Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kukabili Janga la Chumvi

Kukabili Janga la Chumvi

Kukabili Janga la Chumvi

Na mwandishi wa Amkeni! nchini Australia

CHUMVI ni muhimu kwa uhai wa wanadamu na wanyama. Asilimia 1 hivi ya miili yetu imefanyizwa kwa chumvi. Tunaitumia katika chakula, dawa, na vyakula vya mifugo. Kwa kweli, watu ulimwenguni hutumia tani milioni 190 hivi za chumvi kila mwaka. * Hata hivyo, kitu hicho muhimu na kinachopatikana kwa wingi kinasababisha madhara kwa baadhi ya maeneo ya kilimo yanayozaa sana ulimwenguni.

Karibu asilimia 40 ya chakula kinachokuzwa ulimwenguni huzalishwa katika asilimia 15 ya mashamba yanayomwagiliwa maji ulimwenguni. Kwa kweli, kumwagilia maji maeneo makavu kunaweza kuyafanya yachanue kama waridi. Hata hivyo, kumwagilia maji mashamba kunaweza kusababisha chumvi irundamane ndani ya udongo na hivyo kuuharibu pole kwa pole. Tayari uzalishaji wa mazao umepungua kwa sababu ya kuongezeka kwa chumvi katika udongo kwenye asilimia 50 ya mashamba yote yanayomwagiliwa maji ulimwenguni. Ama kweli, inasemekana kwamba eneo lenye ukubwa unaopita ule wa Uswisi kwa zaidi ya mara mbili huharibiwa kila mwaka kwa sababu ya kurundamana kwa chumvi na maji!

Katika kitabu chake Out of the Earth, Daniel Hillel, mwanasayansi maarufu wa udongo, anaonya hivi: “Majanga yote yaliyosababishwa na wanadamu na kudhuru jamii za kale yanatukia katika ulimwengu wa leo . . . lakini kwa kadiri kubwa zaidi.” Inasemekana kwamba kurundamana kwa chumvi kunasababisha hasara ya dola bilioni 5 kila mwaka nchini Marekani kupitia uharibifu wa mazao. Hata hivyo, Australia ni mojawapo ya maeneo yanayokumbwa zaidi na janga hilo.

Janga la Chumvi

Eneo lenye ukubwa wa uwanja wa mpira huharibiwa kila saa moja katika mashamba makubwa ya ngano huko Australia Magharibi. Dakt. Tom Hatton wa Shirika la Utafiti wa Sayansi na Viwanda (CSIRO) anasema: “Bila shaka, hili ndilo tatizo kubwa zaidi la kimazingira ambalo tunakabili.”

Eneo kuu la kilimo mashariki mwa Australia, linaloitwa Eneo la Murray-Darling, ndilo hasa linalokumbwa na kurundamana kwa chumvi. Eneo hilo ni kubwa kama Ufaransa na Hispania zinapounganishwa, na robo tatu ya mashamba yanayomwagiliwa maji nchini Australia hupatikana huko. Karibu nusu ya mapato yote ya kilimo ya Australia hutoka huko. Mito ya Murray na Darling ambayo ndiyo mito mikuu inayotumiwa kumwagilia maji eneo hilo la kilimo, hutosheleza maelfu ya maeneo yenye umajimaji na vilevile ndiyo chanzo cha maji kwa watu milioni tatu.

Kwa kusikitisha, tayari kurundamana kwa chumvi kumeharibu ardhi yenye ukubwa wa kilometa 2,000 za mraba, na wanasayansi wanakadiria kwamba kilometa nyingine 10,000 za mraba zitaharibiwa katika kipindi hiki cha miaka kumi. Kiasi cha chumvi kinaongezeka katika Mito ya Murray na Darling na vijito vyake, na katika maeneo fulani maji hayafai kunywewa. Sehemu zenye umajimaji wenye chumvi zinaongezeka katika maeneo yenye rutuba yaliyo kwenye kingo za mito hiyo.

