Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kisiwa Kilichotokea na Kutoweka

Kisiwa Kilichotokea na Kutoweka

Kisiwa Kilichotokea na Kutoweka

Na mwandishi wa Amkeni! nchini Italia

MNAMO Juni 28, 1831, tetemeko kubwa la nchi lilikumba pwani ya magharibi ya kisiwa cha Sicily katika Bahari ya Mediterania. Huko baharini, baharia mmoja alifikiri meli yake imegonga kilima cha mchanga.

Kwa siku kadhaa, kulikuwa na msukosuko wa maji baharini karibu na pwani ya Sicily. Samaki waliokufa walielea juu ya maji. Kulikuwa na harufu mbaya ya salfa. Mawe ya fuwawe yalisukumwa ufuoni.

Mnamo Julai 10, Giovanni Corrao, nahodha wa meli iliyoitwa Teresina ya Naples, alikuwa akiabiri kwenye Bahari ya Mediterania alipoona jambo la kustaajabisha. Aliona maji mengi na moshi ukipaa meta 20 juu ya bahari. Pia alisikia “kelele kubwa kama ngurumo.”

Ferdinand wa Pili aliyetawala Ufalme wa Sehemu Mbili za Sicily aliamuru meli ya kivita ya Etna ifanye uchunguzi. Habari za tukio hilo zilifika pia Malta, iliyokuwa chini ya Uingereza wakati huo. Kwa kuwa hakutaka kuachwa nyuma, Sir Henry Hotham naibu wa mkuu wa jeshi la wanamaji la Uingereza kwenye kisiwa hicho alituma meli “kuchunguza mahali hususa ambapo tukio hilo lilitokea na kufanya uchunguzi zaidi.”

Hivyo, mgogoro ukaanza na kuendelea hadi leo hii.

Kisiwa Chatokea

Kufikia Julai 19, 1831, kisiwa kipya kilitokea baada ya mlipuko wa volkano ndani ya maji kati ya Sicily na pwani ya Afrika. Charles Swinburne, kamanda wa meli ya Uingereza iliyoitwa Rapid alikuwa akiabiri kwenye ncha ya magharibi ya Sicily alipoona nguzo ndefu ya moshi mweupe sana au mvuke. Swinburne alielekea huko moja kwa moja. Jioni, miale miangavu ilitokea kwenye moshi huo, na ilionekana waziwazi hata katika mbalamwezi. Moto ulilipuka katikati ya moshi huo. Kulipopambazuka, moshi ulikuwa umepungua kidogo, hivyo akaona “kilima kidogo cheusi meta kadhaa juu ya bahari.”

Kwa muda usiozidi mwezi mmoja kisiwa hicho kilikuwa kimefikia karibu meta 65 juu ya maji na kilikuwa na mzingo wa kilometa 3.5 hivi. Gazeti Malta Government Gazette lilisema hivi: “Tukio hilo limewafanya wengi wapendezwe na visiwa hivyo na watu wengi tayari wamefika mahali lilipotukia.” Mmoja wao ni Profesa Friedrich Hoffmann, mwanajiolojia kutoka Prussia aliyekuwa akifanya utafiti huko Sicily. Hoffmann alifika kilometa moja tu kutoka kwenye kisiwa hicho na alikiona “waziwazi kabisa.” Lakini, kwa kuogopa hatari ambazo zingetokea, Hoffmann akakataa kutua kwenye kisiwa hicho.

Nahodha Humphrey Senhouse, hakuogopa chochote kwani inasemekana mnamo Agosti 2 alifika kwenye kisiwa hicho na kusimamisha bendera ya Uingereza. Alikiita kisiwa hicho Kisiwa cha Graham kwa kumkumbuka Sir James Graham aliyekuwa waziri wa jeshi la wanamaji.

Chuo Kikuu cha Catania huko Sicily, kilimpa Carlo Gemellaro, profesa wa uchunguzi wa maumbile, kazi ya kuchunguza kisiwa hicho. Alikiita Ferdinandea, kwa kumkumbuka Ferdinand wa Pili. Kwa kuwa hakufurahishwa na mambo aliyosikia kuhusu bendera ya Uingereza iliyokuwapo, Ferdinand alitangaza rasmi kwamba kisiwa hicho ni sehemu ya ufalme wake hata ingawa kilikuwa nje ya mipaka ya Sicily.

Wafaransa walikuwa wa mwisho kufika huko. Mwanajiolojia Constant Prévost alikiita kisiwa hicho Julia, kwa kuwa kilitokea katika mwezi wa Julai. Yeye pia alisimamisha bendera ya nchi yake kwenye kisiwa hicho. Aliandika kwamba alifanya hivyo ili “kuwajulisha watu wote ambao wangekuja baadaye kwamba Ufaransa haipotezi fursa yoyote ya kuonyesha kwamba inapendezwa na mambo ya sayansi.”

Mabishano kuhusu umiliki wa kisiwa hicho yalizidi. Kulingana na makala ya hivi majuzi katika gazeti Times la London, Italia, Ufaransa, na Uingereza zilikuwa “karibu kupigana” kwa sababu ya sehemu hiyo ndogo.

Kisiwa Chatoweka

Mgogoro kuhusu kisiwa hicho kinachoitwa Julia, Ferdinandea, au Graham * hadi leo hii, haukudumu kwa muda mrefu. Baada ya kutembelea kisiwa hicho mwezi wa Septemba, Hoffmann aliandika hivi: “Kisiwa hicho kinazama polepole kila siku, na ikiwa uharibifu huu ambao tumejionea utaendelea . . . , dhoruba za baridi kali zitakiharibu kabisa kwa miezi michache.”

Kufikia Desemba, kisiwa hicho kilikuwa kimezama hivi kwamba kilibaki tu kama mwamba wa meta kadhaa chini ya usawa wa bahari. Giuseppe Mercalli, ambaye ni mtaalamu wa volkano wa Italia, aliandika hivi: “Kile kilichosalia kuhusu Kisiwa cha Julia ni majina ambayo kilipewa na wasafiri kutoka mataifa mbalimbali waliokuwa na pendeleo la kujionea jinsi kilivyotokea na kutoweka.”

Je, Chatokea Tena?

Je, huo ndio mwisho wake? La hasha! Bado kuna utendaji wa volkano mahali ambapo kisiwa hicho kilikuwa. Kulingana na mwanahistoria wa Sicily, Salvatore Mazzarella, leo eneo hilo ni “muhimu sana kama lilivyokuwa katika karne ya 19.” Wanajiolojia fulani wanaamini kwamba kisiwa hicho kitatokea tena. Tayari kuna wasiwasi kuhusu yule atakayemiliki kisiwa hicho endapo kitatokea.

Simulizi la kisiwa hicho kilichotokea na kutoweka ni jambo lingine la kuhuzunisha katika utawala wa mwanadamu. Mwandishi wa habari Mwitaliano, Filippo D’Arpa, anafafanua hali hiyo vizuri sana anaposema, “huo ni mfano unaoonyesha upumbavu wa mamlaka.”

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 16 Kisiwa hicho kilipewa angalau majina mengine manne, yaani, Corrao, Hotham, Nerita, na Sciacca.

[Picha katika ukurasa wa 26]

Mchoro wa mlipuko wa mwaka wa 1831

[Hisani]

Copyright Peter Francis/The Open University