Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Jinsi ya Kujilinda Dhidi ya Ulaghai

Jinsi ya Kujilinda Dhidi ya Ulaghai

Jinsi ya Kujilinda Dhidi ya Ulaghai

HUENDA umesikia msemo huu, “Huwezi kumdanganya mtu mwaminifu.” Sawa na misemo mingi, msemo huo si wa kweli. Kila siku watu waaminifu hudanganywa na walaghai; uaminifu peke yake hauwalindi. Watu fulani wenye akili sana ulimwenguni wanatunga hila na kutumia mbinu za kuwanyang’anya watu pesa. Zaidi ya miaka mia moja iliyopita, mwandishi mmoja alisema: “Visa fulani vya ulaghai hufanywa kwa ustadi sana hivi kwamba ingekuwa upumbavu kutodanganyika.”

Udanganyifu ulianza zamani sana, katika bustani ya Edeni. (Mwanzo 3:1-5) Mbinu za kale hutumiwa kwa njia mbalimbali, na mbinu mpya hubuniwa kila wakati. Kwa hiyo, unawezaje kujilinda? Huhitaji kujifunza mbinu zote ambazo matapeli hutumia kuwalaghai watu. Kufanya mambo machache ya msingi kutakulinda dhidi ya ulaghai.

Linda Habari za Kibinafsi

Mtu akiiba kitabu chako cha hundi au kadi za mikopo, anaweza kuzitumia kununua vitu. Akiiba habari kuhusu akiba yako ya benki, anaweza kuandika hundi akitumia jina lako. Akiisha fanya hivyo, anaweza kutoa pesa kwenye akiba zako za benki, kununua vitu kwa kadi zako za mikopo, na kuomba mikopo akitumia jina lako. * Hata unaweza kukamatwa kwa kosa ambalo hukufanya!

Ili ujilinde dhidi ya aina hiyo ya ulaghai, uwe mwangalifu kuhusu hati zako zote za kibinafsi kama vile taarifa za benki, vitabu vya hundi, leseni ya kuendesha gari, au kitambulisho. Usikubali kuwapa wengine habari za kibinafsi au za kifedha isipokuwa kuna sababu nzuri ya kufanya hivyo. Hilo linahusu hasa namba za kadi za mikopo na habari kuhusu akiba ya benki. Inafaa kutoa namba ya kadi ya mkopo wakati unaponunua kitu tu.

Matapeli fulani hupekua takataka wakitafuta habari hizo. Badala ya kutupa tu karatasi zenye habari za kibinafsi, ni jambo la hekima kuziteketeza au kuzirarua. Hiyo inatia ndani hundi zilizotumiwa, taarifa za benki na za hisa, na vilevile kadi za mikopo za zamani, leseni za kuendesha gari, na pasipoti. Pia ni jambo la hekima kuharibu fomu za kuomba kadi za mikopo ambazo huzihitaji zinazotumwa kupitia posta, kwa kuwa zina habari zako ambazo mtu mwingine anaweza kutumia vibaya.

Tumia Akili

Katika visa vingi vya ulaghai, watu huahidiwa kwamba watapata faida kubwa wakiingia katika biashara fulani. Mbinu moja inayotumiwa sana ni ile ya kuwahusisha watu wengi katika biashara na kuwaahidi kuwa watatajirika haraka. Ingawa mbinu hiyo hutumiwa kwa njia mbalimbali, kwa kawaida wahusika huwatafuta watu wengine wa kujiunga na biashara hiyo, na wanapofanya hivyo wanalipwa. * Mbinu nyingine inahusisha kuwatumia watu kadhaa barua yenye majina na kuwaomba wamtumie pesa mtu wa kwanza kwenye orodha hiyo ya majina. Mtu huahidiwa kwamba atapokea maelfu ya dola wakati jina lake litakapokuwa la kwanza kwenye orodha hiyo.

Sikuzote biashara hizo huanguka kwa kuwa haiwezekani kuendelea kuwatafuta washiriki wapya. Fikiria mfano unaofuata. Ikiwa watu watano wangeanzisha mradi wa biashara kisha kila mmoja wao awatafute watu watano zaidi, biashara hiyo itakuwa na watu 25 zaidi. Kila mmoja wao akitafuta watu 5 zaidi, watu 125 wataongezwa. Wakifanya hivyo mara tisa, biashara hiyo itakuwa na watu milioni mbili hivi, nao watatafuta zaidi ya watu milioni tisa! Wasimamizi wa miradi hiyo wanajua kwamba kuna kiwango ambacho hakiwezi kupitwa. Wanapogundua kwamba wanakaribia kufikia kiwango hicho, wao hutoroka na pesa. Huenda ukapoteza pesa zako, na watu ambao umewashawishi kujiunga na biashara hiyo watakudai pesa zao. Kumbuka kwamba, katika mradi kama huo, ili upate pesa, ni lazima mtu mwingine apoteze pesa.

