji mahali palipojitenga hivyo? Kwa sababu halingeshambuliwa na adui bila wakazi wake kutambua. Waroma hawakuwa wa kwanza kutambua umuhimu wa eneo hilo lililojitenga. Wanaakiolojia wanasema kwamba watu waliishi katika eneo hilo zaidi ya miaka 4,000 iliyopita. Wafoinike walipowasili karibu na mwaka wa 1000 K.W.K., waliliona Acinipo kuwa muhimu kibiashara kwa sababu liliunganisha majiji ya pwani ya Málaga na Cádiz.

Kulikuwa na mlinzi kwenye lango la kuingia kwenye magofu na baada ya kuzungumza naye kidogo, alituruhusu tuingilie njia ya zamani. Upande wa kulia tuliona nyumba za mviringo za karne ya nane na saba K.W.K. Tulianza kutembea kilimani na tukapata mawe yaliyokuwa sehemu ya jiji hilo lililojengwa na Waroma. Wanapochunguza vitu vilivyochimbwa hapo, wanaakiolojia wanafikia mkataa wa kwamba magofu yaliyopatikana yalikuwa majengo ya umma na kwamba uwanja ulikuwa sehemu kuu ya jiji.

Ukumbi wa Pekee

Tulivutiwa tena na ukuta mrefu kilimani. Tulijiuliza lilikuwa gofu la nini katika enzi ya Waroma. Tulipolikaribia, tuligundua kwamba tulikuwa nyuma ya ukumbi mkubwa. Ulijengwa kwa mawe na ulikuwa na tao kubwa na mnara. Kulingana na desturi ya Waroma, mawe yalichongwa na kupangwa bila kutiwa saruji. Tulipoingia kupitia tao hilo, tulijipata jukwaani tukitazama viti na ngazi zilizotumiwa na watu wapatao elfu moja. Ukumbi huo ulichongwa kwenye mwamba kilimani. Tulifurahi kujua kwamba tulikuwa mahali ambapo waigizaji na wasemaji Waroma walisimama zamani!

Waroma walijua kutumia milima vizuri kwa kuichonga na kuifanya kumbi kubwa. Magofu ya kumbi za Waroma yanapatikana sehemu mbalimbali kama vile Mérida huko magharibi mwa Hispania, Trier huko Ujerumani, na Nîmes na Arles huko Ufaransa, na hata maeneo ya kaskazini kama Caerleon, huko Wales. Yale yanayojulikana sana yako Pompeii na Rome. Watu 50,000 waliketi katika Ukumbi wa Roma! Magofu ya zaidi ya kumbi 75 za Roma yametawanyika kotekote katika Milki ya Roma ya kale. Vikundi vya waigizaji vilisafiri kutoka ukumbi mmoja hadi mwingine vikiwatumbuiza watu.

Ukumbi wa Acinipo ndiyo sehemu ya jiji iliyohifadhiwa vizuri zaidi. Sehemu yake ya kuketi iko katika mwinuko kilimani na hivyo inazuiwa na pepo zinazovuma kutoka milimani. Ukumbi huo umetengenezwa kwa njia ya kwamba sauti inaweza kusambaa kwa urahisi.

Tulipanda hadi juu ya mlima. Kila upande ulikuwa na mandhari yenye kupendeza. Upande wa kushoto, yaani kusini, tuliona jiji la Ronda, na upande wa kulia, yaani kaskazini, tuliona jiji la kale la Olvera. Huku mawingu meusi yakiwa nyuma ya jukwaa, tunaketi ukumbini katika sehemu tulivu ya kilimani tukijaribu kuwazia jinsi watu walivyotazama mchezo wa kuigiza miaka 2,000 hivi iliyopita katika jiji la Roma la Acinipo lililojitenga na lenye shughuli nyingi. Hatujui ni mambo gani mengine ambayo hayajagunduliwa bado katika jiji hilo. Huenda wakazi wa jiji hilo wataeleza yaliyotukia watakapofufuliwa.—Yohana 5:28, 29; Matendo 24:15.

[Ramani katika ukurasa wa 14]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

MADRID

Acinipo

Ronda

Málaga

[Picha katika ukurasa wa 15]

Ishara ya lango: “Kituo cha Acinipo cha Vitu vya Kale”

[Picha katika ukurasa wa 15]

Magofu ya makao ya Waroma

[Picha katika ukurasa wa 15]

Sehemu ya nyuma ya ukumbi

[Picha katika ukurasa wa 15]

Ukumbi na jukwaa

[Picha katika ukurasa wa 15]

Mnara wa ukumbi

[Picha katika ukurasa wa 15]

Acinipo limejengwa juu ya kilele hiki

[Picha katika ukurasa wa 16]

Mbele, misingi ya majengo ya kabla ya enzi ya Waroma