Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuwauzia Watoto Chakula Kisichofaa

Makala moja katika gazeti IHT Asahi Shimbun la Tokyo ilisema kwamba wataalamu wengi wa lishe wanashutumu makampuni yanayouza vyakula visivyojenga mwili kwa kuwa na “matangazo mengi ya biashara yanayoharibu mazoea ya watoto ya kula na yanayosababisha wawe wanene kupita kiasi.” Ripoti hiyo ilisema: “Televisheni ndiyo njia kuu ya kuwatangazia watoto bidhaa,” na isitoshe, makampuni ya chakula “yanatafuta kila njia kuwatangazia watoto bidhaa zao.” Filamu, michezo, vituo vya Internet, vitabu vya hesabu, na vitu vingi vya kuchezea huwa na matangazo ya biashara ya vyakula. Kwa nini wanawatangazia watoto? James McNeal, profesa wa mauzo wa Chuo Kikuu cha Texas A&M, anasema: “Watoto ndio wanunuzi wakuu.” Hata hivyo, Profesa Walter Willet wa Chuo cha Harvard cha Afya ya Umma anasema: “Vyakula vingi wanavyotangaza havifai. Ni mara ngapi unapoona matunda na mboga zikitangazwa?”

Chupa za Maji

Gazeti Better Homes & Gardens linaripoti kwamba uchunguzi uliofanywa na Chuo Kikuu cha Calgary huko Kanada, ulifunua kwamba “chupa za maji ambazo zilitumiwa tena bila kusafishwa zina bakteria nyingi sana.” Uchunguzi huo ulionyesha kwamba zaidi ya asilimia 13 ya chupa zilizotumiwa na wanafunzi wa shule za msingi, zilikuwa na bakteria nyingi hatari. Bakteria hizo zilitia ndani bakteria za kinyesi labda kwa sababu wanafunzi hao hawakunawa mikono vizuri. Mtafiti mmoja anapendekeza kwamba chupa za maji zioshwe kwa ukawaida kwa maji ya moto na sabuni na kukaushwa kabisa kabla ya kutumiwa tena.

Masomo ya Muziki na Kumbukumbu

Gazeti Globe and Mail la Kanada linasema kwamba utafiti mpya unaonyesha kuwa “watoto wanaojifunza muziki huwa na kumbukumbu na msamiati bora kuliko watoto ambao hawajajifunza muziki.” Kulingana na Dakt. Agnes Chan wa Chuo Kikuu cha Hong Kong, huko China, kujifunza muziki huchochea upande wa kushoto wa ubongo na kuboresha utendaji wote wa ubongo na kuuwezesha kufanya kazi nyingine vizuri kama vile kujifunza maneno. Wanafunzi 90 wenye umri kati ya miaka 6 na 15, walichunguzwa kuhusu uwezo wao wa kukumbuka maneno na vitu walivyoona. Wale waliojifunza muziki, walikumbuka maneno mengi sana kuliko wanafunzi ambao hawakujifunza muziki. Kadiri walivyoendelea kujifunza muziki, ndivyo uwezo wao wa kujifunza maneno mapya ulivyoongezeka. Dakt. Chan alisema, “Mazoezi hayo ya ubongo yanasaidia kwa njia nyingi.” Anaamini kwamba wale wanaojifunza muziki “huenda wakajifunza kwa urahisi shuleni.”

Kuna Nyota Ngapi?

Gazeti The Daily Telegraph la London linasema: “Wataalamu wa nyota wamekadiria kwamba kuna nyota 70,000,000,000,000,000,000,000 zinazoonekana kutoka duniani” kwa darubini. Wataalamu hao kutoka Marekani, Australia, na Scotland, “walihesabu galaksi zote zinazopatikana katika eneo dogo la angani lililo karibu na Dunia” na kukadiria idadi ya nyota katika kila galaksi. Kwa kutumia hesabu hiyo walikadiria idadi ya nyota katika sehemu nyingine za anga. Dakt. Simon Driver wa Australia aliyeongoza kikundi hicho alisema: “Hiyo si idadi yote ya nyota angani, lakini ni idadi inayoweza kuonekana na darubini zetu. Hata kwa mtaalamu wa nyota aliyezoea kupiga hesabu kubwa, idadi hiyo ni tata sana.” Ni maelfu kadhaa tu ya nyota yanayoweza kuonwa kutoka katika sehemu zenye giza duniani bila kutumia darubini, na 100 tu ndizo zinazoweza kuonekana kutoka katika majiji makubwa.

