Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Watoto Wenye Urafiki Hupendwa

Gazeti la Ujerumani Psychologie Heute linasema hivi: “Kuwa na jinzi nzuri na vitu vya kisasa hakumfanyi mtoto apendwe. Mtoto hupendwa zaidi na wenzake kwa sababu ni mwenye urafiki wala si kwa kuwa wao ni matajiri.” Judith Schrenk na Christine Gürtler, ambao ni wanasaikolojia katika Taasisi ya Maendeleo ya Max Planck huko Berlin, waliwahoji watoto 234 walio katika darasa la tatu na la tano kutoka shule kumi za msingi. Waligundua kwamba watoto ambao wanaweza kuishi vizuri na wengine, wenye urafiki, na wanaopenda kuzungumza, walipendwa sana. Watoto waliowapiga au kuwacheka wenzao hawakupendwa. Ripoti hiyo inasema kwamba “hata kuwa na sura nzuri au pesa nyingi hakumfanyi mtoto apendwe na wanashule wenzake.”

Umuhimu wa Kitimiri

Ingawa mara nyingi kitimiri hutumiwa kurembesha chakula, hiyo ni chanzo muhimu cha vitamini na madini, lasema gazeti Sunday Telegraph la Australia. “Kikombe kimoja cha kitimiri kina Vitamini A nyingi kuliko karoti kubwa, Vitamini C karibu mara mbili zaidi ya chungwa, na kalisi nyingi kuliko kikombe cha maziwa. Isitoshe, kitimiri ina madini mengi ya chuma kuliko maini, na ni chanzo muhimu cha Vitamini B1 na B2.” Gazeti hilo linasema kwamba katika tiba “kitimiri huongeza mkojo, jambo ambalo huuwezesha mwili kuondoa uchafu.” Inaweza kumsaidia mtu ambaye ana matatizo ya ini, wengu, tumbo, na mkojo. Inapoliwa ikiwa mbichi, “inafanya mdomo unukie vizuri na haigharimu sana.” Hata hivyo, makala hiyo inaonya kwamba “katika hali fulani, kama wakati wa mimba, . . . huwa hatari kwa sababu ina homoni ya estrojeni.”

Je, Kadi za Biashara Zitaacha Kutumiwa?

Mtaalamu wa usalama, Carl Paladini alisema hivi kama ilivyoripotiwa katika jarida la biashara la Brazili, Exame: “Kwa kuwa watu wengi zaidi wanatekwa nyara siku hizi nchini Brazili, afadhali wakurugenzi wasibebe kadi zao za biashara zinazoonyesha kazi wanazofanya na vyeo vyao.” Wahalifu wanaweza kujua kiasi cha pesa alicho nacho mtu wakipata habari hizo za kibinafsi. Vagner D’Angelo, mkurugenzi wa shirika kubwa la usalama la Kroll anasema kwamba “habari zilizo katika mfuko wako zinaweza kuhatarisha maisha yako.” Anawashauri wafanyabiashara katika nchi zenye visa vingi vya utekaji-nyara watoe habari zote kuhusu kazi na vyeo vyao kwenye kadi zao na “wasiwe na kadi zilizotengenezwa kwa karatasi na herufi za hali ya juu.” Wakurugenzi wengine wameamua kutotumia kadi za biashara tena kwani wahalifu huenda wakagundua kwamba kadi za biashara hazionyeshi cheo cha mtu.

Janga la UKIMWI Huko Karibea

Toleo la kimataifa la gazeti The Miami Herald linaripoti kwamba eneo la Karibea ndilo lenye idadi kubwa zaidi ya watu ambao wameambukizwa virusi vya HIV duniani, baada ya Afrika. “Inakadiriwa kwamba asilimia 2.4 ya watu wazima huko Karibea wameambukizwa virusi vya [HIV],” na karibu asilimia 12 wameambukizwa katika miji fulani. Gazeti Herald linasema kwamba “idadi kamili ya watu walioambukizwa haijulikani kwa sababu ya woga, majuto, kubaguliwa, na ukosefu wa huduma za afya. Inaaminika kwamba watu wazima na watoto 40,000 hivi walikufa kutokana na ugonjwa huo huko Karibea katika mwaka wa 2001 pekee.” Mtaalamu wa afya wa Benki ya Dunia katika Karibea na Amerika ya Latini, Patricio Marquez, anasema kwamba UKIMWI “unaambukiza watu wanaoweza kufanya kazi vizuri zaidi walio na umri mzuri zaidi wa kufanya kazi . . . Kuna hatari kwamba kizazi kizima kitaangamizwa.” Nchi inayoathiriwa zaidi ni Haiti, ambapo zaidi ya asilimia 6 wameambukizwa. Gazeti Herald linasema hivi: “Wataalamu wa afya wanaonya kwamba eneo hilo dogo linaweza kuangamia . . . kwani linategemea wafanyakazi, rasilimali chache, na biashara ya utalii.”

