Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Paka Mwenye Masikio ya Ajabu

Paka Mwenye Masikio ya Ajabu

Paka Mwenye Masikio ya Ajabu

MCHUNGAJI mmoja anayeitwa William Ross, alipendezwa na paka wa kiasili. Siku moja mwaka wa 1961, Ross alimtembelea jirani yake huko Perthshire, Scotland. Akiwa huko alimwona Susie, paka wa jirani huyo. Lakini Susie hakufanana na paka wa nyumbani wa kawaida. Alikuwa mweupe naye alikuwa uzao wa aina tofauti za paka, lakini nusu ya masikio yake yalikuwa yamejipinda mbele na kuelekea chini, hivyo kumfanya awe na sura ya kuchekesha. Mwaka mmoja baadaye Susie alizaa watoto, na kwa kuwa Ross alipendezwa na paka huyo, alimchukua mtoto mmoja wa kike mwenye masikio yaliyojipinda.

Kisha Ross akawasiliana na mzalishaji mmoja huko London ambaye hupendezwa na chembe za urithi za paka, nao wakaanzisha programu ya kuzalisha paka kama Susie. Paka hao wakaitwa Scottish Fold. Tangu wakati huo, paka hao wamewavutia watu wengi. Hata hivyo, mashirika ya Uingereza ya paka hayajawaandikisha paka hao kisheria. Watu fulani wamehofia kwamba huenda paka hao wakapatwa na matatizo ya afya kutokana na chembe fulani ya urithi inayoyafanya masikio kujipinda. Lakini mahangaiko yao hayakuzuia paka hao wasiandikishwe kisheria huko Marekani, ambapo programu ya kuwazalisha ilianzishwa mapema katika miaka ya 1970. Kufikia mwishoni mwa miaka hiyo, paka hao walikuwa mabingwa wa maonyesho mbalimbali nchini humo.

Kwa Nini Masikio Yao Yamejipinda?

Watu wanapomwona paka wa Scottish Fold mara ya kwanza, wao huuliza, “Paka wako alifanya nini masikio?” Paka hao wana masikio yaliyojipinda kwa sababu ya badiliko la chembe ya urithi yenye nguvu zaidi. Mtoto wa paka akirithi chembe hiyo hata kutoka kwa mzazi mmoja tu, atakuwa na masikio yaliyojipinda.

Hata hivyo, masikio yao hujipinda kwa njia tofauti. Masikio ya paka fulani hayajajipinda, hali ya wengine yamejipinda mara moja, mara mbili, au hata mara tatu. Masikio ya Susie, paka wa kwanza wa Scottish Fold, yalikuwa yamejipinda mara moja tu. Kwa kawaida, masikio ya paka wa maonyesho huwa yamejipinda mara tatu, nayo huwa yamelala kichwani. Ajabu ni kwamba, paka wa Scottish Fold huzaliwa wakiwa na masikio yaliyosimama. Lakini wanapofikia umri wa majuma matatu hivi, wazalishaji wanaweza kutambua wale watakaokuwa na masikio yaliyojipinda.

Kuwazalisha paka hao ovyoovyo kwaweza kusababisha matatizo ya afya. Kwa mfano, ikiwa dume na jike wana masikio yaliyojipinda, huenda watoto wao wakawa na tatizo la chembe za urithi, kama vile kuwa na kasoro kwenye mifupa. Hivyo, wazalishaji wenye ujuzi hufanya paka wa Scottish Fold wajamiiane na paka wengine wenye masikio yaliyosimama. Kwa kawaida wazalishaji huwazalisha paka hao kwa kutumia paka wa Uingereza na wa Marekani wenye manyoya mafupi.

Pia kuna hatari za kiafya zinazoweza kuletwa na uchafu kwenye masikio ya paka hao, hasa wale wenye masikio yaliyojipinda mara tatu. Kwa sababu masikio yao hujipinda sana karibu na kichwa, huchafuka sana upande wa ndani. Kitabu The Illustrated Encyclopedia of Cat Breeds kinapendekeza kwamba watu wanaofuga paka hao wayasafishe masikio taratibu “upande wa ndani kwa pamba iliyoloweshwa.” Hata hivyo, kulingana na kituo cha Internet cha watu wenye paka kinachoitwa The Cat Site, paka wenye afya “hawapatwi na maambukizo au wadudu kwenye masikio kama vile ilivyodhaniwa miaka kadhaa iliyopita.”

Marafiki Wenye Kupendeza

Paka wa Scottish Fold huonwa kuwa wapole, wanaopendeza, na werevu. Wao huishi miaka 15 hivi, nao hufurahia sana makao yenye kustarehesha. Kitabu The Illustrated Encyclopedia of Cat Breeds kinasema: “Paka wa Scottish Fold ni wanana, watulivu, wenye urafiki, na wanawapenda wanadamu na wanyama wengine wa nyumbani.” Wana sauti nyororo yenye kupendeza na hawaitumii mara nyingi. Hata wakiwa na njaa, watasimama tu na kukukodolea macho mpaka uwalishe.

Sawa na paka wengine, paka hao wana rangi mbalimbali, na vilevile manyoya marefu au mafupi. Lakini wanazidi kupendwa hasa kwa sababu ya masikio yao yaliyojipinda, kichwa chao cha duara, shingo fupi, na uso wao ulio kama wa bundi wenye macho makubwa ya mviringo. Ama kweli, Scottish Fold ni mmojawapo wa paka wanaopendwa zaidi ulimwenguni. Mara nyingi watu wanaotaka kuwanunua paka hao hulazimika kungoja miezi sita au zaidi kabla ya kuwapata. Kwa hakika, ikiwa mnunuzi anataka paka mwenye manyoya ya urefu hususa, rangi, au jinsia fulani, itambidi asubiri muda mrefu zaidi.

Yamkini William Ross alipomwona Susie mwaka wa 1961, hakujua kwamba wazao wa paka huyo wa mashambani wangependwa sana, hasa tukikumbuka kwamba wamekuwa maarufu kwa sababu ya badiliko fulani katika chembe za urithi ambalo huonekana hasa kwenye masikio, wala si kwa sababu wao ni bora kiasili.