Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Milima Yenye Marumaru

Milima Yenye Marumaru

Milima Yenye Marumaru

Na mwandishi wa Amkeni! nchini Italia

NI KANA kwamba vilele vya Carrara na Pietrasanta vimefunikwa kwa theluji. Lakini sivyo ilivyo. Sehemu hizo zinaonekana kuwa nyeupe kwa sababu ya vifusi vinavyosalia baada ya marumaru kuchimbwa. Milima hiyo isiyo ya kawaida inapatikana katika eneo la Apuan Alps huko Tuscany, kaskazini ya kati ya Italia. Milima hiyo ina marumaru. Hakuna mahali pengine duniani palipo na kiasi kikubwa hivyo cha marumaru.

Tangu zamani wanadamu wamechimba mawe kutoka kwenye milima hiyo na kuitumia kutengeneza nguzo, kuta, sakafu, na michongo yenye kupendeza. Kwa kuwa kuna mawe mengi ya marumaru, mafundi wenye uzoefu, na tekinolojia ya hali ya juu, eneo hilo limekuwa maarufu kwa uuzaji wa mawe ulimwenguni. Zaidi ya marumaru ambayo huchimbwa katika eneo hilo, marumaru kutoka sehemu mbalimbali za ulimwengu huletwa kwa meli kwenye bandari ya Marina di Carrara na kutayarishwa katika viwanda maalumu vya eneo hilo kabla ya kusafirishwa hadi sehemu zote za ulimwengu.

Mawe ya Marumaru Yametumiwa Tangu Zamani

Waroma wa zamani walitumia mawe ya eneo hilo katika ujenzi na katika kuchonga vitu. Marumaru meupe ya Carrara ambayo hutumiwa kuchonga vitu ni maridadi sana. Katika mwaka wa 1505, Michelangelo alienda huko kuchagua mawe laini ya marumaru ambayo hayakuwa na alama za rangi mbalimbali wala kasoro zozote na kuyatumia kuchonga baadhi ya sanaa zake maarufu sana.

Mbinu za zamani za kuchimba ziliendelea kutumiwa kwa karne kadhaa. Vipande vya mbao viliingizwa kwenye nyufa au mashimo yaliyochongwa kwenye miamba. Kisha maji yalimwagiliwa kwenye vipande hivyo vya mbao navyo vikapanuka na kutenganisha jiwe la marumaru. Vitu vinavyolipuka vilianza kutumiwa katikati ya karne ya 18, lakini vilivunjavunja miamba sana hivi kwamba ni thuluthi moja tu ya mawe ambayo ingeweza kutumiwa. Mawe makubwa ya marumaru yaliyosalia, yaani, zile sehemu nyeupe zinazofanana na theluji, huthibitisha kwamba mbinu hizo zilitumiwa zamani.

Ilikuwa hatari kuteremsha mawe makubwa kwenye miteremko mikali kwa kutumia vigari na kamba. Kitabu kimoja kinasema: “Ikiwa kamba iliyofungiliwa kwenye kigari ingekatika, msimamizi wa wafanyakazi angekufa kwani alisimama mbele ya jiwe huku akitoa maagizo, na mfanyakazi yeyote ambaye angegongwa na kamba hiyo angekufa.”

Bila shaka, mbinu za kisasa ni tofauti sana. Siku moja nilitembelea eneo la Carrara na kuelezwa jinsi marumaru yanavyochongwa leo. Hebu niwaeleze mambo niliyojifunza.

Kutembelea Machimbo ya Mawe

Ninampata Giovanni katika mojawapo ya machimbo mengi ya mawe yanayopatikana huku Carrara. Yeye ndiye atakayenitembeza. Machimbo hayo huwa na mamia ya mawe ya marumaru yaliyopangwa vizuri, jiwe juu ya jiwe, yakiwa tayari kuuzwa au kutumiwa kutengeneza vitu. Mashine hutumiwa kukata mawe membamba, na nyingine kuyalainisha. Zamani kazi hizo zilifanywa kwa mkono.

Ili kutembelea machimbo hayo, tunasafiri kwa gari la Giovanni na kukata kona kali kisha tunafika kwenye bonde jembamba mlimani ambapo kuna vipande vya mawe meupe kila mahali. Tunaona malori yanayoweza kubeba tani 30 hivi yakiteremka polepole huku yakibeba mawe makubwa sana.

Tunapokata kona, tunaona ukuta mweupe unaong’aa ambao umechongwa mlimani. Ukuta huo ni mkubwa na una ngazi kubwa sana, kila moja ikiwa na kimo cha meta sita hadi tisa hivi. Giovanni anaendesha gari kuelekea ngazi moja kisha analisimamisha.

Tunapoangalia huku na huku tunatambua kwamba tumo ndani ya mojawapo ya machimbo. Tunaona kuta zaidi nyeupe, nyingine zikiwa na kimo cha mamia ya meta, nazo zinaonekana waziwazi mwambani. Kwa kufaa, imesemwa kwamba kuta hizo ni mandhari ya ‘kustaajabisha na yenye kushtua.’

