Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Matibabu Mbalimbali na Masuala Yanayohusika

Matibabu Mbalimbali na Masuala Yanayohusika

Matibabu Mbalimbali na Masuala Yanayohusika

Wazia mfadhaiko wa wenzi fulani wa ndoa wanaotamani sana kupata mtoto lakini hawawezi. Wanatafuta msaada kutoka kwa wanasayansi na wanagundua kwamba mbinu na matibabu mengi yamevumbuliwa ili kushinda tatizo la kutoweza kuzaa. Je, kuna ubaya wakichagua mbinu yoyote ile?

LEO wenzi ambao hawawezi kupata mtoto wanaweza kupata matibabu mbalimbali ambayo hayakuwepo miaka kadhaa iliyopita. Lakini matibabu hayo yanazusha swali hili muhimu, Ni masuala gani ya kimaadili yanayozuka kuhusu njia zisizo za asili za uzazi? Hata hivyo, kabla hatujachunguza jambo hilo hebu tuone jinsi dini mbalimbali zinavyoona matibabu hayo.

Dini Zina Maoni Gani?

Katika mwaka wa 1987 Kanisa Katoliki lilitoa hati iliyoeleza masuala ya kimaadili yanayohusika katika matibabu ya kutoweza kuzaa. Hati hiyo inayoitwa Donum Vitae (Zawadi ya Uhai) ilisema kwamba ikiwa mbinu fulani ya kitiba inasaidia tendo la ndoa kutungisha mimba, basi inakubaliwa. Kwa upande mwingine, hati hiyo ilisema kwamba ikiwa mbinu fulani ya kitiba inachukua mahali pa tendo la ndoa, mbinu hiyo haipatani na maadili. Kulingana na maoni hayo, upasuaji unaofanywa kuzibua mirija ya kupeleka yai kwenye tumbo la uzazi na matumizi ya dawa za uzazi yanapatana na maadili, lakini kutungisha mimba nje ya tumbo la uzazi hakupatani na maadili.

Mwaka uliofuata kamati ya Bunge la Marekani ilichunguza maoni ya dini mbalimbali kuhusu matibabu ya kutoweza kuzaa. Ripoti iliyotolewa mwishoni mwa uchunguzi huo ilionyesha kwamba wengi wao walikubali matibabu ambayo yametumiwa kwa muda mrefu, kuingiza shahawa ya mume ndani ya tumbo la uzazi kwa njia isiyo ya asili, na kutungisha mimba nje ya tumbo la uzazi maadamu yai na shahawa ni za wenzi hao wa ndoa. Hata hivyo, dini nyingi zilizochunguzwa zilisema kwamba mazoea kama vile kuharibiwa kwa viini-tete, kuingizwa kwa shahawa ya mwanamume mwingine ndani ya tumbo la uzazi, na mwanamke kumzalia mwanamke mwingine mtoto, hayapatani na maadili. *

Katika mwaka wa 1997, Tume ya Ulaya ya Makanisa na Jamii ambayo huwakilisha makanisa ya Kiprotestanti, Kianglikana na Kiothodoksi, ilieleza msimamo wao katika hati fulani kwamba hawakubaliani kuhusu njia zisizo za asili za uzazi. Ikikazia kwamba dhamiri ya mtu inahusika na kwamba atahitaji kukabiliana na maamuzi anayofanya, hati hiyo ilisema: “Inaonekana makanisa ya tume hii hayakubaliani kuhusu jambo hilo. Badala yake, kuna maoni mengi mbalimbali.”

Ni kweli kwamba maoni ya watu yanatofautiana sana kuhusu njia zisizo za asili za uzazi. Shirika la Afya Ulimwenguni la Umoja wa Mataifa linakubali kuwa mbinu zisizo za asili za uzazi “huzusha masuala ya kijamii, kiadili, na ya kisheria.” Watu wanapaswa kufikiria mambo gani kabla ya kuamua kutumia mbinu zisizo za asili za uzazi?

Ni Masuala Gani Yanayohusika?

Jambo moja muhimu linalopaswa kufikiriwa ni hali ya kiini-tete cha mwanadamu. Hilo linahusiana na swali hili muhimu, Uhai huanza wakati gani—je, ni wakati mimba inapotungwa au ni baadaye wakati mimba inapoendelea kukua? Jibu la swali hilo litaathiri uamuzi ambao wenzi wengi wa ndoa watafanya kuhusu matibabu hayo. Kwa mfano, ikiwa wanaamini kwamba uhai huanza mimba inapotungwa, basi kuna maswali muhimu wanayopaswa kufikiria.

