Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Bia—Hadithi ya Kinywaji Chenye Rangi ya Dhahabu

Bia—Hadithi ya Kinywaji Chenye Rangi ya Dhahabu

Bia—Hadithi ya Kinywaji Chenye Rangi ya Dhahabu

Na mwandishi wa Amkeni! katika Jamhuri ya Cheki

MARA nyingi mtu mwenye kiu sana hutamani nini? Katika nchi nyingi, awe ni kibarua au mfanyabiashara, huenda akatamani kunywa glasi ya kinywaji akipendacho chenye rangi ya dhahabu. Huenda akawazia povu lake jeupe na ladha yake chungu yenye kuburudisha. Kisha anaweza kusema, ‘Hakuna kitu kizuri kama bia baridi!’

Bia imekuwapo karibu muda wote wa maisha ya mwanadamu. Imependwa na watu wengi kwa maelfu ya miaka, na katika maeneo mengi imekuwa sehemu muhimu ya utamaduni. Kwa kusikitisha, bia imewasababishia matatizo wale wanaoitumia kupita kiasi, hasa katika nchi fulani za Ulaya. Hata hivyo, ubora na ladha yake ya kupendeza inaweza kufurahisha sana ikitumiwa kwa kiasi. Hebu tuchunguze historia ya kinywaji hicho kinachopendwa sana.

Bia Ilianza Kutengenezwa Lini?

Kulingana na mabamba ya kikabari yaliyopatikana katika maeneo ya Wasumeria wa kale huko Mesopotamia, bia ilikuwako huko tangu milenia ya tatu K.W.K. Wakati huo, kinywaji hicho kilitumiwa pia na Wababiloni na Wamisri. Hata Sheria ya Hammurabi ilitumiwa kuelekeza utayarishaji wa bia huko Babiloni, ambapo aina 19 za bia zilitengenezwa. Kwa mfano, sheria hiyo ilionyesha bei ya bia, na kama mtu angeikiuka, angeuawa. Katika Misri ya kale, utayarishaji wa pombe ulienea sana, na bia ilipendwa sana. Akiolojia imegundua maandishi ya zamani zaidi kuhusu utayarishaji wa bia huko Misri.

Hatimaye, ustadi wa kutayarisha bia ukaenea hadi Ulaya. Mwanzoni mwa Wakati Wetu wa Kawaida, baadhi ya wanahistoria Waroma walitaja kwamba bia ilipendwa na Waselti, Wajerumani, na makabila mengine. Maharamia wa Ulaya Kaskazini waliamini kwamba vikombe vya mashujaa wa vita vilifurikwa kwa bia huko Valhalla, yaani jumba ambalo walienda baada ya kufa linalotajwa katika hekaya za kwao.

Katika Zama za Kati, mara nyingi bia ilitengenezwa katika makao ya watawa huko Ulaya. Watawa wa kiume waliboresha ustadi huo kwa kutumia mihopi ili kuhifadhi bia. Kutokana na maendeleo ya kiviwanda ya karne ya 19, mashine zilianza kutumiwa kutayarisha pombe na hiyo ikawa hatua muhimu katika historia ya bia. Kisha, uvumbuzi muhimu sana wa kisayansi ukafanywa.

Mwanasayansi Mfaransa wa kemia na mikrobiolojia, Louis Pasteur, aligundua kwamba hamira inayosababisha uchachishaji wa bia ina vijiumbe hai. Ugunduzi huo ulifanya iwe rahisi kuchachisha sukari iliyo kwenye mchanganyiko wa nafaka na maji na kuifanya kuwa pombe. Mtaalamu wa mimea kutoka Denmark, Emil Christian Hansen akawa maarufu sana katika utengenezaji wa pombe. Alitumia maisha yake kufanya utafiti kuhusu aina mbalimbali za hamira na kuziainisha katika vikundi mbalimbali. Utafiti wake, ulizingatia hasa uzalishaji wa aina fulani ya hamira ambayo ingetumiwa katika utengenezaji wa pombe. Kwa kufanya hivyo, Hansen akabadili sana utengenezaji wa pombe.

Lakini je, kutengeneza bia ni kazi ngumu sana? Huenda usiamini, lakini ni kibarua kigumu sana. Hebu tuchunguze kidogo mambo yanayohusika katika kutengeneza bia.

Jinsi Bia Inavyotengenezwa

Utaratibu wa kutengeneza bia umebadilika sana kwa karne nyingi na hata leo viwanda vya kutengeneza bia hutayarisha bia kwa njia tofauti-tofauti. Hata hivyo, karibu bia zote hutengenezwa kwa vitu vinne: shayiri, mihopi, maji, na hamira. Utengenezaji wa bia unaweza kugawanywa kwa sehemu nne: kutengeneza kimea, kutengeneza kinywaji kitamu, kuchachisha, na kuikoleza.

