Daraja la Pekee Lililobadilisha Kisiwa
Daraja la Pekee Lililobadilisha Kisiwa
Na mwandishi wa Amkeni! nchini Kanada
KISIWA cha Prince Edward chenye umbo la mwezi, ambacho ni mkoa mdogo zaidi nchini Kanada, kiko katikati ya Ghuba ya St. Lawrence kwenye Pwani ya Atlantiki ya Kanada. Mvumbuzi Mfaransa wa karne ya 16, Jacques Cartier, alikifafanua kuwa “nchi bora zaidi iliyopata kuonekana.” Kisiwa cha Prince Edward chenye wakazi zaidi ya 130,000 kinajulikana kwa fuo zake maridadi, viazi vinavyokuzwa katika udongo mwekundu wenye rutuba, na kamba-mti wanaovuliwa kwenye fuo zake. Katika mwaka wa 1873, kisiwa hicho kilifanywa kuwa sehemu ya Kanada, na Daraja la pekee la Confederation likajengwa karne moja baadaye ili kukiunganisha na bara. Daraja hilo limekuwa na matokeo gani kwa kisiwa hicho na wakazi wake?
Kisiwa cha Prince Edward kimetenganishwa na bara kwa eneo dogo la maji, lenye upana wa kilometa 13 hivi mahali ambapo maji yamepungua sana. Hata hivyo, Mlango-Bahari wa Northumberland wenye urefu wa kilometa 300 umewafanya wakazi wa kisiwa hicho, ambao wanapenda sana historia yao, kilimo, na utulivu wa kisiwa hicho kilicho kama bustani, wahisi kwamba wanaishi katika mahali pa pekee.
Mnamo Novemba 1996, kisiwa hicho kiliunganishwa na bara wakati Daraja la Confederation lilipokamilika. Daraja hilo lilifunguliwa rasmi mnamo Mei 31, 1997. Tangu wakati huo, wakazi na wageni wa kisiwa hicho wameweza kuvuka mlango-bahari huo kwa gari kwa muda wa dakika 12 hivi, na hivyo kufurahia kutembelea kisiwa hicho wakati wote wa mwaka.
Lakini ni nini kinachowavutia watu kwenye kisiwa hicho cha mbali? Sababu inapatikana katika kichwa cha kitabu—Anne of Green Gables! Mwandishi wa kitabu hicho maarufu, Lucy Maud Montgomery, (mwaka wa 1874 hadi 1942), alitoka Cavendish, na nyumba yake ingali hapo. Kila mwaka wakati wa kiangazi, zaidi ya watalii 200,000 hutembelea eneo hilo.
Kwa Nini Linasemwa Kuwa Daraja la Pekee?
Leo ulimwenguni kote kuna madaraja mengi makubwa yenye kustaajabisha. Basi, kwa nini daraja hilo linaonwa kuwa la pekee? Ingawa si daraja refu zaidi ulimwenguni, inasemekana kwamba hilo ndilo “daraja refu zaidi linalopita juu ya maji ya barafu” katika majira ya baridi kali.
Mara nyingi, Mlango-Bahari wa Northumberland huwa na barafu katika miezi mitano ya majira ya baridi kali, kwa hiyo daraja hilo limejengwa kustahimili hali ngumu. Kwenye bara, daraja hilo huanza kwenye Kisiwa cha Jourimain, New Brunswick. Kisha linapita mlango-bahari na kufika kwenye ufuo wa kusini-magharibi wenye mawe-mchanga wa Kisiwa cha Prince Edward karibu na kijiji kidogo cha Borden. Je, uko tayari kusafiri kupitia barabara hiyo yenye upana wa meta 11 na yenye njia mbili za magari? Kwa sababu hairuhusiwi kutembea wala kuendesha baiskeli kwenye daraja hilo, abiria na waendeshaji wa baiskeli husafirishwa kwa magari. Mahali ambapo meli hupita, daraja hilo limeinuka kwa meta 60 juu ya maji, urefu unaolingana na jengo la orofa 20. Kwa nini limeinuka sana hivyo? Hilo huwezesha meli kupita chini katika sehemu ya katikati ya daraja hilo.
Lilijengwa kwa Kufikiria Mazingira
Mradi mkubwa wa ujenzi kama huo unahusisha bima ya hali ya juu na mipango ya kuhifadhi mazingira. Jambo lililohitaji uangalifu wa pekee ni jinsi daraja hilo lingeathiri mtiririko wa barafu kwenye mlango-bahari katika majira ya kuchipua. Kuongezeka kwa barafu kungeathiri sana ardhi, makao ya viumbe wa majini, na vilevile uvuvi. Hata takataka zilizo chini ya bahari zilihamishiwa kwenye maeneo maalumu ili kufanyiza makao mapya ya kamba-mti.
