Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Paradiso Ndogo

Paradiso Ndogo

Paradiso Ndogo

Na mwandishi wa Amkeni! nchini Côte d’Ivoire

JE, UNGEPENDA kutembelea misitu ya zamani yenye mimea mingi na wanyama wengi? Je, kuna maeneo kama hayo leo? Eneo moja linaloonwa kuwa paradiso ndogo ni Mbuga ya Kitaifa ya Taï, kwenye pembe ya kusini-magharibi ya Côte d’Ivoire, karibu na mpaka wa Liberia.

Mbuga ya Kitaifa ya Taï ndilo eneo kubwa zaidi linalobaki la msitu wa mvua wa kitropiki ambao hapo zamani ulikuwepo katika eneo la sasa la Côte d’Ivoire, Ghana, Liberia, na Sierra Leone. Zaidi ya nusu ya msitu wa mvua wa Afrika Magharibi unapatikana katika mbuga hiyo. Eneo hilo la pekee limehifadhiwa kwa sababu ya hatua mpya zilizoanza kuchukuliwa mwaka wa 1926. Jiunge nasi tunapotembelea mbuga hiyo yenye viumbe vya aina nyingi.

Msitu wa Mvua Wenye Unamna-namna

Tunapotembea katika msitu huo huku tukitumbuizwa na nyimbo za ndege na milio ya tumbili, tunastaajabu tunapotazama miti ya zamani yenye urefu wa meta 60 iliyo na mashina makubwa. Yule anayetutembeza anatuambia kwamba zaidi ya nusu ya aina 1,300 za mimea iliyomo katika mbuga hii yenye ukubwa wa kilometa 3,500 za mraba, hupatikana tu katika eneo hili la Afrika Magharibi.

Mimea inayopatikana humu husitawi sana na ni ya namna mbalimbali. Aina nyingi za miti ya mbao hupatikana katika msitu huu mkubwa, hasa mbambakofi, mpingo, dabéma, na makore. Inatubidi turuke mizizi ya miti hiyo kwani baadhi yake huinuka kwa meta moja kutoka ardhini nayo huenea kwa meta 15. Nyakati nyingine wanyama hujificha kwenye mizizi hiyo wanapowindwa na wanyama wawindaji au ili kujikinga na dhoruba ya mvua.

Matawi yaliyo juu ya miti huenea na kuzuia mwangaza usipenye hadi chini, hivyo kuzuia ukuzi wa mimea midogo. Hata hivyo, mimea inayotambaa kwenye mimea mingine hupatikana huku. Mimea fulani hujitegemeza kwa kupanda miti, kuifunga, na nyakati nyingine hata kuinyonga. Yule anayetutembeza anatuonyesha mmea fulani uliojizungusha na kukaza shina la mti mkubwa. Muda si muda, mti huo mkubwa utakufa.

Dawa na vyakula vingi hupatikana katika Mbuga ya Taï. Anayetutembeza anatujulisha kwamba watu wa kabila la Kru hutumia ganda la aina fulani ya mgunga kutibu malaria. Tunda la mti mwingine lina protini tamu sana kuliko sukari.

Kuna Wanyama Wengi

Kwa ghafula tunasikia majani yaliyo juu yetu yakipiga kelele. Kelele hizo ni za kundi kubwa la tumbili aina ya Diana na mona. Wanapiga kelele zao huku wakiruka kutoka tawi moja hadi lingine. Tumbili mmoja wa aina ya mona, ambaye ana uso unaochekesha wenye milia myeupe, anatukodolea macho tunapomtazama kwa makini! Tumbili, sokwe, na ndege hula matunda mengi na kokwa nyingi zinazopatikana kwenye matawi ya miti. Ni kawaida kuona tumbili na ndege wakila matunda kutoka kwa mti uleule huku wakipiga kelele.

Kuna aina 50 za wanyama katika Mbuga ya Taï, na wengi wao hupatikana tu katika eneo hili. Nyati, tembo, paa, funo, nguruwe-mwitu wakubwa, chui, na viboko hupatikana huko. Wanyama wadogo wanatia ndani fungo, kanu, nguchiro, kakakuona, na galago wa usiku.

Anayetutembeza anatuonyesha nyayo nyingi za wanyama kama vile za funo, ambaye ni paa mdogo. Kuna aina saba za funo katika msitu huo, kama vile funo wa Jentink’s, zebra, na Ogilby’s. Tunaona mahali ambapo nguruwe-mwitu wakubwa wamepitia wanapokula mizizi. Tunachunguza makao ya kakakuona mkubwa mwenye magamba, ambaye hula chungu na mchwa. Kakakuona wawili walikuwa wamechimba shimo kubwa lenye sehemu mbili. Sehemu hizo za shimo zina urefu wa meta 40 hivi na kina cha meta 5. Kakakuona hula wakati wa usiku, naye hutembea kilometa nyingi na kurejea nyumbani alfajiri. Kakakuona hufukua mashimo ya mchwa kwa kucha zake kali, naye hutumia ulimi wake unaonata kuwanasa wadudu hao.

