Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Origami—Ustadi wa Kukunja Karatasi

Origami—Ustadi wa Kukunja Karatasi

Origami—Ustadi wa Kukunja Karatasi

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI JAPANI

WAZIA karatasi moja tu ikigeuzwa kuwa korongo maridadi. Korongo huyo ana mabawa yaliyonyooka vizuri, umbo la fahari, shingo ndefu nyembamba, kichwa maridadi, na mdomo mrefu. Inashangaza kwamba ndege huyo ametengenezwa kwa kukunja karatasi yenye umbo la mraba kwa kutumia hatua 12.

Kutengeneza maumbo mbalimbali ya kupendeza kwa kukunja na kufungua karatasi ni sanaa ya Japani inayoitwa origami. Neno hilo linamaanisha “karatasi iliyokunjwa.” Ingawa chanzo chake hakijulikani vizuri, inaonekana sanaa ya origami huku Japani ilianza zamani wakati hati rasmi zilipokunjwa kwa njia maridadi. Inasemekana kwamba katika enzi za Edo (1603-1867), watu walifurahia sanaa hiyo ya origami wakati wa mapumziko. Mbinu mpya za kukunja karatasi zilibuniwa wakati huo. Wazazi wamekuwa wakiwafundisha watoto na wajukuu wao sanaa hiyo, na hivyo kuipitisha kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Wajapani wengi hukumbuka kwamba walipokuwa watoto walishangaa kuona jinsi mama zao walivyokunja karatasi kwa ustadi na kuwafanyizia maumbo yenye kupendeza.

Sanaa ya origami imegawanywa katika vikundi viwili kwa kutegemea maumbo ya vitu vinavyotengenezwa. Kikundi kimoja ni origami ya kitamaduni, ambayo inahusisha kutengeneza korongo, vyura, mashua, maputo, wadudu, na mimea kwa karatasi. Kikundi cha pili ni origami ya kubuni, ambayo inahusisha mbinu tofauti na zile za kitamaduni ambazo zimetumiwa kwa karne nyingi. Aina hii ya origami hutumiwa kutengeneza maumbo ya wanyama wakubwa sana, maumbo tata ya wadudu, na maumbo mengine yenye madoido mengi.

Sanaa ya origami inatumiwa katika taaluma nyingi, kama vile katika ujenzi. Sanaa hiyo pia imetumiwa na wataalamu wa tiba katika mazoezi ya kuwasaidia wazee na walemavu.

Kutengeneza Origami

Unawezaje kutengeneza origami? Si vigumu kutengeneza origami ya kitamaduni. Unachohitaji si vifaa vya pekee au mazoezi, bali tu ni kuwa makini na kuwa mwepesi kutambua mambo. Bila shaka, unahitaji karatasi inayofaa na maagizo ya kukunja. Mtu yeyote anayekunja karatasi kwa makini anaweza kufanyiza umbo linalovutia.

Unaweza kutumia karatasi yoyote, kama vile karatasi za gazeti, karatasi zenye matangazo ya biashara, au karatasi maridadi za kufungia vitu. Unaweza kuamua ukubwa, ubora, na rangi ya karatasi ikitegemea kitu unachotaka kutengeneza. Hata hivyo, ukitaka kutengeneza kitu maridadi sana, unapaswa kuzingatia rangi ya karatasi. Ubora wa kazi yako utategemea njia yako ya kukunja karatasi na pia karatasi unayochagua kutumia. Inafaa kutumia karatasi iliyotengenezwa hasa kwa ajili ya sanaa ya origami. Huenda pia ukapenda kutumia washi ambayo ni karatasi ya Kijapani iliyotengenezwa kwa mkono. *

Mara nyingi, ni muhimu karatasi unayotumia iwe na umbo kamili la mraba. Unaweza kuhakikisha kwamba karatasi ni ya mraba kwa kuunganisha pembe zinazoelekeana na kuikunja katika umbo la pembe-tatu. Pembe zote zikilingana kabisa, basi karatasi imekatwa vizuri.

Ukitaka kutokeza umbo maridadi, unapaswa kukunja karatasi ili pembe zipatane na pembe, na ncha zilingane na ncha za karatasi vizuri. Pia, lazima mikunjo hiyo ikazwe vizuri. Unapokunja karatasi mara moja ili kufanyiza umbo la pembe-tatu, shika kwa nguvu pembe zinazoelekeana katikati ya kidole gumba na kidole cha pili kisha kunja sehemu ya chini kwa ule mkono mwingine. Unapokunja karatasi mara moja ili kufanyiza umbo la mstatili, hakikisha kwamba pembe zote za juu zinalingana kabisa, kisha ushike kwa nguvu ncha za juu unapokunja sehemu ya chini.

Ili kutengeneza maumbo fulani ya origami, karatasi hukunjwa kisha hukunjuliwa ili kutokeza mikunjo kabla ya hatua inayofuata. Wakati mwingine karatasi hukunjwa, hupindwa, husokotwa, hufinywa, hubonyezwa, hupulizwa, na kupinduliwa ili kutengeneza maumbo mbalimbali.

Unaweza kufurahia kutengeneza vitu kwa sanaa ya origami mahali popote na wakati wowote. Baada ya kujifunza sanaa hiyo, unachohitaji tu ni karatasi. Kwa kutumia vidole vyako tu unaweza kutokeza maumbo mengi ya kitamaduni au hata maumbo mapya uliyobuni mwenyewe. Huenda ukavunjika moyo kwa kiasi fulani unapojaribu kujifunza sanaa ya origami kwa kutazama michoro. Lakini ukikutana na mtu anayeijua sanaa hiyo, tumia nafasi hiyo kujifunza ustadi wa kukunja karatasi.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 9 Ona makala Washi​Japan’s Ancient Handmade Paper,” katika toleo la Kiingereza la Amkeni! la Januari 8, 1992.