● Je, wenzi wa ndoa wanapaswa kumruhusu daktari atungishe mayai mengi kuliko idadi ya yale yatakayoingizwa katika tumbo la uzazi la mama, na hivyo kuhifadhi viini-tete vingine kwa ajili ya matumizi ya wakati ujao?

● Viini-tete hivyo vilivyohifadhiwa vitafanyiwa nini iwapo wenzi hao hawawezi au hawataki kupata watoto wengine?

● Viini-tete vilivyohifadhiwa vitafanyiwa nini wenzi hao wakitalikiana au mmoja wao akifa?

● Ni nani mwenye daraka la kuamua ikiwa viini-tete hivyo vitaharibiwa?

Suala la jinsi viini-tete ambavyo havikutumiwa au vilivyohifadhiwa vitakavyofanyiwa linapaswa kuchukuliwa kwa uzito. Sasa katika nchi fulani sheria inasema kwamba wenzi wa ndoa wanapaswa kuandika jinsi ambavyo viini-tete vilivyosalia vinapaswa kushughulikiwa, yaani ikiwa vitahifadhiwa, vitatumiwa kwa mwanamke mwingine, vitatumiwa katika utafiti au kuachwa viharibike. Wenzi wa ndoa wanapaswa kujua kwamba katika maeneo fulani ni jambo linalokubalika kwa kliniki za uzazi kuharibu viini-tete vilivyohifadhiwa bila kuwa na cheti chochote kinachotoa kibali ikiwa vimeachwa kwa zaidi ya miaka mitano. Leo mamia ya maelfu ya viini-tete vilivyogandishwa vimehifadhiwa katika kliniki mbalimbali ulimwenguni.

Jambo jingine linalopaswa kufikiriwa ni kwamba wenzi wa ndoa wanaweza kuombwa wakubali viini-tete vya ziada vitumiwe katika utafiti wa chembe za msingi. Kwa mfano, Shirika la Marekani Linaloshughulikia Matatizo ya Kutoweza Kuzaa, limewatia moyo wenzi wa ndoa kuruhusu viini-tete vyao vilivyohifadhiwa vitumiwe katika utafiti. Kusudi moja la utafiti wa chembe za msingi ni kuvumbua tiba mpya za magonjwa. Lakini utafiti huo umeleta ubishi mwingi kwa sababu mbinu zinazotumiwa kutenganisha chembe za msingi kutoka kwenye viini-tete huharibu viini-tete. *

Mbinu mpya za uchunguzi wa chembe za urithi huzusha masuala mengine ya kimaadili. Kwa mfano, fikiria mbinu ya kuchunguza chembe za urithi kabla ya kupandikiza kiini-tete ndani ya tumbo la uzazi. (Ona sanduku “Vipi Kuchagua Viini-Tete Vitakavyoingizwa Katika Tumbo la Uzazi?”) Mbinu hiyo inahusisha kuchunguza chembe za urithi za kiini-tete kisha kuchagua kile ambacho kitapandikizwa ndani ya tumbo la uzazi. Kiini-tete ambacho kitachaguliwa kinaweza kuwa cha jinsia inayotakikana au kisichokuwa na chembe za urithi zinazoweza kusababisha ugonjwa fulani. Wachambuzi wanaonya kwamba mbinu hiyo inaweza kusababisha ubaguzi wa kijinsia au kwamba hatimaye inaweza kutumiwa na wenzi wa ndoa kuchagua watoto wenye sifa fulani, kama vile rangi ya nywele na ya macho. Mbinu hiyo hutokeza swali hili la kimaadili, Itakuwaje kwa viini-tete visivyochaguliwa?

Je, Ndoa Itaathiriwa?

Kuna jambo jingine la kufikiriwa wakati mtu anapochagua tiba ya uzazi. Ndoa itaathiriwaje wenzi wanapomtumia mwanamke mwingine kuwazalia mtoto au kupata shahawa au mayai kutoka kwa mtu mwingine? Mbinu nyingine za tiba ya uzazi zinahusisha mtu mmoja, watu wawili, au watatu nje ya ndoa.

Kuna mambo mengine ambayo watu wote wanaohusika katika tiba fulani za uzazi zinazohusisha kutumia shahawa na mayai ya watu wengine wanahitaji kufikiria.

