Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Jitihada za Muda Mrefu za Kuboresha Afya

Jitihada za Muda Mrefu za Kuboresha Afya

Jitihada za Muda Mrefu za Kuboresha Afya

JOANNE alikuwa akiishi New York, naye alikuwa na ugonjwa wa kifua-kikuu (TB). Lakini TB yake haikuwa ya kawaida. Alikuwa na aina sugu ya ugonjwa huo ambayo haiwezi kutibiwa na karibu dawa zote na ambayo huua nusu ya watu wanaoipata. Hata hivyo, Joanne hakutibiwa kwa ukawaida na tayari alikuwa amewaambukiza watu wengine. Daktari wake aliyekuwa amekata tamaa alisema kwamba ‘anapaswa kufungiwa.’

TB ni ugonjwa wa zamani ambao huua. Mamilioni ya watu wameugua na kufa kutokana na ugonjwa huo. Uthibitisho wa kuwapo kwa ugonjwa huo umepatikana katika maiti za Misri ya kale na Peru. Leo, aina mbalimbali za ugonjwa huo zinazozuka upya huua watu wapatao milioni mbili kila mwaka.

Akiwa amelala kitandani katika kibanda kidogo huko Afrika, Carlitos alikuwa akitokwa na jasho kwenye paji la uso. Malaria ilikuwa imemdhoofisha sana hata hangeweza kulia. Wazazi wake hawakujua la kufanya kwa kuwa hawakuwa na pesa za dawa, wala hakukuwa na kliniki karibu ambapo mtoto wao angeweza kutibiwa. Ugonjwa wake ulizidi, na katika muda wa saa 48 alikuwa amekufa.

Malaria huua watoto wapatao milioni moja kila mwaka, kama ilivyomuua Carlitos. Katika vijiji vya Afrika Mashariki, watoto wengi huumwa na mbu wenye viini vya malaria mara 50 hadi 80 kwa mwezi. Mbu hao wanaenea katika maeneo mapya na dawa za malaria hazina nguvu tena. Inakadiriwa kwamba watu milioni 300 huugua malaria kali kila mwaka.

Kenneth, mwenye umri wa miaka 30, aliyekuwa akiishi huko San Francisco, California, alimwona daktari wake kwa mara ya kwanza mwaka wa 1980. Alikuwa akiendesha na kuhisi uchovu. Mwaka mmoja baadaye alikuwa amekufa. Ingawa alitibiwa na madaktari stadi, alizidi kukonda na hatimaye akafa kutokana na nimonia.

Miaka miwili baadaye, mwanamke mmoja huko kaskazini mwa Tanzania, umbali wa kilometa 16,000 kutoka San Francisco, alikuwa na dalili kama hizo. Baada ya majuma machache akashindwa kutembea, kisha akafa muda mfupi baadaye. Wanakijiji waliuita ugonjwa huo wa ajabu ugonjwa wa Juliana kwa sababu mwanamume aliyekuwa akiuza vitambaa vyenye jina Juliana, alimwambukiza mwanamke huyo na wanawake wengine ugonjwa huo.

Kenneth na mwanamke huyo wa Tanzania walikuwa na ugonjwa uleule: UKIMWI. Mwanzoni mwa miaka ya 1980, wakati ambapo ilionekana kana kwamba wataalamu wa tiba walikuwa wamekomesha viini vilivyo hatari zaidi, ugonjwa huo hatari ulizuka na kuanza kuwasumbua wanadamu. Kwa miaka 20 tu, idadi ya watu waliokufa kutokana na UKIMWI ikafikia idadi ya watu waliokufa kutokana na tauni iliyokumba bara la Ulaya na Asia katika karne ya 14, tauni ambayo haikusahaulika kamwe barani Ulaya.

Tauni

Yaonekana kwamba tauni hiyo ilianza mwaka wa 1347, wakati meli kutoka Crimea ilipotia nanga huko Messina, kwenye kisiwa cha Sicily. Mbali na shehena yake ya kawaida, meli hiyo ilileta tauni pia. * Punde si punde, tauni hiyo ikaenea kotekote nchini Italia.

Mwaka uliofuata Agnolo di Tura, wa Siena, Italia, alisimulia hali yenye kuogofya iliyokumba mji wao: ‘Watu walianza kufa Siena mnamo mwezi wa Mei. Lilikuwa pigo kali lenye kuogofya. Wagonjwa walikufa punde baada ya kuambukizwa. Mamia ya watu walikufa usiku na mchana.’ Aliongezea hivi: ‘Niliwazika watoto wangu watano, na ndivyo walivyofanya wengine wengi pia. Hakuna aliyeomboleza, hata awe alifiwa na nani, kwa kuwa kila mtu alikuwa akitazamia kifo. Watu wengi sana walikufa hivi kwamba wote walidhani mwisho wa dunia umefika.’

