Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kitunguu Kinapendwa Sana

Kitunguu Kinapendwa Sana

Kitunguu Kinapendwa Sana

Na mwandishi wa Amkeni! nchini Mexico

Katika nchi nyingi kitunguu hakiwezi kukosekana jikoni. Bila shaka, kinatumiwa kwa njia mbalimbali kama vile kutayarisha mchuzi, saladi, vyakula tofauti-tofauti, na dawa. Pia kinaweza kufanya tutokwe machozi.

Kitunguu ni mojawapo ya mimea mingi inayochanua maua maridadi. Hata hivyo, watu wengi ulimwenguni hutumia kitunguu kilicho na shina lenye tabaka za mviringo ambalo hukua chini ya ardhi.

Kitunguu ni mojawapo ya mimea ambayo wanadamu wamekuza kwa muda mrefu sana. Ni wazi kwamba kimetumiwa sana kwani Biblia husimulia kwamba wapata mwaka wa 1513 K.W.K., Waisraeli walitamani sana vitunguu walivyokula walipokuwa watumwa huko Misri.—Hesabu 11:5.

Lakini ni nini ambacho kimewafanya watu wengi wavutiwe sana na ladha ya kitunguu? Ni ule mchanganyiko wa umajimaji wa salfa ambao hutokeza harufu kali ya vitunguu. Umajimaji huo ndio unaotufanya tutokwe machozi.

Vitunguu Vina Faida Nyingi

Vitunguu huboresha sana afya ya watu, kwani vina kalisiamu, fosforasi, na asidi askobiki au vitamini C. Hata hivyo, kwa miaka mingi vitunguu vimetumiwa hasa kwa matibabu. Hata leo vinatumiwa kutibu magonjwa mbalimbali kama mafua, kuvimba koo, utando mgumu wa mafuta katika mishipa ya damu, ugonjwa wa moyo, kisukari, na pumu. Pia vitunguu hutumiwa katika dawa za kusafisha vidonda, kuzuia kolesteroli, uvimbe, kuganda kwa damu ndani ya mishipa, na kuzuia athari za kansa.

Vitunguu huwa na rangi tofauti-tofauti kama vile nyeupe, manjano, kahawia, kijani, nyekundu, na zambarau. Unaweza kuvila vikiwa vibichi, vikiwa vimepikwa, na vikiwa vimetayarishwa na kuhifadhiwa katika mikebe. Pia unaweza kula achali ya vitunguu, vitunguu vilivyokaushwa, vilivyosagwa, na vilivyokatwakatwa. Ni wazi kwamba kitunguu ni mmea wa ajabu, hata ikiwa kitafanya utokwe machozi.