Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Msongamano wa Magari

Je, umewahi kujiuliza ni kwa nini kunaweza kuwa na msongamano wa magari kwa muda fulani, halafu ghafula magari yanaanza kwenda kwa mwendo wa kawaida na huoni kilichosababisha msongamano huo? Gazeti The Wall Street Journal linasema “kuna mambo fulani yanayosababisha msongamano wa magari hata wakati ambapo hakuna msiba barabarani wala barabara si mbovu.” Hata kupunguza mwendo kidogo tu kunaweza kufanya magari yaliyo karibu-karibu yasongamane na kwenda polepole. Gazeti hilo linasema kwamba “kulingana na kadirio moja, asilimia 75 ya misongamano ya magari haina kisababishi kinachoonekana. Huenda kilichosababisha msongamano huo kilitokea na kutatuliwa saa nyingi zilizopita, lakini matokeo yake yangalipo.” Mtu anaweza kuepuka misongamano ya magari kwa kubadili njia ikiwa barabara za jiji hazina magari mengi. Lakini kadiri barabara zinavyozidi kusongamana na madereva wengine wanafanya vivyo hivyo, “hawezi kufanikiwa kupata barabara isiyo na msongamano,” makala hiyo inasema. “Madereva wanaotulia hufanikiwa kuliko wale wanaotafuta njia ya haraka zaidi.”

Kuzoea Kuvuta Sigara Ujanani

Kulingana na gazeti National Post la Kanada “kuvuta sigara mara moja tu kunatosha kumfanya kijana awe na mazoea ya kuvuta sigara. Ugunduzi huo wa kustaajabisha unapingana na maoni ya watu wengi kwamba watu huzoea kuvuta sigara hatua kwa hatua baada ya kufanya hivyo sana kwa miaka kadhaa.” Kwa mujibu wa gazeti hilo, watafiti waliowachunguza vijana 1,200 kwa kipindi cha miaka sita hivi waligundua kwamba “kuzoea nikotini hasa ndiko huwafanya vijana wavute sigara kuliko hata ule uvutano wa marika na hilo linawahusu pia vijana wanaovuta sigara mara mojamoja tu.” Kulingana na uchunguzi huo, “vijana wengi huonyesha dalili za kuzoea nikotini wakati ambapo wamevuta sigara kwa mara ya kwanza na wanapozoea kufanya hivyo.” Watafiti hao wanasema kwamba miradi ya kupinga uvutaji wa sigara inapaswa kufanywa ili kuwasaidia vijana kuepuka zoea hilo na pia kuwasaidia wale ambao wanavuta sigara kushinda zoea hilo.

Je, Inawezekana Kuwa Safi Kupita Kiasi?

Watu wengi hupenda kuoga jioni kwa muda mrefu na kwa maji ya moto. Hata hivyo, gazeti The Daily Telegraph la Australia lilionya hivi: “Kuoga sana kunaweza kusababisha matatizo mengi ya ngozi. Watu huoga mara nyingi kupita kiasi na kwa muda mrefu sana wakitumia sabuni zisizofaa.” Dakt. Megan Andrews, mtaalamu wa magonjwa ya ngozi, anasema hivi: “Sote hupenda kutakata, lakini usafi huo unaopita kiasi unaweza kudhuru ngozi . . . Huenda mtu akahisi vizuri lakini anaharibu ngozi yake.” Kwa nini? Kwa kuwa kuoga kupita kiasi hufanya ngozi “ipoteze mafuta ya asili, ipasuke-pasuke na kuwa na makovu, na huvuruga vijiumbe vinavyoikinga,” lilisema gazeti hilo. Kisha gazeti hilo liliongezea kwamba majira makavu ya baridi kali “ndio wakati mbaya zaidi.” Andrews anapendekeza watu waoge kwa muda mfupi mara moja kwa siku.

