Michezo ya Olimpiki Yarudi Nyumbani
Michezo ya Olimpiki Yarudi Nyumbani
UCHIMBUZI wa vitu vya kale ulisababisha kuanzishwa tena kwa Michezo ya Olimpiki. Vitu vilivyochimbuliwa katika Olympia ya kale huko Ugiriki vilimchochea Baroni Mfaransa Pierre de Coubertin kuanzisha jitihada za kufufua michezo hiyo. Hivyo michezo ya kwanza ya Olimpiki katika nyakati za kisasa ilifanywa huko Athens mwaka wa 1896.
Katika miaka iliyotangulia mwaka wa 2004, buldoza na vifaa vingine vya kuchimba vilitumiwa kutayarishia michezo hiyo ambayo itafanywa mahali ilipoanzia. Jiji kuu la Ugiriki lilipokuwa likijengwa upya kwa ajili ya Olimpiki, lilionekana kama eneo kubwa la ujenzi.
Michezo ya Olimpiki ya 2004 imepangiwa kufanywa Agosti 13 hadi 29 huko Athens. Wachezaji 10,000 hivi kutoka nchi 201, ambayo ni idadi kubwa zaidi ya nchi zilizowahi kushiriki, watashiriki katika michezo 28. Michezo hiyo itafanywa katika maeneo 38 tofauti-tofauti, na kutakuwa na zaidi ya sherehe 300 za kuwakabidhi washindi medali. Waandishi wa habari wapatao 21,500 na walinda-usalama 55,000 hivi watakuwapo.
Kushinda Vizuizi
Kwa muda mrefu Athens ilijaribu kurudisha Michezo ya Olimpiki mahali ilipoanzia. Kwa kuwa mwaka wa 1996 ulikuwa mwaka wa 100 wa mashindano hayo katika nyakati za kisasa, ilionekana kwamba huo ni wakati unaofaa zaidi wa kuirudisha michezo ya Olimpiki katika nchi ilimoanzia.
Hata hivyo, ombi la Athens la kupangia michezo hiyo ya mwaka 1996 halikufaulu. Ilisemekana kwamba jiji hilo halikuwa na vifaa na huduma za msingi zilizohitajiwa kwa ajili ya michezo hiyo ya majuma mawili yenye shughuli nyingi.
Kukataliwa kwa ombi hilo kuliwachochea maofisa wa Ugiriki na wa jiji lake kuu kuchukua hatua. Maofisa hao wakaahidi kurekebisha mambo. Wakiwa na makusudi mazuri na mipango madhubuti, walituma maombi yao tena mwaka wa 1997 ili Michezo ya Olimpiki ya 2004 ifanywe katika jiji hilo. Ombi lao likakubaliwa.
Jiji la Athens lilijitayarisha kufanya mabadiliko. Tamaa ya kuipangia michezo hiyo ilichochea jitihada nyingi na maendeleo. Mashine zilitumiwa kuchimba
ardhi ili kuboresha huduma za msingi na kutengeneza barabara na nyanja za michezo. Mashine za kuchimba, kreni, na watu walionekana wakifanya kazi kwa bidii kila mahali mwishoni mwa juma, hata kukiwa na joto kali la kiangazi.Mnamo Machi 2001 ndege ya kwanza ilitua katika uwanja wa ndege wa Athens, ambao umeonwa kuwa mmojawapo wa nyanja maarufu zaidi ulimwenguni. Pia barabara mpya zenye urefu wa kilometa 120 zilipangwa kutengenezwa, na nyingine zenye urefu wa kilometa 90 zilipangwa kurekebishwa. Madaraja 40 yanayopita juu ya barabara yalitiwa ndani ya mpango wa marekebisho ili kupunguza msongamano wa magari. Reli mpya za kupita chini ya ardhi zilijengwa huku kukiwa na mipango ya kuongeza reli nyingine zenye urefu wa kilometa 24. Reli yenye urefu wa kilometa 32 inayopita kwenye vituo vingi vya magari-moshi ilijengwa kupunguza msongamano wa magari na uchafuzi wa hewa.
