Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Tairi Zinaweza Kuathiri Uhai Wako!

Tairi Zinaweza Kuathiri Uhai Wako!

Tairi Zinaweza Kuathiri Uhai Wako!

WAZIA kwamba umefungiwa ndani ya sanduku la mabati yaliyochomelewa na lenye vioo. Asidi na kemikali zinazoweza kuwaka ziko katika vyombo fulani karibu nawe. Kisha inua sanduku hilo hatari sentimeta chache kutoka chini na kuliendesha kwa mwendo wa meta 30 kwa sekunde. Halafu iweke mashine yako pamoja na mashine nyingine zinazofanana nayo na kuzitimua pamoja huku mashine nyingine zikipita kasi upande ule mwingine!

Hivyo ndivyo unavyofanya kila mara unapoingia kwenye gari na kuliendesha. Ni nini ambacho hukusaidia kulidhibiti na kuhisi ukiwa salama unapoliendesha? Hasa ni tairi.

Kazi ya Tairi

Tairi zina kazi nyingi muhimu. Hubeba uzito wa gari lako na kulilinda dhidi ya matuta, mashimo, na matatizo mengine barabarani. Jambo muhimu zaidi ni kwamba tairi hukuwezesha kuongeza mwendo wa gari lako, kuongoza usukani, kupiga breki, na kulielekeza gari mahali unapotaka kwenye barabara mbalimbali. Hata hivyo ni sehemu ndogo tu ya tairi inayogusa chini wakati wowote ule.

Kwa kuwa tairi ni muhimu hivyo, unaweza kufanya nini ili tairi ziendelee kufanya kazi vizuri na kuwa salama? Na utakapofika wakati wa kununua tairi mpya, utachaguaje tairi zinazofaa gari lako? Kabla ya kujibu maswali hayo, hebu tuzungumzie kifupi historia ya tairi.

Wavumbuzi wa Tairi

Ingawa magurudumu yamekuwa yakitumiwa kwa maelfu ya miaka, tairi zilianza kutumiwa karibuni. Tairi zilizotengenezwa kwa mpira wa kiasili ziliunganishwa kwa mara ya kwanza kwenye magurudumu ya mbao au ya chuma mapema katika miaka ya 1800. Lakini, tairi hizo zilikuwa zikichakaa haraka. Kwa hiyo, watu wakapoteza matumaini ya kutumia tairi kwenye magurudumu. Ndivyo mambo yalivyokuwa hadi Charles Goodyear mvumbuzi mwenye azma kutoka Connecticut, Marekani, alipoanza kuchunguza jambo hilo. Mnamo 1839, Goodyear alivumbua mbinu ya kuchanganya mpira na salfa. Mbinu hiyo ilifanya iwe rahisi kutengeneza tairi ambazo zingeweza kudumu kwa muda mrefu zaidi. Tairi ngumu zikaanza kupendwa zaidi ingawa zilifanya safari isiwe yenye kustarehesha.

Mnamo 1845, mhandisi Robert W. Thomson kutoka Scotland alipata kibali cha kutengeneza tairi ya kwanza ya pumzi. Hata hivyo, John Boyd Dunlop wa Scotland alipoboresha tairi za baiskeli ya mwana wake ili aiendeshe kwa starehe zaidi, tairi hizo zikaanza kuuzwa kwa wingi. Mnamo 1888 Dunlop alipata kibali cha kutengeneza tairi zake mpya naye akaanzisha kampuni yake mwenyewe. Hata hivyo, tairi za pumzi zilikabili matatizo makubwa.

Siku moja katika mwaka wa 1891, tairi ya baiskeli ya mwendeshaji mmoja Mfaransa ilitoboka. Alijaribu kuirekebisha lakini akashindwa kwa sababu tairi hiyo ilikuwa imeshikamana na gurudumu. Aliomba msaada wa Mfaransa mwenzake Édouard Michelin, aliyekuwa fundi wa kutengeneza mipira yenye salfa. Michelin alitumia saa tisa kurekebisha tairi hiyo. Tangu hapo akaazimia kutengeneza tairi ya pumzi ambayo ingeweza kutenganishwa na gurudumu na kurekebishwa kwa urahisi.

Tairi za Michelin zilifanikiwa sana hivi kwamba waendeshaji wa baiskeli 10,000 walifurahia kuzitumia mwaka uliofuata. Punde baadaye, tairi za pumzi zikawekwa kwenye magari ya farasi huko Paris na abiria Wafaransa wakazifurahia sana. Ili kuonyesha kwamba tairi za pumzi zingeweza kutumiwa katika magari, mnamo mwaka wa 1895, Édouard na ndugu yake, André, walizitia kwenye gari la mashindano, lakini likawa la mwisho katika mashindano hayo. Hata hivyo, watu walishangazwa sana na tairi hizo za pekee hivi kwamba walijaribu kuzikata ili waone kile ambacho Édouard na André walikuwa wameficha ndani yake!

