Matokeo ya Jitihada za Kupambana na Magonjwa
Matokeo ya Jitihada za Kupambana na Magonjwa
MNAMO Agosti 5, 1942, Dakt. Alexander Fleming aligundua kwamba mmoja wa wagonjwa wake, rafiki yake, alikuwa anakaribia kufa. Mwanamume huyo mwenye umri wa miaka 52 alikuwa na homa ya uti wa mgongo na licha ya jitihada zote za Fleming, sasa rafiki yake alikuwa amepoteza fahamu.
Miaka 15 mapema, Fleming alikuwa amegundua kitu fulani chenye kustaajabisha kilichofanyizwa na kuvu ya rangi ya bluu-kijani. Alikiita penisilini. Aligundua kwamba inaweza kuua bakteria; lakini hakuweza kutenganisha sehemu aliyohitaji kutoka katika zile sehemu nyingine za kuvu, basi akaitumia kuzuia ukuzi wa bakteria tu. Hata hivyo, katika mwaka wa 1938, Howard Florey pamoja na kikundi chake cha watafiti katika Chuo Kikuu cha Oxford walijitahidi kutengeneza kiasi cha kutosha cha penisilini ili ijaribiwe kwa binadamu. Fleming akampigia simu Florey, aliyekubali kumtumia penisilini yote aliyokuwa nayo. Hiyo ndiyo iliyokuwa nafasi ya mwisho ya Fleming kumwokoa rafiki yake.
Kumdunga sindano ya penisilini kwenye misuli hakukutosha, kwa hiyo Fleming akamdunga rafiki yake dawa hiyo moja kwa moja kwenye uti wa mgongo. Penisilini hiyo iliangamiza viini vya ugonjwa huo; na baada ya juma moja tu, mgonjwa wa Fleming akaondoka hospitalini akiwa amepona kabisa. Tangu wakati huo, viuavijasumu vikaanza kutumiwa. Mwanadamu akawa amepiga hatua kubwa katika jitihada zake za kupambana na magonjwa.
Enzi ya Viuavijasumu
Viuavijasumu vilipoanza kutumiwa kwa mara ya kwanza, vilionwa kuwa dawa ya magonjwa yote. Magonjwa yaliyosababishwa na bakteria, kuvu, au viini vingine, ambayo hayakuwa na tiba awali, sasa yangeweza kutibiwa kabisa. Kwa sababu ya dawa hizo mpya, idadi ya watu waliokuwa wakifa kutokana na homa ya uti wa mgongo, nimonia, na homa ya vipele vyekundu ikapungua sana. Magonjwa ambayo watu waliambukizwa wakiwa hospitalini ambayo hapo awali yalisababisha kifo, sasa yalitibiwa kwa siku chache.
Tangu wakati wa Fleming, watafiti wamevumbua viuavijasumu vingi nao wanaendelea kutafuta vingine. Katika miaka 60 iliyopita, viuavijasumu vimekuwa muhimu katika jitihada za kupambana na magonjwa. Kama George Washington angekuwa hai leo, bila shaka madaktari wangeutibu mwasho wake wa koo kwa kiuakijasumu na huenda angepona kwa muda wa juma moja hivi. Viuavijasumu vimesaidia wengi wetu
kupona magonjwa kadhaa. Hata hivyo, ni wazi kwamba viuavijasumu vimepungukiwa kwa njia fulani.Viuavijasumu havitibu magonjwa yanayosababishwa na virusi kama vile UKIMWI au homa kali. Isitoshe, watu fulani huathiriwa na viuavijasumu fulani. Na viuavijasumu ambavyo huua viini vya aina nyingi vinaweza kuua vijiumbe muhimu katika miili yetu. Lakini huenda tatizo kubwa hata zaidi likawa kutumia kupita kiasi dawa hizo au kupunguza kiasi kilichopendekezwa.
Wagonjwa wengine wanapopata nafuu hawamalizi dawa walizopendekezewa na daktari, labda kwa sababu wanahisi vizuri au kwa sababu itawabidi watumie dawa hizo kwa muda mrefu. Kwa hiyo, huenda dawa hizo zisiue bakteria zote zinazoshambulia na hivyo bakteria sugu hubaki na kuongezeka. Watu wengi wanaotibiwa kifua-kikuu wamepatwa na hali hiyo.
