Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kucheka Kunastarehesha

Kwa nini kucheka kunastarehesha sana? Gazeti The Vancouver Sun linasema kwamba uchunguzi umeonyesha kuwa zaidi ya kuchochea sehemu za ubongo zinazohusiana na utambuzi na lugha, kucheka huchochea pia sehemu ya ubongo inayohusiana na furaha na msisimuko. Dakt. Allan Reiss wa Chuo Kikuu cha Stanford, anasema hiyo ni “sehemu ya ubongo yenye nguvu sana.” Reiss anaamini kwamba uchunguzi kuhusu kucheka unaweza kuwasaidia madaktari kuelewa vizuri zaidi tabia za watu. Dakt. Reiss anasema hivi: “Mara nyingi uwezo wa kucheka huonyesha ikiwa mtu ataanzisha urafiki na hata uhusiano wa kudumu wa kimahaba, jinsi atakavyofanya hivyo, na watu watakaokuwa marafiki zake. Pia kucheka huwasaidia watu kukabiliana na matatizo yoyote yale.”

‘Ugonjwa wa Karne ya 21’

Hivyo ndivyo madaktari fulani wa magonjwa ya akili wamefafanua jinsi watu wanavyopenda simu za mkononi kupita kiasi. Kulingana na uchunguzi uliofanywa na Kituo Maalumu cha Tiba na cha Kurekebisha Tabia, wengi kati ya wale wanaopenda simu za mkononi kupita kiasi ni “wanawake waseja walio kati ya umri wa miaka 16 hadi 25, ambao ni wenye haya, hawajakomaa, na wanaokasirika-kasirika,” laripoti gazeti El País la Hispania. Daktari wa magonjwa ya akili Blas Bombín anasema kwamba zoea hilo huwafanya watu “watamani nyakati zote kutumia simu za mkononi kupiga simu na kutuma ujumbe.” Wasipoweza kutumia simu zao za mkononi, wao “huwa na wasiwasi na hukasirika.” Zoea la kutumia simu ya mkononi kupita kiasi haliathiri tu uhusiano pamoja na wengine bali pia linagharimu sana. Kituo hicho cha kurekebisha tabia kinataja visa vya watu ambao wana simu nane za mkononi na ambao huwa na madeni ya kupiga simu ya “dola 1,000 kila mwezi.”

Mitaa ya Mabanda Inaongezeka Ulimwenguni

Hali za sasa zikiendelea, “mtu mmoja kati ya kila watu watatu ulimwenguni ataishi katika mitaa ya mabanda katika miaka 30 ijayo,” lasema gazeti The Guardian la London likinukuu ripoti ya Umoja wa Mataifa. Inasikitisha kwamba ‘tayari watu milioni 940 ulimwenguni wanaishi katika maeneo machafu, yanayohatarisha afya, yasiyo na maji katika sehemu nyingi, yasiyo na vyoo, yasiyo na huduma za umma au mahali ambapo haki zao hazilindwi na sheria.’ Katika eneo la Kibera, Nairobi, Kenya, kuna watu 600,000 hivi wanaoishi katika mitaa ya mabanda. Anna Tibaijuka, mkurugenzi wa mradi wa Umoja wa Mataifa unaoshughulikia makao, anasema: “Ukosefu mkubwa wa usawa na kazi hufanya watu watende maovu. Katika mitaa ya mabanda kuna uovu wa kila aina, hakuna amani na usalama, na vijana hawawezi kupata ulinzi.”

Tatizo la Kuegesha Magari Nchini China

Maendeleo ya haraka ya kiuchumi nchini China yamewawezesha mamilioni ya watu kuwa na magari. Lakini ni vigumu kupata mahali pa kuyaegesha. Nyumba nyingi zilizojengwa katika kipindi cha miaka 25 iliyopita hazina mahali pa kuegesha magari kwa sababu ni watu wachache tu waliokuwa na magari zilipojengwa. Mitaa ya zamani ina vijia vyembamba vinavyojipinda, na hivyo inakuwa vigumu kuegesha magari. Gazeti China Today linasema kwamba “kuna zaidi ya magari milioni 2 huko Beijing, na ni magari 600,000 tu yanayoweza kutoshea katika nafasi za kuegesha.” Nchini kote, karibu asilimia 20 tu ya wenye magari ndio wanaomiliki mahali pa kuegesha. Jambo jingine linaloonyesha kwamba kuna ongezeko la magari ni uhitaji mkubwa wa mafuta. Kulingana na gazeti China Today, “China itaipita Japani, na hivyo kuwa nchi ya pili inayotumia petroli nyingi zaidi.”

