Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Jihadhari na Mimea Inayoua!

Jihadhari na Mimea Inayoua!

Jihadhari na Mimea Inayoua!

Na mwandishi wa Amkeni! nchini Uingereza

KWA kawaida inajulikana kwamba wanyama hula mimea. Lakini je, ulijua kwamba mimea fulani hula wanyama? Kuna jamii 550 hivi za mimea inayokula wadudu, na mingine inaendelea kugunduliwa. Mimea hiyo ya ajabu inaweza kutengeneza chakula, lakini ile inayokua katika udongo mbaya haipati virutubisho vinavyohitajiwa kama vile nitrati. Mimea hiyo hupata virutubisho hivyo muhimu kwa kula wadudu.

Kila mmea una njia yake ya kunasa viumbe. Mingine ina mitego na milango yenye kunasa, huku mingine ikitumia mitego yenye utelezi au yenye kunata inayofanya iwe vigumu kwa viumbe hao kujinasua. Hebu tuchunguze kwa makini mimea hiyo inayokula wadudu.

Mitego na Milango Yenye Kunasa

Inaelekea mmea unaokula wadudu ambao unajulikana sana ni kinasa-nzi, ambao hufikia urefu wa sentimeta 30 hivi. Mmea huo unaopatikana kwenye udongo wenye majimaji katika majimbo ya Carolina huko Amerika Kaskazini, una majani yenye rangi nyangavu yaliyo na tezi zinazotengeneza nekta ambayo huwavutia wadudu! Hilo ndilo hufanya mmea huo kuwa hatari kwa wadudu, kwa kuwa mmea wa kinasa-nzi una nyuzi tatu katikati ya kila sehemu zilizojipinda za jani. Mdudu anapozigusa bila kujua, majani hayo hujifunga. Miiba iliyo kwenye ncha ya majani hushikana na kumzuia mdudu asitoroke kama vile meno ya mtego wa chuma yanavyonasa.

Ikiwa majani yatanasa kitu ambacho kilipeperushwa na upepo kama vile kijiti kikavu, mmea huo utakiondoa baada ya siku kadhaa. Lakini jani hilo linapohisi kwamba kuna nitrojeni, linatokeza vimeng’enya vinavyomsaga-saga mdudu huyo ili mmea uweze kufyonza virutubisho. Utendaji huo huchukua siku 10 hadi 35, ikitegemea ukubwa wa mdudu.

Uzi mmoja tu ukiguswa, labda na tone la mvua, mtego hautafyatuka. Utendaji huo huanza tu nyuzi mbili au zaidi zinapoguswa, hata uzi wa pili ukiguswa baada ya sekunde 20. Mtego huo hufyatuka upesi ikitegemea hali ya joto na mwangaza wa jua. Wakati mwingine unaweza kufyatuka hata kwa nukta za sekunde.

Mitego ya mimea mingine hunasa haraka hata zaidi. Fikiria mmea wa majini unaoitwa bladderwort ambao majani yake huchipuka majini. Majani yake yana vifuko vingi, na kila kimoja kina mlango wa kunasia na nyuzi nyingi ndefu. Mdudu mdogo anapogusa nyuzi hizo, mlango wa kunasia hufunguka. Kwa kuwa shinikizo la maji ndani ya kifuko si kubwa kama shinikizo la nje, mdudu hufyonzwa, na mlango wa kunasia hujifunga. Hilo linaweza kutokea kwa muda mfupi sana!

Mitego Yenye Utelezi

Mojawapo ya mimea mikubwa zaidi inayokula wadudu ni mdumu-mwitu. Mingine, kama ile inayopatikana Kusini-Mashariki mwa Asia, hukua juu ya miti. Mimea hiyo ina mitego inayoweza kubeba lita mbili za umajimaji ili kuwanasa viumbe wakubwa kama vyura. Hata inasemekana kwamba mingine imenasa panya. Lakini mitego hiyo hufanyaje kazi?

