Kuutazama Ulimwengu
Kuutazama Ulimwengu
Tatizo Linalokabili Bustani za Wanyama
Henning Wiesner, mwanazuolojia mkuu kwenye Bustani ya Wanyama ya Hellabrunn huko Munich, anasema: “Kudhibiti idadi ya wanyama ni muhimu katika kila bustani ya wanyama leo.” Wanyama katika bustani hizo huzaana haraka, watoto wao hukua, na inaonekana wao huishi muda mrefu kuliko wale walio mwituni. Lakini bustani hizo hazina nafasi kubwa. Hivyo idadi ya wanyama inahitaji kudhibitiwa. Hata hivyo, kuna tatizo la “kudhibiti uzazi katika bustani hizo. Wanyama hawapendi jambo hilo,” lasema gazeti la Ujerumani Focus. Kwa mfano, dubu hunusa dawa zilizofichwa kwenye chakula na kuziondoa. Pia, dawa za kumeza zinaweza kuwasababishia wanyama fulani matatizo ya afya, kama vile kansa ya matiti. Njia nyingine ni kuwahasi wanyama, lakini kufanya hivyo kunaweza kusababisha matatizo mengine. Tatizo moja ni kwamba njia hizo ni za kudumu na huenda wanyama hao wakahitajiwa kuzaa wakati ujao. Pili, wanyama waliohasiwa huacha kutokeza homoni za uzazi, na badiliko hilo linaweza kuathiri cheo chao kati ya wanyama wengine wa jamii yao. Njia nyingine ni kuua watoto wasiotakikana, lakini hilo huwachukiza watu wengi wanaowapenda wanyama na mashirika ya kuwahifadhi wanyama. Kwa kweli, bustani za wanyama zinakabili tatizo kubwa.
Vifaa vya Elektroni Vinatupwa
Gazeti National Post la Kanada linasema kwamba tani 155,000 hivi za vifaa vya elektroni zilitupwa na Wakanada katika mwaka wa 2002. Kulingana na ripoti moja ya Shirika la Mazingira la Kanada, inakadiriwa kwamba Wakanada walitupa “televisheni milioni mbili, mashine za video milioni 1.1, na mashine za kucheza CD zipatazo 348,000, na nyingi kati ya hizo zilionwa kuwa hazifai baada ya kutumiwa tu kwa miaka michache.” Ripoti hiyo inasema kwamba vifaa vya elektroni “mara nyingi hutupwa kwa sababu haviwapendezi wanaovitumia, wala si kwa sababu vimeharibika.” Sehemu kubwa ya takataka hizo inaweza kuwa hatari. Kwa mfano, gazeti Post linasema kwamba televisheni moja tu, “inaweza kuwa na kilo mbili hivi za risasi.” Na zebaki, inayopatikana hasa kwenye viwambo fulani vya elektroni, sasa inaharibu maeneo ambapo takataka zimefukiwa. Shirika la Mazingira la Kanada linaonya kwamba mambo yakiendelea hivyo, takataka hizo zitaongezeka maradufu kufikia mwaka wa 2010.
Chungu na Viuavijasumu
Toleo la kimataifa la The Miami Herald linasema, “wanasayansi wamegundua kwamba chungu fulani hukuza uyoga ili kulisha watoto wao, nao hutumia viuavijasumu kulinda mimea yao.” Chungu hao hupanda, hupogoa, na kupalilia mimea yao kama mkulima. Kiuakijasumu kinacholinda mimea yao dhidi ya kuvu yenye kudhuru ni cha jamii ya Streptomycete, nacho hufanyizwa na bakteria inayoishi kwenye ngozi ya nje ya mdudu huyo. Ted Schultz, mtaalamu wa wadudu kwenye Jumba la Makumbusho la Kitaifa la Elimu ya Viumbe huko Washington, D.C., anasema kwamba, ijapokuwa wanadamu hulazimika kuvumbua viuavijasumu vipya kila wakati ili kuua viini sugu, chungu hao wamekuwa wakitumia kiuakijasumu kilekile kwa mafanikio kwa miaka mingi sana. Schultz anasema kwamba kuelewa siri ya chungu hao “kunaweza kuwa muhimu sana kwa maisha ya wanadamu.”
Tatizo Kubwa la Afya Ulimwenguni
Kulingana na Profesa mmoja wa Uingereza, Sir George Alberti, ambaye ni msimamizi wa Shirika la Kimataifa la Ugonjwa wa Kisukari, karibuni ulimwengu utakabili “mojawapo ya matatizo makubwa ya afya” yaliyopata kutukia kwa sababu ya ongezeko kubwa la ugonjwa wa kisukari. Gazeti Guardian la Uingereza linaripoti kwamba, kulingana na shirika hilo, zaidi ya watu milioni 300 ulimwenguni wana tatizo la kumeng’enya glukosi ifaavyo, ambalo mara nyingi husababisha ugonjwa wa kisukari. Ugonjwa wa kisukari wa Aina ya 2 ambao ulikuwa unawapata watu wazima hasa, sasa unawaathiri vijana wa Uingereza ambao wamekuwa wanene kupita kiasi kwa sababu ya kutofanya mazoezi na kula vyakula visivyofaidi mwili. Alberti anasema: “Jambo la kuhuzunisha zaidi ni kwamba visa vingi [vya kisukari na madhara yake] vinaweza kuzuiwa kwa kubadili mtindo wa maisha.” Kulingana na gazeti la The Guardian, huenda ugonjwa wa kisukari ukaongezeka katika nchi zinazoendelea kwa kuwa watu wanaiga mazoea ya kula “vyakula visivyofaidi mwili na mitindo ya maisha ya nchi zenye utajiri.”