Madaktari na wakulima hutumia dawa hizo mpya kupita kiasi. Kitabu Man and Microbes kinasema: “Madaktari huko Marekani wamependekeza viuavijasumu hata wakati ambapo havihitajiwi, na katika nchi nyinginezo vinatumiwa ovyoovyo sana. Mifugo imepewa viuavijasumu vingi, si kwa kusudi la kuponya magonjwa, bali kuharakisha ukuzi; na hilo hufanya bakteria
ziwe sugu.” Kitabu hicho kinasema kwamba “huenda viuavijasumu vipya visipatikane.”Lakini, licha ya mahangaiko hayo kuhusu kutofanikiwa kwa viuavijasumu, kulikuwa na mafanikio mengi ya kitiba katika nusu ya pili ya karne ya 20. Ilionekana kwamba watafiti wa kitiba wangeweza kupata dawa za kutibu karibu kila ugonjwa. Pia, ilitazamiwa kwamba chanjo zingeweza kuzuia magonjwa.
Mafanikio ya Sayansi ya Tiba
Jarida la The World Health Report 1999 lilisema hivi: “Kumekuwa na mafanikio mengi sana katika kukinga magonjwa.” Mamilioni ya watu wameokolewa kwa sababu ya miradi ya kuchanja watu ulimwenguni. Mradi wa ulimwenguni pote wa kuchanja watu umekomesha ugonjwa wa ndui, ule ugonjwa hatari ulioua watu wengi kuliko vita vyote vya karne ya 20. Mradi mwingine kama huo unakaribia kukomesha ugonjwa wa polio. (Ona Sanduku “Kushinda Ndui na Polio.”) Leo, watoto wengi huchanjwa ili kuwakinga dhidi ya magonjwa hatari ambayo yameenea sana.
Magonjwa mengine yamepunguzwa kwa kutumia njia nyingine. Magonjwa yanayoenezwa kupitia maji, kama vile kipindupindu, hayaelekei kutokea mahali penye mazingira safi na maji safi. Katika nchi nyingi ambapo ni rahisi kwa watu kwenda hospitalini, magonjwa mengi yanaweza kutambuliwa na kutibiwa kabla hayajawa hatari. Chakula kizuri na makao mazuri, pamoja na kufuata sheria za kushughulikia na kuhifadhi chakula vizuri, ni mambo ambayo yamechangia afya bora ya umma.
Wanasayansi walipogundua vyanzo vya magonjwa ya kuambukiza, maofisa wa afya wangeweza kuchukua hatua za kuzuia magonjwa. Hebu fikiria mfano mmoja. Tauni ya majipu ilipozuka huko San Francisco mwaka wa 1907, ni watu wachache tu waliokufa kwa sababu jiji hilo lilianzisha mara moja mradi wa kuangamiza panya wote, kwa kuwa viroboto vya panya ndivyo vilivyokuwa vikieneza ugonjwa huo. Kwa upande mwingine, kwa miaka 12, kuanzia mwaka wa 1896, ugonjwa huohuo uliua watu milioni kumi nchini India kwa sababu chanzo chake hakikuwa kimegunduliwa.
Kulemewa na Magonjwa
Ni wazi kwamba, kumekuwa na mafanikio mengi makubwa. Hata hivyo, baadhi ya mafanikio hayo yamepatikana katika nchi tajiri tu. Magonjwa yanayoweza kutibiwa bado yanaua mamilioni ya watu kwa sababu ya ukosefu wa pesa za kutosha. Katika nchi zinazoendelea bado watu wengi hawana mazingira safi, hawapati matibabu, wala hawana maji safi. Tatizo hilo linazuka hasa kwa sababu watu wengi katika nchi hizo wanahama kutoka mashambani kwenda katika majiji makubwa. Kwa hiyo, kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni, watu wanaoishi katika nchi maskini ulimwenguni “hulemewa na magonjwa mengi kuliko wale wanaoishi katika nchi tajiri.”
Tatizo hilo hutokana hasa na ubinafsi unaowazuia watu kupangia mambo ya wakati ujao. Kulingana na kitabu Man and Microbes: “Baadhi ya magonjwa hatari ya kuambukiza hayapatikani katika nchi zilizoendelea. . . . Baadhi yake yanapatikana hasa katika maeneo maskini ya tropiki au yaliyo karibu na tropiki.” Kwa kuwa huenda zisifaidike moja kwa moja, nchi tajiri na kampuni za dawa hutoa pesa za kutibu magonjwa hayo shingo upande.
