Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kwa Nini Watu Wengi Huhisi Upweke?

Kwa Nini Watu Wengi Huhisi Upweke?

Kwa Nini Watu Wengi Huhisi Upweke?

LEO watu wengi wa umri, jamii, nyadhifa, na dini mbalimbali huhisi upweke. Je, umewahi kuhisi upweke? Je, unahisi upweke sasa? Kwa kweli, sisi sote wakati mwingine hutamani kuwa na mwandamani, mtu anayeweza kutusikiliza, kututia moyo, au anayeweza kuelewa hisia zetu, maoni yetu, na anayetuelewa kikweli. Tunahitaji mtu anayejali hisia zetu.

Hata hivyo, kuwa peke yetu hakumaanishi kwamba tunahisi upweke. Mtu anaweza kuwa peke yake kwa muda mrefu akifurahia mambo anayofanya pasipo kuhisi upweke hata kidogo. Hata hivyo, kuna watu ambao hawawezi kuwa peke yao. Neno peke humaanisha kutokuwako kwa mtu mwingine zaidi ya yule anayezungumziwa. Neno hilo hukazia kuwa mbali na wengine, lakini si kwamba mtu huyo hana furaha. Nalo neno upweke ni hali ya kukaa katika maisha peke yako, hali ya kukosa mshirika. Mara nyingi neno hilo linadokeza hali ya kushuka moyo inayotokana na kutambua kwamba uko peke yako. Neno ukiwa hukazia kutamani sana kuwa na washirika, yaani, hali yenye kuhuzunisha, msononeko, au mfadhaiko. Mtu mwenye hali hiyo anahitaji faraja na ushirika wenye upendo ili apate furaha tena. Nalo neno jitenga lina wazo la upweke na ukiwa ijapokuwa mara nyingi hukazia wazo la mtu kuwa peke yake kwa kupenda kwake.

Upweke ni hisia yenye nguvu na inaweza kuumiza sana. Humfanya mtu ahisi kwamba maisha hayana kusudi. Mtu huwa na hisia ya kutengwa na kuwa mbali na wengine. Upweke unaweza kumdhoofisha mtu kihisia na kumfanya kuwa mwoga. Je, umewahi kuhisi hivyo? Upweke husababishwa na nini?

Matatizo, matukio, na hali huwaathiri watu kwa njia tofauti-tofauti. Huenda ukahisi kwamba umekataliwa na watu wa rika lako kwa sababu ya sura, jamii, au dini yako. Mtu anaweza kuhisi upweke anapobadili mazingira kama vile kwenda shule mpya, kuanza kazi mpya, au hata kupata majirani wapya, kuhamia jiji au nchi nyingine, kwa sababu anawaacha rafiki zake. Mtu anapofiwa na wazazi wake au mwenzi wa ndoa, anaweza kuwa peke yake kwa miaka mingi. Pia, kadiri tunavyozidi kuzeeka, ndivyo rafiki na watu tuliofahamiana nao wanavyozidi kupungua.

Hata wale waliofunga ndoa wanaweza kuhisi upweke. Kutoelewana au kutopatana kunaweza kumfanya mtu afadhaike na hata kunaweza kuwafanya wenzi wa ndoa au watoto wajitenge. Mbali na upweke unaotokana na kifo cha mtu tunayempenda, talaka, au unaotokana na kujitenga kihalisi au kihisia, kuna upweke wa aina nyingine unaoweza kutuathiri sana. Hali hiyo hutokea wakati tunapohisi kwamba uhusiano kati yetu na Mungu umedhoofika na kwamba tumetengwa naye.

Je, umewahi kuwa katika yoyote ya hali hizo zilizotajwa? Je, mtu anaweza kushinda hisia za upweke?

[Picha katika ukurasa wa 4]

Mabadiliko maishani, iwe ni kwenda shule mpya au kufiwa na mwenzi, yanaweza kumfanya mtu ahisi upweke