Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Muziki—Unaochezwa kwa Vidole

Muziki—Unaochezwa kwa Vidole

MuzikiUnaochezwa kwa Vidole

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI UINGEREZA

“NDIYO ala bora zaidi ya muziki”—hivyo ndivyo watu fulani wanavyosema kuhusu piano. Kwa kuwa inaweza kutumiwa kwa njia mbalimbali na kuwasilisha hisia waziwazi, piano hutumiwa katika muziki wa klasiki, jazi, na muziki unaopendwa na wengi. Piano husikika waziwazi kwenye maonyesho ya muziki hata inapochezwa bila ala nyingine za muziki, na vilevile kutokeza muziki wa sauti ya chini ili kumsaidia mwimbaji mwenye haya. Ni kama “bendi ya mtu mmoja” na inaweza kupatana vizuri na karibu kila ala ya muziki. Imelinganishwa na “rangi za mchoraji” na imewachochea watu kutunga muziki mtamu zaidi. Ni nani aliyeibuni piano, na kwa nini inapendwa na watu wengi hata leo? *

Ala Zilizoitangulia Piano

Kinubi na zeze zilikuwa miongoni mwa ala za kwanza za muziki zenye nyuzi. (Mwanzo 4:21) Kisha kinanda-meza kikabuniwa, ambacho huchezwa kwa vitu vya kugongea. Huko Ulaya katika Zama za Kati, ala za muziki zenye kibodi ya kupiga nyuzi zilibuniwa, na watu walipenda zaidi ala ya marimba-sanduku na kinubi-uzi. Marimba-sanduku ilikuwa kama sanduku la mstatili lenye kifuniko, na nyuzi zake zilipigwa kutoka chini kwa vyuma vidogo vyembamba. Ilitoa sauti nzuri, lakini sauti yake ndogo ilimezwa na sauti za ala nyingine na za waimbaji. Kinubi-uzi kikubwa kilifanana na piano kubwa ya kisasa na kilikuwa na nyuzi ndefu zilizochezwa kwa manyoya au kipande kidogo cha chuma. Kilitokeza mvumo wenye nguvu wa sauti moja.

Kufikia mwaka wa 1700, muziki mpya na wenye kuwasilisha hisia ulikuwa ukitungwa, hivyo wanamuziki walitaka ala yenye kibodi ambayo ingecheza muziki vizuri kama marimba-sanduku na kutoa sauti yenye nguvu kama kinubi-uzi.

Piano Yavumbuliwa

Mtengenezaji wa ala Mwitaliano, Bartolomeo Cristofori, alitengeneza ala mpya ya muziki iliyofanana na kinubi-uzi na iliyochezwa kama marimba-sanduku kwa vifaa vidogo vya mbao vya kugongea nyuzi vilivyofunikwa kwa ngozi. Aliiita ala yake gravicembalo col piano e forte (kinubi-uzi chenye sauti laini na kubwa), na kwa ufupi, pianoforte, au piano. Hatimaye kukawa na ala ya muziki yenye kibodi iliyotoa sauti laini au kubwa.

Kwa kusikitisha, Cristofori alikufa kabla ya kuona matokeo ya ala yake mpya. Kwa kuwa watu wengi hawakupendezwa na ala yake, alirudia kazi yake ya kutengeneza vinubi-uzi. Karibu miaka 30 baada ya Cristofori kuvumbua piano ya kwanza, mtengenezaji wa vinanda Mjerumani, Gottfried Silbermann, alichunguza tena muundo wa piano na kuanza kutengeneza piano zake. Mafundi huko Ujerumani na Austria waliendelea kufanya majaribio, wakijitahidi kutengeneza piano ndogo nyepesi ya mraba.

Kule Uingereza, kikundi kingine cha watengenezaji wa piano kilikuwa kikiendelea kubuni piano mpya. Walikuwa wamehama kutoka Ujerumani katika miaka ya mwisho-mwisho ya 1750. Mmoja wao, aliyeitwa Johannes Zumpe, alibuni piano ya mraba iliyouzwa sana. Sébastien Érard wa Ufaransa na watengenezaji wengine wa piano katika Ulaya na Marekani walitengeneza piano nyingine bora. Fundi stadi wa kabati, Mskoti, John Broadwood, alitambua kwamba piano itawafaa wasichana matajiri. Muda si muda kampuni yake ilikuwa ikiunda piano nyingi za mraba na piano kubwa.