Kila jani la mdumu-mwitu hufanana na jagi, au mdumu, na lina kifuniko kinachozuia mvua. Mdudu hupumbazwa na rangi yake nyangavu na wingi wa nekta ya mmea huo, lakini ukingoni mna utelezi. Mdudu anapojaribu kuchukua nekta, huteleza na kuingia ndani ya umajimaji uliopo ndani ya jani hilo. Nyuzi zilizojipinda ndani ya jani hilo humzuia mdudu huyo kutoroka. Isitoshe, nekta za midumu-mwitu fulani zinalewesha na hivyo humpumbaza mdudu.

Mdumu-mwitu unaovutia zaidi ni swila-mboga, ambao unapatikana katika milima ya California na Oregon huko Marekani. Mmea huo unafanana na swila anayetaka kushambulia. Mdudu huingia kwenye mdomo wa mmea huo kisha anachanganyikiwa na mwangaza unaong’aa ndani ya mmea huo kana kwamba unapitia kwenye madirisha madogo. Mdudu huyo huelekea kwenye mwangaza huo akijaribu kutoroka bila mafanikio. Mdudu huyo anapochoka, huanguka ndani ya umajimaji ulio chini ya mmea huo na kuzama.

Faida za Mimea Hiyo

Mmea unaoitwa butterwort una majani yanayonata ambayo huwavutia wadudu fulani. Wadudu hao huharibu mimea iliyo katika hifadhi za mimea na mimea inayopandwa nyumbani. Mitego ya wadudu iliyotengenezwa na wanadamu husaidia lakini inaua nyuki na wadudu wengine pia. Mmea wa butterwort ni bora kuliko mitego hiyo. Unawakamata wadudu hao wadogo waharibifu tu.

Sasa, midumu-mwitu ya Amerika Kaskazini inapendwa na watunzaji wa bustani. Maua yake maridadi na majani yake yenye maumbo ya kifahari ni kama ya mimea mingine, na ni rahisi kuyakuza. Pia humeza wadudu wengi sana. Kila fungu la majani linaweza kunasa maelfu ya wadudu kwa msimu mmoja. Nyuki hawamo hatarini, kwani hawavutiwi na mimea hiyo. Lakini maua huchavushwaje bila kuwanasa wadudu wanaoyachavusha? Maua huchanua kwanza, huku midumu ikiendelea kukua. Kufikia wakati ambapo midumu imekomaa, maua huwa yamenyauka na wadudu wanaoyachavusha kuondoka.

Mmea mwingine ambao ni rahisi kukuza unaoweza kukua katika halijoto yoyote ile, ni umande-jua wa Australia. Chris Heath, mtaalamu wa mimea katika Kituo cha Walworth cha Elimu ya Utunzaji wa Bustani huko London, anasema, “mmea huo unafaa iwapo unasumbuliwa na mbu unapoketi nje jioni. Panda mmea huo katika kikapu kinachoning’inia ambapo matone yake yanayometameta na yenye kunata yatawavutia mbu.” Mbu yeyote anayegusa jani lake hukwama kwenye nyuzi zake zinazonata, ambazo hujipinda na kumfinyilia kwenye jani.

Kuhifadhi Mimea Inayokula Wadudu

Inasikitisha kwamba mimea mingi inayokula wadudu iko katika maeneo yanayoharibiwa na wanadamu. Kwa mfano, aina fulani ya mdumu-mwitu unaokuzwa huko Kusini-Mashariki mwa Asia umo hatarini kwa sababu ya ukataji wa miti na mimea kwa ajili ya kilimo. Maeneo yenye majimaji yanakaushwa ili kusitawishwa. Jamii fulani za mimea hiyo tayari zimetoweka. *

Je, ungependa kukuza mimea inayokula wadudu? Hakuna haja ya kuichukua mwituni, kwa kuwa inauzwa na wafanyabiashara wanaoizalisha. Maagizo ya kuikuza ni rahisi: Inyunyizie maji ya mvua kila wakati. Pia mimea inayokula wadudu hunawiri kukiwa na jua, lakini jamii zinazopatikana katika maeneo ya joto la wastani hunawiri vizuri zinapowekwa mahali pasipo na baridi nyingi wakati wa majira ya baridi kali. Subira inahitajiwa kwa kuwa huenda mimea fulani ikachukua miaka mitatu kukomaa. Hutahitaji kuilisha kwani inajitafutia chakula!