Vifaa vya shaba nyekundu vya kuzuia barafu vyenye umbo la pia, ambavyo viliwekwa pande zote za nguzo za daraja, ni muhimu. (Ona picha, ukurasa wa 18.) Ni vya kazi gani? Barafu inayosonga inaposukuma vifaa hivyo, inainuka juu hadi inapovunjika kwa sababu ya uzito. Kisha inaanguka majini na kuteleza kwenye upande wowote wa nguzo. Ili kuzuia barafu isirundamane katika mlango-bahari, nguzo hizo zimepigiliwa kwenye miamba na kutenganishwa kwa meta 250 hivi.
Ugumu wa Kutengeneza Daraja Hilo
Visehemu vya daraja vina ukubwa wenye kustaajabisha. Sehemu kubwa nne za daraja ni (1) msingi wa nguzo, ambao uko katika sakafu ya mlango-bahari na umeinuka juu ya maji, (2) nguzo, iliyounganishwa na msingi, (3) mhimili, ambao uko juu ya nguzo, na (4) visehemu vya kuunganisha mihimili. (Ona picha iliyo juu.) Wafanyakazi 6,000 walihusika katika ujenzi huo, na zaidi ya asilimia 80 ya ujenzi huo ulifanyiwa ufuoni “kwenye eneo la ekari 150.” Kisha visehemu vya daraja vilisafirishwa kutoka ufuoni hadi majini na kuunganishiwa huko.
Mhimili uliokamilika una urefu wa meta 192 hivi. Huenda ukauliza, ‘Kitu kikubwa hivyo kinawezaje kusogezwa?’ Inawezekana kwa kutumia kifaa cha kusogezea. Ukitazama kifaa hicho kinapotumiwa, utakifananisha na chungu anayebeba kitu kinachozidi ukubwa wake mara nyingi. Kwa kweli, kubeba mhimili mmoja wenye uzito wa tani 7,500 ni kazi ngumu sana! Kifaa hicho cha kusogezea kilisonga kwa meta tatu tu kila dakika juu ya kijia cha chuma. Kwa sababu ya mwendo huo wa polepole sana vifaa viwili vya kusogezea vilivyotumiwa viliitwa Kasa na Kamba-Mti!
Kwa kuwa vifaa hivyo vingeweza kutumika tu kwenye nchi kavu, kreni yenye viunzi viwili iliyoelea majini, yenye kimo cha meta 102, ilitumiwa. Ripota mmoja alisema kreni hiyo “ina sura mbaya sana, kwani ina shingo ndefu sana na miguu mikubwa ya kutisha” lakini “inasonga kwa madaha kama bata-maji.” Kreni hiyo ilitengenezwa mwaka wa 1990 ili itumiwe katika ujenzi wa daraja lililo kati ya kisiwa cha Funen na Zealand huko Denmark, kisha ikaunganishwa tena na kusafirishwa kutoka Dunkerque, Ufaransa. Kwa kushangaza, kreni hiyo “inaweza kubeba ndege 30 aina ya Boeing 737 na inaweza kusonga upesi baharini.” Kwa kuongozwa na kifaa cha kupokea habari kutoka kwenye setilaiti, kreni hiyo iliweka mihimili na vile visehemu vingine vya daraja hilo kwa usahihi sana.—Ona picha.
Daraja Hilo Limebadilishaje Kisiwa Hicho?
Daraja hilo jipya limeleta maendeleo. Hata hivyo, watu fulani wanahangaikia jinsi mambo yatakavyokuwa wakati ujao. Ingawa miaka saba imepita tangu daraja hilo lilipoanza kutumiwa, ni mapema mno kutabiri matokeo kamili ya daraja hilo, hasa kwa mazingira. Katika mwaka wa 2002, mwanasayansi wa kamba-mti aliripoti kwamba daraja hilo halikuwa limeathiri idadi ya kamba-mti. Pia alisema: “Kumekuwa na ongezeko la kaa katika miaka mitano iliyopita.” Utalii umekuwa na matokeo gani?
Kulingana na ripoti moja, hivi majuzi biashara ya utalii iliongezeka sana kwa “asilimia 61.” Bila shaka, watalii wengi huja katika majira ya kiangazi. Zaidi ya hilo, bidhaa zinazouzwa nje ziliongezeka maradufu kati ya mwaka wa 1996 na 2001. Nafasi za kazi pia ziliongezeka. Matokeo mabaya ni kwamba mishahara ya watu wengi waliofanya kazi na huduma za feri imepungua sana. Wengine wanalalamika kwamba malipo ya kutumia daraja hilo yako juu sana. Lakini, maendeleo yoyote yana hasara zake.