Je, mtu fulani amekuahidi kwamba utapata pesa au faida kubwa kwa urahisi ukijiunga na biashara fulani? Basi zingatia tahadhari hii: Ahadi ikionekana kuwa nzuri sana hivi kwamba haiaminiki, kwa kawaida si ya kweli. Usiamini matangazo ya biashara haraka-haraka ukidhania kwamba, “Kisa hiki ni tofauti na visa vingine.” Kumbuka kwamba watu hawafanyi biashara ili kupeana pesa wala kutoa siri za kuwatajirisha wengine. Ikiwa mtu anadai kwamba ana habari muhimu zitakazokusaidia utajirike, jiulize hivi: ‘Kwa nini hatumii habari hizo kujitajirisha? Kwa nini anapoteza wakati wake ili kunipa habari hizo?’

Vipi ukiambiwa kwamba umeshinda tuzo katika mashindano fulani? Usisisimuke, kwa kuwa huenda huo ni mtego, na wengi wamenaswa kwa njia hiyo. Kwa mfano, mwanamke mmoja huko Uingereza alipokea barua kutoka Kanada iliyomweleza kwamba amejishindia tuzo, lakini anapaswa kutuma dola 25 ili aipokee. Baada ya kutuma pesa hizo, alipata simu kutoka Kanada iliyosema kwamba amekuwa mshindi wa tatu katika mashindano ya bahati-nasibu ya dola 245,000, lakini kwanza anapaswa kutuma sehemu fulani ya kiasi hicho ili apokee pesa zake. Alituma dola 2,450, lakini hakupata chochote. Naam, ukiombwa ulipie “zawadi ya bure” au tuzo, huo ni udanganyifu. Jiulize hivi: ‘Ninawezaje kushinda tuzo katika shindano ambalo sikushiriki?’

Fanya Biashara na Watu Wenye Sifa Nzuri Tu

Je, unaamini kwamba unaweza kutambua watu wasio waaminifu? Uwe mwangalifu! Matapeli wanajua jinsi ya kuwasadikisha watu wawaamini. Wana ustadi wa kuwashawishi watu. Wauzaji waaminifu na wasio waaminifu wanajua kwamba ili wauze bidhaa yoyote, ni lazima wawashawishi watu kuwaamini. Bila shaka, hiyo haimaanishi kwamba unapaswa kumshuku kila mtu, lakini ni muhimu kushuku mambo kwa kiasi fulani ili ujilinde dhidi ya ulaghai. Badala ya kumwamini mtu kwa kutegemea akili yako mwenyewe, uwe macho kutambua dalili hizi mbili za ulaghai: Kwanza, je, ahadi zinazotolewa zinaonekana kuwa nzuri sana hivi kwamba haziwezi kuaminika, na pili, je, muuzaji anataka ufanye uamuzi haraka-haraka?

Kuna biashara nyingi za ulaghai kwenye Intaneti. Ijapokuwa Intaneti hutoa huduma nyingi muhimu, inawawezesha wahalifu kuwalaghai watu haraka na bila kujulikana. Je, una anwani ya barua-pepe? Ikiwa ndivyo, huenda ukapokea matangazo ya biashara kutoka kwa watu usiowajua. Ijapokuwa matangazo hayo huonyesha bidhaa na huduma nyingi zinazotolewa, mengi ni ya ulaghai. Ukijibu barua-pepe ya mtu usiyemjua kwa kutuma pesa kwa ajili ya bidhaa au huduma fulani, huenda usipate chochote. Hata ukipokea kitu, hakitalingana na pesa ulizotuma. Usinunue chochote kutoka kwa mtu usiyemjua ambaye anakutumia ujumbe wa barua-pepe.