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 19 Baadhi ya mimea inayokula wadudu inalindwa na Mkataba wa Kupinga Biashara ya Kimataifa ya Viumbe na Mimea Inayokabili Hatari ya Kutoweka.

[Sanduku katika ukurasa wa 27]

▪Chakula cha Kuvu

Kuvu ndiyo mimea midogo zaidi inayokula wadudu, nayo hunasa minyoo wadogo wanaoishi udongoni. Kuvu nyingine zina nundu zenye kunata kwenye mashina, lakini nyingine zina vitanzi vitatu vyenye unene wa milimeta 0.025 ambavyo humnyonga mnyoo ambaye huvigusa bila kujua. Mara tu mnyoo anaponaswa, anashambuliwa na nyuzi za kuvu na kufa punde baadaye. Kuvu hizo zinachunguzwa ili zionekane kama zitatumiwa kuwaua wadudu waharibifu kwa kuwa minyoo huharibu mazao yenye thamani ya mamia ya mamilioni ya dola kila mwaka.

[Sanduku katika ukurasa wa 27]

▪Wadudu Wanaojitetea!

Sio wadudu wote wanaokubali kuliwa na mimea. Kwa mfano, mdudu mmoja anayeitwa blowfly ana kiungo fulani kwenye miguu. Kama mpanda-milima anavyotumia chuma, viungo hivyo humwezesha mdudu huyo kupanda kwenye nyuzi zilizojipinda za mdumu-mwitu. Mayai ya blowfly yanapoanguliwa, mabuu hula wadudu walionaswa katika mdumu-mwitu. Kisha wanapofikia hatua ya kubadilika, hutoboa mashimo kwenye mdumu na kutoroka. Kwa upande mwingine, viwavi hufunika nyuzi za mdumu-mwitu kwa utando. Kwa ujanja, aina fulani ya buibui hutengeneza utando juu ya midumu-mwitu ili wawanase wadudu kwanza, na buibui mmoja ana ngozi ya pekee inayomwezesha kuishi katika umajimaji wa mmea huo anapohatarishwa.

[Picha katika ukurasa wa 24, 25]

Jani la aina fulani ya mdumu-mwitu

[Picha katika ukurasa wa 24]

Kinasa-nzi

Jani lililo upande wa kushoto linaonyesha mdudu aliyenaswa; la kulia linaonyesha nyuzi za kunasa

[Hisani]

Plants: Copyright Chris Heath, Kentish Town City Farm, London

[Picha katika ukurasa wa 25]

Ua na jani changa la swila-mboga

[Hisani]

Copyright Chris Heath, Kentish Town City Farm, London

[Picha katika ukurasa wa 26]

Mdumu-mwitu wa Amerika Kaskazini

Ua lake lina ukubwa wa chungwa

[Picha katika ukurasa wa 26]

“Butterwort”

Wadudu fulani hunaswa kwenye majani yake yenye kunata

[Picha katika ukurasa wa 26]

Majani ya mdumu-mwitu wa Amerika Kaskazini

Ndani: Mdudu anafyonza nekta ambayo humlewesha

[Picha katika ukurasa wa 26]

Aina fulani ya umande-jua

Mdudu amenaswa na nyuzi zinazonata za jani

[Hisani]

Plants: Copyright Chris Heath, Kentish Town City Farm, London