● Wazazi wa mtoto huyo wataathiriwaje kihisia ikiwa mmoja wao au wote wawili si wazazi halisi wa mtoto huyo?

● Mwana au binti anayezaliwa atahisije anapojua kwamba alizaliwa kutokana na njia hiyo isiyo ya asili?

● Je, mtoto anapaswa kuambiwa wazazi wake halisi ni akina nani na kuruhusiwa kuwatafuta?

● Wale wanaotoa shahawa au mayai wana haki na wajibu gani wa kisheria na wa kimaadili?

Vipi Kuficha Majina ya Wanaohusika?

Katika nchi nyingi majina ya wanaohusika hufichwa. Shirika la Uzazi na Viini-tete, ambalo husimamia matumizi ya chembe zinazotumiwa katika uzazi huko Uingereza, linaeleza: “Wenzi wa ndoa wanaopokea mayai au shahawa za watu waliotoa chembe za uzazi na watoto wanaozaliwa kupitia njia hizo hawataambiwa majina ya waliozitoa, ila tu katika visa ambavyo wenye kutoa chembe za uzazi na wanaozipokea wanafahamiana na walipanga jambo hilo.”

Hata hivyo, kuficha majina ya wahusika kumesababisha ubishi mwingi katika maeneo fulani. Hivyo, sheria zimebadilishwa katika nchi kadhaa. Wale wanaopinga kufichwa kwa majina husisitiza kwamba watoto wanahitaji kufahamishwa kabisa asili yao. Ripoti moja inasema hivi: “Zaidi ya asilimia 80 ya watu ambao hawakulelewa na wazazi wao wa asili huwatafuta watu wao wa ukoo, na wengi wao hufanya hivyo ili kujibu maswali ambayo wamekuwa nayo kwa muda mrefu kuhusu asili yao, sawa na watu wengine. Asilimia 70 hivi hutaka kupata habari muhimu kuhusu magonjwa wanayoweza kurithi kutoka kwa wazazi wao halisi.”

Ripoti nyingine iliyotegemea uchunguzi uliofanywa kuhusu watu wazima 16 waliozaliwa kupitia mbinu zisizo za asili ilionyesha kwamba “wengi walishtuka walipotambua asili yao.” Ripoti hiyo iliongezea: “Watoto wengi walifadhaika kwa sababu ya kutojua asili yao na kuhisi kwamba waliachwa. Walihisi kwamba wamedanganywa na hawakutumaini watu wa familia zao.”

Utaamuaje?

Bila shaka, sayansi itafanya maendeleo zaidi kuhusiana na matibabu ya njia zisizo za asili za uzazi. Watu fulani wanakadiria kwamba wakati ujao asilimia 30 ya watoto watazaliwa kupitia njia hizo. Mjadala kuhusu masuala ya kimaadili utaendelea.

Wakristo wa kweli wanaongozwa na jambo jingine muhimu, yaani, maoni ya Muumba, ambaye alianzisha uzazi. (Zaburi 36:9) Bila shaka, Biblia haizungumzii moja kwa moja njia zisizo za asili za uzazi zinazotumiwa leo kwani mbinu hizo hazikuwepo katika nyakati za Biblia. Hata hivyo, Biblia inatoa kanuni zinazoonyesha maoni ya Mungu. (Ona sanduku “Biblia Ina Maoni Gani?”) Kanuni hizo zinatusaidia kufanya maamuzi yanayopatana na maadili na kutuwezesha kuwa na dhamiri safi mbele za Mungu.—1 Timotheo 1:5.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 6 Mwanamke anayemzalia mwingine mtoto hupata mimba hiyo kwa kuingizwa shahawa kwa njia isiyo ya asili au kupasuliwa na kuingizwa yai lililotungishwa.

^ fu. 16 Ona mfululizo “Je, Sayansi Imevuka Mipaka kwa Kutumia Chembe za Msingi?” katika toleo la Amkeni! la Novemba 22, 2002.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8]

Uhai Huanza Wakati Gani?

Taarifa “kabla ya kuwa kiini-tete” hurejelea yai katika zile siku 14 za kwanza baada ya kutungishwa na kabla halijapandikizwa katika tumbo la uzazi. Baada ya kupandikizwa na mpaka mwishoni mwa juma la nane, huitwa kiini-tete. Baada ya hapo na kuendelea huitwa kijusi. Kwa nini taarifa “kabla ya kuwa kiini-tete” hutumiwa?