Wanahistoria fulani wanasema kwamba tauni hiyo ilienea kotekote barani Ulaya kwa kipindi cha miaka minne na kwamba thuluthi moja hivi ya watu walikufa, watu kati ya milioni 20 na milioni 30. Hata katika nchi ya mbali ya Iceland watu wengi sana walikufa. Inasemekana kwamba katika Mashariki ya Mbali, idadi ya wakaaji wa China ilishuka kutoka milioni 123 mwanzoni mwa karne ya 13 hadi milioni 65 katika karne ya 14, huenda kutokana na tauni hiyo pamoja na njaa kali iliyozuka wakati huohuo.

Hakuna ugonjwa mwingine wowote, vita, au njaa kali iliyokuwa imesababisha kuteseka kulikoenea hivyo. “Ulikuwa msiba usio na kifani katika historia ya wanadamu,” chasema kitabu Man and Microbes. “Ugonjwa huo uliangamiza kati ya asilimia 25 na asilimia 50 ya watu barani Ulaya, Afrika Kaskazini, na sehemu mbalimbali za Asia.”

Mabara ya Amerika hayakupatwa na tauni hiyo kwa sababu yalikuwa mbali na sehemu nyingine za ulimwengu. Hata hivyo, meli zilipoanza kufika huko, magonjwa hayo yakaanza kuenea huko pia. Katika karne ya 16, magonjwa hatari hata kupita tauni yalikumba mabara hayo.

Ndui Yashambulia Mabara ya Amerika

Columbus alipowasili West Indies mwaka wa 1492, alisema kwamba wenyeji walikuwa na ‘sura nzuri, maumbo mazuri, kimo cha wastani, na maungo.’ Hata hivyo, licha ya kuwa na afya nzuri, bado walikumbwa kwa urahisi na magonjwa yaliyoenea kutoka Ulaya.

Mnamo mwaka wa 1518, ugonjwa wa ndui ulizuka katika kisiwa cha Hispaniola. Waamerika wenyeji hawakuwa wameugua ugonjwa huo hapo awali, na matokeo yakawa mabaya sana. Mhispania mmoja aliyejionea hali hiyo, alikadiria kwamba watu elfu moja tu ndio waliookoka katika kisiwa hicho. Punde baadaye ugonjwa huo ulifika Mexico na Peru ukiwa na matokeo hayohayo.

Wakoloni Waingereza walipowasili Massachusetts huko Amerika Kaskazini katika karne iliyofuata, waligundua kwamba wakaaji wengi walikuwa wamekufa kutokana na ndui. Kiongozi wao, John Winthrop, aliandika hivi: “Karibu wenyeji wote wamefagiliwa mbali na ugonjwa wa ndui.”

Zaidi ya ndui, magonjwa mengine pia yalizuka. Kulingana na kitabu kimoja, miaka mia moja hivi baada ya Columbus kuwasili huko, magonjwa kutoka nchi nyingine yalikuwa yameua asilimia 90 ya wakaaji wa mabara ya Amerika. Idadi ya watu wa Mexico ilikuwa imepungua kutoka milioni 30 hadi milioni 3, na ya Peru kutoka milioni 8 hadi milioni moja. Bila shaka si wenyeji wa Amerika tu walioathiriwa na ndui. Kitabu Scourge—The Once and Future Threat of Smallpox kinasema hivi: “Katika historia yote ya binadamu, ndui iliua mamia ya mamilioni ya watu, wengi kuliko waliouawa na tauni . . . na vita vyote vya karne ya ishirini.”

Magonjwa Hayajakomeshwa Kabisa

Magonjwa hatari ya tauni na ndui huenda yasionekane kuwa tisho leo. Katika karne ya 20, wanadamu walikomesha magonjwa mengi ya kuambukiza, hasa katika nchi zilizoendelea. Madaktari waligundua vyanzo vya magonjwa mengi na kuvumbua njia za kuyatibu. (Ona sanduku.) Ilionekana kwamba chanjo mpya na viuavijasumu vipya vitamaliza magonjwa yote, hata magonjwa sugu.

