Kutembelea Kisiwa cha Gilasi
Kutembelea Kisiwa cha Gilasi
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI ITALIA
FUNDI stadi anatia ufito wa kupulizia ndani ya shimo dogo lililo kwenye tanuru lenye moto mkali sana. Anachomoa donge la gilasi iliyoyeyushwa lenye rangi inayong’aa kama jua linalotua. Ufito huo unapochomolewa kwenye tanuru, mwale wa rangi ya machungwa unatokea na kutoweka ghafula. Fundi huyo stadi anaviringisha gilasi hiyo iliyoyeyushwa kwenye meza ya chuma na kufanyiza umbo la silinda. Anapopuliza kidogo tu kupitia ule ufito, gilasi inavimba, kisha anaiviringisha tena, anaiinua, anaichunguza, na kuirudisha tena motoni.
Tuko kwenye kisiwa kidogo cha Murano, kwenye Wangwa wa Venice nchini Italia. Kisiwa hicho kinajulikana sana kwa sababu ya vyombo vya gilasi. Gilasi zimekuwa zikitengenezwa katika eneo hilo kwa zaidi ya miaka 1,000. Kuna mabaki ya kiwanda cha gilasi katika kisiwa cha Torcello ambacho kilianzishwa katika karne ya 7 W.K. Hata hivyo, uthibitisho wa kwanza wa kuwapo kwa vyombo vya gilasi huko Venice kwenyewe unapatikana katika hati ya mwaka wa 982 W.K., iliyotiwa sahihi na “Domenic mtengenezaji wa gilasi.”
Kufikia mwaka wa 1224, watengenezaji wa gilasi wa Venice walikuwa na chama chao. Mnamo mwaka wa 1291, Baraza Kuu la Venice liliamuru matanuru ya gilasi yaondolewe jijini, labda kwa kuhangaikia usalama. Matanuru mengi yalisafirishwa kilometa moja hivi ng’ambo ya wangwa hadi Murano, ambapo yamekuwapo tangu wakati huo.
Umaarufu wa Gilasi za Venice
Kwa kuwa gilasi zimetengenezwa tangu zamani katika sehemu nyingi ulimwenguni, ni nini kinachofanya gilasi za Murano, au za Venice, ziwe za pekee? Inadhaniwa kwamba mafundi wenyeji waliboresha sana ustadi wao kwa sababu wakaaji wa Venice walikuwa wakiwasiliana sana na watu wa maeneo mengine yenye historia ndefu ya kutengeneza gilasi kama vile Misri, Foinike, Siria, na Korintho wakati wa Miliki ya Byzantium. Ama kwa hakika, mbinu za ufundi na bidhaa za zamani zaidi zilizotengenezwa katika viwanda vya Venice zinafanana sana na zile za maeneo ya Mashariki. Mbinu za ufundi zilizotumiwa
huko Murano zilifikia kiwango ambacho huenda hakikufikiwa kamwe na vituo vingine vya kutengeneza gilasi barani Ulaya.Kitabu Glass in Murano kinasema kwamba katika karne ya 13 na 14 huko Ulaya, jiji la Venice “peke yake ndilo lililokuwa likitengeneza vyombo ‘bora zaidi’ vya gilasi.” Bidhaa za Venice ziliuzwa katika maeneo ya mbali sana, kama vile mashariki mwa Mediterania na Ulaya Kaskazini. Mwaka wa 1399, Mfalme Richard wa Pili wa Uingereza aliruhusu meli mbili za Venice zilizotia nanga katika bandari ya London ziuze vyombo vya gilasi. Katika kipindi hicho, gilasi za Venice zilionwa kuwa mali za Wafaransa matajiri tu. Baada ya muda, Murano pakawa maarufu kwa utengenezaji wa vioo, mashada ya taa, gilasi za rangi mbalimbali, mapambo ya dhahabu na enameli, fuwele, johari za kuiga, bilauri za divai, na vyombo vingine vyenye mapambo ya kuvutia.
Ili kuhifadhi siri ya biashara yake, jiji la Venice lilijitahidi juu chini kuzuia viwanda vya kutengeneza gilasi bora visijengwe kwingineko. Tangu karne ya 13, mafundi wa gilasi hawakuruhusiwa kuhamia sehemu nyingine. Hatua za kulinda biashara zilizidi kuwa kali hivi kwamba ni raia tu walioruhusiwa kufanya au kujifunza kazi ya kutengeneza gilasi. Wakati mmoja, mafundi wa gilasi waliotoroka eneo hilo walikamatwa na kutozwa faini kali kisha wakahukumiwa kupiga makasia kwa miaka mitano huku miguu yao ikiwa imefungwa kwa minyororo.
Hata hivyo, mafundi wa gilasi walihamia maeneo mengine ya Italia na Ulaya kinyume cha sheria, na kuanza kushindana na Murano, wakitengeneza bidhaa zilezile na kutumia mbinu zilezile. Kwa kawaida, si rahisi kutofautisha bidhaa zao na zile za Murano, nazo zilikuja kuitwa à la façon de Venise, yaani mtindo wa Venice.
Ufundi wa Venice ulifikia upeo wake katika karne ya 15 na 16. Kutokana na bidhaa zake za maumbo mbalimbali ya fuwele, enameli zilizotiwa rangi, bilauri za rangi nyeupe ya maziwa, gilasi zake zenye madoido, na bidhaa nyinginezo, Murano ilitia fora katika biashara hiyo na bidhaa zake zikatumiwa na wafalme.