Kulingana na jarida International Journal of Sociology and Social Policy, taarifa hiyo “huonwa kuwa sababu ya kutumia kiini-tete cha binadamu katika utafiti” katika kile kipindi cha siku 14 za kwanza tangu kutungishwa kwa yai. Kitabu kimoja cha marejeo kinasema: “Iwapo mtu atafafanua kiini-tete kuwa umbo ambalo hatimaye litakuwa mtoto, basi viungo vyake vya msingi havifanyizwi mpaka baada ya majuma mawili tangu kutungishwa kwa yai.” Lakini je, ingefaa kusema kwamba yai lililotungishwa ni mkusanyiko wa chembe tu unaofaa kutumiwa katika utafiti? Fikiria yanayotukia katika majuma hayo mawili.

Baada ya yai kutungishwa, inachukua saa 24 kwa kromosomu za kiume na za kike kuungana. Katika kipindi cha siku chache zinazofuata, chembe hugawanyika. Katika kipindi cha siku nne au tano tangu kutungishwa kwa yai, kikundi hicho cha chembe hukua na kufanyiza umbo la duara (ambalo ni dogo kuliko kichwa cha pini) lenye tabaka la nje la chembe na kikundi cha chembe upande wa ndani. Chembe hizo hufanyiza kibonge (blastocyst). Chembe nyingi katika tabaka la nje zitasitawi na kuwa tishu ambazo si sehemu ya kiini-tete. Hata hivyo, mtoto atafanyizwa kutokana na chembe za ndani.

Yai hupandikizwa juma moja hivi baada ya kutungishwa. Kibonge cha chembe hujishikamanisha na tumbo la uzazi, na kuanza kufanyiza kondo la nyuma ambalo huwezesha oksijeni na chakula kutoka kwa mfumo wa damu wa mama kumfikia mtoto na pia kutoa uchafu. Kulingana na kitabu Incredible Voyage—Exploring the Human Body, kufikia siku ya tisa hivi chembe za ndani huanza “kumuunda binadamu mpya.” Kinaongeza hivi: “Ni lazima chembe hizo 20 hivi zibadilike na kugawanyika katika kipindi cha siku tano au sita ili kutokeza kiungo cha kwanza cha kiini-tete.” Kwa hiyo, kufikia mwishoni mwa juma la pili, ‘kiungo hicho cha kwanza’ kinachotokeza mfumo wa neva huanza kukua.

Kwa sababu ya utaratibu huo wa hatua kwa hatua unaotokea katika siku za kwanza za kiini-tete, watu fulani husema kwamba “hakuna tukio hususa la kibiolojia linalobainisha mwanzo wa kiini-tete cha mwanadamu.”

Hata hivyo, wakristo wa kweli huamini kuwa uhai huanza wakati yai linapotungishwa. Kwa kuwa chembe ya kwanza iliyotungishwa ina maagizo kuhusu jinsi kondo la nyuma litakavyoundwa, jinsi yai litakavyopandikizwa katika tumbo la uzazi, jinsi kiini-tete kitakavyounganishwa na mishipa ya damu ya mama na kadhalika, hilo huwafanya wavutiwe zaidi na Yehova Mungu, Mbuni wa mifumo hiyo.

[Picha]

Kiini-tete cha siku tatu (ukubwa umezidishwa mara 400 hivi)

[Hisani]

Courtesy of the University of Utah Andrology and IVF Laboratories

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 9]

Vipi Kuchagua Viini-tete Vitakavyoingizwa Katika Tumbo la Uzazi?

Mbinu mpya ya kutungisha yai kwa njia isiyo ya asili inahusisha kuchunguza na kisha kuchagua viini-tete vitakavyoingizwa katika tumbo la uzazi. Kitabu Choosing Assisted Reproduction—Social, Emotional and Ethical Considerations kinasema hivi kuhusu masuala ya kimaadili yanayozuka kuhusu mbinu hiyo:

“Karibuni [wanasayansi] wataweza kujua sifa za kimwili, za kiakili, za kihisia, na za kitabia za kiini-tete. Hivyo, karibuni wazazi wataweza kuchagua sifa fulani za watoto wao. Ijapokuwa watu wengi huenda wakaunga mkono matumizi ya mbinu hiyo kwa ajili ya wenzi wa ndoa walio na ugonjwa hatari, wengi hawataiunga mkono inapotumiwa na wenzi wa ndoa ambao wanatamani kuwa na mtoto wa jinsia fulani hususa, au ambao baadaye wangetaka mtoto mwenye macho ya bluu, mwenye kipawa cha kuimba, au aliye mrefu.

