Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Viumbe Vingi Ajabu Baharini

“Sasa wanabiolojia wa kimataifa wa viumbe wa baharini wanagundua zaidi ya aina mpya 30 za viumbe kila juma,” lasema gazeti Leipziger Volkszeitung la Ujerumani. Tangazo hilo lilitolewa likiwa sehemu ya ripoti ya kwanza ya maendeleo kuhusu Hesabu ya Viumbe vya Majini, ambao ni mradi wa miaka kumi ulioanza mwaka wa 2000 na unahusisha wanasayansi 300 kutoka nchi 53. Watafiti wanaamini kwamba “huenda kuna zaidi ya aina milioni mbili za wanyama na mimea baharini,” lasema gazeti hilo. “Huenda zaidi ya asilimia 95 ya aina za wanyama waliomo baharini hazijulikani.”

Vilivyopotea na Kupatikana

Katika mwaka wa 2002, watu walipeleka zaidi ya dola milioni 23 taslimu kwenye Kituo cha Polisi cha Vitu Vilivyopotea na Kupatikana huko Tokyo Japani, laripoti gazeti la The New York Times. Asilimia 72 ya pesa hizo zilirudishwa kwa wenyewe. Kituo hicho kikubwa pia kina mamia ya maelfu ya vitu vingine kama vile simu za mkononi, funguo, miwani, vifaa vya kuchezea, na hasa miavuli kwani miavuli 330,000 ilipelekwa huko mwaka wa 2002. Gazeti The Times linasema “Watoto hufundishwa toka utotoni kupeleka chochote wanachopata kwa polisi.” Watu mia mbili hadi mia tatu huenda kwenye kituo hicho kila siku kuchukua mali zao. Inashangaza kwamba baadhi ya vitu vilivyopotea ni kama vile mikongojo na viti vya magurudumu. “Sijui kilichowapata wenyewe,” anasema Hitoshi Shitara, afisa ambaye amekuwa akitoa huduma ya vitu vilivyopotea na kupatikana kwa muda mrefu.

Kushinda Tabia ya Kuchelewa

Kampeni ya kitaifa ya kupambana na tabia ya kuchelewa imeanzishwa huko Ekuado. Kulingana na gazeti Economist inakadiriwa kwamba, mbali na madhara yanayosababishwa na tabia hiyo, Ekuado hupoteza dola milioni 742 kila mwaka kwa sababu ya kuchelewa. Hiyo ni asilimia 4.3 ya jumla ya mapato ya taifa hilo. Ripoti hiyo inasema kwamba “zaidi ya asilimia 50 ya shughuli zote za umma hazianzi kwa wakati.” Kampeni hiyo imefanikiwa kwa kadiri fulani. “Wale wanaochelewa hawaruhusiwi kuingia mikutanoni,” lasema gazeti The Economist, na “gazeti moja la habari la huko linachapisha majina ya wale wanaochelewa kwenye shughuli mbalimbali.”

Vijana na Kompyuta

Kulingana na ripoti ya Wizara ya Elimu ya Marekani, nchini humo “asilimia 90 hivi ya watu walio na umri wa kati ya miaka 5 na 17 hutumia kompyuta na asilimia 59 kati yao hutumia Intaneti—idadi hiyo inapita idadi ya watu wazima wanaotumia kompyuta,” laeleza jarida la The Wall Street Journal. Watu huanza kutumia kompyuta wakiwa wachanga. “Karibu robo tatu ya watoto huanza kutumia kompyuta wakiwa na umri wa miaka mitano, na wengi wao huanza kutumia Intaneti wakiwa na umri wa miaka tisa,” ripoti hiyo inasema. Ingawa zaidi ya asilimia 50 ya vijana hutumia Intaneti kuwasiliana na marafiki au kucheza michezo, “karibu asilimia 75 hutumia Intaneti kufanya kazi za shule,” laeleza jarida hilo. “Wasichana, ambao kufikia karibuni hawakuwa wakitumia kompyuta na Intaneti sana kama wavulana, sasa wanaitumia kwa muda mwingi kama wavulana.”