Tatizo lingine lilikuwa kubuni piano ndogo ambayo ilitoa sauti kubwa kama piano kubwa. Kwa hiyo, piano zilitengenezwa zikiwa na umbo refu badala ya umbo pana, hivyo zikawa kubwa zaidi. Nyuzi za piano moja iliyotengenezwa na Broadwood ziliinuka meta 2.7 juu ya kibodi na kusababisha sehemu ya juu ya piano kuwa nzito na hatari kucheza! Aina nyingine ya piano iliyoitwa piano ya twiga, ilikuwa piano kubwa nayo iliinuka kwenye upande wake mwembamba. Katika mwaka wa 1800, John Isaac Hawkins, mwanamume Mwingereza, alibuni piano refu ya kwanza yenye mafanikio kwa kuweka sehemu ya chini ya nyuzi za piano karibu na sakafu. Hatimaye piano ya mraba ikaacha kutumiwa.

Watungaji wa Muziki Wavutiwa na Piano

Wakati huohuo, watungaji wa muziki walianza kuvutiwa na piano. Kijana Wolfgang Amadeus Mozart alipotembelea karakana ya Johann Stein huko Bavaria mwaka wa 1777 ili ajaribu kutumia ala hiyo mpya, alivutiwa sana. Muda si muda akaanza kutunga muziki utakaochezwa kwa piano. Kwa miaka minne tu alitunga nyimbo 15 za kuchezwa na piano! Lakini, miaka michache baadaye, Ludwig van Beethoven alitumia sana ala hiyo mpya ya muziki. Alifanya muziki wa piano uvutie sana, na kuifanya piano ionekane kana kwamba ilikuwa ikiimba yenyewe. Wanamuziki walikuwa wametazamia sana ala kama hiyo, na muziki mpya wa kuwasilisha hisia ukatokea. Frédéric François Chopin, “mtunzi wa piano,” aliiona kuwa ala bora ya kuwasilisha mawazo na hisia. Franz Liszt aliandika muziki wenye kupendeza uliosikika kana kwamba unachezwa na bendi ya wanamuziki. Pia alichangamsha umati katika maonyesho yake kwa nyimbo nzuri ajabu.

Hata hivyo, inasikitisha kwamba mbao na nyuzi nyembamba za piano hazingeweza kustahimili sauti kubwa ya muziki kwenye maonyesho. Hivyo, watengenezaji wa piano walianza kuongeza vyuma na mwishowe wakabuni piano yenye kiunzi imara cha chuma. Sasa wangeweza kutumia nyuzi nzito zaidi na vifaa vizito vya kugongea ili kutokeza sauti kubwa zaidi. Sauti yenye kukwaruza iliyotokezwa ilirekebishwa kwa kufunika vifaa vya kugongea kwa vitambaa. Kamba ndefu zaidi zilizokingamana na kamba fupi, ziliboresha sauti na hivyo hazikuchukua nafasi kubwa. Hivyo piano ya kisasa ikavumbuliwa na majumba ya maonyesho yakafurikwa na wachezaji stadi wa piano waliotumbuiza umati wenye shauku ambao ulikuwa na hamu kubwa ya kusikiliza muziki wa piano uliokuwa ukiongezeka. Wakati huohuo, kwa sababu watu wengi walitaka sana kuwa na piano, watengenezaji wa piano katika Ulaya na Marekani walitengeneza haraka piano nyingi sana.

Piano Zaenea

Mwanzoni mwa karne ya 20, kwa kuwa piano ilionwa kuwa kitu muhimu sana, kila familia ilihitaji kuwa nayo, iwe watu walijua kuicheza au la. Wachezaji wa piano walihitajiwa sana ili kuwatumbuiza wateja na wasafiri, kutayarisha muziki kwa ajili ya sinema mpya zisizo na maneno, na kuwafundisha watu wengi waliotaka kujua kucheza piano. Familia zilicheza piano zilipofanya sherehe. Wachezaji wa piano wasio na ustadi walifanya maonyesho yao. Muziki mpya uliochezwa kwa piano ulitungwa kwa ukawaida. Kulikuwa na njia mbalimbali za kucheza piano kama vile, kucheza muziki wenye kuchochea na kuvutia, muziki wa polepole na taratibu, na muziki wenye mdundo wa kurudia-rudia.

Mambo yalianza kwenda mrama baada ya Vita vya Kwanza vya Ulimwengu. Mauzo ya piano yalianza kushuka, kutoka kilele cha piano 600,000 zilizotengenezwa ulimwenguni pote mwaka wa 1910. Gramafoni, redio, kinanda, na hatimaye televisheni ndizo zilizotumiwa kwa ajili ya burudani nyumbani. Lakini huo haukuwa mwisho wa piano. Maendeleo ya tekinolojia baada ya Vita vya Pili vya Ulimwengu yaliwafanya watu wavutiwe tena na piano. Kufikia mwaka wa 1980, idadi ya piano zilizotengenezwa ilizidi 800,000. Leo, piano nyepesi hutengenezwa kwa plastiki na mchanganyiko wa vifaa vingine, na vibonyezo vyake vyeupe hufunikwa kwa vifaa vya sanisia badala ya pembe za tembo. Japani imekuwa mojawapo ya nchi zinazotengeneza piano nyingi ulimwenguni, na huko China ala hiyo inatumiwa sana hivi kwamba inaitwa “malkia wa ala za muziki.”

