Bidii Kama ya Nyuki wa Carniola
Bidii Kama ya Nyuki wa Carniola
Na mwandishi wa Amkeni! nchini Slovenia
NYUKI wanajulikana kwa bidii yao. Hata hivyo, aina moja ya nyuki wana bidii kuliko wengine, yaani, nyuki wa Carniola. * Nyuki huyo amepewa jina la wilaya ya Carniola, ambayo leo iko magharibi mwa Slovenia. Mwanzoni, nyuki huyo alipatikana tu katika Rasi ya Balkan na sehemu za kaskazini kwenye Milima ya Carpathian. Hata hivyo, nyuki wa Carniola wanapendwa sana leo na wafugaji wa nyuki na wameongezeka sana duniani.
Kwa nini nyuki wa Carniola wamekuwa maarufu sana? Zaidi ya kutengeneza asali ya hali ya juu na kuhimili magonjwa na baridi, nyuki wa Carniola ni wapole. Ingawa wana tabia ya kuwa pamoja katika vikundi vikubwa, ambayo inafanya iwe vigumu kuwafuga, mbinu fulani ya uzalishaji imepunguza tabia hiyo. Lakini ni nini ambacho huwafanya nyuki wa Carniola wawe na bidii kuliko nyuki wengine? Jambo moja ni kwamba wao huondoka mizingani mapema asubuhi kuliko nyuki wengine. Hivyo, wao hukusanya umajimaji mwingi wenye sukari kwa ajili ya kutengeneza asali na wanaweza kuuleta kutoka mbali.
“Taifa la Wafugaji wa Nyuki”
Ufugaji wa nyuki una historia ndefu na yenye kupendeza nchini Slovenia. Mwanabiolojia Mslovenia, Janez Gregori, hata anawafafanua wananchi wenzake kuwa “taifa la wafugaji wa nyuki.” Na kwa hakika, Waslovenia walijulikana kuwa wafugaji wa nyuki wenye ujuzi tangu karne ya 8 W.K. Kuanzia wakati huo mpaka miaka ya 1800 walitumia mizinga iliyochongwa kutokana na magogo ya miti. Mizinga hiyo
iliitwa korita, au vihori, katika maeneo fulani ya Slovenia. Hata hivyo, karibu na karne ya 15, mizinga ya zamani iliondolewa na mahali pake kuchukuliwa na mizinga ya mbao kwa sababu mashine za kupasua mbao zilikuwa zimevumbuliwa. Mizinga hiyo iliitwa kwa mzaha truge, yaani majeneza, kwa sababu ya muundo wake.Kwa sababu watu wengi walitumia asali na nta ya nyuki, ufugaji wa nyuki ulisitawi sana hivi kwamba uliwavutia watawala ambao waliwapatia watu fulani hususa haki za kufuga nyuki. Watawala hao walipendezwa na biashara hiyo kwa sababu nta ilitumiwa kutengeneza mishumaa, hasa iliyotumiwa makanisani na kwenye majumba ya watawa, na asali ilikuwa chanzo pekee cha sukari wakati huo. Katika miaka ya 1500, nafaka fulani inayoliwa na nyuki ilianza kuzalishwa, hivyo uzalishaji wa asali ukaongezeka zaidi. Muda si muda, wilaya ya Carniola ilikuwa inauza kiasi kikubwa cha asali na nta ya nyuki katika nchi za nje. Katika karne ya 17 msomi mmoja wa Carniola, Valvasor, aliandika kwamba kufikia katikati ya karne hiyo, wilaya ya Carniola iliuza “maelfu ya tani” za asali kwenye eneo la Salzburg, Austria kila mwaka.
Umashuhuri wa Nyuki wa Carniola Waenea
Kwa miaka mingi eneo la Carniola limechangia sana utafiti na ufugaji wa nyuki. Katika mwaka wa 1770, Malkia Maria Theresa alimteua Anton Janša, mkazi wa Upper Carniola kuwa mwalimu wa kwanza katika shule ya ufugaji wa nyuki iliyokuwa imeanzishwa huko Vienna nchini Austria. Kufikia mwishoni mwa karne ya 19 utafiti wa nyuki ulionyesha kwamba nyuki wa Carniola wanaweza kufaana na mazingira mbalimbali. Wakati huo pia nyuki hao walipewa jina la Carniola na kuanza kuenezwa ulimwenguni. Kufikia mwanzoni mwa karne ya 20, eneo la Carniola liliuza “mizinga mingi ya nyuki iliyojaa katika mabehewa ya gari la moshi,” kila mzinga ukiwa na nyuki wa Carniola.
