Je, Wajua?
Je, Wajua?
(Majibu ya maswali haya yanapatikana katika maandiko ya Biblia ambayo yameonyeshwa, na orodha kamili ya majibu imechapwa katika ukurasa wa 24. Unaweza kupata habari zaidi katika kichapo “Insight on the Scriptures,” kilichochapishwa na Mashahidi wa Yehova.)
1. Abrahamu alinunua nini kutoka kwa wana wa Hethi kwa shekeli 400 za fedha? (Mwanzo 23:16-20)
2. Ni vitu gani viwili vilivyotumiwa katika zile ishara mbili ambazo Gideoni aliomba ili athibitishiwe kwamba Mungu angemsaidia kupigana na Wamidiani? (Waamuzi 6:36-40)
3. Ni nini kilichomvutia Akani sana hata akapuuza amri ya Mungu na kuwafanya Waisraeli washindwe huko Ai? (Yoshua 7:21)
4. Mungu alipomuumbia Adamu mke, aliagiza kwamba tangu wakati huo na kuendelea wenzi wa ndoa wangekuwa nini? (Mwanzo 2:24)
5. Ni mazoea gani ya kuwasiliana na pepo yanayoshutumiwa katika Biblia? (Kumbukumbu la Torati 18:10, 11)
6. Mfalme Ahasuero aliadhimishaje kutawazwa kwa Esta kuwa malkia wake? (Esta 2:18)
7. Yesu alitabiri kwamba wafuasi wake watafanywa nini kwa sababu ya jina lake? (Mathayo 10:22)
8. Yule mwanamke Mmidiani aliyeuawa na Finehasi wakati ambapo Zimri alimleta ndani ya kambi ya Israeli kwa makusudi mapotovu alikuwa nani? (Hesabu 25:15)
9. Ni nani anayefafanuliwa katika sura ya 31 ya Methali? (Methali 31:10)
10. Ni nani aliyesababisha kifo cha Amnoni, mwana wa kwanza wa Daudi, ambaye licha ya hayo Daudi alimsamehe baadaye? (2 Samweli 13:32, 33)
11. Kwa nini mke wa Daudi, Mikali, ‘alimdharau moyoni mwake’ na hivyo akafa bila mtoto? (2 Samweli 6:14-16, 20-23)
12. Biblia huhusianisha Har–Magedoni na nini? (Ufunuo 16:14, 16)
13. Kwa nini umati uliacha ghafula kutaka kumtolea Paulo dhabihu na kuanza kumpiga kwa mawe huko Listra? (Matendo 14:19)
14. Petro alifanya nini alipokuwa akijaribu kumlinda Yesu dhidi ya askari-jeshi waliokuwa wamekuja kumkamata? (Yohana 18:10)
15. Katika jaribu la tatu nyikani, Ibilisi alijaribu kumshawishi Yesu afanye nini? (Mathayo 4:9)
16. Ni kitu gani ambacho hutumiwa katika Biblia kuwakilisha dhambi au kuharibika? (Mathayo 16:6)
17. Inasemekana kwamba hekima ya Sulemani ilipita hekima ya nani wengine? (1 Wafalme 4:31)
Majibu ya Maswali
1. Mahali pa familia pa kuzikia
2. Umande na manyoya ya kondoo
3. “Vazi rasmi kutoka Shinari” pamoja na fedha na dhahabu
4. “Mwili mmoja”
5. Uaguzi, uchawi, kutafuta ishara za bahati, ulozi, kufunga wengine kwa kuwatakia maovu, kutafuta shauri kwa mwenye kuwasiliana na pepo, kubashiri matukio, na kadhalika
6. Alifanya karamu kubwa, akatoa msamaha kwa wilaya zake za utawala, na kutoa zawadi
7. ‘Watachukiwa’
8. Kozbi, binti ya Suri
9. “Mke mwenye uwezo”
10. Mwana wa tatu wa Daudi, Absalomu
11. Alipinga jinsi Daudi alivyokuwa “akiruka na kucheza dansi huku na huku mbele za Yehova” kwa shangwe
12. “Vita vya ile siku kuu ya Mungu Mweza-Yote”
13. Wayahudi kutoka Antiokia na Ikoniamu walifika, wakaushawishi umati ufanye hivyo
14. Aliuchomoa upanga wake na kumpiga yule mtumwa aliyeitwa Malko, akalikata sikio lake la kuume
15. Amfanyie “tendo la ibada”
16. Chachu
17. Ethani, Hemani, Kalkoli, na Darda