Magurudumu Yasiyo na Pumzi

Taarifa moja katika gazeti Valeurs actuelles la Ufaransa inasema: “Msiba mmoja kati ya misiba 17 ya barabarani unahusiana moja kwa moja na hali ya magurudumu.” Uchunguzi mbalimbali uliofanywa na kampuni ya magurudumu ya Michelin ulionyesha kwamba “katika mwaka wa 2002, magari 2 kati ya 3 yalikuwa na angalau gurudumu moja lisilo na pumzi ya kutosha.” Kulingana na Pierre Menendes, mkurugenzi wa teknolojia ya mawasiliano katika kampuni ya Michelin, “madereva hufikiria kimakosa kwamba magurudumu yao yanaweza kupasuka yanapokuwa na pumzi nyingi sana na kwamba ni hatari kuliko magurudumu yenye pumzi kidogo sana. Hata hivyo, pumzi kidogo sana ni hatari kuliko pumzi nyingi sana.” Kulingana na ripoti hiyo, pumzi inapopungua sana kwenye gurudumu, inakuwa vigumu kufunga breki haraka, magurudumu huteleza kwenye njia zinazopinda, na “dereva anaweza kushindwa kudhibiti gari anapogeuza usukani ghafula.” Isitoshe, pumzi inapopungua, umbo la gurudumu hubadilika. Hilo husababisha sehemu zake ziwe moto na hatimaye gurudumu huharibika.

Imani ya Wafaransa Inapungua

Gazeti Le Monde la Ufaransa linasema kwamba “watu wengi wanaacha dini” huko Ufaransa. Ijapokuwa asilimia 73 ya Wafaransa hudai kufuata dini, ni asilimia 24 tu “wanaosadiki” kwamba Mungu yupo. Asilimia 34 walisema kwamba “huenda” yupo, asilimia 19 walisema “haielekei” yupo, na asilimia 22 wakasema kwamba “hayupo.” Ni asilimia 12 tu ya watu waliohojiwa ambao huhudhuria ibada angalau mara moja kwa juma, na asilimia 25 husali “kila siku” au “mara nyingi zaidi.” Mwanasosiolojia Régis Debray alisema kwamba siku hizi watu wanafuata dini si kwa sababu ya imani, bali ili kuwa washiriki tu. Alisema: “Siku hizi dini ni kama kitambulisho tu.”

Tarumbeta za Makombe

Gazeti New Scientist linaripoti hivi: “Huenda tarumbeta zilizotumiwa zamani na Waperu na kutengenezwa kwa makombe ya Strombus zilitumiwa kutoa ishara kutoka mbali.” Watafiti wamegundua tarumbeta 20 za makombe zenye mapambo huko Peru, ambazo zilitengenezwa na sehemu ya kupulizia. Zilipojaribiwa, tarumbeta hizo zilitoa sauti ya desibeli 111. Gazeti New Scientist linasema hivi: “Katika milima ya Andes yenye utulivu, sauti ya tarumbeta hizo ingesikika kufikia umbali wa angalau kilometa nne.”

Kadi za Mikopo na Arusi

Kwenye arusi zinazofanywa huko Uturuki, watu wenye nia njema humpa bibi arusi vito na bwana arusi pesa. Lakini, kama ilivyo katika nchi nyingi, kadi za mikopo zimeanza kutumiwa sana nchini Uturuki. Gazeti Frankfurter Allgemeine Zeitung linaripoti kwamba kwenye arusi moja iliyofanywa hivi majuzi huko Antalya, bwana na bibi arusi walileta mashine ya kadi za mikopo kwenye karamu. Marafiki na watu wa ukoo walitumia kadi zao kuingiza pesa katika akaunti ya benki ya wenzi hao, kisha wakawapa risiti.

Jinsi Mizinga Inavyopashwa Joto

Gazeti Frankfurter Allgemeine Zeitung linasema kwamba nyuki hufanyiza joto “kwa kutikisa misuli yao ya kuruka” ili kustahimili baridi kali. Lakini joto la mzinga hutofautiana. Nyuki wanapokuwa katikati ya mzinga, joto lao huwa nyuzi 30 Selsiasi, na wanapokuwa karibu na kuta za mzinga, joto lao huwa karibu nyuzi 12 Selsiasi chini ya kipimo cha mgando. Wanasayansi kwenye Chuo Kikuu cha Graz, Austria, wamegundua kwamba nyuki walio katikati ya mzinga hutikisa misuli yao mara nyingi zaidi ya wale walio karibu na kuta. Kwa njia hiyo, nyuki hao huhifadhi joto jingi ndani ya mzinga na kupunguza mahitaji yao ya chakula wakati wa baridi kali. Lakini swali ni: Nyuki walio katikati ya mzinga hujuaje kwamba wanapaswa kufanyiza joto jingi kuliko nyuki walio karibu na kuta?