“Sawa na tekinolojia nyingine, mbinu ya kuchunguza kiini-tete kabla ya kukiingiza katika tumbo la uzazi huzusha suala hili: Je, ni lazima kufanya jambo eti kwa sababu tu linaweza kufanywa?. . . . Ni vigumu kuweka mipaka yoyote katika visa vinavyohusisha mbinu hii ya hali ya juu.”

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 10]

BIBLIA INA MAONI GANI?

Bila shaka, Biblia haizungumzii moja kwa moja mbinu za uzazi zisizo za asili zinazotumiwa leo. Hata hivyo, Biblia inatusaidia kujua maoni ya Mungu kuhusu masuala fulani muhimu. Na kupata majibu ya maswali mawili muhimu kunaweza kuwasaidia Wakristo wa kweli kufanya maamuzi yanayompendeza Mungu.

Uhai wa mwanadamu huanza lini? Biblia inasema kwamba uhai huanza wakati yai linapotungishwa. Fikiria maneno ya mtunga-zaburi Daudi, aliyeongozwa na roho kusema hivi kumhusu Mungu: “Macho yako yalikiona kiini-tete changu, na katika kitabu chako sehemu zake zote zilikuwa zimeandikwa.” (Zaburi 139:16) Fikiria pia Kutoka 21:22, 23, ambapo maandishi ya lugha ya awali huonyesha kwamba mtu angetozwa hesabu kwa kumuumiza mtoto ambaye hajazaliwa. Tunajifunza kwamba Muumba wetu huuona uhai kuwa wenye thamani, hata katika siku za kwanza za ukuzi katika tumbo la uzazi. Mungu huona kuharibu kiini-tete kimakusudi kuwa utoaji-mimba. *

Je, kuna vizuizi vyovyote kuhusu jinsi nguvu za uzazi za mtu zinavyotumiwa? Maoni ya Mungu yanapatikana katika andiko la Mambo ya Walawi 18:20, linalosema: “Nawe usimpe mke wa mwenzako shahawa inayokutoka awe asiye safi kutokana nayo.” Kanuni ya msingi inayopatikana katika andiko hilo ni hii: Shahawa ya mwanamume inapaswa kutumiwa kumtungisha mimba mke wake tu wala si mtu mwingine yeyote, na mwanamke hapaswi kuchukua mimba ya mtu mwingine ila ya mume wake tu. Kwa maneno mengine, nguvu za uzazi hazipaswi kutumiwa kwa mtu mwingine ila tu mwenzi wako wa ndoa. Hivyo, Wakristo wa kweli huepuka zoea la mama kumzalia mtu mwingine mtoto na mbinu zinazohusisha matumizi ya shahawa, mayai, au viini-tete kutoka kwa watu wengine. *

Wakristo wa kweli wanapofanya maamuzi kuhusu mbinu za uzazi zisizo za asili, wanapaswa kufikiria kwa uzito maoni ya Mungu katika Biblia. * Yeye ndiye Mwanzilishi wa ndoa na maisha ya familia.—Waefeso 3:14, 15.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 55 Ona makala The Bible’s Viewpoint: When Does Human Life Begin?katika toleo la Kiingereza la Amkeni! la Oktoba 8, 1990.

^ fu. 56 Ona makala “Maoni ya Biblia: Mama Kumzalia Mwanamke Mwingine Mtoto—Je, Kwafaa Wakristo?” katika toleo la Amkeni! la Machi 8, 1993, na What Is the Bible’s View?—Is Artificial Insemination Acceptable to God?katika toleo la Kiingereza la Agosti 8, 1974.

^ fu. 57 Kwa mazungumzo kuhusu mbinu ya kutungisha yai nje ya mwili, ambapo yai la mke hutungishwa kwa shahawa ya mume wake, ona makala “Maswali Kutoka kwa Wasomaji,” katika gazeti Mnara wa Mlinzi la Julai 15, 1983, au Juni 1, 1981, Kiingereza.

[Picha katika ukurasa wa 7]

Viini-tete vilivyogandishwa na kuhifadhiwa

[Hisani]

© Firefly Productions/CORBIS