Chakula Chenye Afya cha Ugiriki

Gazeti Readers Digest linaripoti kwamba “wanasayansi wa Chuo Kikuu cha Harvard na wa Shule ya Tiba ya Chuo Kikuu cha Athens walichunguza mazoea ya kula ya Wagiriki 22,043 kwa karibu miaka minne na kutambua kwamba chakula cha maeneo ya Mediterania hupunguza uwezekano wa kufa kutokana na kansa na magonjwa ya moyo kwa asilimia 25 au zaidi. Wagiriki hula sana njugu, matunda, mboga, maharagwe, nafaka, mafuta ya mzeituni, na samaki, pia wao hutumia kwa kiasi mazao ya maziwa, kileo, na nyama kidogo.” Faida za kiafya za vyakula vinavyoliwa katika maeneo ya Mediterania zimeonekana mara nyingi.

Watoto Wanaolazimika Kuishi Barabarani

Gazeti Wprost linasema kwamba umaskini umewalazimisha watoto zaidi ya milioni moja huko Poland waishi barabarani. Kwa kawaida, watoto hao wana umri wa kati ya miaka 8 na 15 na “tayari wao ndio wanaotafutia familia zao riziki,” kulipa kodi ya nyumba na kuwaandalia ndugu zao wadogo chakula, hata kuwapa pesa wazazi wao walio na mazoea sugu ya kutumia kileo. Ingawa mwanzoni huenda wakachuma pesa kwa njia halali, wengi wao hugeukia “wizi, ulanguzi wa dawa za kulevya na kileo, kulaghai vijana wenzao, na ukahaba.” Kulingana na Marek Liciński wa Kituo cha Kijamii cha Powiślańska, “tatizo kubwa wanalokabili watoto hao si jeuri wala uhalifu; bali ni kwamba hawana makwao wala watu wa kuwategemeza.”

Vyakula vya Ngozi

Vyakula vinazidi kutumiwa katika vipodozi na bidhaa za kuboresha afya. Zaidi ya chokoleti, vyakula vingine vya msingi kama vile mafuta ya mzeituni vinatumiwa. Gazeti la Ujerumani Frankfurter Allgemeine Sonntagszeitung linaripoti kwamba “wengine wanaamini kwamba kuoga kwa kakao yenye povu kukiwa na nuru ya mishumaa, kisha kukandwa mwili kwa mafuta ya kakao moto na umajimaji wa chokoleti husaidia kuzuia ngozi isizeeke. Je, jambo hilo ni kweli? Profesa Volker Steinkraus wa Taasisi ya Elimu ya Ngozi huko Hamburg anasema: “Ingawa inadhaniwa kwamba krimu zilizotengenezwa kwa kakao zinaweza kuzuia mtu asizeeke haraka, jambo hilo halijathibitishwa kisayansi.”

Wanawake Wanatafuta Ponografia

Gazeti Plain Dealer la Cleveland, Ohio, Marekani, linasema: “Katika miaka ya karibuni, mamilioni ya wanawake wamevutiwa sana na ponografia kwa sababu wanaweza kuipata kwa urahisi, na kwa gharama ya chini na bila kujulikana kwenye Intaneti. Yaelekea mmoja kati ya watu watatu wanaotazama vituo vya Intaneti vyenye picha chafu ni mwanamke.” Mama mmoja mwenye umri wa miaka 42 alianza kutazama ponografia “ili kufahamu kilichomvutia mume wake wa zamani.” Muda si muda, alikuwa akitumia saa 30 hivi kwa juma akitazama Intaneti ili kuamsha nyege.”

Hatari Zilizofichika za Deni la Usingizi

Gazeti Science News linaripoti hivi: “Mara nyingi watu wasiolala vya kutosha hawatambui kwamba uwezo wao wa kufikiri unapungua, na huenda wasisinzie.” Watu wenye umri wa kati ya miaka 21 na 38 walipojitolea kuchunguzwa kwa majuma mawili, ilionekana kwamba kutolala vya kutosha kwa siku chache tu kulipunguza uwezo wao wa kufikiri, kutia ndani kuwa chonjo na kuliathiri muda ambao wanatumia kuelewa mambo na kutenda. Kabla ya uchunguzi huo, wote walikuwa wakilala kwa saa saba hadi nane hivi kila usiku, lakini walipokuwa wakichunguzwa waligawanywa katika vikundi vinne. Kikundi kimoja kililala kwa saa nane, kingine kwa saa sita, na kingine kwa saa nne. Kikundi cha mwisho hakikuruhusiwa kulala hata kidogo kwa siku tatu. Walipopewa mitihani, ilionekana kwamba uwezo wa kufikiri wa wale waliolala kwa saa sita ulipungua na wa wale waliolala kwa saa nne ulipungua hata zaidi, lakini uwezo wa kufikiri wa wale waliolala kwa saa nane haukupungua.