Methusela Mlimani
Methusela Mlimani
KATIKA Milima White iliyo magharibi mwa Marekani, kuna msonobari aina ya bristlecone kwenye mwinuko wa meta 3,000, unaoitwa Methusela au Mzee, na unaaminika kuwa mti mzee zaidi duniani. Methusela ni mti mzee kati ya misonobari inayoitwa Miti ya Methusela na unakadiriwa kuwa na miaka zaidi ya 4,700. *
Miti hiyo hukua katika hali ngumu sana. Ripoti moja katika gazeti New Scientist inasema hivi: “Mvua hunyesha kidogo sana na mara nyingi inanyesha ikiwa theluji na haizidi sentimeta 30 kwa mwaka, hivyo miti hiyo haipati maji ya kutosha. Isitoshe, miti hiyo hukua kwenye udongo wa chokaa wenye kiasi kidogo sana cha rutuba.” Zaidi ya hilo, “hali ya hewa huwa joto au baridi kupita kiasi na pepo kali sana huvuma.”
Hali hizo ngumu ndizo hufanya miti hiyo iishi kwa muda mrefu. Gazeti New Scientist linaeleza hivi: “Huwa kuna ukavu sana hivi kwamba virusi na bakteria haviwezi kusitawi. Isitoshe, shina la msonobari wa bristlecone ni gumu sana na lina utomvu mwingi sana hivi kwamba wadudu hawawezi kulipenya. Kwa kuwa radi inaweza kuwasha moto, miti hiyo iko mbalimbali hivyo moto hauwezi kusambaa.”
Kila msimu wa ukuzi huchukua siku 45 hivi. Miti hiyo huhifadhi virutubisho kwa kukua polepole sana. Upana wake huongezeka kwa milimeta 25 kwa miaka 100, na majani yake huishi kwa miaka 30. Mti mrefu zaidi huwa na meta 18 hivi. Watafiti wanakadiria kwamba misonobari ambayo imeishi kwa miaka mingi huenda ikaishi kwa miaka 500 mingine zaidi.
Katika miaka ya karibuni, watu ambao wanataka kuongeza uhai wa mwanadamu, wameuchunguza msonobari huo wakitumaini kujua kinachofanya uishi kwa muda mrefu hivyo. Hata hivyo, siri ya kuishi muda mrefu haipatikani kwa kupanda milima mirefu ili kujifunza kuhusu mti huo wa kale, bali inapatikana kwa urahisi zaidi. Kitabu cha kale zaidi ulimwenguni, Biblia, kinasema: “Uzima wa milele ndio huu, waendelee kupata ujuzi juu yako wewe, Mungu wa pekee wa kweli, na juu ya yule uliyemtuma, Yesu Kristo.” (Yohana 17:3) Kila mtu anaweza kupata ujuzi huo. Mbona usijichunguzie mwenyewe?
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 2 Methusela, babu ya Noa, aliishi miaka 969 na ndiye aliyeishi miaka mingi zaidi kuliko mtu mwingine yeyote anayetajwa katika Biblia.—Mwanzo 5:27; Luka 3:36, 37.
[Picha katika ukurasa wa 15]
Mojawapo ya misonobari ya “bristlecone” katika Miti ya Methusela