Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Wasichana Wenye Watoto

Wasichana Wenye Watoto

Wasichana Wenye Watoto

“Mpenzi wangu alikuwa mwenye kuvutia. Alikuwa na pesa, nasi tulikuwa tukitembelea sehemu mbalimbali na kujifurahisha. Nilitambua kwamba nina mimba nilipokosa kupata hedhi. Sikujua nitakavyomwambia mama yangu. Sikuamini kwamba nimepatwa na jambo hilo. Nilikuwa na umri wa miaka 16 tu, nami sikujua la kufanya.”—Nicole.

SASA Nicole * ana umri wa miaka 30 na kitu, naye ni mama ya watoto watatu mwenye uhakika na bidii. Mtoto wake wa kwanza ana umri wa miaka 20. Naam, miaka kadhaa iliyopita alikuwa mmoja wa mamilioni ya vijana wanaopata mimba kabla ya kufunga ndoa. Sawa na akina mama wengine wachanga, alikabili magumu mengi, maamuzi mazito, na wasiwasi kuhusu wakati ujao.

Mara nyingi Nicole haelezi jinsi alivyoshtuka, alivyokataa kukubali hali yake, alivyoogopa, alivyokasirika, na alivyofadhaika katika miaka yake ya ujana, huku vijana wenzake wakihangaikia mavazi na maksi za shule. Hata hivyo, Nicole alikuwa na tumaini. Familia yao ilikuwa yenye upendo na alikuwa amefundishwa maadili bora. Ingawa kwa muda alipuuza maadili hayo na kupata matokeo mabaya, baadaye maadili hayohayo yalimsaidia afanikiwe maishani. Sikuzote alichochewa na maneno haya: “Bado kuna tumaini.”

Inasikitisha kwamba si akina mama wote wachanga wanaotegemezwa na familia zao au kuwa na mtazamo unaofaa. Wengi hutumbukia katika umaskini. Wengine hulazimika kuvumilia maumivu ya kihisia yanayotokana na kubakwa na jeuri.

Mambo hayo huwaathiri watoto wa mama hao wachanga. Kitabu Teen Moms—The Pain and the Promise, kinasema kwamba watoto wa akina mama wachanga “mara nyingi huzaliwa wakiwa na uzani mdogo, hupatwa na magonjwa mengi ya watoto, hufa wakiwa wachanga, hawapati matibabu yanayofaa, huteseka kutokana na njaa na kukosa chakula kinachofaa, hukabili jeuri zaidi, nao hukua polepole kuliko watoto waliozaliwa na akina mama wenye umri mkubwa.” Kwa hakika, kuna uwezekano mkubwa kwa binti za akina mama wachanga kupata watoto wakiwa wachanga kuliko binti za akina mama wenye umri mkubwa.

Tatizo la akina mama wachanga limeenea kadiri gani? Mama hao wanaweza kukabilianaje na magumu ya kuwalea watoto wao? Je, kuna njia ya kuwasaidia vijana kuepuka matatizo hayo? Makala zinazofuata zinajibu maswali hayo.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 3 Baadhi ya majina katika mfululizo huu yamebadilishwa.