Ninapotazama mandhari hiyo, kwa ghafula ninaona mashine ya kuchimba ambayo ina kifaa chenye ncha kali kinachotumiwa kupindua sehemu fulani ya mwamba. Kipande cha mwamba huo, ambacho kina umbo la mraba na urefu wa meta 11, upana wa meta 2, na kimo cha meta 6, kinaanguka juu ya vifusi vilivyowekwa chini ili kukizuia kisivunjike-vunjike. Lakini vipande vikubwa hivyo vya mwamba huondolewaje?

Franco, baba ya Giovanni, ambaye amefanya kazi katika machimbo hayo maisha yake yote, anajibu swali hilo. Ananionyesha mashine inayoendesha mkanda mrefu wa chuma ambao unakata sehemu ya ndani ya mwamba kutoka juu hadi chini. Shimo la sentimeta nane linafanyizwa kwenye mwamba kuanzia kushoto hadi kulia kisha lingine linafanyizwa kuanzia chini hadi juu. Ni lazima mashimo hayo yakutane. Mkanda wa chuma wenye almasi huingizwa kwenye mashimo hayo na kufanyiza umbo la mkufu mkubwa. Mkanda huo unapokazwa na kuendeshwa kwa kasi sana kwa mashine ya umeme, unakata mwamba. Baada ya sehemu zote kukatwa, kipande hicho cha mwamba hupinduliwa. Kisha kwa kutumia mkanda huohuo, mwamba huo hukatwa vipande-vipande ili uweze kusafirishwa. Mbinu hizo hutumiwa katika machimbo ya ardhini yaliyo karibu, wakati mawe ya marumaru yanapochimbwa katika sehemu za ndani za milima hiyo.

Viwanda vya eneo hili hutumia mawe hayo kutengeneza bidhaa mbalimbali kama vile vigae, viunzi vya ujenzi, na mapambo. Mawe ya Carrara yamekuwa yakitumiwa na yangali yanatumiwa hasa katika ujenzi.

Karakana fulani huwatengenezea wateja mapambo ya sakafu, na mapambo yanayotumiwa nje na ndani ya nyumba. Nyingine hutengeneza vifaa maridadi vinavyowekwa juu ya mahali pa kuotea moto, vifaa vya bafu, meza, na kadhalika. Vitu vinavyotengenezwa katika eneo hili kwa mawe yenye maumbo maridadi na rangi za kupendeza hutumiwa kurembesha nyua za umma na vilevile majengo ya umma na ya watu binafsi kama vile majengo ya ibada, majumba ya ukumbusho, maduka makubwa, viwanja vya ndege, na majengo marefu ulimwenguni pote.

Inapendeza kujua jinsi marumaru inavyotumiwa katika ujenzi, lakini ninataka pia kuona jinsi inavyotumiwa katika mapambo na sanaa. Ninaenda Pietrasanta alasiri, ili kujifunza zaidi kuhusu sanaa hiyo.

Karakana za Marumaru

Kijitabu kimoja cha kuwaongoza watalii kinasema hivi, “Tembelea karakana za mafundi,” nao “watafurahia kukuonyesha ustadi wao.” Pietrasanta ni mahali padogo penye watu wenye urafiki, kwa hiyo ninajihisi huru kutembelea karakana mbalimbali zilizo katika eneo hilo la zamani ili kujionea vitu vinavyotengenezwa huko.

Ninawaona wachongaji kutoka nchi nyingi wakibuni na kuunda vyombo vya sanaa, na mafundi wenyeji wanachonga kwa makini huku mikono na nyuso zao zikiwa zimefunikwa kwa vumbi jeupe. Majumba ya maonyesho yana vyombo vingi sana vyenye thamani, vya zamani na vya kisasa.

Kutengeneza mchongo ni kazi ngumu. Kwa mfano, jiwe lenye uzito wa tani mbili linaweza kukatwa katika umbo fulani, lakini itachukua miezi mitatu hadi mitano kulichonga vizuri na kulikamilisha. Wakati jiwe linapochongwa, tani moja ya marumaru huondolewa. Vifaa vilivyotumiwa zamani vilikuwa nyundo, patasi, na tupa. Leo, mashine maalumu za kukata na patasi za hali ya juu hurahisisha kazi, lakini sehemu ndogo-ndogo zinahitaji kuchongwa kwa mkono. Vitu vinavyotengenezwa huwa maridadi sana.

Katika sehemu nyingi, ufundi wa zamani wa kuchonga vitu vya marumaru umetokomea. Hata hivyo, kwa sababu ya kupatikana kwa marumaru katika eneo hili, mafundi stadi wenye ujuzi wa miaka mingi, na wasanii wanaokuja huku kujifunza kazi, maeneo ya Carrara na Pietrasanta yanaweza kuitwa “chuo kikuu cha sanaa ya marumaru.”

[Picha katika ukurasa wa 24]

Machimbo ya mawe ya ardhini

[Picha katika ukurasa wa 24]

Mkanda wenye almasi hutumiwa kukata mawe ya marumaru

[Picha katika ukurasa wa 25]

Machimbo ya marumaru katika eneo la Carrara, Italia

[Picha katika ukurasa wa 25]

Mchongo wa marumaru wa Maliki Augusto, karne ya kwanza W.K.

[Hisani]

Scala/Art Resource, NY

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 23]

Studio SEM, Pietrasanta