Je, Ungependa Kuonja Maua ya Mung’unye?
Je, Ungependa Kuonja Maua ya Mung’unye?
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI MEXICO
WAKATI mimea ya mung’unye inapochanua, shamba la mboga hufanana na bustani ya maua. Ijapokuwa maua hayo ya manjano yenye kuvutia yenye umbo sahili la kifahari hayatoi harufu nzuri, yana ladha ya kupendeza. Je, tunamaanisha kwamba watu hula maua? Ndiyo. Kwa kweli, kulingana na jarida la Cuadernos de Nutrición, inasemekana kwamba vyakula vingi nchini Mexico hutayarishwa kwa maua.
Kwa karne nyingi maua ya mung’unye yameliwa huku Mexico. Kati ya aina nyingi za mung’unye, huenda ua la zucchini ndilo huliwa sana. Lakini ikiwa tunataka kufurahia mboga hizo, ni lazima tutumie maua ya kiume tu. Tunatazama shina la mmea. Shina lenye tunda dogo linaonyesha kwamba ua ni la kike na hivyo hatupaswi kulichuma.
Ladha nzuri ya ua la mung’unye hupatana vizuri na vyakula vingine. Kwa kawaida, tunakaanga vitunguu saumu na vitunguu na labda pilipili kidogo. Vitu hivyo vikishakolea na vitunguu saumu kuiva, tunaongeza maua yaliyooshwa, yaliyokatwa, na kuondolewa mashina. Kisha tunafunika mchanganyiko huo na kuuacha uive polepole kwa dakika chache. Vipande vya zucchini, nafaka za mahindi, siagi kidogo, na vikolezo vyenye harufu nzuri vinaweza kuongezwa pia kwenye maua hayo. Tunaweka mchanganyiko huo kwenye unga uliokandwa ambao umetandazwa kama chapati na kuukunja. Kisha tunauacha uive ili kutokeza chakula kitamu cha maua ya mung’unye.
Mbali na ladha yake tamu, chakula hicho kinaboresha afya pia kwani ua la mung’unye lina kiasi kidogo cha protini, kalisi, chuma, thiamini, niacin, asidi askobiki, na retinol.
Pia tunatengeneza mchuzi mtamu kwa maua hayo. Tunafuata utaratibu ulioonyeshwa hapo juu, kisha tunaongeza mchuzi wa nyama ya kuku na kuuandaa ukiwa moto. Tukipenda tunaweza kupamba chakula hicho kwa jibini na vipande vya chapati.
Maua hayo yanaweza kutumiwa kutayarisha vyakula vingine vingi. Basi kwa nini usitayarishe mlo wa maua ya mung’unye? Utaufurahia wee!