Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Monteverde—Hifadhi ya Viumbe Mawinguni

Monteverde—Hifadhi ya Viumbe Mawinguni

Monteverde—Hifadhi ya Viumbe Mawinguni

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI KOSTA RIKA

Pepo zenye joto za Karibea zinavuma kutoka baharini, na kugonga milima yenye urefu wa meta 1,700 hivi. Pepo hizo zinapanda milima hiyo kisha zinapoa na mvuke uliomo unagandamana. Mawingu mazito yanafanyizwa karibu na milima hiyo na kutokeza mvua milimani au kuifunika kwa ukungu. Hilo hutokeza nini? Msitu maridadi sana uliofunikwa na mawingu.

KATIKA mwaka wa 1951, wafuasi 44 wa dini ya Quakers waliondoka nyumbani kwao huko Alabama nchini Marekani, ili kutafuta mahali pa kuanzisha makao ya kidini yenye amani. Katika pilikapilika hizo walifika kwenye milima iliyofunikwa na mawingu kusini-magharibi mwa Kosta Rika, katika Amerika ya Kati. Mashamba ya eneo hilo yako mbali, yana rutuba, na si bei ghali.

Hata hivyo, haikuwa rahisi kujenga makao na kulima katika eneo hilo. Marvin Rockwell, mmoja wa wakazi wa kwanza wa eneo hilo, anakumbuka hivi: “Njia pekee ya kufika mlimani ilikuwa njia ya mkokoteni na tuliirekebisha kwa sululu na sepetu ili magari yetu yaweze kupita.” Wenyeji wa eneo hilo waliwasaidia kujenga makao yao milimani. Basi kwa kufaa wakaliita eneo hilo Monteverde, jina la Kihispania linalomaanisha, “Mlima wa Kijani.”

Wakazi hao wa mapema walifanya maamuzi mawili muhimu. Walitambua kwamba walihitaji kujitegemea. Lakini ni zao lipi ambalo lingeweza kustahimili safari ndefu ya kutoka mlimani hadi sokoni bila kuharibika? Waliamua kwamba jibini ndiyo inayofaa. Ingawa wakati huo jibini ilikuwa ikitokezwa kwa kiwango kidogo, sasa zaidi ya kilo 4,000 za jibini hutokezwa kila siku mbali na bidhaa nyingine za maziwa kama vile krimu ya mtindi, krimu ya jibini, na aiskrimu.

Wakazi hao pia waliamua kutenga eneo la msitu lenye ukubwa wa ekari 1,335 juu ya nyumba zao. Waliamua kuhifadhi eneo hilo lenye maji kwa sababu walilitumia kutokeza umeme kwa kiwango kidogo. Hata hivyo, muda si muda, mimea na wanyama wengi wa eneo hilo lenye maji waliwavutia wanasayansi, hasa baada ya chura wa aina fulani kupatikana. (Ona sanduku kuhusu chura.) Katika miaka ya 1960, kikundi cha wanasayansi na wenyeji wa eneo hilo walianzisha hifadhi ya viumbe huko Monteverde, ambayo ilipanuliwa punde baadaye ili kutia ndani eneo hilo lenye maji. Tangu wakati huo, hifadhi hiyo imepanuliwa zaidi na kufikia ukubwa wa ekari 26,000 hivi.

Hifadhi hiyo ni mojawapo ya maeneo ambayo hutembelewa sana nchini Kosta Rika. Kila mwaka, watalii wapatao 50,000 hufika Monteverde kwa kupitia barabara ya vumbi inayojipinda na yenye mteremko mkali. Watu wanaowapenda ndege na wataalamu wa viumbe huja kwa wingi kuona maelfu ya aina mbalimbali za ndege, wanyama, na mimea inayopatikana katika hifadhi hiyo na katika maeneo ya karibu.

Mimea

Aina 500 hivi za miti hutegemeza viumbe wengine katika hifadhi hiyo. Miti fulani hushikilia kwa nguvu miamba iliyotokeza ili kustahimili pepo zinazozuia ukuzi na kuifanya ijipinde. Miti inayokua katika maeneo yasiyopata upepo huwa na mimea mbalimbali kwenye mashina yake. Mimea hiyo huwezaje kukua bila kutia mizizi ardhini? Kitabu kimoja kinasema: “Katika eneo hili lenye umajimaji, mimea inayotambaa kwenye miti hupata maji mengi hata bila kuwa na mizizi mirefu. Majani yaliyonyauka ya miti huanguka juu ya mimea hiyo na kutokeza chakula.”

Aina 300 za okidi hurembesha eneo hilo la kijani kwa rangi mbalimbali. Sehemu nyingine ya eneo hilo ina aina 200 za kangaga, na nyingine zina urefu wa meta 12 hivi na zimeishi kwa miaka 150.

Kwa nini kuna unamna-namna wa viumbe na mimea katika eneo hilo dogo? Sababu moja ni kwamba hifadhi hiyo imefika kwenye Bahari ya Pasifiki na Karibea. Tofauti kubwa za unyevu na joto katika maeneo mbalimbali ya mlimani hufanya viumbe wengi wa aina mbalimbali wapatikane katika sehemu sita kuu.

