Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mnara wa London Jengo la Ukumbusho la Nyakati za Maasi

Mnara wa London Jengo la Ukumbusho la Nyakati za Maasi

Mnara wa London Jengo la Ukumbusho la Nyakati za Maasi

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI UINGEREZA

HUKO London Mashariki, kwenye kilima kinachokabili Mto Thames, kuna mojawapo ya majengo ya ukumbusho yaliyo maarufu zaidi ulimwenguni, ule Mnara wa London. Kwa karibu miaka elfu moja, wakati wa maasi nchini Uingereza, mnara huo mkubwa ulitumiwa kama ngome, jumba la kifalme, na gereza. Wafalme, malkia, maofisa wa jumba la kifalme, wanadini, wanasiasa, na mahakimu walipitia malango ya mnara huo, baadhi yao wakifurahia ushindi na wengine kwa mara ya mwisho wasionekane tena wakiwa hai. Kwa nini Mnara huo ulijengwa, na ni mambo gani yaliyofanywa humo yaliyoathiri historia ya Uingereza?

Ngome ya Kifalme

Baada ya Mtawala Mdogo William wa Normandy kuvamia Uingereza mnamo mwaka wa 1066, alijenga kasri kadhaa kuwatisha Wasaksoni wakatili wa Uingereza. Jengo kubwa zaidi likajengwa jijini London. Mwanzoni, ngome ya mbao ilijengwa pembeni mwa kuta za kale za Kiroma, upande wa kusini-mashariki, lakini muda si muda jengo kubwa la mawe linaloitwa Mnara Mkuu likajengwa badala yake. Likiwa na umbo la mraba hivi, lenye upana wa meta 32, urefu wa meta 36, na kimo cha meta 27, liliwaogopesha wenyeji wa eneo hilo. Mfalme mmoja aliyetawala baadaye alipoagiza lipakwe chokaa, likaanza kuitwa Mnara Mweupe.

Wafalme waliotawala baadaye walilifanya jengo hilo kuwa mojawapo ya ngome imara zaidi barani Ulaya walipoongeza minara yenye ukubwa mbalimbali, kuta mbili kubwa za kuzingira, na handaki lenye kina kirefu. Ama kweli, nyakati nyingine watawala walijificha nyuma ya kuta za Mnara huo kuwaepuka raia waasi. Wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe, washindi ndio walioumiliki Mnara huo, ambao ulionwa kuwa ishara ya nguvu na mamlaka. Kulipokuwa na amani, msafara wa kumtawaza mfalme mpya ulianzia kwenye Mnara huo. Walipokaa humo, mfalme na watu wake waliishi katika vyumba vilivyopambwa sana, ambamo waliwafanyia rafiki zao karamu kubwakubwa. Hata hivyo, adui za mfalme walitendewa tofauti.

Gereza la Serikali

Yasemekana kwamba mfungwa wa kwanza alifungwa katika Mnara huo mwaka wa 1100, lakini gereza hilo lilikuwa tofauti sana. Lilikuwa gereza la waheshimiwa na watu mashuhuri. Miongoni mwa watu mashuhuri waliofungwa humo ni wafalme wa Scotland na Ufaransa walioshindwa vitani, na maofisa wa serikali na wakuu wa kanisa waliokuwa wamepoteza kibali au kubadilika kuwa wasaliti. Wakati mwingine waliuawa. Henry wa Sita, Edward wa Tano mwenye umri wa miaka 12, na ndugu ya Edward mdogo, waliuawa katika Mnara huo.

Wafungwa waliwekwa popote palipokuwa na nafasi na walikuwa chini ya ulinzi mkali au waliruhusiwa kutembea-tembea ndani ya kasri. Wengine walifungwa kwa muda mfupi na wengine kwa muda mrefu. William Penn, ambaye baadaye alivumbua koloni ya Pennsylvania huko Amerika, alifungwa miezi minane kwa sababu ya imani yake ya kidini. Baada ya kushindwa vitani, Charles, mpwa wa mfalme wa Ufaransa, aliyekuwa Mtawala Mdogo wa Orléans, alifungwa kwa vipindi fulani kwa miaka 25 mpaka fidia yake kubwa ilipolipwa. Sir Walter Raleigh, aliyekuwa ofisa wa jumba la kifalme, mvumbuzi, na mwandishi, alikaa humo kwa miaka 13 akiandika kitabu chake History of the World kabla ya kuachiliwa kwa muda na hatimaye kuuawa.