Badiliko Katika Familia za Italia
Kuanzia mwaka wa 1995 hadi 2001, idadi ya watu wanaoishi pamoja bila kuoana huko Italia iliongezeka karibu maradufu, idadi ya watu waliofunga ndoa ilipungua, na idadi ya watu wanaoishi peke yao iliongezeka. Uchunguzi huo uliochapishwa katika gazeti La Repubblica, unategemea habari zilizokusanywa na Taasisi ya Kitaifa ya Takwimu ya Italia. Katika kipindi hichohicho, idadi ya wastani ya washiriki wa familia ilipungua kufikia washiriki 2.6 tu. Kulingana na taasisi hiyo, watu wengi wanaamua kuishi pamoja bila kufunga ndoa kwa “kipindi cha majaribio” wakikusudia kufunga ndoa baadaye.
Hisi za Bundi za Pekee
Gazeti Australian Geographic linaripoti kwamba bundi ndio “wanyama wanaoona vizuri zaidi usiku” hasa kwa sababu wana macho makubwa na wanayatumia yote mawili kuona. Na wengi wao “wanaweza kusikia sauti za chini sana, mara 10 ya uwezo wa kusikia wa wanadamu.” Ni nini kinachowawezesha kusikia vizuri hivyo? Makala hiyo inasema: “Ijapokuwa wanatofautiana, jamii mbalimbali za bundi zina masikio yasiyo ya kawaida kwani sikio moja huwa juu kuliko lingine.” Mpangilio huo wa masikio humsaidia bundi kutambua kwa urahisi windo linalosonga. Bundi wa jamii ya Tyto wana uwezo mkubwa zaidi kwa kuwa wana manyoya usoni. Manyoya hayo yanayoweza kunyumbulika hunasa sauti na kuielekeza sikioni. Isitoshe, medula ya bundi, ile sehemu ya ubongo inayohusiana na uwezo wa kusikia, ni tata kuliko ya ndege wengine.
Maambukizo ya Ini Yanayoweza Kuepukwa
Mengi ya “maambukizo ya mchochota wa ini hutokana na uchafu wa wafanyakazi wa hospitali,” lasema gazeti Polityka la Poland. Mnamo mwaka wa 1997, Taasisi ya Kitaifa ya Afya huko Poland iliripoti maambukizo 992 ya hepatitis C (aina fulani ya mchochota wa ini), lakini miaka mitano baadaye idadi hiyo ilifikia 1,892. Mwandishi wa makala hiyo alilalamika kwamba hakuna chanjo halali ya ugonjwa huo kufikia sasa. Profesa Andrzej Gładysz, mtaalamu wa kitaifa wa magonjwa ya kuambukiza, anasema: “Hatutii chumvi tunaposema kwamba nchini Poland watu 500 elfu hadi 600 elfu wameambukizwa virusi vya hepatitis C.” Na mengi ya maambukizo hayo ‘hutokea katika ofisi za madaktari wa meno na madaktari wengineo,’ anasema Jacek Juszczyk wa Kliniki ya Magonjwa ya Kuambukiza kwenye Chuo Kikuu cha Kitiba huko Poznan. Gazeti Polityka linatoa kauli hii: “Tunapokuwa mikononi mwa daktari, tungependa kuwa na hakika kwamba mikono yake ni safi kabisa.”
Ongezeko la Mitaa ya Mabanda
Gazeti El Universal la Mexico City linasema kwamba “watu wapatao bilioni moja, yaani asilimia 32 ya wakaaji wa majiji ulimwenguni, huishi katika maeneo ya umaskini mijini.” Uchunguzi wa Umoja wa Mataifa unataja Bogotá, Havana, Mexico City, Quito, na Rio de Janeiro kuwa mifano ya majiji yenye ongezeko la mitaa ya mabanda. Ni nini kinachosababisha hali hiyo? Kulingana na ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa, ongezeko la mitaa ya mabanda huko Bogotá limesababishwa na “ongezeko la haraka la idadi ya watu, idadi kubwa ya watu wanaohama kutoka mashambani, na jeuri ambayo imeacha jamii nzima-nzima bila makao,” lasema gazeti hilo. Isitoshe, asilimia 23 ya wakaaji wa jiji hilo walihesabiwa kuwa maskini mwaka wa 2000 ikilinganishwa na asilimia 19.4 mwaka wa 1994.