Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Mawingu na Tembo

Wingu lina uzito gani? Kulingana na shirika la habari la ABC, wingu moja la kumulasi lina tani 550 hivi za maji. Mtaalamu wa utabiri wa hali ya hewa, Peggy LeMone anasema: “Ili kueleza hilo kwa njia rahisi, . . . linganisha uzani huo na ule wa tembo.” Tukikadiria kwamba tembo mmoja ana uzani wa tani sita hivi, basi maji yaliyo katika wingu moja la kumulasi yana uzito wa tembo 100 hivi. Maji yote hayo yanaelea yakiwa matone madogo-madogo juu ya hewa yenye joto inayopaa kutoka chini. Tofauti na wingu la kumulasi, wingu kubwa la dhoruba linaweza kuwa na maji yenye uzito wa tembo 200,000 hivi. Vipi kimbunga? LeMone alikadiria uzito wa maji katika meta moja ya mchemraba ya wingu la kimbunga na akazidisha idadi hiyo kwa ukubwa wa kimbunga. Matokeo yalikuwa nini? Alipata kwamba maji yaliyomo yana uzito wa tembo milioni arobaini. Ripoti hiyo inasema: “Hilo linamaanisha kwamba maji yaliyomo katika kimbunga kimoja yana uzito unaozidi ule wa tembo wote waliopo duniani au hata tembo wote waliopata kuishi.”

Wakati Mzuri wa Kupiga Mswaki

Gazeti Milenio la Mexico City linasema kwamba kupiga mswaki punde baada ya kunywa vinywaji vyenye asidi au kula chakula chenye asidi kunaweza kudhuru gamba la jino. Likiripoti uchunguzi uliofanywa kwenye Chuo Kikuu cha Göttingen huko Ujerumani, gazeti hilo lilionya kwamba vyakula vyenye asidi “hudhoofisha gamba la jino kwa muda mfupi.” Hivyo, kupiga mswaki punde baada ya mlo kunaweza kuwa hatari. Badala yake, “inafaa kusubiri dakika chache ili meno yapate nguvu tena.”

Ndege Mpya Apatikana Baada ya Makao Kuharibiwa

Jarida Daily Journal la Caracas linaripoti kwamba wakati msitu wa eneo lisilokaliwa la Kisiwa cha Carrizal kwenye Mto Caroní huko Venezuela ulipokatwa ili kutengeneza bwawa la maji, ndege fulani asiyejulikana alipatikana. Iligunduliwa baadaye kwamba kati ya aina mbalimbali za ndege waliochukuliwa kabla ya miti kukatwa, alikuwemo shorewanda mdogo mwenye madoadoa ya bluu ambaye aliishi kwenye msitu wa mianzi wa kisiwa hicho. Wataalamu wa elimu ya viumbe wanatumaini kupata ndege zaidi wa aina hiyo katika maeneo ya karibu. Wakati huohuo, mtafiti Robin Restall anasema kwamba, “ugunduzi wa ndege huyo wa Carrizal anayekula mbegu . . . umeharibiwa na uhakika wa kwamba tumeharibu mahali ambapo ndege huyo aliishi na kujificha kwa muda mrefu.”

Safisha Ubao wa Kukatia Vyakula!

Ni ubao upi ulio salama, je, ni wa mbao au wa plastiki? Jarida UC Berkeley Wellness Letter linasema: “Ubao wowote ni mzuri mradi tu usafishwe vizuri sana. Iwe unatumia ubao wa mbao au wa plastiki kukatia nyama mbichi au kuku, baada ya kuutumia usugue kabisa kwa kutumia maji ya moto yenye sabuni.” Ikiwa ubao huo una mianya au mafuta, usafishe kwa uangalifu zaidi. Jarida Wellness Letter linasema: “Unaweza pia kuua viini kwenye ubao kwa kuulowesha katika maji yenye dawa ya kuondoa madoa (milimeta 5 za dawa ya kuondoa madoa zichanganywe na lita moja ya maji).” Unapaswa pia kunawa mikono vizuri, kuikausha kabisa, kusafisha visu kabisa, na kuhakikisha vimekaushwa.