Ndege na Wanyama

Eneo la Monteverde lina ndege wengi maridadi. Katika mwaka wa 1996, aina za ndege zilihesabiwa katika eneo lenye ukubwa wa kilometa 25 kutia ndani sehemu fulani za Monteverde. Aina 369 za ndege zilionekana katika muda wa saa 24 tu! Ndege mdogo anayeitwa hummingbird na yule ndege maridadi anayeitwa quetzal wanapatikana katika eneo hilo. Ama kwa hakika, watu wengi huja hasa kumwona quetzal, mmojawapo wa ndege wenye manyoya yenye kuvutia zaidi katika maeneo ya Tropiki. Kuna vikundi 100 hivi vya quetzal wa kiume na wa kike huko Monteverde, lakini ni vigumu kuwaona kwa sababu rangi yao ya kijani inafanana sana na ya mimea. Hata hivyo, ni rahisi kuwaona hummingbird kwa sababu wao hupenda kula vyakula walivyowekewa katika vyombo nje ya maduka na mikahawa. Ndege hao maridadi wenye rangi nyangavu ya zambarau, zumaridi, na feruzi, hupita haraka sana kati ya vyombo hivyo na maua hivi kwamba huwezi hata kuona jinsi mabawa yao yanavyopigapiga.

Pia kuna aina 100 za wanyama wanaoishi Monteverde. Kitabu Costa Rica Handbook kinasema: “Ni mojawapo ya maeneo machache yanayobaki ambamo jamii . . . tano za paka hupatikana: jaguar, ocelot, puma, margay na jaguarundi.” Hata hivyo, paka hao wakubwa hujitenga na watu. Rafael Bolaños, msimamizi wa hifadhi ya Monteverde aliliambia Amkeni! hivi: “Puma huonekana baada ya kila miezi sita hivi. Jaguar huonekana baada ya kila miaka mitatu hivi.” Lakini ni rahisi kuona mojawapo ya aina 120 za wanyama wa jamii ya amfibia na wanyama wanaotambaa.

Hifadhi ya Monteverde itakuwaje wakati ujao? Mipango inafanywa ili kupanua eneo hilo. Hifadhi hiyo ilipanuliwa zaidi ya mara mbili hivi majuzi wakati Hifadhi ya Msitu wa Santa Elena na Msitu wa Mvua wa Watoto ulipoongezwa kwenye eneo lake. (Ona sanduku lililo hapa chini.) Inatazamiwa kwamba mipango hiyo itawawezesha viumbe wengi kuendelea kupatikana huko.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 17]

Kutoweka kwa Chura

Katika miaka ya 1960, mwanabiolojia Jay Savage aligundua chura fulani mwenye rangi ya machungwa, anayeitwa golden toad, katika misitu ya Monteverde. Inaonekana chura huyo hupatikana tu huko Monteverde. Rafael Bolaños, msimamizi wa hifadhi ya viumbe huko Monteverde anasema: “Katika mwaka wa 1985, vyura 1,000 hivi walionekana. Lakini miaka miwili baadaye, ni wachache tu waliopatikana.” Sasa inadhaniwa kwamba chura huyo ametoweka.

Dakt. Alan Pounds, ambaye amechunguza kutoweka kwa aina 20 za vyura katika hifadhi ya Monteverde anasema kwamba “kunyesha kwa viwango visivyo vya kawaida kila siku . . . kulichangia kuangamia na kutoweka kwa aina nyingi za wanyama wanaoishi majini na kwenye nchi kavu, kutia ndani chura aina ya golden toad.”

[Hisani]

◀ © 2003 Richard Sage

[Sanduku katika ukurasa wa 18]

Msitu wa Mvua wa Watoto

Wanafunzi wenye umri wa miaka tisa katika shule moja ya msingi kwenye eneo la mashambani nchini Sweden, walitaka kujua jinsi wanavyoweza kuokoa msitu wa mvua. Mwalimu wao aliwasaidia kukusanya pesa ambazo zilitumiwa katika mwaka wa 1988 kununua msitu wa mvua uliokuwa hatarini wenye ukubwa wa ekari 15. Hivyo ndivyo Msitu wa Mvua wa Watoto ulivyoanzishwa. Habari kuhusu mradi huo zilienea, na watoto kutoka nchi 44 wakajiunga nao. Watoto wamekusanya pesa za kutosha ili kununua maelfu ya ekari, na hivyo pande tatu za eneo hilo zitapakana na hifadhi ya viumbe ya Monteverde.

[Ramani katika ukurasa wa 16]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Monteverde

[Picha katika ukurasa wa 16]

Mimea inayotambaa juu ya miti

[Picha katika ukurasa wa 16]

Kangaga

[Picha katika ukurasa wa 17]

Okidi

[Picha katika ukurasa wa 18]

Ndege wa “hummingbird”

[Hisani]

THE HUMMINGBIRD SOCIETY / Newark Delaware USA

[Picha katika ukurasa wa 18]

Ndege wa “quetzal”

[Hisani]

© Anthony Mercieca/SuperStock ▸

[Picha katika ukurasa wa 18]

Chura

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 17]

Background and orchid: © Michael and Patricia Fogden