Hata hivyo, si mashamba tu yanayokabili hatari. Wanasayansi wa Shirika la CSIRO wanasema kwamba kwa sababu ya kurundamana kwa chumvi mimea na wanyama elfu moja wa Australia wanakabili hatari ya kutoweka. Pia, hali hiyo ikiendelea, huenda nusu ya jamii za ndege katika Eneo la Murray-Darling zitatoweka katika miaka 50 ijayo. Hebu fikiria jinsi kutopangia mambo kumesababisha tatizo hili la kimazingira.

Chanzo cha Chumvi Hiyo

Wanasayansi wanakata kauli kwamba kiasi kikubwa cha chumvi katika Australia kilitokana na ukungu kutoka baharini uliosukumwa bara kwa muda mrefu. Mvua iliponyesha, chumvi iliyokuwa katika ukungu ilifika ardhini. Pia wanasema kwamba kiasi kingine cha chumvi kilibaki katika maeneo ambayo zamani yalikuwa yamefunikwa na bahari. Chumvi hiyo iliyeyushwa na maji ya mvua kisha maji hayo yakapenya kwenye matabaka ya udongo, na matabaka ya maji yakafanyizwa pole kwa pole chini ya udongo wenye chumvi.

Baada ya muda, mikalitusi na mimea mingine ilienea katika bara hilo na kutokeza mizizi iliyopenya zaidi ya meta 30-40 chini ya ardhi. Mimea hiyo ilifyonza maji mengi ya mvua yaliyofika ardhini na kuyarudisha juu, kisha yakavukizwa kutoka kwenye majani. Hilo lilifanya matabaka ya maji yashuke chini sana ardhini. Lakini mbinu za kilimo za Ulaya, zilizoleta ufanisi na maendeleo huko Australia, zilihusisha ukataji wa miti na mimea katika mashamba makubwa. Kwa sababu ya kukatwa kwa miti hiyo yenye mizizi mirefu na kuenea kwa mbinu ya kumwagilia maji mashamba, matabaka ya maji yaliinuka. Hivyo, chumvi iliyokuwa ardhini kwa muda mrefu ikayeyushwa na kuinuliwa karibu na udongo wa juu wenye rutuba.

Visababishi vya Tatizo la Kurundamana kwa Chumvi

Kumwagilia maji mashamba kwa kiasi huongeza uzalishaji wa mazao katika Eneo la Murray-Darling. Hata hivyo, mbinu hiyo huinua haraka matabaka ya maji kwenye mashamba hayo. Kisha maji hayo yenye chumvi yaliyo chini ya ardhi huingia kwenye mito na kuchafua maji safi. Hilo ni tatizo lingine. Maji hayo yenye chumvi hurudishwa wakati mashamba yanapomwagiliwa maji na tatizo hilo huongezeka na kujirudia-rudia.

Hata hivyo, kurundamana kwa chumvi kunaweza pia kusababishwa na aina ya mimea inayokuzwa wala si kwa sababu ya kumwaga maji kwenye mashamba. Katika eneo lote la Murray-Darling, miti yenye mizizi mirefu imekatwa na badala yake kuna nyasi na mimea inayokuzwa kila mwaka yenye mizizi inayopenya meta chache tu udongoni. Maji ya mvua ambayo hapo awali yalifyonzwa na miti sasa yanapenya chini ardhini.

Hivyo, wanasayansi wanakadiria kwamba kiasi cha maji kinachopenya kwenye tabaka la maji chini ya ardhi ni mara 10 hadi 100 zaidi ya ilivyokuwa wakati miti ilipokuwapo katika eneo hilo. Maji mengi sana yamepenya ardhini katika muda wa miaka mia moja iliyopita hivi kwamba matabaka ya maji yameinuka kwa meta 60 au zaidi katika sehemu fulani za Eneo la Murray-Darling. Matabaka hayo ya maji ya chumvi yanapofikia meta chache tu kutoka juu ya ardhi, wakulima huanza kukabili matatizo.

Sehemu fulani za mashamba yaliyokuwa na rutuba zamani hazizalishi vizuri tena. Muda mrefu kabla ya chumvi kuanza kurundamana katika sehemu fulani, maji yenye chumvi karibu na uso wa ardhi, huvukizwa. Mwanzoni, mimea hustahimili hali hiyo, lakini kadiri chumvi nyingi zaidi inavyovukizwa na kuongezeka kwenye udongo wa juu, ndivyo ardhi inavyopoteza rutuba.