Katika miaka ya 1930 na 1940, vifaa vipya vyenye kudumu kama vile rayoni, nailoni, na poliesta vilianza kutumiwa badala ya vifaa ambavyo vingeweza kuharibika kwa urahisi kama vile pamba na mpira wa asili. Baada ya Vita vya Pili vya Ulimwengu, jitihada zilifanywa kuvumbua tairi ambayo ingeweza kuziba pumzi isitoke, na hivyo haingehitaji kuwa na tyubu ndani. Baadaye, marekebisho zaidi yakafanywa.

Leo, mali ghafi zaidi ya 200 hutumiwa kutengeneza tairi. Na kwa kutumia tekinolojia ya kisasa, tairi fulani zinaweza kusafiri umbali wa kilometa 130,000 au zaidi, na nyingine zinaweza kustahimili mwendo wa mamia ya kilometa kwa saa katika magari ya mashindano. Wakati huohuo, gharama ya tairi imekuwa ikishuka.

Kuchagua Tairi

Ikiwa una gari, huenda ikawa vigumu kuchagua tairi mpya. Unawezaje kujua kwamba tairi zako zinahitaji kubadilishwa? Kwa kuchunguza tairi kwa ukawaida ili kuona kama zina dalili zozote za kuzeeka au kuharibika. * Tairi hutengenezwa zikiwa na tepe zinazoonyesha ikiwa zimezeeka. Tepe hizo huonekana kwenye uso wa tairi. Pia ni muhimu kuangalia ikiwa tredi zimetengana na tairi, ikiwa kuna nyaya zinazoonekana, ikiwa tairi zimevimba kando-kando, na ikiwa zina matatizo mengine. Ikiwa tairi zina yoyote kati ya dalili hizo, usiendeshe gari hilo mpaka zitakaporekebishwa au kubadilishwa. Iwapo ulinunua tairi mpya, muuzaji anaweza kukuuzia nyingine kwa bei nafuu ikiwa tairi ulizonunua zilikuwa na dhamana.

Inafaa kubadili tairi mbili-mbili, za mbele au za nyuma. Ikiwa unabadili tairi moja tu, iambatanishe na tairi nyingine yenye tredi mpya zaidi ili ishike barabara vizuri unapopiga breki.

Si rahisi kuchagua tairi kwa sababu kuna tairi za aina nyingi, ukubwa, na miundo mbalimbali. Hata hivyo, kwa kuchunguza mambo machache ya msingi, itakuwa rahisi zaidi. Kwanza, soma mapendekezo ya mtengenezaji wa gari lako. Unahitaji kuchunguza mambo fulani hususa kuhusu gari lako, kama vile ukubwa wa tairi na gurudumu, mwanya kati ya gari na barabara, na uzito ambao gari linaweza kubeba. Muundo wa gari lako ni muhimu pia. Magari mengi ya siku hizi yenye mifumo ambayo huzuia magurudumu yasiache kuzunguka na kuanza kuteleza na mfumo unaoyawezesha kwenda kwa magurudumu yote manne, yanahitaji tairi za pekee. Kwa kawaida, maagizo kuhusu tairi hupatikana katika kitabu cha mwongozo cha mtengenezaji wa magari.

Ni muhimu pia kujua hali ya barabara. Je, mara nyingi utaliendesha gari lako kwenye barabara ya vumbi au ya lami, wakati wa mvua au wa kiangazi? Labda wewe huendesha gari lako katika hali mbalimbali. Basi, huenda ukahitaji tairi zinazofaa barabara na hali mbalimbali.

Pia unapaswa kufikiria muda ambao tairi hiyo itadumu na jinsi inavyoshika barabara. Kwa kawaida, tredi ikiwa laini, inashika barabara vizuri lakini inazeeka haraka. Kwa upande mwingine, ikiwa tredi ni ngumu kiasi, tairi haishiki vizuri lakini yaelekea itadumu kwa muda mrefu zaidi. Kwa kawaida ubora wa tairi mbalimbali hupatikana kwenye vitabu vya mauzo kwenye maduka ya tairi. Kumbuka kwamba watengenezaji wa tairi hupima ubora wa tairi zao kwa njia tofauti-tofauti.

Baada ya kuzingatia mambo hayo, huenda sasa uamuzi wako utategemea bei. Kwa kawaida watengenezaji wanaojulikana sana, huuza bidhaa bora na hutoa dhamana kwa ajili ya bidhaa zao.

Kutunza Tairi

Utunzaji unaofaa wa tairi unatia ndani mambo matatu: kuzitia pumzi ya kutosha, kuhamisha kwa ukawaida tairi za mbele na kuzipeleka nyuma na kupeleka za nyuma mbele, kuzisawazisha na kuzinyoosha. Ni muhimu sana kudumisha kiasi kinachofaa cha pumzi. Ikiwa tairi ina pumzi nyingi kupita kiasi, sehemu ya katikati ya tredi itaisha mapema. Kwa upande mwingine, tairi ikiwa na pumzi kidogo sana, sehemu za kandokando za tairi zitazeeka upesi nalo gari litatumia mafuta mengi.

