Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kwa Nini Wengi Hupata Homa Inayosababishwa na Vumbi?

Kwa Nini Wengi Hupata Homa Inayosababishwa na Vumbi?

Kwa Nini Wengi Hupata Homa Inayosababishwa na Vumbi?

Na mwandishi wa Amkeni! nchini Hispania

MACHO yako yanawasha na yanatoa machozi, unapiga chafya kila wakati, unatoa kamasi saa zote, na unashindwa kupumua. Tatizo ni nini? Huenda una mafua. Lakini ukihisi hivyo unapokuwa karibu na mimea, basi huenda una homa inayosababishwa na vumbi. Ikiwa ndivyo, basi wewe ni mmoja kati ya wengi walio na homa hiyo. Idadi ya watu wanaopata homa hiyo huongezeka kila mwaka.

Kulingana na gazeti Mujer de Hoy, “homa inayosababishwa na vumbi hutokea wakati mwili unapodhani kwamba umevamiwa na kitu hatari. Mfumo wa kinga wa watu wenye mizio hukataa vitu vyote vya kigeni, kutia ndani chavuo, ingawa kwa kweli vitu hivyo si hatari.” Na mfumo wa kinga unapofanya hivyo, hutokeza dalili zenye kusumbua zilizotajwa mwanzoni.

Mnamo mwaka wa 1819, daktari Mwingereza John Bostock alifafanua homa inayosababishwa na vumbi, naye alikuwa wa kwanza kufanya hivyo. Bostock alieleza matatizo yaliyokuwa yakimpata wakati wa majira ya homa. Aliamini kwamba matatizo yake yalitokana na nyasi zilizokuwa zimekatwa karibuni. Baadaye, iligunduliwa kwamba matatizo hayo husababishwa na chavuo za aina mbalimbali. Mwanzoni mwa karne ya 19, Bostock aligundua kwamba ni watu wachache sana waliokuwa na matatizo hayo kotekote Uingereza.

Hata hivyo, kwa nini watu wengi leo hupata homa inayosababishwa na vumbi? Dakt. Javier Subiza, mkurugenzi wa Kituo cha Pumu na Mizio huko Madrid Hispania, anataja dhana mbili zinazochunguzwa na watafiti. Dhana moja inasema kwamba matatizo hayo husababishwa na mashine zinazotumia dizeli. Inaaminika kwamba chembe zinazotoka katika dizeli inayowaka zinaweza kusababisha matatizo ya mizio. Kulingana na daktari wa mizio, Juan Kothny Pommer, “asilimia 20 ya watu katika nchi zilizoendelea kiviwanda hupata homa hiyo, hasa wakaaji wa majiji.”

Dhana ya pili inadokeza kwamba homa hiyo husababishwa na usafi wa kupita kiasi. Dakt. Subiza anaeleza kwamba, ‘sisi huzaliwa katika chumba cha upasuaji, tunakula vyakula vyenye kemikali za kuua viini, tunapata chanjo za magonjwa mengi, nasi hutumia viuavijasumu mara tu tunapokuwa wagonjwa. Kwa hiyo, tangu utotoni, mfumo wetu wa kinga unaweza kusababisha mizio.’

Ikiwa wewe hupatwa na homa hiyo, usiwe na wasiwasi! Ukipimwa vizuri na kutibiwa, unaweza kupunguza mara ambazo unapata homa hiyo na ukali wake.