Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, Kuna Ngamia Huko Andes?

Je, Kuna Ngamia Huko Andes?

Je, Kuna Ngamia Huko Andes?

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI PERU

JE, KUNA ngamia huko Amerika Kusini? Wazo lenyewe huenda likashangaza kwani mnyama huyo wa jangwani mara nyingi hupatikana Afrika au Asia. Hata hivyo, ngamia wanaopatikana Afrika na Asia ni wa jamii ya wanyama wanaoitwa lamoid wa Amerika Kusini. * Hata hivyo, tofauti na ngamia wa Afrika, wanyama hao wa Amerika Kusini hawana nundu. Isitoshe, ni warefu kama mtu wa wastani na hawafiki hata kwenye bega la ngamia wa kawaida au mwenye nundu mbili.

Unaweza kuwaona wanyama hao wa Amerika Kusini ukiwa katika Milima ya Andes, hasa huko Bolivia na Peru. Pia wanapatikana katika sehemu nyingine za Amerika Kusini, kutia ndani Patagonia na Tierra del Fuego huko Argentina na Chile.

Kinachopendeza hasa kuhusu wanyama hao ni jinsi wanavyotembea kasi na kwa madaha. Ni jambo lenye kupendeza pia kuona jinsi wanavyopanda milima yenye miamba. Miguu yao haiumii wanapotembea kwa sababu wana nyayo za pekee zilizo bora kuliko viatu vya kisasa vya kutembea.

Milima ya Andes haina nyasi nyingi wala udongo mwingi. Hata hivyo, kwato za wanyama hao wa Amerika Kusini haziharibu udongo sana kama za farasi na nyumbu. Isitoshe, meno na kaakaa za wanyama hao huwawezesha kula nyasi bila kuharibu mizizi.

Wanyama wengi hawawezi kustahimili maeneo ya milimani. Lakini kwa sababu wana chembe nyingi nyekundu za damu, wanyama hao wa Amerika Kusini wanaweza kuishi bila matatizo hata kwenye Milima ya Andes.

Katika maeneo yasiyo na kuni, kinyesi kilichokauka cha wanyama hao wa Amerika Kusini hutumiwa. Kwa kuwa wanyama wa mwituni huweka kinyesi kwenye mipaka ya makao yao, ni rahisi kukikusanya na kukitumia kama kuni. Kinyesi hicho hukaushwa upesi na hewa kavu ya Milima ya Andes, na hivyo inakuwa rahisi kutumiwa.

Zamani, wanyama hao walitumiwa katika desturi za kidini. Kwa mfano, Wachiribaya wa kusini mwa Peru waliwazika llama na alpaca waliotolewa dhabihu chini ya sakafu ya nyumba zao. Wanahistoria wanadai kwamba kila mwezi llama weupe mia moja walitolewa dhabihu katika jengo kuu la Huayaca Pata huko Cuzco, na wengine wachache walitolewa dhabihu kwa mungu-jua katika sherehe inayoitwa Inti Raymi. Ingawa leo wanyama hao hawatumiwi katika desturi za kidini, nyama yao iliyo na ladha kama ya kondoo, inapendwa sana.

Zamani kabla ya friji kuanza kutumiwa, kabila la Inca lilihifadhi nyama ya wanyama hao kwa kuikausha katika barafu ya Milima ya Andes. Waliiita nyama hiyo iliyokaushwa ch’arki.

Bila shaka, tunapaswa kuwathamini wanyama hao maridadi si kwa sababu tu ya kazi zao, lakini kwa sababu wao ni sehemu ya uumbaji wa ajabu wa Mungu, ambao unamsifu!—Zaburi 148:10, 13.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 3 Aina nne za wanyama hao zinapatikana huko Amerika Kusini: alpaca, guanaco, llama, na vicuña. Wanyama hao mbalimbali wanaweza kuzaana wao kwa wao.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 16]

Guanaco—Mnyama Maridadi Anayestahimili Hali Ngumu

Huenda ikaonekana kwamba kiumbe huyo maridadi mwenye viungo dhaifu anahitaji kubembelezwa sana. Lakini ngamia aina ya guanaco hupatikana katika maeneo yenye hali ngumu, kama kwenye Milima ya Andes, Patagonia, na Tierra del Fuego, huko kusini mwa Argentina na Chile. Katika maeneo hayo magumu, guanaco hula visiki, mizizi, na kunywa maji, hata kama si safi sana. Mnyama huyo anaweza kuogelea vizuri na kukimbia kilometa 65 kwa saa moja. Kope zake nyingi humlinda na upepo, jua, na vumbi. Kwa kusikitisha, wawindaji-haramu humwinda mnyama huyo ili wapate nyama, ngozi yake, na sufu, ambayo ni laini kuliko ile ya ngamia aina ya alpaca.

