Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Ongezeko la Watoto Wanaozaliwa kwa Njia Zisizo za Asili

Ongezeko la Watoto Wanaozaliwa kwa Njia Zisizo za Asili

Ongezeko la Watoto Wanaozaliwa kwa Njia Zisizo za Asili

Katika Julai 25, 1978, msichana wa pekee anayeitwa Louise Joy Brown alizaliwa huko Oldham, Uingereza. Louise alikuwa mtoto wa kwanza kuzalishwa kwenye maabara.

MIEZI tisa mapema, mimba ya Louise ilitungwa kwenye maabara. Yai la mama yake lilitolewa na kuunganishwa na shahawa kwenye chombo cha glasi. Siku mbili na nusu baadaye, yai hilo lilikuwa limegawanyika na kuwa chembe nane ndogo sana, kisha chembe hizo nane zilizokuwa zikigawanyika zikaingizwa ndani ya tumbo la uzazi la mama yake ili zikue kwa njia ya kawaida. Kuzaliwa kwa Louise kulitokeza maendeleo makubwa katika tiba ya kutoweza kuzaa.

Mbinu hiyo ya kutungisha mimba nje ya tumbo la uzazi ilileta maendeleo katika matibabu mbalimbali ya hali ya kutoweza kuzaa. Fikiria mifano kadhaa. Katika mwaka wa 1984, mwanamke mmoja huko California, Marekani, alizaa mtoto kutokana na yai la mwanamke mwingine. Mwaka huohuo, huko Australia, mtoto mmoja alizaliwa kutokana na kiini-tete kilichokuwa kimegandishwa. Katika mwaka wa 1994, mwanamke mwenye umri wa miaka 62 huko Italia, alizaa kutokana na mayai ya mwanamke mwingine na shahawa za mume wake.

Maendeleo ya Hatua kwa Hatua

Sasa miaka 25 hivi imepita tangu Louise Joy Brown alipozaliwa, na watafiti wamevumbua dawa nyingi na mbinu za hali ya juu ambazo zimebadilisha kabisa tiba ya kutoweza kuzaa. (Ona masanduku yenye vichwa, “Baadhi ya Matibabu ya Kutoweza Kuzaa” na “Kuna Hatari Gani?”) Maendeleo hayo yamesababisha ongezeko la watoto wanaozaliwa kupitia njia zisizo za asili. Kwa mfano, katika mwaka wa 1999, watoto zaidi ya 30,000 walizaliwa kupitia mbinu hizo nchini Marekani pekee. Katika nchi fulani za Skandinavia, asilimia 2 hadi 3 ya watoto wanaozaliwa kila mwaka huzalishwa kupitia mbinu hizo. Ulimwenguni pote, watoto wapatao 100,000 huzaliwa kila mwaka kupitia mbinu ya kutungisha mimba nje ya tumbo la uzazi. Imekadiriwa kwamba mbinu hiyo imetumiwa kuzalisha watoto wapatao milioni moja tangu mwaka wa 1978.

Njia zisizo za asili za kuzalisha hutumiwa hasa katika nchi zilizoendelea. Tiba ya aina hiyo hugharimu maelfu ya dola, na mara nyingi huduma za afya za umma, miradi inayodhaminiwa na waajiri, na bima za kibinafsi hazilipii matibabu hayo. Gazeti Time lilisema kwamba “mwanamke mwenye umri wa miaka 45 ambaye ametumia mara saba mbinu ya kutungisha mimba nje ya tumbo la uzazi atakuwa ametumia dola 100,000 kwa matibabu hayo.” Hata hivyo, mbinu hizo zisizo za asili za kuzalisha zimewafaidi wenzi wasioweza kuzaa ambao wamekuwa wakilea watoto wa wengine. Sasa njia mbalimbali za kutibu hali ya kutoweza kuzaa zinashughulikia visababishi vingi vya kutoweza kuzaa miongoni mwa wanawake na wanaume. *

Kwa Nini Tiba Hiyo Inapendwa Sana?

Mtindo wa kisasa wa maisha ni sababu moja inayofanya njia zisizo za asili za kuzalisha zipendwe. Ripoti moja iliyochapishwa na Shirika la Marekani la Tiba ya Uzazi inasema: “Umri wa wastani wa kuzaa umeongezeka katika miaka 30 iliyopita kwa sababu wanawake wengi wanafuatia elimu ya juu na kazi, huku wakiahirisha kuolewa. Wakati huohuo, idadi kubwa ya wanawake waliozaliwa kati ya miaka ya 1946 na 1964, wakati ambapo watoto wengi walizaliwa, wamefikia umri wa kutoweza kuzaa, na hivyo wengi wao wanatafuta matibabu ya kuwasaidia kuzaa.”

Huenda wanawake fulani wasitambue jinsi uwezo wao wa kuzaa unavyopungua haraka kadiri wanavyozeeka. Kulingana na Vituo vya Marekani vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa, mwanamke anapofikia umri wa miaka 42, uwezekano wa kupata mtoto kwa kutumia mayai yake mwenyewe ni chini ya asilimia 10. Hivyo, mara nyingi wanawake wenye umri mkubwa wanaotumia njia za kuzalisha zisizo za asili hupewa mayai ya mtu mwingine.