Je, Ungependa Kucheza Piano?

Ili kutokeza sauti kwa kutumia ala nyingine za muziki mtu anahitaji mazoezi mengi, lakini ukibonyeza piano mara chache tu kwa utaratibu, unaweza kutokeza muziki! Watu wachache wana kipawa cha kucheza muziki bila kusoma noti za muziki. Hata hivyo, watu wengi wameona kwamba kwa kutumia vitabu vya maagizo wanaweza kujifunza kucheza melodia kwa mkono wa kulia na kuipatanisha na muziki mwingine kwa mkono wa kushoto. Hebu wazia jinsi utakavyofurahi ukiweza kucheza muziki unaopenda sana kwa kutumia noti zilizoandikwa! Huenda ukaamua kucheza muziki wenye mdundo wa kusisimua, msowero taratibu, au labda muziki unaopenda. Labda utaamua kucheza muziki wa Amerika ya Latini au aina fulani ya jazi. Inafurahisha sana kucheza piano pamoja na rafiki! Pia, fikiria jinsi unavyoweza kuwafurahisha marafiki unapocheza piano huku wakiimba au kucheza ala nyingine za muziki. Je, ungependa kujaribu kucheza piano?

[Maelezo ya Chini]

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 21]

Piano Inayojicheza Yenyewe

Piano hii iliwafaa sana watu ambao hawakuwa na ujuzi mwingi wa kupiga kibodi. Ala hiyo ilikuwa na kisanduku cha muziki na piano, na sehemu za kubonyeza zilijisogeza juu na chini ziliposukumwa na matundu katika karatasi iliyovingirishwa ambayo ilisonga. Piano za kwanza za aina hiyo za miaka ya 1890 zilikuwa na kifaa cha mbao kilichobonyeza piano huku mchezaji akikanyaga vikanyagio. Katika ala za baadaye, kifaa hicho kiliingizwa ndani ya piano. Piano nyingine za hali ya juu zilirekodi muziki uliochezwa na wachezaji stadi na rekodi hizo zikanakiliwa na kuuzwa sawa na diski na kaseti za kisasa. Kufikia mwaka wa 1925, piano za aina hiyo zilikuwa zikitengenezwa kwa wingi huko Marekani kuliko piano za kawaida. Hata hivyo, kwa sababu ya uvumbuzi wa redio na gramafoni, kufikia miaka ya 1930 piano hizo hazikuwa zikitumiwa tena.

[Hisani]

Culver Pictures

[Sanduku[Mchoro katika ukurasa wa 22, 23]

Jinsi Piano Kubwa Inavyofanya Kazi

Zaidi ya nyuzi 200 za chuma za piano zilizo sambamba na zilizokazwa sana hutokeza noti 88. Nyuzi fupi na nyembamba ambazo hutetemeka haraka sana hutokeza noti za juu, hali nyuzi ndefu zilizo nzito, ambazo mara nyingi hufunikwa kwa shaba-nyekundu, hutokeza sauti nzito. Sauti zote isipokuwa sauti nzito za chini hutokezwa na nyuzi mbili au tatu zilizopatanishwa.

Mchezaji anapobonyeza piano (1), nyenzo husogeza kifaa cha kugongea ambacho hugonga uzi mmoja au zaidi wa kibonyezo na kuruka mara moja. Kuendelea kubonyeza hufanya uzi uendelee kutetemeka na sauti kupungua polepole. Wakati mchezaji anapoondoa kidole kwenye kibonyezo (2), kidude fulani kilichofunikwa kwa kitambaa hufinya uzi na kuunyamazisha. Kikanyagio cha upande wa kulia wa piano kinapokanyagwa, huzuia vidude hivyo visisonge na hivyo kupatanisha noti za muziki.

Nyuzi hupita juu ya vipande vya mbao (3), vilivyounganishwa na kibao cha kupazia sauti (4), ambacho hutetemeka na kuongeza nguvu na mdundo wa nyuzi. Ubao unaozunguka huongeza sauti.

Nyuzi huunganishwa kwenye kiunzi cha chuma kwa pini za chuma (5). Kiunzi cha piano kubwa kinahitaji kuwa imara vya kutosha kuhimili mvuto wa nyuzi zote ambao unaweza kufikia tani 30.

[Mchoro]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Kidude kilichofunikwa kwa kitambaa

uzi

Kifaa cha kugongea

Kibonyezo kilichofinywa

Kibonyezo kilichoinuka

[Picha]

Piano ya kwanza ya Cristofori, mwaka wa 1720

[Hisani]

The Metropolitan Museum of Art, The Crosby Brown Collection of Musical Instruments, 1889. (89.4.1219) Photograph ©1983 The Metropolitan Museum of Art