Ndivyo ilivyo pia na watu wanaopiga simu ili wakuuzie bidhaa. Ingawa biashara nyingi zinazofanywa kupitia simu ni halali, biashara za ulaghai zinazofanywa kupitia simu huwasababishia watu hasara ya mabilioni ya dola kila mwaka. Haiwezekani kujua ikiwa biashara ni halali ukizungumza na mtu kwa simu tu. Tapeli anaweza kujifanya kuwa mwakilishi wa benki au wa shirika la kulinda kadi za mikopo. Mtu anayedai kuwa mwakilishi wa benki au kampuni inayokuhudumia akikupigia simu na kuomba habari ambazo tayari kampuni hiyo inapaswa kuwa nazo, jihadhari. Hilo likitukia, unaweza kumwomba namba yake ya simu. Kisha umpigie baada ya kuhakikisha kwamba namba hiyo ni ya benki au kampuni hiyo.

Si jambo la busara kumpa mtu usiyemjua namba yako ya kadi ya mkopo au habari nyingine za kibinafsi anapokupigia simu. Mtu akikupigia simu ili kukuuzia bidhaa usiyotaka, unaweza kumwambia hivi kwa upole, “Samahani, mimi sifanyi biashara kwa simu na watu nisiowajua.” Kisha kata simu. Hakuna haja ya kuzungumza na mtu usiyemjua ambaye huenda anajaribu kukulaghai.

Fanya biashara na mashirika yanayoaminika na watu wenye sifa nzuri tu. Kuna makampuni mengi halali ambayo unaweza kushughulika nayo kwa simu au Intaneti bila kujihatarisha. Ikiwezekana, pata habari kuhusu muuzaji, kampuni, na biashara hiyo kupitia shirika lingine. Tafuta habari kuhusu biashara hiyo, na uzisome kwa uangalifu ili uhakikishe kwamba ni za kweli. Usikubali kuharakishwa wala kulazimishwa kufanya uamuzi.

Andika Mambo Yote

Nyakati nyingine biashara halali inaweza kubadilika kuwa biashara ya ulaghai. Inapokuwa hivyo, wasimamizi wanaweza kuingiwa na wasiwasi na kutumia ulaghai ili kulipia hasara walizopata. Huenda umesikia kuhusu wasimamizi wa biashara ambao walidanganya kuhusu mapato na faida, kisha biashara ilipoanguka wakatoroka na pesa.

Ili kujilinda dhidi ya ulaghai na hali za kutoelewana, unapaswa kuandika habari zote kabla ya kujiingiza katika biashara yoyote kubwa. Mapatano yoyote unayotia sahihi yanapaswa kuwa na habari zote kuhusu biashara hiyo na ahadi zilizotolewa. Pia, tambua kwamba, hata biashara ikionekana kuwa thabiti kadiri gani, hakuna mtu anayeweza kukuhakikishia kwamba mambo yatakuwa shwari. (Mhubiri 9:11) Kwa kweli, biashara yoyote inaweza kupata matatizo. Hivyo, mapatano yaliyoandikwa yanapaswa kuonyesha wazi wajibu na madaraka ya kila mtu iwapo biashara hiyo itaanguka.

Ukijua na kutumia kanuni za msingi ambazo tumezungumzia kwa ufupi, hutatumbukia kwa urahisi katika mtego wa walaghai. Methali moja ya kale ya Biblia inatoa shauri bora. Inasema hivi: “Mtu asiye na uzoefu huamini kila neno, lakini mtu mwerevu huzifikiria hatua zake.” (Methali 14:15) Matapeli hupenda kuwalaghai watu wanaoamini kila neno. Inasikitisha kwamba watu wengi hawajihadhari na ulaghai.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 9 Huu ni mradi mkubwa wa biashara ambapo watu hulipa kiasi fulani cha pesa ili wajiunge na kuwatafuta watu wengine wanaotaka kujiunga na biashara hiyo. Mara nyingi biashara za aina hiyo hazitoi huduma wala bidhaa zozote.

[Blabu katika ukurasa wa 7]

Ahadi ikionekana kuwa nzuri sana hivi kwamba haiaminiki, kwa kawaida si ya kweli

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 6]

Shauri kwa Watu Wanaokumbwa na Ulaghai

Watu wanaokumbwa na ulaghai huaibika sana, huhisi hatia, na kujilaumu kwa hasira. Usijilaumu. Wewe ndiye uliyekosewa; yule aliyekulaghai ndiye anayepaswa kulaumiwa. Ikiwa umefanya kosa, kubali na usahau jambo hilo. Usijione kuwa mjinga. Kumbuka kwamba matapeli hufaulu kuwalaghai watu wenye akili nyingi kama vile, wakuu wa nchi, wasimamizi wa benki, wakurugenzi, wasimamizi wa fedha, mawakili, na wengineo.