Anayetutembeza anatuonyesha kundi la sokwe ambao hutembea katika eneo hili lenye ukubwa wa kilometa 20 za mraba. Kuna zaidi ya sokwe 2,000 katika mbuga hii. Tumesikia kwamba wao hutumia mawe au matawi wanayobeba kupasua makokwa. Tunasisimuka tunapomwona sokwe mmoja akiwa ameketi chini msituni meta 5 hivi kutoka mahali tuliposimama, huku akipasua gamba la kokwa kwa kutumia tawi.

Sehemu Inayowavutia Wapenzi wa Ndege

Siku inayofuata, tunasafiri kwa mtumbwi kwenye Mto Hana. Wenye kututembeza wanapiga makasia polepole, huku wakitaja majina ya aina nyingi za ndege tunaowaona. Tunasikia kelele za hondohondo, anayejulikana kwa kupiga kelele kwa mabawa yake na mlio wake mkali. Aina saba kati ya aina nyingi za hondohondo huishi katika Mbuga ya Taï. Zaidi ya aina 200 za ndege hupatikana huku. Hiyo inatia ndani aina sita za mdiria, kozi, dura, kasuku, hua, njiwa, kwale, chozi, na chechele. Pia ndege maridadi asiyepatikana kwa urahisi anayeitwa narina trogon amewahi kuonekana huku. Ndege wa kiume wa jamii hiyo huwa na mabawa yanayong’aa ya kijani, kifua chekundu, na mkia wenye manyoya meupe. Tunaona ndege wengi maridadi sana, kama vile blue plantain eater, aina moja ya hua, kasuku wa kijivu, mdiria mwenye kifua cha bluu, na kwarara fulani mwenye manyoya yanayong’aa ya kijani. Mbuga ya Taï ni sehemu inayowavutia sana wapenzi wa ndege!

Kando ya mto kuna nyayo zaidi za wanyama, kutia ndani zile za kiboko fulani ambaye ni mdogo kuliko kiboko wa kawaida. Ukubwa wake ni kama wa nguruwe mkubwa. Viboko hao wadogo hawatumii muda mwingi majini kama viboko wa kawaida, nao hawatembei katika vikundi. Wanapatikana tu Afrika Magharibi. Pia tunaona mburukenge, ambaye huwa na madoa-doa na anafanana na mamba, ijapokuwa ni mdogo. Katika msitu huu, kuna aina 3 za mamba, aina 34 za nyoka, aina nyingi za mjusi, na wadudu wengi sana. Wadudu wengi bado hawajagunduliwa.

Inasikitisha kwamba misitu ya mvua katika sayari yetu inaharibiwa upesi sana. Inaharibiwa hasa kwa sababu ya upanuzi wa mashamba na biashara ya mbao. Inafariji kujua kwamba Muumba mwenyewe ndiye atakayeamua wakati ujao wa dunia yetu.—Zaburi 96:12, 13.

[Ramani katika ukurasa wa 14]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Sierra Leone

Liberia

Côte d’Ivoire

Mbuga ya Kitaifa ya Taï

Ghana

[Picha katika ukurasa wa 15]

Mizizi ya miti iliyotokea juu ya ardhi

Mbambakofi

[Picha katika ukurasa wa 15]

Mtoto wa tembo

[Picha katika ukurasa wa 15]

Aina ya paka wa Afrika

[Picha katika ukurasa wa 15]

Funo wa aina ya “bay”

[Picha katika ukurasa wa 15]

Funo wa aina ya “zebra”

[Picha katika ukurasa wa 15]

Nyati wa Afrika

[Picha katika ukurasa wa 16]

Ndege aina ya “narina trogon”

[Picha katika ukurasa wa 16]

Tai wa mtoni wa Afrika Magharibi

[Picha katika ukurasa wa 16]

Ndege wanaoitwa “blue plantain eater”

[Picha katika ukurasa wa 16]

Kwarara

[Picha katika ukurasa wa 16]

Mdiria mwenye kifua cha bluu

[Picha katika ukurasa wa 16]

Kakakuona mwenye mkia mrefu

[Picha katika ukurasa wa 16]

Kiboko mdogo

[Picha katika ukurasa wa 16]

Chura

[Picha katika ukurasa wa 16]

Mburukenge

[Picha katika ukurasa wa 16]

Nguchiro mweusi

[Picha katika ukurasa wa 17]

Tumbili wa “mona”

[Picha katika ukurasa wa 17]

Mbega

[Picha katika ukurasa wa 17]

Sokwe

[Picha katika ukurasa wa 17]

Tumbili mwenye pua nyeupe

[Picha katika ukurasa wa 17]

Chui

[Picha katika ukurasa wa 17]

Nguruwe-mwitu

[Picha katika ukurasa wa 17]

Fungo wa Afrika

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 14]

Parc National de Taï

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 15]

Golden cat: © Art Wolfe/Photo Researchers, Inc.; all other photos except elephant: Parc National de Taï

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 16]

Ibis: © Joe McDonald/Visuals Unlimited; kingfisher: Keith Warmington; hippo: © NHPA/Anthony Bannister; narina trogon: © P&H Harris; all other photos: Parc National de Taï

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 17]

Pig: © Ken Lucas/Visuals Unlimited; all other photos except chimp and leopard: Parc National de Taï