Mauaji Yaongezeka

Mnara huo ulipata sifa yake ya kuwatesa wafungwa kwa ukatili tangu wakati wa Mageuzi ya Kidini. Henry wa Nane alitaka sana kuwa na mrithi wa kiume, hivyo akajitenga na Kanisa Katoliki na kuanza kuwaua watu waliokataa kumtambua kuwa mkuu wa Kanisa la Anglikana. Mke wake wa pili, Anne Boleyn, alishindwa kupata mwana, naye akakatwa kichwa katika Mnara huo kwa mashtaka ya uasi na uzinzi, pamoja na ndugu yake na watu wengine wanne. Catherine Howard, mke wa tano wa Henry, alikatwa kichwa pia. Zaidi ya hayo, waheshimiwa wengi wa ukoo wa kifalme, walioonwa kuwa tishio kwa serikali, walifungwa katika Mnara huo na kuuawa.

Mwana mchanga wa Henry, Edward wa Sita, ambaye alikuwa Mprotestanti, aliendeleza mauaji hayo alipokuwa mfalme. Alikufa baada ya miaka sita na mahali pake pakachukuliwa na Mary, binti ya Henry, aliyekuwa Mkatoliki mwenye bidii. Bila kukawia, alimkata kichwa Lady Jane Grey aliyekuwa na umri wa miaka 16 na mume wake kijana, waliotumiwa na wengine kupigania mamlaka. Kisha Waprotestanti, walioonwa kuwa adui, wakaanza kuuawa. Elizabeth, dada wa kambo wa Mary, alifungwa kwa majuma mengi katika Mnara huo kisha akaachiliwa, lakini alipotawazwa kuwa malkia aliwatia gerezani na kuwaua wale waliokataa kuacha Ukatoliki au waliopinga utawala wake.

Ingawa maelfu ya watu walifungiwa katika Mnara huo, ni wanawake watano na wanaume wawili tu waliokatwa kichwa humo na kuepuka aibu ya kuuawa hadharani. Kati ya wanawake hao, watatu walikuwa malkia, yaani, Anne Boleyn, Catherine Howard, na Jane Grey, ambaye aliuawa baada ya kutawala siku tisa tu. Watu wengi, hasa wale waliokatwa kichwa, waliuawa mbele ya umati mkubwa wenye fujo kwenye kilima kinachoitwa Tower Hill karibu na Mnara huo. Kichwa kilichokatwa kiliangikwa kwenye Daraja la London ili kuwaonya wengine, nao mwili ukarudishwa kwenye Mnara ili uzikwe chini ya kanisa. Baada ya muda, zaidi ya maiti 1,500 zilizikwa humo.

Wakati mwingine wafungwa waliteswa ili waungame, kwa kawaida baada ya ruhusa kutolewa. Katika mwaka wa 1605, Guy Fawkes, aliyekuwa amejaribu kumlipua mfalme na Bunge katika ile Njama ya Gunpowder, alilazwa kwenye kitanda cha kuwatesea wafungwa katika Mnara huo ili ataje majina ya washiriki wenzake kabla ya kuuawa.

Katika miaka ya 1600, Oliver Cromwell na Wabunge walimiliki Uingereza na Mnara huo kwa muda mfupi, lakini Charles wa Pili aliporudishwa mamlakani, si wafungwa wengi waliopelekwa kwenye Mnara huo. Katika mwaka wa 1747, mtu wa mwisho alikatwa kichwa huko Tower Hill, lakini Mnara ukaendelea kutumiwa kama gereza la serikali. Wakati wa Vita vya Kwanza vya Ulimwengu, majasusi 11 Wajerumani walifungwa humo na kuuawa na kikosi cha wauaji. Katika Vita vya Pili vya Ulimwengu, mateka wa vita walifungwa katika Mnara huo kwa muda mfupi, akiwemo Rudolf Hess, aliyekuwa msaidizi wa makamu wa Hitler. Jasusi Joseph Jakobs ndiye aliyekuwa wa mwisho kuuawa katika Mnara huo, alipofyatuliwa risasi mnamo Agosti 1941.

Askari na Vito

Tangu Mnara huo ulipojengwa, askari wamelinda wafungwa wake na majengo yake. Lakini, katika mwaka wa 1485, mfalme alianza kuwa na askari walinzi. Wakati huo, kwa kawaida wafungwa waliletwa kupitia mtoni na kuingia kwenye Mnara huo kupitia Lango la Traitor. Wakati mfungwa aliporudi baada ya kesi kufanywa, watazamaji walikuwa macho kuona jinsi askari mlinzi aliyeandamana naye alivyokuwa ameshika shoka lake. Ikiwa ubapa wa shoka ulielekezwa kwa mfungwa, hiyo ilimaanisha kifo.