Kutengeneza kimea. Katika hatua hii, shayiri hutenganishwa, hupimwa, na kuondolewa taka. Baadaye, inaloweshwa katika maji ili kuiwezesha kuota. Uotaji unachukua kati ya siku tano hadi saba katika halijoto ya nyuzi 14 hivi Selsiasi. Hatua hiyo hutokeza kimea, ambacho huingizwa kwenye majoko maalumu ili kikaushwe. Mvuke ulio katika kimea hupunguzwa kufikia asilimia 2 hadi 5 ili kukomesha uotaji. Baada ya kukaushwa, miche iliyoota huondolewa kwenye kimea, kisha kimea husagwa. Sasa kimea kiko tayari kwa ajili ya hatua inayofuata.

Kutengeneza kinywaji kitamu. Kimea kilichosagwa huchanganywa na maji na kupashwa joto polepole. Halijoto inapofikia kiwango fulani, vimeng’enya huanza kubadili wanga kuwa sukari rahisi. Hatua hiyo huchukua zaidi ya saa nne na hutokeza kinywaji kitamu, ambacho huchujwa ili kuondoa makapi. Kisha kinywaji hicho huchemshwa ili kukomesha utendaji wa vimeng’enya. Kinywaji hicho kinapochemshwa, mihopi huongezwa ili kutokeza ladha chungu ya bia. Baada ya kuchemshwa kwa saa mbili hivi, kinywaji hicho hupozwa kufikia halijoto inayohitajika.

Uchachishaji. Huenda hii ndiyo hatua muhimu zaidi ya utengenezaji wa bia. Hamira hutumiwa kubadilisha sukari rahisi zilizo katika kinywaji kitamu kuwa kileo na kaboni-dioksidi. Muda wa kuchachusha, ambao hauzidi juma moja, na halijoto inayohitajiwa hutegemea aina ya bia inayotengenezwa. Bia hiyo ambayo haijawa tayari kabisa huhamishiwa kwenye matangi yaliyo katika hifadhi ya bia ili ikolee.

Kukoleza. Katika hatua hii, bia hupata ladha na harufu yake, nayo kaboni-dioksidi huifanya iwe na povu. Hatua hii huchukua kati ya majuma matatu na miezi michache, ikitegemea aina ya bia. Hatimaye, bia iliyo tayari hutiwa katika mapipa au chupa na kusafirishwa—na huenda mwishowe itafika nyumbani kwako! Lakini ungependelea bia gani?

Kuna Aina Nyingi za Bia

Ukweli ni kwamba aina za bia hutofautiana sana. Kuna bia zenye rangi nyangavu au nyeusi, tamu au chungu, na bia zilizotengenezwa kwa shayiri au ngano. Ladha ya bia hutegemea mambo mengi, kama vile maji yaliyotumiwa, aina ya kimea, utaratibu uliotumiwa, na hamira.

Mojawapo ya bia maarufu zaidi ni pilsner, ambayo ina rangi hafifu. Viwanda vingi ulimwenguni hutengeneza bia hiyo. Hata hivyo, pilsner halisi hutengenezwa tu katika mji wa Plzeň, au Pilsen, katika Jamhuri ya Cheki. Ubora wake hautokani tu na utaratibu wa kuitengeneza bali pia mali ghafi zinazotumiwa kama vile, maji yasiyo na madini, kimea cha hali ya juu, na hamira inayofaa.—Ona sanduku.

Bia nyingine bora ni bia ya weiss, ambayo hutengenezwa kwa ngano na inapendwa sana nchini Ujerumani. Waingereza wanapenda bia ya porter na stout. Bia ya porter hutengenezwa kwa hamira inayoinuka na kimea kilichochomwa ambacho huifanya iwe nyeusi. Bia hiyo ilitengenezwa kwa mara ya kwanza huko London katika karne ya 18. Mwanzoni, ilikusudiwa kwa ajili ya watu waliofanya kazi ngumu, kama vile wachukuzi wa mizigo. Bia ya stout, iliyo nyeusi sana na nzito, ilipata umaarufu wake nchini Ireland na ulimwenguni kupitia familia ya Guinness na inatofautiana na bia ya porter. Unaweza kujaribu bia tamu ya stout ya Uingereza ambayo kwa kawaida huwa na laktosi (sukari ya maziwa), au stout ya Ireland ambayo ni chungu na ina kileo kingi.

Watu wengi wanaopenda bia huzingatia jinsi itakavyonywewa, iwe ni kutoka kwenye chupa, mkebe, au pipa. Wamarekani hupenda bia baridi sana. Wengine huipendelea ikiwa na halijoto ya nyuzi 20 hivi Selsiasi au ikiwa baridi kidogo na ikiwa imeandaliwa moja kwa moja kutoka kwenye mapipa ya bia.

