Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Bata wa Plastiki Waogelea

Katika Januari 1992 meli moja iliyotoka Hong Kong ikielekea Marekani ilikumbwa na dhoruba kali na kupoteza shehena la bata wa plastiki 29,000, lasema gazeti Frankfurter Allgemeine Zeitung la Ujerumani. Bata wa kwanza walionekana katika Kisiwa cha Baranof, huko Alaska, mnamo Novemba 1992. Wengine walipatikana kwenye “barafu inayoelea kaskazini ya Mlango-Bahari wa Bering” miaka miwili baada ya dhoruba. Inatazamiwa kwamba bata hao wa plastiki wataonekana pia kwenye pwani ya New England huko Amerika Kaskazini. Kulingana na gazeti hilo, jambo hilo limewasaidia wanasayansi kuthibitisha dhana yao kwamba maji ya bahari hutiririka “kutoka Pasifiki moja kwa moja hadi Bahari ya Aktiki kisha Atlantiki.”

Mbawakavu Watatua Tatizo!

Gazeti New Scientist lasema kwamba “jamii mbili za mbawakavu zimeokoa dola milioni 260 ambazo zingetumiwa kwa kipindi cha miaka 20 na nchi ya Benin ya Afrika Magharibi. Mbawakavu hao wameshambulia gugu-maji sugu ambalo huua samaki, huzuia usafiri wa mashua na kuharibu mazingira ya maziwa.” Ripoti hiyo inaendelea kusema kwamba “gugu hilo linaloelea linaweza kukua maradufu kwa kipindi kisichozidi majuma mawili huku uzito wa majani yake ukizuia uvuvi na usafiri wa mashua.” Mmea huo humaliza oksijeni majini, huongeza asidi ya maji, na kupunguza mwendo wake, huku ukiongeza mchanga-tope. Gugu hilo pia huwaficha mamba, na hilo husababisha hatari kwa watu wanaoteka maji. Mashine zimeshindwa kuliondoa gugu hilo na kemikali zinaweza kuchafua maji na kuua mimea mingine, lakini jamii hizo mbili za mbawakavu ambazo hula gugu-maji tu zimefaulu kuliondoa, lasema gazeti New Scientist.

Wake Wanaocheza Kamari

Gazeti Sunday Telegraph la London lasema kwamba huko Uingereza “wake wengi wamekuwa na mazoea ya kucheza kamari kwenye Intaneti na hivyo wamepata madeni makubwa kwa kutumia saa nyingi kila siku katika mchezo huo.” Wanawake ambao huenda wakaogopa kucheza kamari kwenye kasino, hufanya hivyo kwenye Intaneti. Isitoshe, kucheza kamari kunaweza kuwa sehemu ya shughuli zao za kila siku nyumbani. Wanawake wengi wana mazoea ya kucheza kamari, lakini kwa sababu inaonwa kuwa ni aibu kwa wanawake kucheza kamari, mara nyingi hawakubali kwamba wana tatizo la kucheza kamari. Kulingana na gazeti hilo, Profesa Mark Griffiths, wa Chuo Kikuu cha Nottingham alisema kwamba, zoea la kucheza kamari kwenye Intaneti “ni badiliko kubwa katika mchezo wa kamari kwani watu wanaweza kucheza kazini au nyumbani badala ya kwenda kwenye kasino.” Pia alisema, “ikiwa una tatizo la kucheza kamari, . . . inaelekea utazuiwa kuingia kwenye kasino au mahali penginepo pa kuchezea kamari. Lakini huwezi kuzuiwa kwenye Intaneti.”

Vijana Wengi Hawana Makao

Toleo la Kiingereza la gazeti El País la Hispania linasema, “idadi ya vijana ambao hawana makao huko Madrid imeongezeka.” Kulingana na uchunguzi wa chuo kikuu kimoja, “inakadiriwa kwamba kati ya watu 5,000 wasio na makao huko Madrid, 1,250 walikuwa chini ya umri wa miaka 20 walipoanza kuishi mitaani.” Uchunguzi huo ulionyesha kwamba, “vijana wengi wasio na makao wanatoka katika familia zilizovunjika na bila shaka maisha yao yamevurugika.” Kwa hakika, “vijana wawili kati ya watatu wana wazazi walevi au wanaotumia dawa za kulevya na walitendwa vibaya nyumbani.” Mwandishi wa ripoti hiyo, Manuel Muñoz, alisema kwamba “uhusiano wa karibu uliokuwapo katika familia za eneo la Mediterania umeanza kudhoofika.”

