Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Wasichana Wanaopata Mimba Tatizo la Ulimwenguni Pote

Wasichana Wanaopata Mimba Tatizo la Ulimwenguni Pote

Wasichana Wanaopata Mimba Tatizo la Ulimwenguni Pote

TATIZO la vijana kupata mimba limeenea sana. Hata hivyo, uzito wa tatizo hilo huonekana wakati msichana anaposhtuka kwamba amepata mimba. Maisha ya msichana huyo hubadilika sana na kumwathiri yeye, familia yake, na wapendwa wake.

Vijana walio kati ya umri wa miaka 13 hadi 19 wako katika kipindi ambacho Biblia hukiita “upeo wa ujana,” yaani, wakati ambapo hamu ya ngono ni yenye nguvu sana. (1 Wakorintho 7:36) Hata hivyo, kudhania kwamba mimba za vijana zinasababishwa na kutotumia njia ya kupanga uzazi tu, ni kupunguza uzito wa jambo hilo. Uthibitisho unaonyesha kwamba vijana wachanga hupata mimba kwa sababu ya hali mbalimbali za kijamii na kihisia.

Visababishi

Utafiti unaonyesha kwamba akina mama wengi wachanga hutoka katika familia zilizovunjika. Vijana wengi wanaopata mimba wakiwa wachanga husema hivi: “Laiti familia yetu ingekuwa na wazazi wote wawili.” Hivyo, kuvunjika kwa familia kunaweza kuchangia vijana wapate mimba. Mradi mmoja wa kuwasaidia akina mama wachanga uligundua kwamba mara nyingi vijana hao “huwa na uhusiano mbaya na mama zao na hawana uhusiano wowote na baba zao.” Anita aliyepata mtoto akiwa na umri wa miaka 18 anakumbuka kwamba ingawa mama yake ambaye hakuwa na mwenzi wa ndoa alijitahidi kumtimizia mahitaji yake ya msingi, bado alihisi pengo fulani kwa kukosa baba yake.

Wasichana wengine hupata mimba kwa sababu ya kubakwa. Baadaye maishani, baadhi ya wasichana wanaobakwa wanaweza kuumia sana kihisia na kujihusisha na mambo yanayoweza kuharibu maisha yao. Kwa mfano, Jasmine alibakwa alipokuwa na umri wa miaka 15. Anasema hivi: “Baada ya tukio hilo, sikujali chochote. Nilipata mimba nikiwa na umri wa miaka 19.” Kutendewa vibaya kingono pia kunaweza kumfanya mtu ahisi kwamba hafai. Jasmine anakumbuka hivi kwa majonzi: “Nilihisi kuwa sifai kitu.” Anita pia alipatwa na hali kama hiyo yenye kuhuzunisha. Anasema: “Nilipokuwa kati ya umri wa miaka 7 na 11, nilibakwa na kijana fulani. Nilijichukia na kujilaumu.” Alipata mimba akiwa na umri wa miaka 17.

Kwa upande mwingine, vijana fulani hupata mimba kwa sababu ya kujiamini kupita kiasi na kuwa wadadisi. Nicole aliyenukuliwa katika makala iliyotangulia anakubali hivi: “Nilifikiri ninajua kila kitu na kwamba ninaweza kufanya chochote. Inasikitisha pia kwamba ningeweza kupata mtoto.” Carol, ambaye pia alipata mimba akiwa mchanga, alichochewa na udadisi kufanya ngono. Anasema: “Nilihisi kwamba kuna mambo ninayokosa.”

Kisababishi kingine ni kutofahamu matokeo ya kufanya ngono. Kulingana na wanasoshiolojia, Karen Rowlingson na Stephen McKay, huko Uingereza, vijana fulani ‘hawajui matokeo ya kuingia katika mahusiano wala matokeo ya kupata mimba.’ Inaonekana vijana wengine hawajui kwamba kufanya ngono kunaweza kutokeza mimba. Katika uchunguzi mmoja, akina mama wengi wachanga “waliripoti kwamba walishtuka au kushangaa walipogundua kwamba wana mimba ingawa hawakuwa wametumia njia za kupanga uzazi.”

Hata hivyo, kubadilika kwa maoni ya watu kuhusu ngono ndiyo sababu kubwa zaidi ya vijana kupata mimba wakiwa wachanga. Tunaishi wakati ambapo watu ‘wanapenda raha badala ya kumpenda Mungu.’ (2 Timotheo 3:1-4) Watafiti wa Australia, Ailsa Burns na Cath Scott, wanasema “viwango vya kijamii, kidini, na vya kiuchumi vinavyopinga watu kufanya ngono nje ya ndoa vimelegezwa.” Kupata mtoto nje ya ndoa si jambo la kuaibikia kama ilivyokuwa zamani. Huenda vijana katika maeneo fulani wakaona kwamba kupata mtoto ni jambo linalomfanya mtu aheshimiwe au kusifiwa!

Kuathiriwa Kihisia

Mambo yanayowapata akina mama wachanga ni tofauti sana na maoni ambayo vijana huwa nayo. Mara nyingi, wasichana husumbuka sana kihisia wanapogundua kwamba wana mimba. Wengi husema kwamba wameshtuka. Chama cha Marekani cha Matatizo ya Akili ya Watoto na Vijana kinasema: “Mara nyingi wao hukasirika, huhisi hatia, na hawakubali kwamba wana mimba.” Hata hivyo, kutokubali hali ni hatari kwani kunaweza kumfanya msichana asiende kupata matibabu yanayohitajiwa.