Tairi zinaweza kupoteza nusu kilo ya pumzi au zaidi kila mwezi. Kwa hiyo usidhani unaweza kujua ikiwa tairi zina pumzi ya kutosha kwa kuzitazama. Kulingana na Shirika la Watengenezaji wa Mpira, “tairi inaweza kupoteza nusu ya pumzi na bado mtu asitambue kwa kuitazama!” Kwa hiyo, tumia kifaa cha kupima kiasi cha pumzi, na ufanye hivyo angalau mara moja kwa mwezi. Watu wengi wenye magari hubeba kifaa hicho ndani ya magari yao. Chunguza tairi kila mara unapobadili mafuta ya injini na zikiwa baridi, yaani, baada ya gari kutulia kwa angalau saa tatu au ikiwa gari halijaenda kwa zaidi ya kilometa moja na nusu. Kwa kawaida kiwango kinachofaa cha pumzi ya tairi hupatikana katika kitabu cha mwongozo, kwenye kibandiko karibu na mlango wa dereva, au kwenye kisanduku cha glavu. Ikiwa unataka kusafiri kwa starehe, usijaze pumzi kufikia kiwango cha juu zaidi kinachoonyeshwa kwenye ubavu wa tairi.

Tairi zitadumu muda mrefu na kwisha wakati uleule ikiwa mara kwa mara tairi za mbele zinahamishiwa nyuma na za nyuma kupelekwa mbele. Isipokuwa mtengenezaji wa gari lako apendekeze vingine, kwa kawaida ni vizuri kufanya hivyo kila baada ya kilometa 10,000 hadi 13,000. Unapofanya hivyo, chunguza kitabu cha mwongozo.

Kila mwaka au wakati wowote unapogundua tatizo kwenye usukani au ikiwa usukani unatikisika-tikisika, peleka gari lako ili magurudumu yanyooshwe. Ingawa springi na shokamzoba za gari zinaweza kunyoosha magurudumu kulingana na uzito unaobebwa na gari, inafaa kuchunguza na kunyoosha magurudumu mara kwa mara kwa sababu ya matatizo ya kawaida ya gari. Fundi anayestahili mwenye ustadi wa kurekebisha magurudumu anaweza kudumisha magurudumu ya gari lako yakiwa yamenyooka ili tairi zidumu kwa muda mrefu na safari iwe yenye kustarehesha.

Tairi Zinazobadilika Kulingana na Hali

Magari fulani yenye kompyuta huwaonya madereva wakati ambapo pumzi ya tairi imepungua sana. Tairi fulani zinaweza kuendelea kutumiwa kwa vipindi vifupi bila pumzi, na nyingine hujiziba zinapotoboka. Kwa kweli, wahandisi wanabuni tairi zinazoweza kustahimili hali nyingi.

Kadiri ambavyo mali ghafi za kutengeneza tairi, miundo ya tredi, springi na shokamzoba, usukani, na mifumo ya breki inavyozidi kuboreshwa katika magari ya kisasa, itakuwa rahisi na salama zaidi kuendesha gari.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 15 Ona chati kwenye ukurasa wa 21 upate madokezo ya jinsi ya kuchunguza tairi.

[Chati/Picha katika ukurasa wa 21]

Chati ya Utunzaji wa Tairi

Mambo ya kuchunguza:

❑ Je, ubavu wa tairi umevimba?

❑ Je, nyaya zinaonekana kwenye tredi?

❑ Je, tredi zimeisha?

Pia fikiria:

❑ Je, kiasi cha pumzi kwenye tairi kinapatana na mapendekezo ya mtengenezaji?

❑ Je, ni wakati wa kubadili tairi za mbele ziende nyuma, na za nyuma ziende mbele? (Tumia mapendekezo ya mtengenezaji.)

❑ Je, unahitaji kubadili tairi kwa sababu ya badiliko katika hali ya hewa?

[Picha]

Utepe unaoonyesha kwamba tairi imezeeka

[Mchoro katika ukurasa wa 20]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Sehemu za Tairi

Tredi hushika barabara na kusaidia kupiga kona

Mishipi hutegemeza na kuimarisha tredi

Ubavu wa tairi hulinda tairi isiharibiwe na barabara

Tabaka za tairi huimarisha tairi na kuifanya inyumbulike

Tabaka la ndani huhifadhi pumzi ndani ya tairi

Ukingo hufanya tairi ishikamane kabisa na gurudumu

[Picha katika ukurasa wa 19]

Mojawapo ya baiskeli na magari ya kwanza yenye tairi za pumzi; wafanyakazi katika kiwanda cha tairi cha zamani

[Hisani]

The Goodyear Tire & Rubber Company