Mwanahistoria mmoja wa vyombo vya gilasi anasema kwamba wakati huo, “mtalii yeyote mwenye udadisi ambaye alitembelea wangwa huo kulipokuwa na matanuru, hangekosa kwenda kuyaona.” Sisi pia tungependa kuyaona. Kwa hiyo, leo asubuhi tutapanda mashua, kutoka Grand Canal hadi Murano. Njoo twende pamoja.
Matanuru na Vyumba vya Maonyesho
Mara tu tunaposhuka kutoka kwenye mashua hiyo huko Murano, watu wanatuelekeza kwenye viwanda vya gilasi vilivyo karibu ambako hatuhitaji kulipa ili kuona jinsi gilasi zinavyotengenezwa. Tunamtazama fundi akipuliza ufito na kufanyiza puto refu la gilasi iliyoyeyushwa mwishoni mwa ufito huo. Kisha kwa ustadi anatumia koleo na makasi kuvuta, kukata, na kufinya puto hilo lisilo na umbo lolote ili kufanyiza kichwa, miguu, na mkia wa farasi anayeruka.
Tunapoondoka kiwanda cha kwanza, tunatembea polepole kando ya mahali patulivu panapoitwa Rio dei vetrai, ambapo kama ilivyo katika sehemu nyingi za Venice, watu wanatembea kando-kando au wanaabiri kwenye mashua. Hapa tunaona maduka na vyumba vingi vya maonyesho vya Murano. Baadhi yake yana vyombo vya fahari na thamani, kama vile vyombo vya chai, vinara vya taa, na michongo mikubwa, ambavyo bila shaka vimetengenezwa kwa ustadi wa hali ya juu na kwa makini sana. Maduka mengine yana vyombo vya bei nafuu,
kama vile shanga, chupa za maua, na vyombo vya rangi mbalimbali vya kukinga karatasi zisipeperushwe. Vyombo vingi ni maridadi ajabu. Vyote vimetengenezwa kwa mikono.Tunastaajabu kuona jinsi vyombo mbalimbali vinavyotengenezwa. Gilasi za Murano—ambazo ni asilimia 70 mchanga na asilimia 30 magadi, chokaa, nitrati, na aseniki—huyeyuka zinapofikia nyuzi 1,400 Selsiasi na kuganda zinapofikia nyuzi 500 hivi Selsiasi. Katika kiwango kinachofaa cha joto kati ya viwango hivyo viwili, gilasi hiyo huwa laini na rahisi kuunda. Kwa hiyo, ili mtu aipulize gilasi hiyo au kuunda umbo fulani, lazima airudishe motoni mara nyingi ili iwe laini. Mafundi huketi kwenye viti vya kazi ambapo wanaweza kuweka na kuviringisha fito zao. Wanapozigeuza kwa mkono mmoja, ule mkono mwingine hushika kifaa fulani au kalibu isiyoweza kupata moto, ili kuunda donge la gilasi.
Tunamtazama fundi mmoja akipuliza puto la gilasi katika kalibu yenye sehemu zilizobonyea, kisha msaidizi wake anakata ncha ya puto hilo, halafu fundi anazungusha ufito wake wa kupulizia ili kulifungua puto kama vile tumba la ua linavyofunguka. Gilasi hiyo inapashwa joto, inaundwa, na kutiwa ukingo ili kutokeza shada la taa lenye umbo la yungiyungi.
Ili kutia rangi kwenye donge la gilasi, fundi hulinyunyizia rangi ya ungaunga unaoweza kuyeyuka. Mapambo ya maua yanaweza kuongezwa kwa kutumia vipande vyembamba vya gilasi vyenye rangi mbalimbali vinavyofanana na sarafu. Donge la mviringo linaweza kuviringishwa na kufunikwa kwa vipande hivyo vya gilasi au kutiwa vipande kadhaa vilivyo sambamba linapoviringishwa kwenye meza ya chuma. Donge hilo linaporudishwa kwenye tanuru, vipande hivyo vyenye rangi mbalimbali, mapambo au madoido, huungana na kushikamana nalo, na sasa linaweza kupulizwa na kuwa chupa ya maua, taa, au umbo lingine lolote linalotakikana. Gilasi nene zenye matabaka ya rangi mbalimbali au zisizo na rangi hufanyizwa kwa kuzichovya kwenye vyombo tofauti-tofauti vya kuyeyushia.
Naam, kila chombo ni cha pekee na kimeundwa kwa njia yake maalumu. Kwa kuendeleza tamaduni zao za karne nyingi, watengenezaji wa gilasi wa kisiwa hicho maarufu cha Venice hutumia moto kutengeneza vyombo vya fahari na vyenye kumetameta kutokana na mchanga.
[Picha katika ukurasa wa 16]
Rio dei vetrai, Murano, Italia
[Picha katika ukurasa wa 17]
“Kikombe cha Barovier” cha karne ya 15
[Picha katika ukurasa wa 17]
Bilauri ya divai ya karne ya 16 yenye maumbo ya almasi
[Picha katika ukurasa wa 18]
1. Shimo dogo kwenye tanuru
2. Fundi anaunda donge la gilasi
3. Gilasi inapashwa moto tena ili iwe laini
4. Fundi anatumia koleo na makasi kufanyiza miguu ya farasi anayeruka
5. Chombo kilichokamilika
[Hisani]
Photos courtesy http://philip.greenspun.com