Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mwangaza Unaometameta Baharini

Mwangaza Unaometameta Baharini

Mwangaza Unaometameta Baharini

Mpiga-mbizi alipokuwa akiogelea kando ya mwamba, alimwona ngisi mwenye urefu wa sentimeta 60 karibu na ufa, huku akiwa amefichwa kabisa katika mazingira yenye rangi ya bluu na kijivu. Mpiga-mbizi alipomkaribia, ngisi huyo alibadilisha rangi yake na kuwa mwenye rangi nyekundu nyangavu. Mpiga-mbizi aliporudi nyuma, ngisi huyo alirudia rangi yake ya awali. Je, umewahi kujiuliza jinsi viumbe hao wa ajabu, kutia ndani pweza na ngisi wa aina nyingine, wanavyoweza kubadilisha rangi yao?

Wanaweza kufanya hivyo kwa sababu wana chembe za rangi kwenye ngozi. Neva hufanya misuli inyumbulike na kubadili-badili ukubwa wa chembe hizo, na hivyo kumwezesha kiumbe huyo kubadilisha rangi yake na kutokeza maumbo mbalimbali ya rangi.

Zaidi ya kubadilisha rangi ya ngozi yao, aina nyingi za ngisi hata hutokeza mwangaza, kama anavyofanya kimulimuli. Mwangaza huo unaotokezwa na viumbe wengi wa majini, kama vile viwavi wa baharini na uduvi, hutokana na utendaji tata wa kemikali ndani ya chembe au viungo fulani. Pia bakteria fulani ambazo huishi ndani ya viumbe hao, zina uwezo wa kutokeza mwangaza.

Viumbe wanaotokeza mwangaza kupitia utendaji tata wa kemikali huwa na chembe na viungo vilivyo na kemikali ambayo inapoungana na oksijeni na kimeng’enya fulani hutokeza mwangaza wa bluu na kijani. Jarida Scientific American linasema kwamba viungo fulani vinavyotoa mwangaza, “ni viungo tata vyenye lenzi, sehemu ya kuchuja rangi, au sehemu inayonyumbulika ambayo inadhibiti mwangaza. Ngisi wenye chembe na viungo vinavyotokeza rangi ngozini mwao huweza kudhibiti rangi na kiasi cha mwangaza unaofanyizwa.”

Viumbe wanaotoa mwangaza kwa kutegemea bakteria huwa na bakteria hizo ndani ya viungo vya pekee ambavyo huwa na damu nyingi. Kwa kuwa bakteria hupata chakula kutoka kwa damu, ni kana kwamba viumbe hao wanalipia “gharama ya umeme.”

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 31]

◀ Inset: Courtesy Jeffrey Jeffords/www.divegallery.com

◀ © David Nicholson/Lepus/Photo Researchers, Inc.