Kwa ufupi, kwa miaka michache tu Athens limebadilika na kuwa jiji jipya, lenye mimea, mazingira safi, na mfumo mpya wa usafiri. Jacques Rogge, msimamizi wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki alisema: “Watu waliojua jiji la Athens kabla ya michezo hiyo na kuliona baada ya michezo hiyo hawatalitambua.”
Matayarisho ya Muda Mrefu
Kadiri sherehe ya ufunguzi ilivyozidi kukaribia, ndivyo jitihada zilivyozidishwa. Rogge, msimamizi wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki, aliyalinganisha matayarisho na maendeleo ya ujenzi na dansi ya utamaduni ya Kigiriki inayoitwa syrtaki. Alisema hivi kwa utani: “Ninaweza kuyafananisha na muziki kama vile syrtaki. Huanza polepole sana, kisha mwendo wake unazidi kuongezeka, na hatimaye huwezi kufuatana nao.”
Kupatana na maelezo hayo, Kijiji cha Olimpiki “ambacho ni sehemu kuu ya matayarisho ya Michezo ya Olimpiki,” kilichipuka haraka katika mojawapo ya viunga vya kaskazini huko Athens. Mradi wa kujenga kijiji hicho ambacho kitakuwa makao ya wanariadha 16,000 na maafisa wa timu wakati wa michezo ya Olimpiki, ndio mradi mkubwa wa ujenzi kuwahi kufanywa nchini Ugiriki. Baada ya michezo hiyo wakazi 10,000 wataishi humo.
Wasimamizi wa Olimpiki wamezingatia uhusiano kati ya historia ya kale na michezo ya kisasa. Sherehe fulani zitafanywa katika Olympia ya kale. Huku michezo ya Olimpiki ikiendelea, kutakuwa na maonyesho ya tamaduni na watu watatembelea maeneo ambamo vitu vya kale vimechimbuliwa. Kituo cha kupeleka mashua kilijengwa karibu na mahali ambapo vile vita vya Marathon vinavyojulikana sana vilipiganiwa. Wakimbiaji wa mbio za masafa marefu wataweza kusema kwamba wamepitia njia iliyotumiwa
awali. Wasimamizi wa michezo hiyo wamechagua njia ileile iliyotumiwa na askari-jeshi Mwathene ambaye katika mwaka wa 490 K.W.K., alikimbia kilometa 42 kutoka Marathon hadi Athens ili kutangaza kushindwa kwa Waajemi.Mshindi wa Dhahabu Ni . . .
Fataki zitakapolipuliwa kwenye sherehe za ufunguzi za mashindano hayo, macho yote yataelekezwa kwenye Uwanja wa Olimpiki unaotoshea watu 75,000. Kwa wengi, uwanja huo uliorekebishwa ndio sehemu ya pekee zaidi kati ya vituo vyote vya Olimpiki huko Athens. Kinachofanya uwanja huo kuwa wa pekee ni paa yake iliyobuniwa na Santiago Calatrava, msanifu-ujenzi maarufu kutoka Hispania.
Paa hiyo ni kazi bora ya sanaa kwani imetengenezwa kwa vioo vyenye uzito wa tani 16,000 na ina ukubwa wa meta 10,000 za mraba. Itashikiliwa na matao mawili makubwa sana kila moja likiwa na urefu wa meta 304 na kimo cha meta 80—imezidi ukubwa wa Daraja la Bandari ya Sydney huko Australia kwa thuluthi mbili! Kulingana na mtaalamu mmoja wa ujenzi, kila chuma kilichotumiwa kutengeneza matao hayo kina uzito wa kati ya tani 9,000 na 10,000 na “kina upana mkubwa kuliko basi.” Inatazamiwa kwamba uzito wa paa hiyo utakuwa mara mbili ya ule wa Mnara wa Eiffel huko Paris.