Kutojali kwa watu pia kumechangia kuenea kwa magonjwa. Hilo laonekana wazi hasa katika kisa cha UKIMWI, ambao huenezwa kutoka kwa mtu mmoja hadi kwa mwingine kupitia umajimaji wa mwili. Kwa miaka michache tu, ugonjwa huo umeenea ulimwenguni pote. (Ona sanduku “UKIMWI—Tauni ya Siku Zetu.”) Mtaalamu mmoja wa magonjwa ya kuambukiza, Joe McCormick anasema: “Wanadamu wamejiletea wenyewe tatizo hilo. Hatujaribu kuchambua maadili ya watu, huo ndio ukweli wa mambo.”
Wanadamu walienezaje UKIMWI bila kujua? Kitabu The Coming Plague kinataja mambo yafuatayo: Mabadiliko ya maisha ya watu—hasa yale mazoea ya kufanya ngono na watu wengi—yalisababisha kuenea kwa magonjwa ya zinaa, jambo ambalo hufanya virusi viongezeke sana na iwe rahisi mtu mmoja kuwaambukiza watu wengine wengi. Kutibu watu katika nchi zinazoendelea kwa kutumia sindano ambazo
tayari zimetumiwa au kujidunga dawa za kulevya kwa sindano ambazo tayari zimetumiwa kulichangia pia kuenea kwa ugonjwa huo. Biashara ya damu inayoleta mabilioni ya dola pia iliwezesha virusi vya UKIMWI kuenea kutoka kwa mtu mmoja hadi kwa watu wengi.Kama ilivyotangulia kutajwa, kutumia viuavijasumu kupita kiasi au kupunguza kiasi kilichopendekezwa kumechangia kuwapo tena kwa viini sugu. Hilo ni tatizo kubwa na linaendelea kuzidi. Bakteria inayoitwa staphylococcus, ambayo mara nyingi huambukiza vidonda, ilikuwa ikikomeshwa kwa urahisi kwa kutumia dawa zenye penisilini. Lakini sasa, viuavijasumu hivyo vya zamani mara nyingi havifaulu. Kwa hiyo, ni lazima madaktari waanze kutumia viuavijasumu vipya ambavyo ni ghali na huenda nchi zinazoendelea zisiweze kuvigharimia. Hata viuavijasumu vipya kabisa huenda visiangamize viini fulani, hivyo kufanya magonjwa ambayo watu huambukizwa hospitalini yaenee na kuwa hatari zaidi. Dakt. Richard Krause, aliyekuwa mkurugenzi wa Taasisi ya Kitaifa ya Mizio na Magonjwa ya Kuambukiza ya Marekani, alifafanua waziwazi hali ya sasa kuwa “mlipuko wa viini sugu.”
“Je, Mambo Ni Afadhali Leo?”
Ni wazi kwamba tisho la magonjwa bado liko hata sasa, mwanzoni mwa karne hii ya 21. Kuenea kwa UKIMWI, kuzuka kwa viini sugu, na kutokea upya kwa magonjwa hatari ya zamani kama vile kifua-kikuu na malaria kwaonyesha kwamba vita dhidi ya magonjwa vinaendelea.
Joshua Lederberg aliyeshinda Tuzo ya Nobeli, aliuliza hivi: “Je, mambo ni afadhali leo kuliko yalivyokuwa karne moja iliyopita? Katika nyanja nyingi, mambo ni mabaya zaidi. Tumepuuza viini, nasi tunavuna matokeo ya uzembe wetu.” Je, jitihada za sayansi ya tiba na mataifa yote ya ulimwengu zitasuluhisha matatizo hayo? Je, hatimaye magonjwa ya kuambukiza yatakomeshwa kama vile ugonjwa wa ndui ulivyokomeshwa? Makala yetu inayofuata itajibu maswali hayo.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8]
Kushinda Ndui na Polio
Mwishoni mwa Oktoba 1977, Shirika la Afya Ulimwenguni lilimpata mtu wa mwisho aliyekuwa akiugua ugonjwa wa ndui. Ali Maow Maalin, mpishi wa hospitali aliyekuwa akiishi Somalia, hakulemewa sana na ugonjwa huo, naye alipona baada ya majuma machache. Watu wote waliokuwa wameshirikiana naye walichanjwa.
