Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Vitiligo Ni Nini?

Vitiligo Ni Nini?

Vitiligo Ni Nini?

Na mwandishi wa Amkeni! nchini Afrika Kusini

Nyakati nyingine Sibongile husema kwa utani kuhusu ngozi yake. Anasema hivi akitabasamu, “Nilipozaliwa nilikuwa mweusi, kisha nikawa mweupe, na sasa sijui nina ngozi ya rangi gani.” Ana ugonjwa wa vitiligo.

Ugonjwa wa vitiligo, ambao pia huitwa leukoderma, husababishwa na ukosefu wa chembe zinazotokeza rangi ya ngozi. Hilo husababisha madoa na mabaka meupe kwenye ngozi. Wagonjwa wengine huwa na baka moja tu. Lakini, kwa watu wengine ugonjwa huo huenea ngozini upesi. Isitoshe, nyakati nyingine ugonjwa huo huenea polepole kwa miaka mingi. Ugonjwa huo hausababishi maumivu wala hauambukizwi.

Tofauti na kisa cha Sibongile, nyakati nyingine ugonjwa huo hauonekani waziwazi kwa sababu unaonekana hasa kwa watu wenye ngozi nyeusi. Lakini watu wengi wanaathiriwa na ugonjwa huo kwa njia mbalimbali. Habari zinaonyesha kwamba kati ya asilimia 1 na 2 ya watu wana vitiligo. Ugonjwa huo huwapata watu wa jamii zote na huwaathiri wanaume na wanawake kwa kiwango kilekile. Chanzo cha ugonjwa huo bado hakijulikani.

Ingawa hakuna dawa ya kukomesha ugonjwa wa vitiligo, kuna njia nyingi za kushughulika nao. Kwa mfano, watu walio na ngozi nyeupe wanapochomwa na jua kwenye sehemu ambazo hazijaathiriwa, ugonjwa huo huonekana zaidi. Hivyo, mgonjwa akiepuka kuchomwa na jua, ugonjwa huo hauwezi kuonekana sana. Watu wenye ngozi nyeusi wanaweza kutumia vipodozi vya pekee kufunika mabaka na madoa. Matibabu fulani yanayorudisha rangi ya ngozi yamewasaidia wagonjwa wengine. Matibabu hayo yanahusisha kutumia dawa kwa miezi mingi na kutibiwa kwa kifaa cha pekee. Katika visa vingine, matibabu hayo yamerudisha rangi ya ngozi kwenye sehemu fulani zilizoathiriwa. Wagonjwa wengine huchagua matibabu yanayoondoa rangi ya ngozi. Kusudi la matibabu hayo ni kuondoa rangi iliyobaki kwa kuharibu chembe zilizosalia za kutokeza rangi ya ngozi.

Ugonjwa wa vitiligo unaweza kumfanya mtu afadhaike sana hasa unapoenea usoni. Sibongile anasema: “Hivi majuzi, watoto wawili walinitazama na kutoroka huku wakipiga mayowe. Wengine husita kuzungumza nami kwa sababu wanafikiri kwamba nina ugonjwa wa kuambukiza au nimelaaniwa. Ningependa wengine waelewe kwamba hawapaswi kuwaogopa watu wenye ugonjwa huu. Hawawezi kuambukizwa ugonjwa wa vitiligo kwa kugusana na mgonjwa wala kupitia hewa.”

Sibongile ni Shahidi wa Yehova, naye haruhusu hali yake imzuie kufanya kazi anayoipenda sana ya kuwafundisha wengine Biblia. Kazi hiyo inahusisha kuwatembelea watu nyumbani na kuzungumza nao uso kwa uso. Anasema: “Nimejifunza kuipenda sura yangu. Nimeridhika na hali yangu, na ninatazamia kwa hamu wakati ambapo nitarudishiwa rangi ya ngozi yangu katika dunia Paradiso ambayo Yehova Mungu ameahidi.”—Ufunuo 21:3-5.

[Picha katika ukurasa wa 22]

Mwaka wa 1967, kabla ya kuugua