Kwa nini paa kubwa sana hivyo inahitajiwa? Fikiria joto kali la mwezi wa Agosti huko Athens! Vioo hivyo vimetandazwa rangi ya pekee inayorudisha asilimia 60 ya mwangaza wa jua. Kuna sababu nyingine pia. Muundo wa paa hiyo ulionwa kuwa sehemu ya pekee zaidi ya michezo hiyo. Kama vile aliyekuwa waziri wa utamaduni wa Ugiriki, Evangelos Venizelos alivyosema, “paa hiyo ndiyo sehemu ya kuvutia ya ujenzi na inawakilisha michezo ya Olimpiki ya Athens.”
Baada ya sherehe za kufunga, sehemu hizo za kuvutia zitawakumbusha watu kazi ngumu iliyofanywa kupangia tukio kubwa kama hilo. Waathene wanatumaini kwamba vifaa na huduma zote za msingi zilizotayarishwa kwa ajili ya Olimpiki, zitaboresha hali ya maisha katika jiji lao. Na kama kawaida, wataendelea kushughulikia matatizo yao kwa utaratibu, kama wanavyocheza dansi ya syrtaki.
[Sanduku katika ukurasa wa 15]
Maadili ya Mashindano Yajaribiwa
Wasimamizi wa Olimpiki hupenda kukazia maadili yanayohusianishwa na michezo hiyo, yaani, “mashindano yanayofaa, michezo, amani, tamaduni, na elimu.” Hata hivyo, mambo yasiyofaa kuhusu michezo hiyo yanatia ndani siasa, utaifa, biashara, na ufisadi.
Kama kawaida, Olimpiki hutazamwa na watu wengi sana kwenye televisheni na imekuwa njia ya kutangaza biashara, na hivyo kudhamini mashindano hayo ni nafasi kubwa sana ya kutangaza bidhaa mbalimbali. Mtafiti Mwaustralia Murray Phillips alisema: “Sasa Olimpiki ni biashara kubwa na maamuzi mengi hufanywa hasa kwa sababu za kibiashara.”
Wengine wanashutumu utaifa unaoonyeshwa wazi katika michezo hiyo. Jitihada zinafanywa kuanzisha mkataba wa Olimpiki ambao utakomesha uhasama na vita wakati wa michezo hiyo. Hata hivyo, mkataba huo hauwezi kufanikiwa ikiwa visababishi vya uhasama havijakomeshwa. Profesa wa sayansi, Brian Martin alisema: “Michezo hiyo hutumiwa kuendeleza siasa za mabavu.” Aliongezea hivi: “Katika Olimpiki, mashindano baina ya wanariadha huonwa kuwa mashindano kati ya nchi mbalimbali. Wanariadha hawawezi kushiriki iwapo nchi zao hazishiriki. Ushindi wa wachezaji mmoja-mmoja na vikundi vya wachezaji huonwa kuwa ushindi wa taifa, unaowakilishwa na bendera na nyimbo za taifa . . . [Olimpiki] pamekuwa mahali pa kuendeleza jeuri kati ya wanamichezo na kati ya nchi mbalimbali zinazopigania mamlaka na cheo. . . . Wasimamizi na wadhamini wa Olimpiki wameshindwa kutimiza kusudi la awali la michezo hiyo la kuendeleza amani.”
[Picha katika ukurasa wa 15]
Uwanja wa michezo ya Olimpiki wa Athens
Muundo wa medali za 2004
[Hisani]
Aerial photo: AP Photo/Thanassis Stavrakis; medal design: © ATHOC
[Picha katika ukurasa wa 16]
Gari-moshi la chini ya ardhi huko Athens
Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Athens ➤
[Hisani]
© ATHOC
[Picha katika ukurasa wa 17]
Ujenzi wa Kijiji cha Olimpiki
Kituo cha Mashua cha Agios Kosmas
[Hisani]
© ATHOC/Photo: K. Vergas
[Picha katika ukurasa wa 16, 17]
Ujenzi wa paa ya Uwanja wa Olimpiki
[Picha katika ukurasa wa 17]
Mfano mdogo wa paa iliyokamilishwa
[Hisani]
© ATHOC
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 14]
© ATHOC