Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kazini Au vitani?

Kazini Au vitani?

Kazini Au vitani?

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI UJERUMANI

“Singevumilia tena. Nilifanya kazi katika kampuni hiyo kwa zaidi ya miaka 30. Hata nilikuwa msimamizi kazini. Kisha tukapata meneja mpya. Alikuwa kijana mwenye uwezo na akili nyingi. Aliniona kuwa kizuizi kwa maendeleo ya kampuni, kwa hiyo akaanza kunionea. Baada ya kunitusi, kusema uwongo juu yangu, na kuniaibisha kwa miezi kadhaa, nilichoka kiakili. Nilipoahidiwa na kampuni hiyo kwamba ningepata malipo ya kustaafu, nilikubali kuacha kazi.”—Peter. *

PETER, anayeishi Ujerumani, alikuwa akidhulumiwa kazini. Inakadiriwa kwamba watu milioni 1.2 hudhulumiwa kazini nchini humo. Nchini Uholanzi, mtu 1 kati ya 4 atadhulumiwa kazini wakati fulani maishani. Na kulingana na ripoti moja ya Shirika la Kimataifa la Wafanyakazi, tatizo la kudhulumiwa kazini linaongezeka nchini Australia, Austria, Denmark, Marekani, Sweden, na Uingereza. Lakini, ni nini hutokea mtu anapodhulumiwa kazini?

‘Kuteseka Akili’

Kulingana na gazeti Focus la Ujerumani, mtu anayedhulumiwa kazini “huonewa mara nyingi kwa njia maalumu.” Kudhulumiwa kazini kunahusisha mengi zaidi ya kudhihakiwa, kuchambuliwa, kuchokozwa, na kufanyiwa mzaha. Wafanyakazi hupanga kumtesa mfanyakazi mwenzao kiakili. Lengo ni kumfanya yule anayedhulumiwa ahisi kwamba hafai hata kidogo. *

Mbinu za kumdhulumu mtu hutia ndani dhihaka za kitoto na hata jeuri. Anayedhulumiwa huharibiwa jina, hutukanwa, huchokozwa, na kunyamaziwa. Wengine hupewa kazi nyingi kupita kiasi au kila wakati wanapewa kazi mbaya-mbaya ambazo wafanyakazi wengine hawataki kuzifanya. Huenda wafanyakazi wengine wakamzuia mtu kufanya kazi vizuri, labda kwa kutompa habari anazohitaji. Katika visa fulani, wafanyakazi wengine wamepasua tairi za gari au kuingilia na kuharibu kompyuta ya mtu wanayemdhulumu.

Watu fulani hudhulumiwa na mtu mmoja. Lakini mara nyingi mtu hudhulumiwa na wafanyakazi wengi.

Jambo la kushangaza ni kwamba mara nyingi mameneja huruhusu dhuluma kazini. Katika uchunguzi uliofanywa huko Ulaya, wasimamizi walihusika sana katika asilimia 50 hivi ya visa vya dhuluma, na mara nyingi wao ndio waliowadhulumu wengine. Kulingana na gazeti Frankfurter Allgemeine Zeitung la Ujerumani, mbinu hizo zote za dhuluma huwafanya wafanyakazi “wateseke sana kiakili.”

Madhara ya Kudhulumiwa

Mara nyingi, dhuluma inayotokea kazini husababisha madhara mengine maishani. Watu wengi hupatwa na magonjwa mabaya sana kwa sababu ya kudhulumiwa. Baadhi ya madhara ya kudhulumiwa ni kushuka moyo, kukosa usingizi, na kushtuka mara kwa mara. Ni madhara gani yaliyompata Peter, aliyetajwa mwanzoni? Alijiona kuwa hafai kabisa. Mwanamke mmoja anayeitwa Margaret, ambaye anaishi Ujerumani pia, alishauriwa na daktari wake apate matibabu kwenye hospitali ya wagonjwa wa akili. Kwa nini? Kwa sababu ya kudhulumiwa kazini. Pia kudhulumiwa kunaweza kuathiri ndoa au maisha ya familia.

Huko Ujerumani, dhuluma imeongezeka sana kazini hivi kwamba kampuni moja ya bima ya afya imeanzisha huduma za kuwashauri watu wenye matatizo au maswali kupitia simu. Kampuni hiyo iligundua kwamba zaidi ya nusu ya watu waliopiga simu hawakuweza kufanya kazi kwa majuma sita, thuluthi moja hivi hawakuweza kufanya kazi kwa miezi mitatu, na zaidi ya asilimia 10 hawakuweza kufanya kazi kwa zaidi ya miezi mitatu. Jarida moja la kitiba la Ujerumani linakadiria kwamba “asilimia 20 ya visa vya kujiua husababishwa na kudhulumiwa kazini.”

Kwa kweli, mtu anaweza kuogopa sana anapodhulumiwa kazini. Je, dhuluma hiyo inaweza kuzuiwa? Wafanyakazi wanaweza kufanya nini ili kuwe na amani kazini?

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 3 Majina yaliyotumiwa katika mfululizo huu wa makala yamebadilishwa.

^ fu. 6 Ripoti zinaonyesha kwamba wanawake ndio hudhulumiwa zaidi kazini kuliko wanaume, labda kwa sababu wanawake huzungumzia tatizo hilo na kutafuta msaada kuliko wanaume.

[Picha katika ukurasa wa 4]

Watu wanaodhulumiwa kazini huteseka kiakili