Athari za Kompyuta kwa Watoto Ambao Hawajaenda Shule

Gazeti Vancouver Sun linaripoti kwamba watafiti fulani wanasema kuwa “kutumia kompyuta kwa muda mrefu badala ya kucheza kama ilivyokuwa zamani” hakuwafaidi watoto ambao hawajaenda shule na “kunaweza kuwafanya wajitenge na wengine, wawe na matatizo ya kukaza fikira, washindwe kuwa wabunifu na hata kushuka moyo na kuwa na mahangaiko.” Mwanasaikolojia Sharna Olfman anasema kwamba kompyuta humfanya mtoto awe na “maisha ya kuwazia tu anayoyaona kwenye kompyuta badala ya maisha halisi.” Watafiti husisitiza umuhimu wa “wazazi kucheza michezo ya kawaida na watoto” ili kuwafundisha “maneno mapya, rangi, maumbo, namba, adabu, na matukio ya kila siku.” Mwanasaikolojia Jane Healy anasema kwamba michezo iliyochezwa zamani ni muhimu sana tangu mtoto anapozaliwa hadi anapokuwa na umri wa miaka saba. Michezo hiyo inaweza kuwasaidia watoto kukaza fikira, lakini kompyuta ina matokeo tofauti.

Televisheni Ni Kama “Dawa ya Kulevya”

Gazeti La Vanguardia la Hispania linaripoti kwamba “watoto wanaotazama televisheni kwa zaidi ya saa mbili kila siku hawafanyi vizuri shuleni.” Ingawa anaamini kwamba televisheni inaweza kusaidia sana kuelimisha, daktari wa magonjwa ya watoto Francisco Muñoz anataja athari za kutazama televisheni kwa kiwango hicho. Muñoz anaamini kwamba watoto wengi wanaotazama televisheni kupita kiasi hawafanyi vizuri shuleni kwa sababu “wao huchukua muda mrefu kukomaa na uwezo wao wa kuelewa mambo hupungua.” Pia anasema: “Kuna uhusiano ulio wazi kati ya kutazama vipindi fulani vya televisheni, matangazo ya biashara, video za muziki na matumizi ya vileo, tumbaku, na dawa za kulevya miongoni mwa vijana waliobalehe.” Ingawa mtaalamu wa magonjwa ya akili ya watoto, Paulino Castells, anakubali kwamba si vijana wote ambao huiga mwenendo mbaya wanaouona kwenye televisheni, anaiita televisheni “dawa ya kulevya” kwa sababu ya “jinsi inavyodhuru akili za watoto wachanga.”

Madarasa Yenye Kelele

Gazeti Der Spiegel la Ujerumani linaripoti kwamba miangwi na kelele nyingine darasani hufanya iwe vigumu kwa wanafunzi kusikia. Mwanasaikolojia Maria Klatte anasema kwamba “kadiri ilivyo vigumu kwa watoto kuelewa, ndivyo ilivyo vigumu kwao kukumbuka.” Katika shule fulani za Ujerumani, watafiti walipata kwamba viwango vya sauti ni kati ya desibeli 70 na 90. Mtafiti wa sauti Gerhart Tiesler anaeleza hivi: “Katika maeneo ya kazi ambapo watu wanatakiwa kukaza fikira sana, kiwango cha sauti hakipaswi kupita desibeli 55. Watu wanapofanya kazi katika viwanda, inapendekezwa kutumia vifaa vya kuziba masikio kunapokuwa na kelele za desibeli 85 na zaidi.” Isitoshe, mwangwi unaotokea chumbani unapodumu kwa muda mrefu, iwe ni mwangwi wa maneno, msukumo wa kiti, au kukohoa, inakuwa vigumu zaidi kukaza fikira. Madari yanayozuia sauti na mwangwi usipenye, yanaweza kulinda neva na kuwasaidia walimu na wanafunzi wasipaaze sauti sana, lakini shule nyingi haziwezi kuyagharimia.

Maduka Makubwa Yanachukua Mahali pa Maduka Madogo

Jarida la sayansi la Ujerumani wissenschaft-online linasema: “Kuongezeka kwa maduka makubwa mashariki na kusini mwa Afrika kunahatarisha masoko madogo, na hivyo kuathiri njia ya kujiruzuku ya wakulima wa mashambani.” Tayari maduka makubwa 200 na maduka makubwa zaidi 10 huuza asilimia 30 ya chakula kinachouzwa nchini Kenya—kiasi hicho kinalingana na kile kinachouzwa na maduka madogo 90,000. Kulingana na Kostas Stamoulis wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo, ongezeko la haraka la watu wanaohamia mijini na kuenea kwa biashara za kimataifa “kunaonyesha kwamba kutakuwa na badiliko kubwa katika uuzaji wa chakula huko Afrika kuliko katika nchi zilizoendelea.” Wataalamu wanasema kwamba ili kuepuka matatizo ya kiuchumi, mashirika yanapaswa kuanzishwa ili kuuza mazao yanayotokezwa nchini na kuwaelimisha wakulima kukabiliana na badiliko hilo.