Mrujuani—Una Harufu Nzuri
Mrujuani—Una Harufu Nzuri
Na mwandishi wa Amkeni! nchini Australia
MALKIA ELIZABETH wa Kwanza wa Uingereza aliagiza kitu hicho kitumiwe kuhifadhi chakula. Charles wa Sita wa Ufaransa alikalia mito iliyotengenezwa nacho. Malkia Victoria wa Uingereza alioga nacho. Ni nini hicho kilichowapendeza watawala hao? Ni mmea wenye harufu nzuri unaoitwa mrujuani. Mtu yeyote ambaye amewahi kusimama katika shamba la mrujuani lenye rangi ya zambarau, ataelewa ni kwa nini watu wengi sana wanavutiwa na mmea huo wenye harufu nzuri.
Kuna zaidi ya aina 30 za mmea wa mrujuani. Mmea huo unaweza kustahimili hali mbalimbali za hewa, kama vile baridi ya Milima ya Alps ya Ufaransa na joto kavu la Mashariki ya Kati. Jina la kisayansi la mmea huo, Lavandula, linatokana na neno la Kilatini lavare linalomaanisha “kusafisha.” Neno hilo linatokana na desturi ya Waroma wa kale, ambao walitia marashi kwenye maji ya kuoga kwa mafuta ya mrujuani.
Dawa Iliyotumiwa kwa Muda Mrefu
Mrujuani ulianza kutumiwa katika tiba miaka 2,000 hivi iliyopita. Katika Zama za Kati, mrujuani ulitumiwa hasa katika mchanganyiko ulioitwa siki ya wezi wanne, ambao ulitumiwa kupambana na tauni. Yaelekea jina la siki hiyo lilitokana na zoea la wezi wa makaburi la kuiba vitu vya watu waliokufa kutokana na tauni kisha kujiosha kwa umajimaji huo wenye mrujuani. Ingawa kazi yao ilikuwa hatari, yaonekana hawakuambukizwa ugonjwa huo.
Madaktari wa mitishamba wa karne ya 16 walidai kwamba, mbali na kutibu tu mafua na maumivu ya kichwa, mrujuani ulitibu kupooza kwa miguu na mikono na pia magonjwa ya akili. Pia waliamini kwamba kuvaa kofia iliyotengenezwa kwa mrujuani kungemfanya mtu awe na akili nyingi. Wakati wa Vita vya Kwanza vya Ulimwengu, serikali fulani ziliwaomba raia wake wakusanye mrujuani kutoka katika mashamba yao ili mafuta yanayotokana na mrujuani yatumiwe kutibu vidonda vya wanajeshi.
Uchunguzi Kuhusu Matibabu ya Kale
Inaonekana mafuta mengine ya mrujuani, hasa ya mmea wa Lavandula
angustifolia, huangamiza aina fulani za bakteria na kuvu. Watafiti fulani wamesema kwamba mafuta ya mrujuani yanaweza kutibu maambukizo ya bakteria zinazokinza dawa. “Mafuta ya mrujuani yanatumiwa pia katika ukunga,” yasema makala moja ya utafiti ya hivi majuzi. “Katika uchunguzi mkubwa wa kitiba, iligunduliwa kwamba akina mama wanaotumia mafuta ya mrujuani [katika maji ya kuoga] kwa ukawaida, hawakupata maumivu mengi siku 3 hadi 5 baada ya kujifungua . . . Kwa sasa mafuta ya mrujuani yanatumiwa katika hospitali nyingi za kujifungua kwa sababu yanawatuliza akina mama.”Vipi tamaa ya Malkia Elizabeth ya kukoleza chakula chake kwa mrujuani? Je, kweli mrujuani huliwa? Katika kitabu chake Lavender, Sweet Lavender, Judyth McLeod, anasema: ‘Mrujuani ulipendwa sana katika mapishi ya karne ya 15 na ya enzi ya Malkia Elizabeth wa Kwanza na ulitumiwa kukoleza nyama za wanyama wa mwituni, nyama choma, saladi za matunda, vyakula vitamu au kutengeneza halua.’ Leo, aina fulani za mrujuani hutumiwa kuongeza ladha kwenye biskuti, keki, na aiskrimu. Kwa upande mwingine, aina nyingine hazipendwi, hasa na wadudu. Uchunguzi mmoja unasema kwamba, “mafuta ya mrujuani au ungaunga wa majani na maua ya mrujuani unaweza kutumiwa pia kumaliza wadudu . . . kwani mrujuani huzuia utitiri, wadudu wanaokula nafaka, na nondo wanaokula nguo.”