Kwa kweli, kuna aina nyingi za bia. Huenda ukapata faida fulani za kiafya ukinywa bia kwa kiasi. Kwa hakika, bia ina vitamini na madini muhimu kama vile riboflavini, asidi ya foliki, kromiamu, na zinki. Kulingana na wataalamu fulani, kutumia bia kwa kiasi kunaweza kuzuia ugonjwa wa moyo na magonjwa ya ngozi. Huenda ukafurahia kinywaji hiki kitamu na kinachoburudisha ikiwa utachagua bia inayofaa kati ya aina nyingi za bia zilizopo na ikiwa utaitumia kwa kiasi. Kwa hiyo, utakapokunywa kinywaji hicho chenye rangi ya dhahabu na povu jeupe, kumbuka hadithi yake yenye kupendeza!

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 13]

Watengenezaji Maarufu wa Bia

Zamani, wataalamu wengi walishiriki kutengeneza bia. Wafuatao ni baadhi yao.

Mtengenezaji wa kimea—ndiye mhusika wa kwanza katika utengenezaji wa bia. Alifanya kazi ya kutengeneza kimea kutokana na shayiri au ngano. Alisimamia uotaji wa nafaka na kukausha kimea. Alikuwa na wajibu mzito, kwani ladha ya bia inategemea sana ubora wa kimea.

Mtengenezaji wa kinywaji kitamu (aliyeonyeshwa juu)—ndiye aliyesimamia hatua ya kuchemsha. Kwanza, alichanganya maji na kimea kisha kilipokuwa kikichemshwa aliongeza mihopi na hivyo kutokeza kinywaji kitamu.

Msimamizi wa hifadhi—alikuwa mtaalamu aliyechachusha bia katika matangi na kuikoleza katika hifadhi. Baadaye, alitia bia iliyo tayari katika vyombo vidogo.

[Hisani]

◀ S laskavým svolením Pivovarského muzea v Plzni

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 14]

Pilsner—Ni Bia Iliyoigizwa Sana

Bia hiyo ilianza kutengenezwa mwaka wa 1295. Mfalme wa Bohemia, Wenceslas wa Pili, alianzisha mji wa Plzeň, na muda mfupi baadaye aliwapa raia 260 wa mji huo kibali cha kutengeneza bia. Mwanzoni, raia hao walitengeneza bia kidogo nyumbani kwao, lakini baadaye walianzisha vyama na viwanda vya bia. Hata hivyo, baada ya muda, uchumi na utamaduni wa Bohemia ulizorota, na hilo likaathiri utengenezaji wa bia. Watengenezaji hao walitumia ustadi wao wenyewe na kupuuza ustadi uliotumiwa tangu kale, na hivyo mara nyingi wakatokeza kinywaji chenye ladha mbovu sana ambacho hakikustahili kuitwa bia.

Wakati huohuo, aina mbili za bia zilikuwa zikitokezwa huko Ulaya. Huko Bohemia hasa, bia ilitengenezwa kwa hamira inayoinuka, hali huko Bavaria bia ilitengenezwa kwa hamira inayoshuka, nayo ilikuwa bora zaidi. Kulikuwa na tofauti kubwa kati ya bia za Bavaria na zile za Plzeň.

Badiliko kubwa lilitokea mwaka wa 1839. Wakazi 200 hivi wa Plzeň waliamua kurekebisha hali hiyo. Walianzisha Kiwanda cha Bia cha Burgess, ambacho kilitengeneza tu bia ya hamira inayoshuka, au ile bia ya Bavaria. Mtengenezaji wa bia maarufu, Josef Groll, aliitwa kutoka Bavaria. Alianza mara moja kutengeneza bia ya Bavaria. Matokeo yalikuwa tofauti kabisa lakini yalikuwa bora kuliko alivyotazamia. Ujuzi wa Groll na mali ghafi bora alizotumia zilitokeza bia iliyopendwa sana ulimwenguni. Kwa nini? Kwa sababu ya ladha yake yenye kupendeza, rangi yake, na harufu yake. Hata hivyo, ubora wa bia ya Plzeň ulikuwa na matatizo yake. Watengenezaji wengi wa bia waliotaka kujinufaisha kutokana na bia hiyo bora walianza kuita bia zao pilsner. Hivyo pilsner haikuwa tu bia maarufu bali pia ikawa bia iliyoigwa zaidi.

[Picha]

Josef Groll

Mnara wa maji kwenye kiwanda cha bia cha Plzeň

[Hisani]

S laskavým svolením Pivovarského muzea v Plzni

[Ramani katika ukurasa wa 12]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Plzeň

[Picha katika ukurasa wa 12, 13]

Picha ya Kimisri inayoonyesha utengenezaji wa mkate na bia

[Hisani]

Su concessione del Ministero per i Beni e le Attività Culturali - Museo Egizio - Torino

[Picha katika ukurasa wa 15]

Mihopi, kimea, na kiwanda cha bia