Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mbegu Inayosafiri Baharini

Mbegu Inayosafiri Baharini

Mbegu Inayosafiri Baharini

Na mwandishi wa Amkeni! nchini Uingereza

NILIPOKUWA nikitembea kwenye ufuo wenye mchanga ulio na mwani wa baharini na vipande vya miti kwenye pwani ya mashariki ya Uingereza, niliona kijiwe cha ajabu na kukiokota. Kilikuwa laini na chenye rangi ya kahawia, lakini kumbe hakikuwa kijiwe! Kilikuwa nini? Mbegu iliyobebwa na maji kutoka maeneo ya tropiki. Mbegu hiyo ilifikaje huko?

Chanzo cha Mbegu Hiyo

Mbegu hiyo inatokana na mmea mkubwa unaoitwa mtambaa. Kulingana na The Concise Oxford Dictionary, mtambaa ni “mmea unaotambaa ambao huning’inia kwenye miti, hasa katika misitu ya mvua ya tropiki.” Mmea huo hutumia vikonyo vyake kutambaa kwenye mti, na nyakati nyingine hufikia urefu wa meta 30 kutoka chini. Mmea huo hupatikana sana kwenye pwani na mito iliyo katikati na magharibi mwa Afrika, Kolombia, West Indies, na Amerika ya Kati. Huko Kosta Rika, ambako nyani huutumia kuruka kutoka mti mmoja hadi mwingine, mmea huo huitwa ngazi ya nyani.

Mbegu hiyo huwa na upana wa sentimeta 6 na hufanyizwa katika ganda kubwa linaloning’inia kwenye mti. Ganda hilo kubwa linaweza kukua kufikia urefu wa meta 2. Lina sehemu za mviringo, kila moja ikiwa na mbegu moja. Mbegu hizo hugawanywa na kistari chembamba kilichobonyea. Kama mbegu nyingi, ganda hilo linapotokea mara ya kwanza huwa laini na lenye rangi ya kijani. Lakini linapokomaa linakuwa gumu, linakauka, na kuwa zito. Pia linakuwa na rangi ya kahawia na kufanana na kijiti.

Hatimaye, ganda hilo linapokuwa zito zaidi, linaanguka mtoni au baharini. Ganda linapobebwa na maji, sehemu zake hutengana. Sasa, kila mbegu huelekea upande tofauti-tofauti ikiwa kwenye ganda lake. Mbegu fulani zinaweza kukwama na kuota kwenye matope yaliyo ukingoni mwa mto. Hata hivyo, mbegu nyingi huelea majini na nyakati nyingine husafiri kilometa nyingi hadi mahali ambapo mto unaungana na bahari. Mbegu ikipitia katikati ya visiwa kadhaa, mawimbi yanaweza kuibeba hadi ufuo ulio karibu.

Mbegu Inayosafiri

Mbegu inayoelea baharini hupatwa na nini? Ganda lake huoza hatua kwa hatua na mbegu hutoka. Je, mbegu hiyo huzama? Hapana, kwa kuwa haipenywi na maji. Mbegu hiyo huelea kwa sababu ya uwazi unaofanyizwa wakati jani la kwanza lililo ndani ya mbegu hiyo linaponywea. Kwa sababu ya muundo wake wa ajabu, mbegu hiyo yenye umbo la moyo inaweza kusafiri baharini bila kuharibika kwa miezi, au hata miaka, kabla ya kufika kwenye ufuo wa mbali.

Mbegu hiyo huwezaje kufika maeneo ya mbali kama vile British Isles, Scandinavia, na sehemu nyingine za Ulaya Magharibi? Kwa karne nyingi, mbegu hizo zimebebwa na mkondo wa maji unaoitwa Gulf Stream na kuvuka Bahari ya Atlantiki. Mamilioni ya mbegu hizo hubebwa daima na mikondo ya bahari ulimwenguni pote!

Je, mbegu hiyo inaweza kuota baada ya safari hiyo ndefu na ngumu? Jaribu kukata ganda lake la nje kwa tupa au msumeno, hasa karibu na mahali ambapo mbegu inaungana na kifumba-mbegu. Kisha ipande mbegu hiyo kwenye udongo, itie maji, na uiache mahali penye joto. Yaelekea itaota.

Hata hivyo, ni nini huipata mbegu inayobebwa na maji hadi kwenye fuo za Ulaya zenye baridi kali ambako ni vigumu kuota? Mtu anayeipata anaweza kuiweka ili ajikumbushe kuhusu sehemu hiyo, lakini mbegu nyingi huokotwa na kuuzwa, na nyakati nyingine zinaunganishwa pamoja na makoa au shanga kutengeneza mapambo maridadi ya kuvaliwa shingoni. Mbegu zenye umbo la moyo lenye kuvutia huuzwa kwa bei ghali.

Watu kutoka sehemu za Ulaya Kaskazini hutumia mbegu hizo na nyingine zenye umbo la mstatili kutengeneza visanduku vya tumbaku, viberiti, na vibweta. Huko Uingereza, watoto huwekewa mbegu hizo mdomoni kabla ya meno kuota. Mara nyingi mabaharia hutumia mbegu hizo kama hirizi. Wanaamini kwamba kwa kuwa mbegu hizo zinaweza kusafiri mbali baharini na kupitia magumu mengi hivyo, basi zinaweza kuwalinda pia.

Kwa hiyo, utakapotembea ufuoni, chunguza kwa makini kati ya mwani na vipande vya miti. Huenda wewe pia ukapata mbegu ambayo imekuwa ikisafiri baharini.

[Picha katika ukurasa wa 23]

Ganda linaloning’inia la mbegu hiyo linaweza kukua kufikia urefu wa meta mbili

[Hisani]

Courtesy Jean-Jacques Segalen/ Barbadine.com

[Picha katika ukurasa wa 23]

Mapambo ya mbegu za baharini