[Hisani]

© Joe McDonald

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 16]

Alpaca—Mwenye Manyoya Mengi

Kwa kuwa mnyama huyo ana manyoya mengi mazito yanayomfunika mwili mzima, anaweza kustahimili eneo la baridi ambapo halijoto inaweza kubadilika kwa nyuzi 50 Selsiasi kwa siku. Manyoya laini ya alpaca hudumu kwa muda mrefu kuliko ya kondoo. Ingawa pua yake ndefu humwezesha kufikia nyasi zinazomea katika nyufa nyembamba katikati ya miamba huko Andes, mnyama huyo mwenye kupendeza hupendelea sehemu zenye majimaji zilizo na nyasi laini. Hata hivyo, kama ngamia wengine, anaweza kukaa kwa siku nyingi bila kunywa maji.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 17]

Vicuña—Ana Manyoya ya Bei

Ingawa ngamia aina ya vicuña huishi katika Milima ya Andes yenye baridi kali, ana manyoya mepesi mafupi ambayo yanaonwa kuwa bora zaidi ya manyoya mengine yote duniani. Ana manyoya kifuani yaliyo kama skafu. Vicuña aliyekomaa anaweza kutokeza manyoya yasiyozidi kilogramu moja kila miaka miwili, kwa hiyo manyoya hayo ni adimu na ghali sana. Kitambaa cha meta moja cha manyoya yake kinaweza kugharimu zaidi ya dola 3,000.

Wakati wa utawala wa Miliki ya Inca kulikuwa na sheria za kuwalinda vicuña. Sherehe ya kunyoa iliyoitwa chaccu ilianzishwa, na ni familia ya kifalme tu iliyokuwa na pendeleo la kuvaa mavazi yaliyotengenezwa kwa manyoya ya vicuña. Sherehe hiyo imerudishwa tena katika miaka ya karibuni, na kwa mara nyingine tena sheria zimetungwa kuwalinda wanyama hao kutokana na wawindaji-haramu.

Sehemu muhimu ya sherehe hizo ni kuwakamata vicuña wa mwituni katika mitego yenye umbo la faneli iliyo na midomo yenye upana wa meta 300. Baada ya hapo wanyama hao hunyolewa na kuachiliwa mara moja.

[Hisani]

© Wilfredo Loayza/PromPerú ▸

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 17]

Llama—Hutumiwa Kufanya Kazi Kwenye Milima ya Andes

Llama si mwenye nguvu kama punda wala hana mbio kama farasi. Hata hivyo, mnyama huyo ni bingwa wa kubeba mizigo kuliko punda na farasi. Ama kweli, anaweza kubeba mizigo ya kilogramu 60 mgongoni. Akihisi kwamba mzigo ni mzito sana, yeye huketi bila kusonga, hadi mzigo huo upunguzwe. Ukijaribu kumlazimisha, mnyama huyo hutapika chakula kilicho kwenye tumbo lake la kwanza kati ya matumbo yake matatu na kukitema kwa nguvu.

Kwa kawaida, llama ni wapole, na mchungaji mwenye fadhili anaweza kuwaongoza llama wengi milimani ambapo wanyama wengine wa kubeba mizigo hawawezi kustahimili ukosefu wa oksijeni. Kutokana na uwezo wao wa kupanda milima, mbali na kutumiwa katika Milima ya Andes, sasa wanatumiwa pia kubeba mizigo katika Milima ya Alps huko Italia. Kamba, hatamu, na blanketi inayotumiwa kumfunika mnyama huyo inaweza kutengenezwa kutokana na manyoya yake.

[Hisani]

© Anibal Solimano/PromPerú

[Picha katika ukurasa wa 18]

“Alpaca” aliyenyolewa hivi karibuni

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 15]

Mtoto wa “llama” akiwa na pambo sikioni

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 15]

Map: Mountain High Maps® Copyright © 1997 Digital Wisdom, Inc.; llamas: © Alejandro Balaguer/PromPerú