Wakati huohuo pia, mizinga ya zamani ya mbao ilianza kuitwa kranjič, au “mizinga ya Carniola.” Jambo linalofanya mizinga ya kranjič ipendeze sana ni michoro yake ya tangu zamani. (Ona sanduku lenye kichwa “Michoro ya Mizinga,” kwenye ukurasa wa 24.) Leo nchini Slovenia kuna zaidi ya wafugaji 7,000 wa nyuki wenye mizinga zaidi ya 160,000. Hata kuna jengo la makumbusho lenye vitu vya kale vya ufugaji wa nyuki katika mji wa Radovljica nchini Slovenia.
Ishara Inayopendwa
Kwa muda mrefu, Waslovenia wamewaona nyuki kuwa ishara ya bidii na hekima. Chama cha kwanza cha wanasayansi kilichoanzishwa mwaka wa 1693 katika nchi ambayo sasa ni Slovenia, kiliitwa Chama cha Wenye Bidii na nembo yake ilikuwa nyuki. Wanachama wake hata walijiita apes, neno la Kilatini linalomaanisha “nyuki.” Kwa kuwa Waslovenia wanawaona kuwa ishara ya mafanikio, nyuki wametumiwa hata katika biashara. Unaweza kuona ishara ya nyuki kwenye majalada ya vitabu vya benki na nyuma ya sarafu kadhaa za Slovenia.
Waslovenia hujihusianisha na nyuki kwa sababu ya bidii yao. Kuna msemo wa Kislovenia unaosema, “Watazame nyuki na uwaige.” Kwa hiyo, wakati wowote unapowaona nyuki au kuonja asali—matokeo mazuri ya kazi yao—huenda ukawakumbuka nyuki wenye bidii wa Carniola.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 3 Nyuki wa Carniola ana manyoya ya kijivu kuzunguka tumbo lake.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 24]
Michoro ya Mizinga
Katika sehemu za kufugia nyuki huko Slovenia, mizinga hupangwa pamoja kama droo zenye umbo la mstatili, upande mfupi ukiangalia mbele. Ustadi wa kupaka rangi za mafuta kwenye sehemu za mbele za mizinga ulisitawi tangu miaka ya 1700 mpaka miaka ya 1900. Ingawa mizinga 3,000 ya aina hiyo imehifadhiwa, hiyo ni idadi ndogo tu ya mizinga ambayo imewahi kutengenezwa na kurembeshwa.
Mizinga hiyo ina michoro ya kidini hasa, inayoonyesha picha za “watakatifu” na hadithi za Biblia. Lakini michoro hiyo pia ina picha za wanyama na watu wakifanya kazi zao pamoja na mandhari mbalimbali zenye kuchekesha. Baadhi ya michoro hiyo inahusu familia. Kwa mfano, picha fulani huonyesha roho waovu wawili wakisaga ulimi wa mwanamke mchongezi kwa kutumia jiwe la kusagia, huku nyingine zikionyesha mke anayemburuta mume wake kutoka katika baa.
Michoro hiyo kwenye mizinga imesemwa kuwa “lulu za utamaduni wa Kislovenia,” “ensaiklopedia ya hekima ya watu wa kale,” na “labda ustadi halisi wa watu wa Slovenia.” Lakini michoro hiyo ilikusudiwa kutimiza kusudi fulani muhimu pia. Kwa kuwa kulikuwa na mizinga mingi mahali pamoja, nyuki angeweza kupotea na kuingia mzinga mwingine ambamo angefikiriwa kuwa mvamizi na kuuawa. Wafugaji wa nyuki waliamini kwamba michoro ya rangi mbalimbali nyuma ya mizinga, iliwaongoza nyuki kwenye mizinga yao.
[Picha]
“Adamu na Hawa”
“Yosefu Auzwa Misri”
“Yesu Awasili Yerusalemu”
Mizinga ya Slovenia iliyopakwa rangi
[Hisani]
All apiary photos: Z dovoljenjem upravitelja rojstne hiše pisatelja Josipa Jurčiča
[Ramani katika ukurasa wa 21]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
AUSTRIA
ITALIA
SLOVENIA
Carniola
KROATIA
BAHARI YA ADRIATIKI
[Hisani]
Map: Mountain High Maps® Copyright © 1997 Digital Wisdom, Inc.
[Picha katika ukurasa wa 22]
Sarafu ya Slovenia iliyo na picha ya nyuki maarufu wa Carniola
[Picha katika ukurasa wa 23]
Nyuki wa Carniola anajulikana kwa kuwa mpole
[Picha katika ukurasa wa 23]
Viluwiluwi
[Picha katika ukurasa wa 23]
Malkia akiwa amezungukwa na nyuki wachanga wa kazi
[Hisani]
Foto: Janez Gregori