Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mtoto Wako Anapoendelea Kulia

Mtoto Wako Anapoendelea Kulia

Mtoto Wako Anapoendelea Kulia

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI KANADA

DAKTARI alithibitisha jambo ambalo tayari mama alikuwa amedhania. Mtoto wake alisokotwa sana na tumbo. Kulingana na gazeti Globe and Mail la Kanada, “mtoto mmoja kati ya wanne” ana ugonjwa huo. Mtoto anapolia kwa saa kadhaa kwa angalau siku tatu kwa juma, hiyo inaonyesha ana ugonjwa huo. Mzazi anaweza kufanya nini? Wataalamu wa magonjwa ya watoto wanasema kwamba katika visa vingi wazazi na watoto wanapaswa kuwa na subira. Lakini kwa muda gani?

Akina mama walio na watoto wanaougua ugonjwa huo walipochunguzwa hivi majuzi huko Kanada, iligunduliwa kwamba zaidi ya asilimia 85 ya watoto walipona walipofikia umri wa miezi mitatu. Uchunguzi huo ulioanzishwa na Dakt. Tammy Clifford, msimamizi wa elimu ya magonjwa ya mlipuko katika Taasisi ya Utafiti ya Hospitali ya Watoto ya Ontario Mashariki, ulionyesha pia kwamba mama mwenye mtoto anayesokotwa sana na tumbo haathiriwi kiakili kwa muda mrefu. Dakt. Clifford anasema: “Kufikia miezi sita baada ya kujifungua, akina mama hao huwa sawa kabisa. Baada ya watoto kuacha kulia kwa muda mrefu mama hao husahau tatizo hilo kabisa.”

Gazeti Globe lasema kwamba uchu- nguzi huo mpya ulioanzishwa na Dakt. Clifford na wenzake “umefunua habari muhimu za kisayansi kuhusu msokoto mkali wa tumbo kwa sababu unaonyesha kuna aina tatu tofauti za watoto wenye tatizo hilo: watoto ambao huwa na ugonjwa huo na kisha kupona wanapofikia umri wa miezi mitatu; wale wanaoendelea kuugua ugonjwa huo kwa miezi kadhaa bila kupona; na wachache ambao huugua ugonjwa huo miezi michache baada ya kuzaliwa.” Uchunguzi mwingine unafanywa kuona maendeleo ya watoto wenye msokoto mkali wa tumbo wanapoendelea kukua, na ni kikundi hicho cha tatu ambacho hasa kinashangaza.

Inaaminiwa kwamba watoto wanaolia bila kuacha ndio hupatwa na magonjwa yanayotokana na kutikiswa-tikiswa wanapobembelezwa. Kama ilivyoandikwa kwenye gazeti la Globe, “kulia hakuwezi kumdhuru mtoto, lakini kumtikisa sana, hata kwa muda mfupi, kunaweza kusababisha madhara ya kudumu ya mishipa ya neva, na hata kifo.”

Kwa upande mwingine, huenda kukawa na faida mtoto mchanga anapolia, hata kama analia kwa muda mrefu. Gazeti Globe linasema, “uchunguzi umethibitisha kwamba watoto wanaolia sana hushughulikiwa zaidi na watunzaji wao kwa kuguswa, kuonyeshwa tabasamu, kuzungumziwa, na kukumbatiwa.”