Kurundamana kwa chumvi kunakosababishwa na aina ya mimea inayokuzwa hakuathiri tu wakulima. Tayari kumeharibu barabara fulani kuu, na kupunguza muda ambao barabara hizo zingetumika kwa asilimia 75. Pia kunaharibu majengo, mabomba ya maji safi na ya maji machafu katika miji ya mashambani kotekote katika Eneo la Murray-Darling.

Je, Hali Hiyo Inaweza Kurekebishwa?

Inaonekana kwamba mengi ya matabaka ya maji ya chumvi yataendelea kuinuka katika miaka 50 hadi 100 ijayo. Ripoti moja inasema kwamba kufikia wakati ambapo mtoto anayezaliwa leo atafikia umri wa miaka 30, eneo lenye ukubwa unaolingana na jimbo la Victoria, au unaokaribia ukubwa wa Uingereza, litaharibiwa. Ni nini kinachohitajiwa kurekebisha hali hiyo?

Ripoti moja ya serikali inasema kwamba “tunahitaji kubadili kabisa usimamizi na matumizi ya mali asili za Eneo hilo [la Murray-Darling] ili kudumisha mifumo ya ikolojia na kupata mazao. Kutakuwa na gharama nyingi . . . Hata hivyo, gharama hizo si kubwa sana zikilinganishwa na hasara zisizoepukika za kiuchumi, kimazingira, na kijamii zitakazotokea ikiwa njia za usimamizi za sasa hazitabadilishwa.”

Kupanda miti kwa wingi kunaweza kusuluhisha tatizo hilo, lakini kwa sasa hatua hiyo haionekani kuwa yenye faida. Ripoti moja ya kisayansi ilisema: “Hatuwezi kurudia hali za kiasili. Kwa sehemu kubwa, maendeleo yoyote yanayoweza kutukia [kwa kupanda miti] yatatukia polepole.”

Kwa sasa, wakulima wanatiwa moyo kupanda mimea yenye mizizi mirefu au mimea inayoweza kustahimili chumvi. Hata wafanyabiashara fulani wanakusanya chumvi ambayo imeharibu mashamba yao na kujiruzuku kwa njia hiyo. Wengine wanapanga kutumia vidimbwi vya maji ya chumvi kufuga na kisha kuuza samaki wa baharini, kamba, na hata magugu-maji.

Si Australia peke yake inayokumbwa na hali hiyo. Hata hivyo, ni kweli kwamba mabadiliko makubwa yasipotukia haraka, maneno haya ya mwanafalsafa Mgiriki Plato kuhusu Ugiriki ya kale yataonekana kuwa utabiri wenye kuhuzunisha: “Kinachosalia katika nchi hiyo iliyokuwa yenye rutuba ni kama mifupa mitupu ya mtu mgonjwa, huku sehemu bora ya nchi ikiwa imeharibika na udongo kupoteza rutuba.”

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 3 Chumvi inayotumiwa sana ni kloridi-sodiamu. Chumvi nyingine muhimu ni kloridi-potasiamu na naitreti ya amonia.

[Ramani katika ukurasa wa 25]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

ENEO LA MURRAY- DARLING

[Hisani]

Map: Mountain High Maps® Copyright © 1997 Digital Wisdom, Inc.

[Picha katika ukurasa wa 25]

Mabaki ya chumvi yakiwa kwenye gogo la mti katikati ya eneo lililojaa maji

Mashamba yaliyokuwa na rutuba yaharibiwa kwa kurundamana kwa chumvi kwenye udongo wa juu

[Hisani]

© CSIRO Land and Water

[Picha katika ukurasa wa 26]

Ishara za kwanza za janga hilo—sehemu zisizo na rutuba katika mashamba yenye rutuba

Chumvi inayoinuka na kufika kwenye udongo wa juu huua mimea

Madhara ya chumvi katika mashamba yaliyokuwa yakizaa sana

Matokeo ya mwisho ya matabaka ya maji yaliyo chini ya ardhi yanayoinuka

[Hisani]

All photos: © CSIRO Land and Water