Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Matunda ya Pekee Kutoka Amazoni

Matunda ya Pekee Kutoka Amazoni

Matunda ya Pekee Kutoka Amazoni

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI BRAZILI

AÇAÍ, BACURI, NA CUPUAÇU. Je, unajua maneno hayo yanamaanisha nini? Huenda unajua, ikiwa unaishi Brazili. Hayo ni majina ya matunda matatu ya pekee kutoka eneo la Amazoni. Wabrazili hasa hufurahia ladha mbalimbali za matunda hayo yanapotumiwa kutayarisha vyakula fulani vya barafu. Lakini yanatumiwa kwa njia nyinginezo pia. Hebu tujifunze kuhusu matunda hayo ya pekee kutoka msituni.

Tunda la Açaí Linalofaidi Mwili

Mti wa açaí (Euterpe oleracea), ambao ni aina fulani ya mchikichi wa tropiki, ni mwembamba na husitawi katika maeneo yenye umajimaji, vinamasi, na hasa kwenye milango ya Mto Amazoni na Tocantins katika jimbo la Pará. Mti huo hupatikana katika Pwani ya Atlantiki ya Brazili, toka Jimbo la Pará hadi Jimbo la Bahia. Kwa sababu kuna joto jingi katika maeneo ambayo miti ya açaí inakuzwa, inaelekea utatokwa jasho sana. Shina jembamba na lenye nguvu la mti wa açaí lina urefu wa meta 23 hivi na huwa na majani kwenye kilele chake.

Kati ya mwezi wa Agosti na Desemba, mchikichi huo huwa na vichala sita hadi nane vya matunda ya açaí, kila kimoja kikiwa na matunda 700 hadi 900. Lakini mtu huwezaje kuyachuma matunda hayo? Watu wanaochuma matunda hutengeneza mshipi kwa kusokota nyuzi za miti midogo ya açaí. Kisha wanaifunga miguu yao kwa mshipi huo na kuufinyilia kwenye shina. Miguu inapokuwa imeshikiliwa vizuri kwenye shina, wao huinua mikono na kujivuta juu huku wakisogeza miguu yao hatua kwa hatua hadi wanapofika juu. Kisha wanachuma kichala cha matunda. Je, wao hukitupa chini? Hapana, kwani wakifanya hivyo watayaharibu matunda. Wanashuka kama walivyopanda, lakini wanahitaji kubeba matunda kwa uangalifu.

Tunda la açaí hutayarishwaje? Kijana mmoja kutoka Pará anayeitwa Eduardo anaeleza: “Mama yangu huweka tunda hilo katika sufuria lenye maji ya moto. Kisha anakoroga tunda hilo mpaka ngozi yake na tabaka jembamba la bluu linapotengana na mbegu zake kubwa.” Tunda hilo lina kalori nyingi, chuma, kalisi, fosforasi, potasiamu, na vitamini B1 na B2. Si ajabu kwamba wanariadha hulitumia kuongeza nguvu na akina mama hulitumia kuwalisha watoto wao! Wabrazili wengi hupenda kunywa maji ya açaí yaliyochanganywa na maji, sukari, na wanga wa mhogo. Eduardo anapenda kutumia tunda la açaí kukoleza mihogo na uduvi uliokaushwa. Tunda hili hupondwa katika maji ya moto na kuchujwa kwa kichungi na kutokeza kinywaji kizito chenye harufu nzuri. Hata hivyo, hiyo ni faida moja tu ya açaí.

Mti wa açaí una matumizi mengine mengi. Kabeji ya mti huo inayoitwa palmito huwa laini na nyeupe na hupatikana kwenye tumba la mwisho, na watu hupenda kuitumia katika saladi. Mizizi yake hutumiwa kutengeneza dawa za kuua vimelea, na nyuzi zake hutumiwa kutengeneza fagio. Majani yake hutumiwa kulisha wanyama na kutengeneza karatasi, na shina lake hutokeza mbao nzuri za ujenzi.

Mti wa Bacuri na Cupuaçu

Mti wa bacuri (Platonia insignis) ni maridadi, na una urefu wa kati ya meta 20 na 30. Matawi yake ya juu yana umbo la pia iliyopinduliwa. Ukubwa wa tunda hilo umekaribiana na ule wa chungwa na lina umbo la yai na ngozi nzito ya manjano. Tabaka lake jeupe linalofunika mbegu huwa tamu na chungu, lenye kunata, na lenye harufu nzuri. Tabaka hilo lenye umajimaji huwa na fosforasi, chuma, na vitamini C nyingi. Wabrazili husaga bacuri kutengeneza shira, jeli, rojo, na vinywaji. Mbegu zake nyeusi zenye wekundu-wekundu na zenye mafuta hazitupwi bali hutumiwa kutibu magonjwa ya ngozi. Mbao za manjano za bacuri hutumiwa katika ujenzi.

Mti wa cupuaçu (Theobroma grandiflorum) ni wa jamii ya mti wa kakao ambao unajulikana sana (Theobroma cacao). Mafuta yaliyo katika mbegu za cupuaçu yanafanana na siagi ya kakao inayotumiwa kutengeneza chokoleti. Ingawa mti wa cupuaçu hukua kiasili katika eneo la Amazoni lenye joto, unakuzwa pia kotekote nchini Brazili. Mti huo husitawi vizuri hasa katika jimbo la pwani la Espírito Santo.

Kwanza mti wa cupuaçu hupata gome lenye rangi ya kahawia-nyekundu ambalo lina nguvu na hutumiwa kutokeza mbao. Kisha unapofikia mwaka wa nane, mti huo huchanua maua na kutokeza matunda. Matawi yake marefu yenye majani ya kahawia-nyekundu huwa na matunda ya kahawia yenye umbo la yai. Kila tunda huwa na uzito wa kati ya kilo 1 na 1.5. Mwanzoni, huenda ukachukia harufu yake kali. Lakini tabaka lake jeupe la ndani, lenye harufu nzuri na asidi, linafaa sana katika utayarishaji wa vyakula vitamu.

Iwapo utatembelea Brazili, jaribu kuonja ladha ya matunda mbalimbali yanayopatikana huko. Maduka ya aiskrimu katika majiji makubwa ya Brazili yanauza aiskrimu nyingi zenye ladha mbalimbali. Ni kweli kwamba unapoagiza vyakula hivyo vitamu itakuwa vigumu kutamka majina yake kama vile, jaca, umbu, biribá, buriti, mangaba, murici, sapoti, cajarana, graviola, maracujá, au jabuticaba. Lakini utafurahia ladha yake!

[Picha katika ukurasa wa 15]

“Açaí”

[Hisani]

André Valentim/Tyba/BrazilPhotos

[Picha katika ukurasa wa 15]

Mtu anayechuma “açaí” akipanda mti

[Hisani]

Lena Trindade/BrazilPhotos

[Picha katika ukurasa wa 16]

Matunda ya “Bacuri,” na mti upande wa kushoto

[Hisani]

Bacuri fruit: Geyson Magno/Ag. Lumiar

[Picha katika ukurasa wa 17]

“Cupuaçu”

[Picha katika ukurasa wa 17]

Aiskrimu tamu ya “cupuaçu” na mti ukiwa nyuma

[Hisani]

Background: Silvestre Silva/Reflexo