Leo askari walinzi bado hulinda Mnara huo na kuwatembeza wageni wengi wanaotembelea huko. Wakati wa sherehe rasmi wao huvaa sare zao zenye kupendeza, zinazotia ndani kanzu fupi za rangi nyekundu na dhahabu na vazi jeupe la shingoni. Lakini kwa kawaida wao huvalia sare za bluu na nyekundu za enzi ya Victoria. Askari hao huitwa walaji wa nyama ya ng’ombe, jina la utani ambalo huenda walipewa wakati wa njaa. Wakati wakaaji wa London walipokosa chakula, sikuzote askari hao walipewa posho lao la nyama ya ng’ombe ili kuhakikisha kwamba walibaki waaminifu kwa mfalme.

Askari mmoja hutunza kunguru wanaoishi kwenye Mnara huo. Kulingana na ushirikina, inasemekana kwamba msiba unaweza kutokea Uingereza iwapo ndege hao wataondoka kwenye Mnara huo, hivyo mabawa yao hukatwa.

Askari wa Nyumba ya Vito hulinda vito maarufu vya kifalme huko Uingereza, ambavyo vilianza kuonyeshwa umma tangu karne ya 17. Cullinan ya 1 ndiyo almasi kubwa zaidi iliyokatwa yenye thamani kubwa sana ulimwenguni. Almasi hiyo ni mojawapo ya mawe yenye thamani zaidi yanayopatikana katika mataji, vitufe, na fimbo zinazotumiwa hadi sasa na familia ya kifalme.

Wanyama, Sarafu, na Silaha

Mwanzoni mwa karne ya 13, Mfalme John alifuga simba katika Mnara huo, lakini wanyama-mwitu walianza kuhifadhiwa kwa wingi wakati mtawala aliyemfuata, Henry wa Tatu, alipopokea chui watatu, dubu, na tembo kutoka kwa watawala fulani wa Ulaya. Ingawa wanyama hao walikusudiwa kumfurahisha mfalme na watumishi wake, dubu huyo alipoenda kuogelea na kuvua samaki katika Mto Thames akiwa amefungwa kamba, wakaaji wa London walifurahia mandhari hayo. Kadiri miaka ilivyopita, wanyama wengine kutoka nchi nyingine walipelekwa kwenye hifadhi hiyo, na watu wameruhusiwa kuwaona tangu siku za Malkia Elizabeth. Hifadhi hiyo ilifungwa katika miaka ya 1830, wakati wanyama hao walipohamishiwa kwenye Bustani ya Regent iliyokuwa imefunguliwa karibuni huko London.

Kwa zaidi ya miaka 500, ofisi kubwa ya tawi la shirika la kutengeneza sarafu huko Uingereza ilikuwa kwenye Mnara huo. Kulikuwa na kazi nyingi sana huko wakati wa utawala wa Henry wa Nane, wakati ambapo fedha iliyoporwa kutoka kwenye makao ya watawa yaliyokuwa yamefungwa hivi karibuni ilitumiwa kutengeneza sarafu. Hati muhimu za serikali na za kisheria zilihifadhiwa katika Mnara huo, na silaha za mfalme na jeshi lake zilitengenezwa na kuhifadhiwa humo.

Kikumbusho cha Wakati Uliopita

Leo, Mnara wa London ni mojawapo ya mambo yanayowavutia sana watalii nchini Uingereza. Kwa kuwa Mnara huo ungali jinsi ulivyokuwa zamani, si rahisi kutembea kwenye vijia vyake vya mawe na majengo yake ya kijivu yenye kutisha bila kukumbuka jeuri, mateso, na mauaji ya watu yaliyotukia humo kwa karne nyingi. Historia yake mbaya inaonyeshwa vizuri na jukwaa la kukatia vichwa vya wahalifu huko Tower Hill. Bamba dogo linalopatikana huko linatukumbusha ‘historia mbaya, na visa vingi vya mauaji ya watu waliokubali kuhatarisha maisha yao kwa sababu ya imani, nchi, au kanuni zao.’

[Picha katika ukurasa wa 13]

Anne Boleyn

Catherine Howard

Jane Grey

William Penn

[Hisani]

Boleyn and Howard: From the book Heroes of the Reformation, 1904; Grey: From the book The World’s Famous Events; Penn: From the book The Library of Historic Characters and Famous Events, Vol. V, 1895

[Picha katika ukurasa wa 13]

Sehemu ya mnara iliyotumiwa baadaye kama gereza

[Hisani]

Copyright Historic Royal Palaces

[Picha katika ukurasa wa 14]

Askari mlinzi

[Hisani]

Copyright Historic Royal Palaces

[Picha katika ukurasa wa 15]

Baadhi ya vito vya mfalme

[Hisani]

Crown ©/The Royal Collection © 2004, Her Majesty Queen Elizabeth II ▸

[Picha katika ukurasa wa 15]

Sarafu ya fedha ya karne ya 16 inayoonyesha Henry wa Nane

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 12]

Top: © London Aerial Photo Library/CORBIS; inset: Copyright Historic Royal Palaces