Elvenia anapokumbuka hisia alizokuwa nazo alipokabili matokeo ya kufanya ngono anasema hivi: “Niliogopa sana.” Wasichana wengi waja-wazito hukosa mtu wa kueleza jinsi wanavyohisi au wanaona haya sana kuzungumzia hali yao. Basi, si ajabu kwamba wengine hulemewa na hisia za hatia na woga. Pia wengi wao hushuka moyo sana. “Sikujali kuishi au kufa,” asema Jasmine. *

Ingawa msichana anaweza kuwa na hisia mbalimbali anapopata mimba, bado atahitaji kufanya maamuzi mazito yanayomhusu yeye na mtoto wake. Makala inayofuata itazungumzia jinsi msichana anavyoweza kufanya maamuzi hayo kwa hekima.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 12 Kwa habari kuhusu kukabiliana na hisia za kutaka kujiua, ona makala “Uhai Una Thamani,” katika toleo la Amkeni! la Oktoba 22, 2001.

[Sanduku katika ukurasa wa 7]

Habari Zenye Kushtua Kuhusu Vijana Wanaopata Mimba

Ingawa habari zifuatazo zinaonyesha jinsi hali ilivyo huko Marekani, zinaonyesha pia matatizo ambayo vijana wanaopata mimba wanakabili ulimwenguni pote.

● Wasichana 4 kati ya 10 hupata mimba kabla ya kufikia umri wa miaka 20, na hizo ni zaidi ya mimba 900,000 kila mwaka.

● Asilimia 40 hivi ya wasichana wenye watoto hawajafikia umri wa miaka 18.

● Watoto wa wazazi wachanga hutendewa vibaya na kupuuzwa kuliko watoto wa wazazi waliokomaa.

● Asilimia 40 tu ya akina mama walio chini ya umri wa miaka 18 ndio humaliza shule ya sekondari.

● Asilimia 80 hivi ya wanaume hawaoi wasichana wanaowatunga mimba.

● Asilimia 30 tu ya akina mama wachanga wanaoolewa baada ya kupata mtoto ndio wanaobaki katika ndoa hizo; uwezekano wa kuvunjika kwa ndoa za vijana ni mara mbili zaidi ya uwezekano wa kuvunjika kwa ndoa zinazofungwa mwanamke anapokuwa na angalau miaka 25.

● Watoto wa akina mama wachanga hukabili uwezekano mkubwa wa kuzaliwa kabla ya wakati na wakiwa na uzani mdogo, na hivyo kuongeza uwezekano wa kufa wakiwa wachanga, kuwa vipofu, kuwa viziwi, kupata magonjwa hatari ya kupumua, magonjwa ya akili, mtindio wa ubongo, kutoweza kusoma, na kukosa utulivu.

[Hisani]

Habari hiyo inategemea Not Just Another Single Issue: Teen Pregnancy Prevention’s Link to Other Critical Social Issues, The National Campaign to Prevent Teen Pregnancy, February 2002.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 7]

Vijana Hupata Mimba Ulimwenguni Pote

BRAZILI: Inasemekana kwamba “wasichana 698,439 walio chini ya umri wa miaka 19 walijifungua mwaka wa 1998 kwa kutumia Mfumo wa Afya wa Kitaifa wa Brazili . . . wasichana 31,857 kati yao walikuwa watoto waliokuwa kati ya umri wa miaka 10 na 14, na kwa hakika huo ni umri mdogo sana kupata mtoto.”—Folha de S. Paulo, Agosti 25, 1999.

UINGEREZA: “Vijana wengi zaidi hupata watoto nchini Uingereza kuliko katika nchi nyingine yoyote ya Ulaya Magharibi . . . Katika mwaka wa 1997 wasichana 90,000 walipata mimba huko Uingereza. Inakadiriwa kwamba wasichana watatu kati ya watano walijifungua (56,000) na asilimia 90 ya vijana waliojifungua mwaka wa 1997, hawakuwa wamefunga ndoa (50,000 hivi).”—Lone Parent Families, 2002.

MALASIA: “Idadi ya watoto wanaozaliwa nje ya ndoa nchini humo imeongezeka tangu mwaka wa 1998, na mama wengi wakiwa wanakaribia miaka 20.”—New Straits Times–Management Times, Aprili 1, 2002.

URUSI: “Kulingana na habari za serikali, karibu thuluthi moja ya watoto waliozaliwa huko Urusi, walizaliwa na akina mama ambao hawajafunga ndoa, na hiyo ni mara mbili ya wale waliozaliwa miaka 10 kabla ya hapo na ndiyo idadi kubwa zaidi tangu Vita vya Pili vya Ulimwengu. Zaidi ya asilimia 40 ya watoto hao walizaliwa na wasichana wachanga.”—The Moscow Times, Novemba 29, 2001.

MAREKANI: “Licha ya kupungua kwa idadi ya wasichana wachanga wanaopata mimba, wasichana 4 kati ya 10 hupata mimba angalau mara moja kabla ya kufikisha umri wa miaka 20.”—Whatever Happened to Childhood? The Problem of Teen Pregnancy in the United States, 1997.

[Picha katika ukurasa wa 5]

Wazazi wanapotengana, uwezekano wa vijana kupata mimba huongezeka

[Picha katika ukurasa wa 6]

Inaonekana vijana wengine hawajui kwamba kufanya ngono kunaweza kutokeza mimba

[Picha katika ukurasa wa 6]

Msichana anapopata mimba, hilo humwathiri sana na vilevile wapendwa wake