Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuwahubiria Mbilikimo Kweli za Biblia

Kuwahubiria Mbilikimo Kweli za Biblia

Kuwahubiria Mbilikimo Kweli za Biblia

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI KAMERUN

Katika nchi zaidi ya 230 ulimwenguni, Mashahidi wa Yehova hujaribu kuwafikia “watu wa namna zote” wakiwa na ujumbe kuhusu Ufalme wa Mungu. (1 Timotheo 2:4; Mathayo 24:14) Watu hao wanatia ndani jamii ndogo ya Mbilikimo wa Afrika ambao kwa wastani huwa na kimo cha kati ya futi nne na futi nne na nusu. Wao huishi hasa katika misitu ya Jamhuri ya Afrika ya Kati, eneo la Kongo, na kusini-mashariki mwa Kamerun.

Mbilikimo walikutana na watu wa sehemu nyingine kwa mara ya kwanza wakati Farao Neferirkare wa Misri alipotuma kikundi cha wavumbuzi ili kutafuta chanzo cha Mto Nile. Wavumbuzi hao walisema kwamba walikutana na watu wafupi katika misitu iliyo katikati ya Afrika. Homer, mwandishi Mgiriki wa baadaye na mwanafalsafa Aristotle wanawataja Mbilikimo. Wazungu walikutana na watu hao katika karne ya 16 na 17.

Katika nyakati za kisasa, Mashahidi wa Yehova wamekuwa wakihubiri katika misitu ya Afrika. Ingawa Mbilikimo wamekubali ujumbe wa Ufalme, jitihada za kuwarudia hazijafanikiwa sana. Hiyo ni kwa sababu Mbilikimo hupenda kuhamahama kutoka sehemu moja hadi nyingine baada ya miezi kadhaa.

Mbilikimo ni watu wanaopenda amani na wenye haya, na inakadiriwa kwamba katika Afrika, idadi yao ni kati ya 150,000 na 300,000. Serikali, mashirika ya kimataifa, na makanisa yamejenga shule hasa kwa ajili ya Mbilikimo, na vilevile nyumba ndogo zinazofaana na maisha yao. Hata hivyo, jitihada nyingi ambazo zimefanywa kuwashawishi waishi mahali pamoja hazijafanikiwa sana.

Janvier Mbaki ametofautiana sana na wenzake kwani ndiye Mbilikimo wa kwanza kuripotiwa kuwa Shahidi nchini Kamerun. Alikubali ujumbe wa Biblia baada ya kusoma kitabu chenye picha kinachoitwa Unaweza Kuishi Milele Katika Paradiso Duniani, na vitabu vingine. * Janvier alibatizwa katika mwaka wa 2002 na sasa anatumikia akiwa painia, jina ambalo Mashahidi wa Yehova huwapa waeneza-injili wao wa wakati wote. Pia, yeye ni mtumishi wa huduma katika kutaniko la Kikristo analoshirikiana nalo huko Mbang, mji mdogo kusini-mashariki mwa nchi hiyo. Tutaona ikiwa Mbilikimo wengine huko Kamerun wataamua kumwabudu Yehova, Mungu wa pekee wa kweli, anayewapenda “watu wa namna zote.”

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 7 Kilichochapishwa na Mashahidi wa Yehova lakini hakichapishwi tena.

[Picha katika ukurasa wa 24]

Janvier Mbaki—Mbilikimo wa kwanza kuripotiwa kuwa Shahidi—akihubiri