Madaktari walisubiri kwa miaka miwili. Mtu yeyote ambaye angeripoti kisa kingine cha kweli cha mtu anayeugua ndui angepata zawadi ya dola 1,000. Hakuna yeyote aliyeripoti kisa cha kweli, na mnamo Mei 8, 1980, Shirika la Afya Ulimwenguni likatangaza rasmi kwamba “Ulimwengu na wakazi wake wote wameushinda ugonjwa wa ndui.” Miaka kumi tu iliyotangulia, ugonjwa wa ndui ulikuwa ukiua watu milioni mbili kila mwaka. Kwa mara ya kwanza katika historia, ugonjwa hatari wa kuambukiza ukawa umekomeshwa. *
Ugonjwa wa polio, ambao hulemaza watu utotoni, ulionekana pia ungeweza kukomeshwa. Mwaka wa 1955, Jonas Salk, alivumbua chanjo ya polio, na miradi ya kuchanja watu dhidi ya polio ikaanza Marekani na katika nchi nyingine. Baadaye, chanjo iliyopitishwa mdomoni ikavumbuliwa. Mwaka wa 1988, Shirika la Afya Ulimwenguni lilianzisha mradi wa ulimwenguni pote wa kuondoa polio.
Dakt. Gro Harlem Brundtland, aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa Shirika la Afya Ulimwenguni, anaeleza hivi: “Tulipoanza jitihada za kuondolea mbali polio ulimwenguni katika mwaka wa 1988, ugonjwa huo ulikuwa ukilemaza watoto 1000 kila siku. Katika mwaka wa 2001, kulikuwa na visa vinavyopungua 1000 kwa mwaka mzima.” Sasa polio inapatikana katika chini ya nchi kumi, ingawa pesa zaidi zitahitajiwa kusaidia nchi hizo kuukomesha kabisa ugonjwa huo.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 28 Ugonjwa wa ndui ulifaulu kukomeshwa ulimwenguni pote kupitia chanjo kwa sababu, tofauti na magonjwa mengine ambayo huenezwa vinginevyo kama vile kupitia panya na wadudu, virusi vya ndui huishi mwilini mwa binadamu tu.
[Picha]
Mvulana Mwethiopia apokea chanjo ya polio
[Hisani]
© WHO/P. Virot
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 10]
UKIMWI—Tauni ya Siku Zetu
UKIMWI umekuwa tisho ulimwenguni pote. Miaka 20 hivi tangu ulipogunduliwa, watu zaidi ya milioni 60 wameambukizwa. Maofisa wa afya wanaonya kwamba UKIMWI ungali katika “hatua za kwanza-kwanza.” Idadi ya watu wanaoambukizwa “inazidi kuongezeka kuliko ilivyodhaniwa awali,” nayo matokeo katika sehemu zenye idadi kubwa zaidi ya watu wanaougua ugonjwa huo yanasikitisha.
Ripoti moja ya Umoja wa Mataifa inaeleza hivi: “Walio wengi kati ya watu wanaougua UKIMWI ulimwenguni wako katika umri ambao wanaweza kufanya kazi vizuri zaidi.” Kwa hiyo, inasemekana kwamba nchi nyingi zilizo kusini mwa Afrika zitapoteza asilimia 10 hadi 20 ya wafanyakazi wake kufikia mwaka wa 2005. Ripoti hiyo pia inasema: “Katika nchi zilizo kusini mwa Sahara, watu hutarajiwa kuishi miaka 47. Bila UKIMWI watu wangeweza kuishi wastani wa miaka 62.”
Kufikia sasa chanjo ya UKIMWI haijapatikana, na ni asilimia 4 tu ya watu milioni 6 wanaougua UKIMWI katika nchi zinazoendelea ambao wanapata matibabu ya aina fulani. Kwa sasa hakuna dawa ya UKIMWI, na madaktari wanahofia kwamba watu wengi ambao wameambukizwa virusi vya ugonjwa huo hatimaye wataugua UKIMWI.
[Picha]
Chembe za “T lymphocyte” zilizoambukizwa virusi vya UKIMWI
[Hisani]
Godo-Foto
[Picha katika ukurasa wa 7]
Mfanyakazi katika maabara achunguza aina sugu ya virusi
[Hisani]
CDC/Anthony Sanchez