Ugonjwa wa Kisonono Waongezeka Kanada

Gazeti Vancouver Sun la Kanada lasema, “baada ya miaka 20 ya kupungua kwa ugonjwa wa kisonono, idadi ya watu wanaougua imeongezeka kwa zaidi ya asilimia 40 katika miaka mitano iliyopita.” Kisonono ni ugonjwa wa zinaa unaoweza kumfanya mtu kuwa tasa na “unaweza kusambazwa kwenye viungo kupitia damu na kusababisha mwasho na uvimbe.” Gazeti Sun linasema kwamba bakteria inayosababisha kisonono inazidi kukinza “dawa zote.” Inahofiwa kwamba “kuongezeka kwa kisonono kutafanya wengi zaidi waambukizwe virusi vya UKIMWI kwa sababu watu wenye magonjwa ya zinaa hukabili hatari kubwa zaidi ya kupata au kusambaza virusi vya UKIMWI.” Hata madaktari wanasema kwamba kuongezeka kwa kisonono kunafanya watu wasiogope UKIMWI. Dakt. David Fisman, mtaalamu wa magonjwa ya zinaa anasema, “watu hawajali wanafanya ngono na nani au na watu wangapi.”

Kukodi Nyanya na Babu

Kulingana na gazeti Nassauische Neue Presse la Ujerumani, “zaidi ya akina mama na baba 1,000 wasio na wenzi ambao hata wana watoto wenye umri wa miaka kumi au chini wamewachagulia watoto wao nyanya na babu.” Melanie mwenye umri wa miaka saba anasema, “babu na nyanya yangu wanaishi mbali sana na Berlin. Lakini Nyanya Klara ni jirani yetu. Yeye hunichukua kutoka shuleni na hunipeleka kwenye bustani ya wanyama, kwenye uwanja wa michezo, na mahali pa kuogelea. Yeye hupika pia, naye hula pamoja nami na mama yangu nyumbani.” Nyanya Klara alitumwa na kampuni moja inayowawezesha watu wazee kuwatumikia wazazi wasio na wenzi kwa dola 3 hadi 5 kwa saa. Ripoti hiyo yasema kwamba, “huo ni mpango unaowafaa wazazi wasio na wenzi ambao hawana pesa nyingi.”

Ufuo wa Watu Wanene

Gazeti El Economista linasema kwamba huko Mexico hoteli moja imetenga sehemu fulani kwa ajili ya watu wanaoona haya kuchangamana na watu wembamba kwenye fuo. Hoteli hiyo ya ufuoni huko Cancún inawatia moyo kwa maneno haya, “Furahia Unene Wako.” Hoteli hiyo inakusudia “kuwavutia watu wanaoogopa kwenda ufuoni na mavazi ya kuogelea kwa sababu wao ni wanene kupita kiasi.” Kulingana na ripoti hiyo, wafanyakazi wa hoteli hiyo ni watu wenye uzito mbalimbali na wamezoezwa wasiwabague wageni “kwani wao hubaguliwa kila siku maishani.”

Ongezeko la Joto Katika Bahari ya Mediterania

Maurizio Wurtz, mtaalamu wa masuala ya bahari katika Chuo Kikuu cha Genoa nchini Italia anasema, “kwa miaka kumi tumekuwa tukirekodi . . . ongezeko la joto katika bahari ya Mediterania.” Ripoti hiyo iliyochapishwa katika gazeti La Repubblica la Italia inasema kwamba jamii mpya za mimea na viumbe vya baharini zinahamia kwenye maji hayo yenye joto. Wurtz anasema, “jamii nyingi zinahamia kaskazini mwa Mediterania kutoka pwani ya Afrika.” Jamii hizo zinazohamia huko zinatia ndani samaki wa pono waliotoka kwenye maji ya maeneo ya joto; samaki wa damselfish waliotoka kwenye maeneo yenye joto ya Atlantiki; samaki wanaoitwa tundu ambao kwa kawaida wanapatikana katika Bahari ya Hindi na Pasifiki; na mmea wa mwani ambao umefika Mediterania kupitia Mfereji wa Suez.