Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Safari ya Mwisho ya Ndege ya Concorde

Safari ya Mwisho ya Ndege ya Concorde

Safari ya Mwisho ya Ndege ya Concorde

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI UFARANSA

Baada ya kuwahudumia watu kwa miaka 27, Concorde—“ndege ya abiria inayoenda kasi zaidi”—imeacha kutumiwa. Shirika la British Airways liliondoa ndege zake saba za mwisho za Concorde mnamo Oktoba 2003, kwa sababu ya kuongezeka kwa gharama na kupungua kwa idadi ya wateja. Miezi mitano mapema, Air France, ambalo ndilo shirika lingine pekee lenye ndege za Concorde, ambazo huwa na mabawa yenye umbo la pembetatu, lilikuwa limeondoa ndege zake tano.

Hivyo, huo ndio uliokuwa mwisho wa enzi ya ndege hizo iliyoanza mwaka wa 1962, wakati wahandisi Waingereza na Wafaransa walipoungana kubuni ndege inayosafiri masafa marefu kwa kasi sana. Ndege za majaribio zilitumiwa kwa mara ya kwanza mwaka wa 1969, na mnamo Januari 1976, watu wakaanza kusafiri kwa Concorde wakati ambapo zilianza kwenda Bahrain na Rio de Janeiro.

Ingawa kubuniwa kwa Concorde kulionwa kuwa hatua kubwa ya teknolojia, ndege hiyo haikutia fora kibiashara. Matatizo ya mafuta katika miaka ya 1970 yalisababisha hasara kubwa, kwa kuwa Concorde moja hutumia zaidi ya lita 25,600 za mafuta kwa saa—mara tatu ya kiasi cha mafuta kinachotumiwa na ndege ya kawaida kwa wastani wa kila abiria. Pia, Concorde ingeweza kusafiri tu kilometa 6,900 na kubeba abiria 100 tu. Hivyo, ndege hiyo haikufaidi mashirika ya ndege. Jambo lingine lililozuia ndege hiyo isitie fora ni upinzani uliozuka wakati ilipoanza kutumiwa Marekani, hasa kwa sababu ya kelele.

Tatizo lingine ni nauli. Tiketi ziligharimu maelfu ya dola. Kwa hiyo, ni abiria wachache tu walioweza kusafiri kwa Concorde. Kulingana na mfanyabiashara mmoja, Concorde “ndiyo aina bora zaidi ya usafiri ambayo mtu angeweza kupata” kwa sababu ya milo ya hali ya juu na divai bora iliyoandaliwa. “Faida yake kubwa zaidi ilikuwa kuokoa wakati. Haikuwa safari yenye kustarehesha sana. Lakini ilisisimua sana.”

Kuvuka Atlantiki Haraka Sana

Zilipokuwa zikitumika, Concorde zilisafirisha abiria wapatao milioni nne. Hiyo si idadi kubwa tukizingatia kwamba ndege zote ulimwenguni aina ya Boeing 747 husafirisha idadi hiyo ya abiria kwa majuma kadhaa tu. Basi, ni nini kilichofanya Concorde iwe ndege ya kuvutia sana?

Fikiria jambo hili: Concorde ilikuwa ikisafiri kilometa 2,150 kwa saa—mara mbili kuliko mwendo wa sauti—ikiwa kwenye urefu wa meta 18,000. Ndege hiyo yenye urefu wa meta 62 ilisafiri haraka sana hivi kwamba ilipanuka kwa karibu sentimeta 24 ilipokuwa hewani kwa sababu ya joto lililosababishwa na msuguano. Kwa kawaida, safari ya kutoka Paris hadi New York kwa Concorde ilichukua saa 3 na dakika 55 tu, karibu nusu ya wakati uliotumiwa na ndege za kawaida. Ilisafiri kwa kasi sana hivi kwamba, kwa sababu ya tofauti ya wakati kati ya maeneo mbalimbali, abiria waliosafiri kutoka Paris walifika New York kabla ya saa walizoondoka Paris!

Historia ya Concorde ilitiwa doa na msiba mmoja tu. Mnamo Julai 25, 2000, ndege ya Air France ilianguka ilipokuwa ikiondoka Uwanja wa Ndege wa Charles de Gaulle huko Paris na kuwaua watu 113, kutia ndani watu 4 waliokuwa chini. Baada ya ndege hizo kurekebishwa ili ziwe salama, zilianza kutumiwa tena mwaka uliofuata. Lakini, hatimaye ilibidi ndege hizo ziache kutumiwa kwa sababu ya matatizo ya kifedha.

Ndege ya Concorde, ambayo haina kifani, itawekwa katika majumba ya ukumbusho ya ndege ulimwenguni. Jean-Cyril Spinetta, mwenyekiti wa Air France, anaeleza hivi: “Concorde haitasahaulika, kwa kuwa itaendelea kusafiri katika akili za watu.”

[Picha katika ukurasa wa 26]

Juu: Divai inaandaliwa

Katikati: Rubani mkuu akiwa katika chumba chake

Chini: Concorde ya majaribio, huko Ufaransa, mwaka wa 1968

[Hisani]

All photos except prototype: NewsCast; prototype: AFP/Getty Images