Umuhimu wa Mazingira ya Asili
Umuhimu wa Mazingira ya Asili
Hivi majuzi wanasayansi na wataalamu wa uchumi walishirikiana kuchunguza makao matano ya asili yaliyogeuzwa ili yatumiwe na wanadamu na kwa ajili ya biashara. Msitu wa tropiki huko Malaysia uliharibiwa kabisa kwa sababu ya ukataji wa miti kwa ajili ya biashara, msitu wa tropiki huko Kamerun uligeuzwa na kuwa mashamba ya michikichi na miti ya mipira, bwawa la mikoko huko Thailand liligeuzwa ili kufuga uduvi, bwawa la maji huko Kanada lilikaushwa kwa ajili ya kilimo, na tumbawe huko Ufilipino lililipuliwa kwa baruti ili kukamata samaki.
Watafiti hao waligundua mambo ya kushangaza. Ikiwa makao hayo matano ya asili hayangeharibiwa, yangefaidi jamii kwa asilimia 14 hadi 75 zaidi. Mazingira yanapoharibiwa na wanadamu, thamani yake hupungua kwa asilimia 50 kwa wastani, na kila mwaka inagharimu dola bilioni 250 kugeuza mazingira kwa ajili ya biashara. Kwa upande mwingine, kuhifadhi makao ya asili kungegharimu dola bilioni 45. Kulingana na gazeti The Guardian la London, watafiti hao wanasema kwamba “bidhaa na huduma” zinazotolewa na mazingira ya asili, yaani, chakula, maji, hewa, makao, fueli, mavazi, dawa, na ulinzi dhidi ya dhoruba na mafuriko, zina thamani ya angalau dola trilioni 4.4, au faida ya asilimia 100 kwa kila gharama ya asilimia 1. Dakt. Andrew Balmford wa Chuo Kikuu cha Cambridge huko Uingereza, aliyeongoza uchunguzi huo alisema: “Hakuna faida nyingi za kiuchumi. Tulifikiri kwamba kuna faida ya kuhifadhi mazingira, lakini hatukudhani ingekuwa kubwa hivyo.”
Kwa kusikitisha, tangu Kongamano la Dunia la mwaka wa 1992 huko Rio de Janeiro, asilimia 11.4 ya mazingira ya asili ya dunia yamegeuzwa kwa ajili ya matumizi mengine hasa kwa sababu ya kutojua hasara zinazohusika na kwa ajili ya faida za kiuchumi za muda mfupi. Miaka kumi baadaye, kwenye Kongamano la Ulimwengu la Maendeleo Yasiyoharibu Mazingira lililofanywa huko Johannesburg, hakukuwa na masuluhisho tosha ya tatizo hilo. Dakt. Balmford alieleza hangaiko lake aliposema hivi: “Thuluthi moja ya mazingira ya asili ya ulimwengu yametokomea tangu nilipokuwa mtoto, wakati ambapo nilisikia kwa mara ya kwanza kuhusu ‘kuhifadhi mazingira.’ Hilo ndilo jambo linalonitia wasiwasi.”
Hata hivyo, wasomaji wa Biblia wanaweza kupata tumaini katika ahadi ya Muumba kwenye Ufunuo 11:18. Andiko hilo linasema kwamba hivi karibuni ‘atawaharibu wale wanaoiharibu dunia.’ Mazingira ya asili ya dunia yatarudishwa katika hali yake ya awali ili kuwafaidi wanadamu milele.