Hata hivyo, Dakt. Richard Krause, aliyekuwa mkurugenzi wa Taasisi ya Kitaifa ya Mizio na Magonjwa ya Kuambukiza ya Marekani, anasema kwamba “tauni ni kama kifo na kodi, haziepukiki.” Magonjwa ya TB na malaria hayajakomeshwa. Na kwa kusikitisha, kuzuka kwa UKIMWI hivi majuzi kunathibitisha kwamba magonjwa ya kuambukiza yangali duniani. Kitabu Man and Microbes kinasema hivi: “Magonjwa ya kuambukiza yangali kisababishi kikuu cha vifo ulimwenguni, na hivyo ndivyo mambo yatakavyoendelea kwa muda mrefu.”

Madaktari fulani wanahofia kwamba licha ya mafanikio katika kutibu magonjwa, mafanikio ambayo yamepatikana katika miongo michache iliyopita si ya kudumu. Mtaalamu wa magonjwa ya kuambukiza, Robert Shope, anaonya hivi: “Hatari ya magonjwa ya kuambukiza haijatoweka, inazidi kuongezeka.” Makala inayofuata itaeleza sababu.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 10 Tauni hiyo ilijitokeza kwa njia mbalimbali, kama vile tauni ya majipu na tauni ya nimonia. Viroboto vya panya hasa vilieneza tauni ya majipu, nayo tauni ya nimonia ilienezwa hasa na watu wenye ugonjwa huo, walipokohoa au kupiga chafya.

[Blabu katika ukurasa wa 5]

Kwa miaka 20 tu, idadi ya watu waliokufa kutokana na UKIMWI ikafikia idadi ya watu waliokufa kutokana na tauni iliyokumba bara la Ulaya na Asia katika karne ya 14

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 6]

Mambo ya Hakika na Ushirikina

Katika karne ya 14, wakati ambapo tauni ilikumba nyumba ya papa huko Avignon, daktari wake alimjulisha kwamba mpangilio wa sayari tatu, yaani Zohali, Sumbula, na Mars, uliofanyiza umbo la Aquarius ndio uliosababisha tauni hiyo.

Karne nne hivi baadaye, George Washington alianza kuwashwa na koo. Madaktari watatu maarufu waliutibu ugonjwa huo kwa kumtoa lita mbili za damu. Mgonjwa huyo akafa baada ya saa chache. Matibabu ya kutoa damu yalitumiwa sana kwa miaka 2,500 tangu wakati wa Hippocrates hadi katikati ya karne ya 19.

Ingawa ushirikina na mapokeo yalichelewesha maendeleo ya kitiba, madaktari walijitoa mhanga kugundua vyanzo na dawa za magonjwa ya kuambukiza. Yafuatayo ni baadhi ya mafanikio yao.

Ndui. Mnamo 1798, Edward Jenner alivumbua chanjo ya ndui. Katika karne ya 20, chanjo zimezuia magonjwa mengine kama polio, homa ya manjano, na ukambi, na surua.

Kifua-kikuu. Mnamo 1882, Robert Koch aligundua bakteria inayosababisha kifua-kikuu na kuvumbua njia ya kuupima ugonjwa huo. Miaka 60 hivi baadaye, kiuakijasumu kinachoitwa streptomycin kinachotibu ugonjwa wa kifua-kikuu kikavumbuliwa. Dawa hiyo ilitumiwa pia kutibu tauni ya majipu.

Malaria. Tangu karne ya 17, kwinini inayotokana na gamba la mti wa cinchona iliokoa uhai wa mamilioni ya watu waliougua malaria. Mnamo 1897, Ronald Ross aligundua kwamba mbu anayeitwa Anopheles ndiye hueneza viini vya ugonjwa huo, na jitihada zilifanywa kuwaangamiza mbu ili kupunguza idadi ya vifo katika nchi za tropiki.

[Picha]

Chati ya nyota za unajimu (juu) na kutoa damu

[Hisani]

Both: Biblioteca Histórica “Marqués de Valdecilla”

[Picha katika ukurasa wa 3]

Leo, aina mbalimbali za kifua-kikuu zinazozuka upya huua watu wapatao milioni mbili kila mwaka

[Hisani]

X ray: New Jersey Medical School–National Tuberculosis Center; man: Photo: WHO/Thierry Falise

[Picha katika ukurasa wa 4]

Mchongo wa Kijerumani wa mwaka wa 1500 hivi, unaoonyesha daktari ambaye amejifunika kitambaa ili kujikinga na tauni. Sehemu iliyofunika mdomo ina marashi

[Hisani]

Godo-Foto

[Picha katika ukurasa wa 4]

Bakteria iliyosababisha tauni ya majipu

[Hisani]

© Gary Gaugler/Visuals Unlimited