Wenzi fulani wa ndoa wasioweza kuzaa wameamua kuomba kiini-tete kilichosalia wakati wenzi wengine wa ndoa walipokuwa wakipata matibabu ya kuzalisha kwa njia zisizo za asili. Inakadiriwa kwamba katika Marekani pekee, karibu viini-tete 200,000 vilivyogandishwa vinahifadhiwa. Ripoti moja ya habari ya hivi majuzi ya shirika la CBS ilisema: “Watu wachache wamekuwa wakipewa viini-tete kichinichini kwa miaka mingi.”

Si ajabu kwamba maendeleo ya kuzalisha kwa njia zisizo za asili hutokeza maswali fulani. Je, njia hizo za uzazi zinapatana na maadili? Biblia ina maoni gani kuhusu tiba hizo? Maswali haya na mengine yatazungumziwa katika makala inayofuata.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 7 Baadhi ya visababishi vya wanawake kutoweza kuzaa ni tatizo kwenye mfumo wa kutokeza yai, mirija ya kupeleka yai kwenye tumbo la uzazi, au kuwepo kwa utando wa tumbo la uzazi mahali pasipofaa. Mara nyingi, hali ya kutoweza kuzaa miongoni mwa wanaume husababishwa na kuwa na shahawa kidogo au ukosefu wa shahawa kabisa.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 4]

BAADHI YA MATIBABU YA KUTOWEZA KUZAA

KUWEKA SHAHAWA NDANI YA VIUNGO VYA UZAZI VYA MWANAMKE KWA NJIA ISIYO YA ASILI. Madaktari hujaribu kutumia mbinu hii kwanza kabla ya kutumia mbinu nyingine zilizoonyeshwa hapa chini.

KUTIA CHEMBE ZA UZAZI KATIKA MRIJA WA KUPELEKA YAI. Mbinu hii inahusisha kutoa mayai ya mwanamke na kuyaunganisha na shahawa kisha kwa kutumia kifaa cha kuchunguza tumbo kuyaweka mayai na shahawa katika mrija unaopeleka yai kwenye tumbo la uzazi kwa kupasua kidogo tumbo la mwanamke.

KUINGIZA SHAHAWA NDANI YA YAI. Katika mbinu hii chembe moja ya shahawa huingizwa moja kwa moja ndani ya yai.

KUTUNGISHA MIMBA NJE YA TUMBO LA UZAZI. (Picha iliyoongezwa ukubwa kushoto) Mbinu hii inahusisha kuondoa mayai ya mwanamke na kuyatungisha mimba nje ya mwili wake. Viini-tete hutokezwa na kuingizwa katika tumbo lake la uzazi kupitia mlango wa kizazi.

YAI LILILOTUNGISHWA NJE YA MWILI NA KUINGIZWA KWENYE MRIJA. Mbinu hii inahusisha kuondoa mayai ya mwanamke na kuyatungisha mimba nje ya mwili wake. Baada ya kupasuliwa kidogo tumboni, yai lililotungishwa huingizwa ndani ya mrija unaolipeleka kwenye tumbo la uzazi.

[Hisani]

Habari hizi zimepatikana kupitia Chanzo cha Habari za Tiba ya Uzazi Katika Vituo vya Marekani vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa.

Courtesy of the University of Utah Andrology and IVF Laboratories

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 5]

KUNA HATARI GANI?

MAKOSA YA MWANADAMU. Kliniki zinazotoa matibabu ya kutoweza kuzaa nchini Marekani, Uholanzi, na Uingereza, zimeingiza kimakosa shahawa na viini-tete katika tumbo la mwanamke mwingine badala ya yule aliyekusudiwa. Katika kisa kimoja wenzi fulani wa ndoa walipata mapacha wa jamii tofauti na yao, na katika kisa kingine mwanamke mmoja alizaa mapacha wa jamii mbili tofauti.

KUZAA WATOTO WENGI. Uchunguzi mbalimbali umeonyesha kwamba kuzaa watoto wengi kunakosababishwa na kuingiza viini-tete vingi katika tumbo la uzazi huongeza uwezekano wa kuzaa watoto kabla ya wakati, kuzaa watoto wenye uzani mdogo, kuzaa watoto ambao wamekufa, na kuzaa watoto wenye kasoro za kudumu.

KASORO ZA KUZALIWA. Kulingana na uchunguzi mmoja, watoto wanaozaliwa kupitia mbinu za kutungisha mimba nje ya tumbo la uzazi hukabili uwezekano mkubwa wa kupata kasoro za kuzaliwa kama vile magonjwa ya moyo au ya figo, mwanya kwenye kaakaa, na mapumbu kuwa mahali pasipofaa.

AFYA YA MAMA. Matatizo yanayotokana na matibabu ya homoni au kupata mimba ya watoto wengi huhatarisha zaidi uhai wa mama.