Vijana Wenye Maumivu Yanayosababishwa na Mazoea

Gazeti The Globe and Mail la Kanada linaripoti kwamba vijana wengi zaidi huenda kutibiwa maumivu yanayosababishwa na mazoea. Gazeti hilo linasema: “Madaktari na wataalamu wa viungo wanasema kwamba watu wanaopatwa na maumivu hayo ni wachanga zaidi kwani watoto wasiofanya mazoezi wanatumia kompyuta kwa muda mrefu nyumbani na shuleni.” Gazeti Globe linasema kwamba kupiga chapa kwa ukawaida na kubonyeza-bonyeza kifaa cha mchezo wa video kunaweza kusababisha maumivu na uvimbe ambao mara nyingi huwapata watu wenye tatizo hilo. Wazazi wanashauriwa kuangalia jinsi watoto wao wanavyoketi na kusimama na kuwa macho kuona dalili za tatizo hilo kama vile mtoto anaposugua viwiko na mikono, anaposhikwa na ganzi, au anapowashwa.

Je, Kuna Hatari Kazini?

Kulingana na jarida The Wall Street Journal, uchunguzi mmoja uliofanywa nchini Sweden ulionyesha kwamba “kufanya kazi na watu wa jinsia tofauti ni hatari kwa ndoa yako.” Mwandishi wa uchunguzi huo, Yvonne Aberg, alichunguza rekodi za serikali za talaka na kazi na kugundua kwamba “kufanya kazi na watu wa jinsia tofauti . . . huongeza idadi ya talaka kwa asilimia 70, ikilinganishwa na kufanya kazi na watu wa jinsia moja.” Aberg pia aligundua kwamba hali hiyo hutukia hata ikiwa wafanyakazi ni waseja au wamefunga ndoa. Uchunguzi huo wa miaka saba uliohusisha wafanyakazi 37,000 katika sehemu 1,500 ulitegemea habari zilizothibitishwa badala ya maoni ya watu ambayo mara nyingi si sahihi. Makala hiyo ilisema kwamba njia moja ya kupunguza uwezekano wa talaka kwa asilimia 50 ni kufanya kazi ofisini pamoja na mwenzi wako.

Kasisi Asiye na Imani

Kasisi mmoja wa dini ya Kilutheri alipata umaarufu mwaka uliopita kwa kusema “hakuna Mungu wa mbinguni, hakuna uzima wa milele, na hakuna ufufuo.” Shirika la habari la BBC linaripoti kwamba baada ya kusimamishwa kazi kwa muda mfupi aliruhusiwa kurudia kazi yake ya kuhubiri. Kulingana na Askofu Lise-Lotte Rebel wa dayosisi ya Helsingør, Thorkild Grosbøl wa kanisa la Tårbæk karibu na Copenhagen “aliomba msamaha kwa taarifa alizotoa” na kukubali kwamba anawajibika kwa kanisa hilo. Hata hivyo, Grosbøl aliendelea kuhubiri mambo hayohayo. Katika Juni 2004, askofu huyo alisema kwamba ikiwa Grosbøl hatajiuzulu, kesi itafanywa ili iamuliwe ikiwa anapaswa kuendelea kuwa kasisi.

Maandishi ya Kale ya Injili

Gazeti Frankfurter Allgemeine Zeitung la Ujerumani linaripoti kwamba kwa mara ya kwanza wasomi huko Palestina wamegundua mstari kutoka katika Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo uliochongwa kwenye kaburi la zamani. Maandishi yaliyo kwenye kaburi linaloitwa Kaburi la Absalomu yalipatikana bila kutazamiwa. Mtaalamu wa asili ya binadamu, Joe Zias, aliona maandishi yaliyofifia kwenye picha iliyopigwa jioni moja. Karatasi zilizosagwa na kuchanganywa na gundi zilipakwa kwenye maandishi hayo, na mstari huo wa Biblia ukaweza kusomeka. Maandishi hayo ni ya Luka 2:25 na yanapatana na hati ya Codex Sinaiticus ya karne ya nne. Huo ni ugunduzi wa pekee kwani zoea la kuchonga maandishi ya Biblia kwenye mawe ya makaburi lilienea sana wapata mwaka wa 1000 W.K.