Shauri Lisilofaa

Gazeti the The Guardian Weekly linasema: “Kufikia miaka ya 1970, wenyeji wa vijiji vingi huko Bangladesh na Bengal Magharibi [India] walikuwa na visima vyenye kina kifupi au waliteka maji kwenye mabwawa au mito na mara nyingi waliugua kipindupindu, ugonjwa wa kuhara damu na magonjwa mengine yanayosababishwa na maji. Kisha Umoja wa Mataifa ukawashauri watu wachimbe ‘visima vya mabomba’ vyenye kina kirefu kwenye miamba yenye maji ili wapate maji safi yasiyo na viini.” Karibu visima milioni 20 vilichimbwa huko Bangladesh, Vietnam, Laos, Burma (ambayo sasa ni Myanmar), Thailand, Nepal, China, Pakistan, Kambodia, na Bengal Magharibi huko India. Hata hivyo, visima vingi vilifikia sehemu zenye aseniki zilizo chini ya ardhi. Hivyo, watu wengi wameathiriwa na sumu ya aseniki hivi kwamba Shirika la Afya Ulimwenguni lilisema kwamba hicho ndicho “kisa cha watu wengi zaidi ulimwenguni kuathiriwa na sumu.” Watu wapatao milioni 150 wamekuwa wakinywa maji machafu katika kipindi cha miaka 20 iliyopita. Watu 15,000 wameathiriwa sana na sumu nchini Bangladesh pekee. Mashirika ya eneo hilo, serikali, na Umoja wa Mataifa yamekuwa yakifikiria hatua za kuchukua, lakini hayajafanikiwa kupata namna ya kutatua tatizo hilo.

Watoto Wanaojiua

Gazeti Milenio la Mexico City linasema: “Asilimia 80 ya watoto wanaojaribu kujiua au ambao hufanikiwa kujiua husema-sema au huandika kwamba watajiua siku au miezi kadhaa kabla ya kufanya hivyo.” Sababu hasa zinazofanya watoto watake kujiua ni kudhulumiwa (kimwili, kihisia, au kwa maneno), kutendewa vibaya kingono, kuvunjika kwa familia, na matatizo wanayokabili shuleni. Kulingana na José Luis Vázquez, mtaalamu wa magonjwa ya akili kwenye Taasisi ya Huduma za Kijamii ya Mexico, televisheni, filamu, michezo ya video, na vitabu huonyesha kwamba kifo ni jambo la kawaida hivi kwamba watoto hawaoni uhai kuwa muhimu. Anaongezea kwamba watoto 15 kati ya 100 walio kati ya umri wa miaka 8 na 10 hutaka kujiua na kwamba asilimia 5 kati yao hufaulu kujiua. Gazeti hilo linapendekeza kutopuuza wakati watoto wanaposema watajiua na kutoona jambo hilo kuwa tisho tu au njia ya kutaka kutambuliwa. Linaongezea hivi: “Wazazi wanapaswa kutumia wakati na watoto wao, kucheza nao, kuwasiliana nao, na kuwaonyesha kuwa wanawapenda nyakati zote.”

Hasira Ni Hatari

Kulingana na Valentina D’Urso, mwalimu wa saikolojia katika Chuo Kikuu cha Padua nchini Italia, “hasira ni jambo la kawaida katika jamii, lakini inaathiri mwili.” Misuli hukazika, mpigo wa moyo huongezeka, mtu hupumua haraka, na mwili hufadhaika. Hasira inaweza pia kumzuia mtu kufikiri vizuri na kujidhibiti. D’Urso anasema hivi: ‘Inafaa tutambue mapema hali zinazoweza kutukasirisha. Inafaa tujizuie tusikasirike nasi tutakuwa na maisha bora.’

Madaktari Waliofadhaika

Gazeti Vancouver Sun linasema kwamba hivi karibuni Shirika la Kitiba la Kanada liliwachunguza madaktari 2,251 nchini humo na “kugundua kwamba asilimia 45.7 walikuwa wachovu kupindukia, walikuwa na matatizo ya kihisia, wenye mtazamo mbaya, na kuhisi kwamba hawatimizi kazi yao.” Kulingana na Dakt. Paul Farnan, msimamizi wa Mradi wa Kuwategemeza Madaktari huko British Columbia, mambo yanayochangia mfadhaiko wa madaktari wengi yanatia ndani kushindwa kupata watu wa kuwasaidia wanapotaka kwenda likizo, kuhitajika mara nyingi katika hospitali mbalimbali, na kazi nyingi ofisini. Dakt. Farnan anawatia moyo madaktari waliofadhaika wawe na usawaziko maishani mwao kwa kutumia wakati pamoja na familia zao na kushiriki katika shughuli zinazowatosheleza kiroho au kihisia.