Wanang’aa Chini ya Miale ya Urujuanimno

Kwa muda mrefu wanasayansi wameamini kwamba rangi zinazong’aa za ndege fulani huwasaidia kuvutia ndege wa jinsia tofauti. Wanabiolojia katika Chuo Kikuu cha Queen’s huko Kingston, Ontario, Kanada, wamegundua kwamba manyoya ya aina fulani ya ndege hurudisha miale ya urujuanimno. Jarida Canadian Geographic linasema hivi: “Wakitumia kifaa cha kutambua nuru hiyo kinachofanana na kalamu, watafiti wamegundua jambo ambalo hatuwezi kuona kuhusu manyoya yasiyong’aa ya ndege aitwaye black-capped chickadee.” Kifaa hicho kilionyesha kwamba “ndege wa kiume hutoa rangi nyeupe inayong’aa sana wakilinganishwa na wa kike. Sehemu ya chini ya mdomo wa ndege wanaowavutia ndege wa kike hutoa mng’ao wa urujuanimno, ambao wanadamu hawawezi kuona.” Gazeti Canadian Geographic linasema kwamba uvumbuzi huo unaunga mkono dhana ya kwamba ndege “huona rangi nyingi vizuri kuliko wanadamu.”

Mlipuko Mkubwa Zaidi Ulimwenguni

Mwezi wa sayari ya Sumbula, unaoitwa Io, ulipata “mlipuko mkubwa zaidi wa volkano kuwahi kutokea ulimwenguni,” laripoti gazeti Science News. “Nguvu za uvutano za sayari ya Sumbula huusonga sana mwezi huo na kuupasha joto sana, hivyo kuufanya ulipuke. Mwezi huo hulipuka mara nyingi sana kila mwaka.” Kulingana na makala hiyo, “inaonekana vitu vilivyotokana na mlipuko huo wa ajabu vilifunika eneo la ukubwa wa kilometa 1,900 za mraba, ambalo ni kubwa karibu mara elfu moja kuliko Mlima Etna wa Italia, ambao ni mmojawapo wa milima inayolipuka sana duniani.” Wanasayansi walitambua mlipuko huo wakitumia darubini yenye nguvu sana, inayoitwa Keck 2, iliyo katika Mlima Mauna Kea, huko Hawaii, ambao umeacha kulipuka. Gazeti Science News linasema kwamba darubini hiyo ilitambua milipuko hiyo kwa sababu imewekewa mitambo ya hali ya juu, ambayo “inaweza kupima milipuko licha ya msukosuko katika angahewa la Dunia.”

Jinsi Wazazi Wanavyoathiriwa na Kifo cha Mtoto

Kulingana na gazeti The Times la London, watafiti katika Chuo Kikuu cha Århus, huko Denmark, “wamechunguza maisha ya wazazi 21,062 nchini Denmark waliofiwa na watoto wao walio chini ya umri wa miaka 18 kwa sababu ya ugonjwa, msiba wa barabarani, kuuawa, au kujiua.” Walilinganisha hali ya wazazi hao na ile ya wazazi 300,000 ambao hawakufiwa na watoto. “Katika miaka mitatu ya kwanza baada ya kufiwa, mama hao walikuwa na uwezekano wa karibu mara nne wa kufa kutokana na sababu zisizo za kiasili kama vile msiba wa barabarani au kujiua, na akina baba walikuwa na hatari ya asilimia 57 zaidi.” Watafiti hao wanasema kwamba huenda mfadhaiko ndio sababu kuu ya vifo hivyo.