Mrujuani Unazidi Kupendwa
Katika miaka ya karibuni, watu wengi wameanza kuupenda tena mrujuani. Sasa mrujuani unakuzwa huko Amerika Kaskazini, Australia, Japani, New Zealand, na Ulaya. “Mrujuani ni kama divai,” asema kijana mmoja anayeitwa Byron ambaye hukuza mimea ya mrujuani kwenye shamba la ekari 25 kusini-mashariki mwa Victoria, nchini Australia. “Mafuta yanayotokana na mimea ya aina moja hutofautiana katika sehemu mbalimbali kwa sababu ya udongo na hali ya hewa. Hata wakati wa kuvuna na mbinu za kuvuna, zinaweza kuathiri mafuta ya mrujuani.”
Tofauti na divai, mafuta ya mrujuani hutokezwa kwa mvuke wala si kwa kupondwa. Byron anaeleza: “Kilo 250 za mrujuani zinahitajiwa ili kutokeza lita moja ya mafuta. Maua, vikonyo, na majani yaliyokatwa, hushinikizwa ndani ya pipa kubwa la chuma. Mvuke hushinikizwa chini ya pipa hilo, na unapoinuka na kupitia sehemu hizo za mmea, unafanyiza mafuta. Mvuke na mafuta hupitia chombo cha kupoza na kuingia kwenye chombo kingine ambapo mafuta hutengana na maji na kuinuka. Mafuta huondolewa na kuhifadhiwa katika vyombo vilivyotandazwa kauri na kuachwa kwa miezi kadhaa ili yawe tayari kabisa.”
Mafuta ya mrujuani kutoka shamba la Byron hutumiwa kutengeneza sabuni, krimu, na mishumaa. Maua huuzwa baada ya kukatwa tu au yakiisha kukaushwa, na maua madogo yaliyo kwenye vikonyo hutumiwa sana katika mchanganyiko wa manukato. Maelfu ya watalii huja kila mwaka kuonja peremende za mrujuani na kutazama na kunusia harufu nzuri ya shamba la mrujuani. Mara nyingi Byron huwakumbusha wageni hao wenye shauku hivi: “Hatutengenezi mafuta haya, tunayakamua tu. Mbuni wa mrujuani Ndiye aliyetupatia mmea huu ili tufurahie harufu yake nzuri.”
[Sanduku katika ukurasa wa 11]
Aina tatu za mafuta ya mrujuani hutengenezwa viwandani
Mafuta halisi ya mrujuani hutokana na aina ya mmea unaoitwa, “Lavandula angustifolia.” Tofauti na mafuta yaliyotajwa hapa chini, mafuta haya hayana harufu ya kafuri. Tani 200 hivi za mafuta hayo hutokezwa kila mwaka
Aina nyingine ya mafuta hutokana na mmea wa “Lavandula latifolia.” Tani 200 hivi zinaweza kutokezwa kwa mwaka
Mafuta mengine hutokezwa kwa kuzalisha mbegu za mimea hiyo miwili iliyotajwa juu. Zaidi ya tani elfu moja za mafuta hayo huuzwa ulimwenguni pote kila mwaka
[Picha katika ukurasa wa 10]
Katika mashamba mengi, njia za kale za kuvuna mrujuani bado zinatumiwa
[Picha katika ukurasa wa 10]
Mafuta ya mrujuani hukamuliwa katika mapipa makubwa
[Picha katika ukurasa wa 10]
Mafuta ya mrujuani huachwa yasitawi katika vyombo vya chuma vilivyotandazwa kauri kabla hayajatumiwa kutengeneza bidhaa mbalimbali