Je, kufika haraka kwenye bara kumewafanya watu wasivutiwe tena na kisiwa hicho? Watu fulani wanaokuja “kutoka mbali” kufurahia utulivu wa kisiwa hicho wanaweza kujiuliza ikiwa watatulia kutokana na shughuli nyingi za bara katika maeneo yasiyoharibiwa na marundo ya mchanga ya Abegweit, jina la kisiwa hicho linalomaanisha “kitanda kidogo katika mawimbi” ambalo linatumiwa na watu wa kabila la Micmac wanaoishi katika eneo hilo.
Bila shaka, ujenzi wa Daraja la Confederation umeleta maendeleo makubwa. Je, madereva husinzia wanapopitia daraja hilo? La. Muundo wa daraja hilo wenye umbo la herufi S utawawezesha kukaa macho ili kufurahia safari yao. Huenda daraja hilo likakuchochea kutembelea ‘Bustani hiyo ya Ghuba’ na kufurahia utulivu wake, iwe unapenda kitabu Anne of Green Gables au la.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 19]
Magumu ya Usafiri Wakati wa Baridi Kali
Wazungu wa kwanza kukaa katika Kisiwa cha Prince Edward waligundua kwamba barafu nyingi inayosonga iliwazuia kufika bara kwa miezi mitano kila mwaka. Ilikuwa kazi ngumu kuvuka barafu hiyo, ambayo mara nyingi ilirundamana iliposukumwa na upepo mkali. Kwa hakika, hiyo haikuwa safari ya mtu mwoga. Wazungu hao walijaribu kuvuka barafu hiyo kwa mara ya kwanza mwaka wa 1775 kwa kutumia mitumbwi iliyokuwa na sehemu za kutelezea, wakiwaiga wenyeji wa kabila la Micmac. Kuanzia wakati huo, barua zilisafirishwa, na abiria walivuka mlango-bahari wakati wote wa baridi kali kwa ukawaida, ijapokuwa “wasafiri wengi hawakutaka kuhatarisha maisha yao kwa kutumia mitumbwi hiyo,” chasema kitabu Lifeline—The Story of the Atlantic Ferries and Coastal Boats. Katika kitabu chake Maritime Advocate and Busy East F. H. MacArthur anasema: “Wanawake walilipa nauli maradufu kwani hawakupaswa kufanya kazi ngumu. Abiria wanaume walifungiliwa kwenye mashua kwa mishipi ya ngozi ambayo ilitumiwa kuvuta mashua na kuwazuia wasizame ikiwa wangeanguka majini. Mashua zilikuwa na urefu wa meta tano hivi, upana wa meta moja, na upande wa mbele ulikuwa umeinuliwa kama sehemu ya chini ya kigari cha kutelezea. Sehemu ya nje ya mashua ilikuwa imefunikwa kwa madini mazito ya bati.” Inadhaniwa kwamba safari ya mwisho ya kuvuka kwa mitumbwi ilifanywa Aprili 28, 1917, na baada ya hapo serikali ilinunua meli ya kuvunja barafu ambayo ilipita kwenye barafu kwa ukawaida na kwa usalama kuliko mitumbwi.
[Picha]
Mitumbwi ilivuka Mlango-Bahari wa Northumberland hadi mwaka wa 1917
[Hisani]
Public Archives and Records Office of Prince Edward Island, Accession No. 2301-273
[Mchoro katika ukurasa wa 18]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
3 Mhimili, ambao uko
juu ya nguzo 4 Visehemu vya kuunganisha mihimili
2 Nguzo, iliyounganishwa na msingi
Kifaa cha kuzuia barafu
1 Msingi wa nguzo
[Ramani katika ukurasa wa 16]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Kisiwa cha Prince Edward
[Picha katika ukurasa wa 17]
Mamia ya maelfu ya watalii hutembelea Kisiwa cha Prince Edward kila mwaka
[Picha katika ukurasa wa 18]
Kreni ikiweka mhimili juu ya nguzo
[Hisani]
Photo courtesy of Public Works & Government Services Canada and Boily Photo of Summerside
[Picha katika ukurasa wa 18]
Sehemu ya katikati ya daraja imeinuka kwa meta 60 juu ya maji ili kuwezesha meli kupita
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 17]
Tourism Prince Edward Island/John Sylvester ▸