Zaidi ya kunyang’anywa pesa na mali zao, watu wanaokumbwa na ulaghai huacha kujiheshimu pia. “Rafiki” yako anapokulaghai, anaharibu uhusiano wenu. Mtu huumia sana anapolaghaiwa. Jipe muda wa kuhuzunika. Mara nyingi ni vizuri kuzungumza na mtu fulani unayemwamini kuhusu jambo hilo. Sala pia inaweza kukufariji sana. (Wafilipi 4:6-8) Hata hivyo, tambua kwamba baada ya muda, unapaswa kusahau jambo hilo. Kwa nini uendelee kuhuzunika? Jiwekee miradi na ujitahidi kuifikia.

Jihadhari na matapeli wanaojitolea kukusaidia kupata pesa ulizopoteza. Matapeli humpigia simu mtu aliyekumbwa na ulaghai ili kumwahidi kwamba watamsaidia kupata pesa zilizopotea. Kusudi lao ni kumlaghai mtu huyo tena.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8, 9]

Mbinu Sita Zinazotumiwa Kwenye Barua-pepe

1. Biashara za kuwatafuta washiriki wapya: Biashara hizo huonwa kuwa njia ya kujitajirisha bila jitihada yoyote wala kutumia pesa nyingi. Watu wengine hupewa kompyuta au kifaa kingine cha elektroni wanapolipa pesa za kujiunga na biashara hizo na kutafuta washiriki wengine. Wakati mwingine watu hutumiwa barua zenye orodha ya majina. Mara nyingi barua hizo si halali. Watu wengi wanaojiingiza katika biashara hizo hupoteza pesa zao.

2. Mbinu za kujitengenezea vitu nyumbani: Njia moja inahusisha kuwapa watu kazi ya kutengeneza vito, vitu vya watoto vya kuchezea, au bidhaa nyinginezo. Watu hutumia pesa na wakati mwingi kununua vifaa vya kutengeneza vitu hivyo na kuvitengeneza, lakini mwishowe wenye biashara wanakataa kuvinunua kwa sababu wanaviona kuwa havifai.

3. Mbinu zinazohusu afya na lishe: Kuna matangazo mengi ya biashara kwenye Intaneti kuhusu bidhaa mbalimbali, kama vile dawa zinazomsaidia mtu kupunguza uzito bila kuhitaji kufanya mazoezi au kubadili mazoea ya kula, dawa za kuongeza nguvu za kujamiiana, na krimu za kuzuia upara. Nyakati nyingine matangazo hayo huambatana na maelezo ya wanunuzi ambao wanasifu bidhaa hizo. Baadhi ya misemo inayotumiwa mara nyingi katika matangazo hayo ni kama vile “hatua kubwa ya kisayansi,” “dawa ya magonjwa yote,” na “siri ya mafanikio.” Ukweli ni kwamba nyingi ya bidhaa hizo hazifanyi kazi.

4. Nafasi za kutega uchumi: Katika mbinu hii, watu huahidiwa watapata faida kubwa bila hasara au hatari zozote. Mbinu inayotumiwa sana inahusisha kutega uchumi katika benki iliyo katika nchi nyingine. Watu wanaotega uchumi hushawishiwa kwa kuhakikishiwa kwamba wale wanaoshughulika na pesa zao wana uhusiano na mashirika makubwa na wana habari muhimu.

5. Kuondolewa lawama: Katika mbinu hii, watu huahidiwa kwamba habari zisizofaa kuwahusu zitaondolewa kwenye rekodi zao za biashara ili waweze kupata kadi ya mkopo, mkopo wa kununua gari, au wapate kazi. Ijapokuwa wanatoa ahadi nyingi, watu wanaofanya biashara hizo hawazitekelezi.

6. Kujishindia likizo: Katika mbinu hii, mtu hupata ujumbe wa barua-pepe unaompongeza kwa kujishindia likizo ya bei nafuu. Ujumbe mwingine husema kwamba ni wewe tu uliyechaguliwa kati ya wengi. Inafaa kukumbuka kwamba huenda mamilioni ya watu wametumiwa ujumbe huo na huduma utakazopata zitakuwa duni zikilinganishwa na yale yaliyosemwa katika matangazo yao.

[Hisani]

Source: U.S. Federal Trade Commission

[Picha katika ukurasa wa 7]

Sikuzote, biashara za kuwatafuta washiriki wapya huanguka

[Picha katika ukurasa wa 9]

Mapatano yoyote unayotia sahihi yanapaswa kuwa na habari zote kuhusu biashara hiyo na ahadi zilizotolewa