Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kukadiria Uwezekano wa Furaha Katika Ndoa

Watafiti fulani huko Seattle, Washington, Marekani, walipiga picha za video za mamia ya wenzi wa ndoa walipokuwa wakizungumza kuhusu mambo muhimu, kama vile masuala kuhusu pesa na ngono. Kisha wakakadiria uwezekano wa kufanikiwa kwa ndoa hizo, wakizingatia “maoni ya wenzi wa ndoa kuhusu maisha, uwezo wao wa kujadiliana na kukubali maoni ya wengine, na jinsi wanavyoathiriwa na pongezi au dhihaka za wenzi wao wa ndoa,” laripoti Science News. Miaka minne baadaye, makadirio hayo yalitimia kwa asilimia 94 ya wenzi wa ndoa ambao walikuwa wamefanyiwa uchunguzi. Ni mambo gani yaliyoathiri furaha katika ndoa? Makala hiyo inasema kwamba “katika ndoa zenye mafanikio, mawasiliano mazuri yaliyotia ndani kucheka na kufanya utani wakati wenzi wa ndoa walipokuwa wakipigwa picha za video yalikuwa mengi kuliko ugomvi, kwani yalizidi kwa uwiano wa 5 kwa 1. Dalili moja muhimu ya uwezekano wa talaka kutukia ilikuwa kuonyesha dharau kwa ishara ya uso wakati mwenzi wa ndoa alipokuwa akizungumza.” Mchunguzi mmoja alisema hivi: “Dharau hudhoofisha upendo kama vile asidi inavyoharibu chuma.” Watafiti hao wanatumia mambo waliyogundua kuwasaidia wenzi wa ndoa walio na matatizo. Baada ya kushauriwa kwa siku chache, thuluthi moja hivi ya wenzi wa ndoa wameboresha hali yao.

Ndege Werevu

Ripoti ya gazeti The Sunday Times la London kuhusu uchunguzi uliofanywa karibuni inaonyesha kwamba “ndege wamewashinda sokwe na pomboo katika shindano la wanyama walio werevu zaidi.” Wachunguzi katika Chuo Kikuu cha Cambridge, walitoboa tundu kwenye mrija unaopenyeza nuru halafu wakaulaza juu ya mrija mwingine uliokuwa umesimamishwa wima huku lile tundu likielekea chini kwenye mrija huo, kisha wakaweka chakula karibu na tundu ndani ya mrija uliokuwa umelazwa. Sokwe walijaribu kusukuma chakula ili kitoke nje ya mrija huo, nacho kikatumbukia ndani ya tundu hilo. Lakini vigogota walitumia kijiti kuvuta chakula bila kukitumbukiza kwenye tundu. Kabla ya wakati huo, wachunguzi katika Chuo Kikuu cha Oxford walimtazama kunguru anayeitwa Betty akikunja waya unaopindika vyepesi na kuutumia kufanya mambo mbalimbali, jambo ambalo sokwe hawajawahi kufanya. Gazeti Times linasema matokeo ya uchunguzi huo “yanapinga maoni ambayo watu wengi wamekuwa nayo kwa muda mrefu” kwamba mamalia tu ndio walio na uwezo wa kutengeneza vifaa mbalimbali.

Jinsi Televisheni Inavyoathiri Ukuzi wa Akili ya Mtoto

Gazeti Mainichi Daily News linaripoti kwamba madaktari wa Shirika la Japani la Magonjwa ya Watoto wanasema huenda ikawa vigumu kwa watoto wanaotumia muda mrefu kutazama televisheni kuwasiliana. Matatizo wanayokabili yanatia ndani kushindwa kukumbuka maneno, kuwatazama wazazi wao kwa muda mrefu wanapozungumza nao, na kufanya urafiki. Hiromi Utsumi, ambaye ni mwanachama wa shirika hilo, anasema kwamba “watoto wasipocheza kwa muda mrefu na wazazi wao, au wasipocheza nje ya nyumba, akili yao haitasitawi vizuri.” Shirika hilo linapendekeza “wazazi wazime televisheni wakati wa kula na wakati wanapowanyonyesha watoto, na kwamba televisheni, video na kompyuta zisiwekwe katika vyumba vya watoto,” yasema ripoti hiyo. Inaongezea kusema kwamba mawasiliano yaliboreka “wazazi walipofuata shauri la daktari la kuwazuia watoto kutazama televisheni na video.”

Maktaba Zilizoko “Chini ya Ardhi”

Mradi wa kuazima vitabu umeanzishwa katika mfumo wa usafiri wa magari-moshi ya chini ya ardhi wa Mexico City, ili kuwatia watu moyo wasome. Katika vituo vya gari-moshi, msafiri anaweza kuazima kitabu cha chapa kubwa kilicho na habari mbalimbali zilizotolewa katika vitabu vya Wamexico, akisome anapokuwa akisafiri, na akirudishe kwenye kituo cha gari-moshi anapomaliza safari yake. Msimamizi wa mradi huo, Aarón López Bravo, anasema kwamba “watu wengi wamefurahia hatua hiyo. Mradi huo umewapa watu nafasi ya kutumia wakati ambao kwa kawaida hupotea bure, ili kujifunza na kujifurahisha.” Toleo la kimataifa la gazeti The Miami Herald linasema kwamba katika mwezi wa kwanza watu waliazima zaidi ya vitabu 130,000 kutoka katika vibanda mbalimbali vilivyojengwa kwa ajili ya kusudi hilo. Mradi huo ulianzishwa katika vituo 21 vya barabara moja tu, hata hivyo wasimamizi wake wanakusudia kuueneza katika mfumo mzima wa magari-moshi ya chini ya ardhi, ambao kila siku husafirisha karibu abiria milioni tano.

Kujifungua Nchini Uingereza

Gazeti The Independent la London, linasema kwamba kwa mara ya kwanza nchini Uingereza, idadi ya watoto wanaozaliwa kwa msaada wa madaktari imepita ile ya watoto wanaozaliwa bila msaada huo, na hiyo ni hatua mpya na muhimu katika historia ya tiba nchini Uingereza. Tarakimu za mwaka wa 2001-2002 zilizochapishwa na Idara ya Afya ya Uingereza zinaonyesha kwamba ni asilimia 45 pekee ya akina mama waliojifungua bila kufanyiwa upasuaji. Matumizi ya mbinu ya upasuaji wa kumtoa mtoto wakati wa kujifungua yaliongezeka kutoka asilimia 9 katika 1980, hadi asilimia 22.3 katika 2001-2002. Asilimia 56 ya akina mama katika chumba kimoja cha kujifungua walitumia mbinu hiyo. Peter Bowen Simpkins wa Britain’s Royal College of Obstetricians, alisema kwamba “wanawake wengi zaidi wanasisitiza mbinu hiyo itumiwe wanapojifungua. Wanawake wanaofanya kazi . . . wanataka kuja na kujifungua siku hususa. . . . Upasuaji huonwa kuwa salama zaidi. Hata hivyo, ukweli ni kwamba mbinu hiyo imesababisha vifo vya watu wengi.” Pia watafiti wanaonya kwamba itakuwa vigumu kupata mimba tena ikiwa mama anayejifungua mtoto kwa mara kwanza atapasuliwa, na kuna uwezekano mkubwa kwamba hataweza kujifungua mtoto wa pili kwa njia ya kawaida.

Vijana Wanaojinyima Vyakula Fulani Huongeza Uzito

Gazeti U.S.News & World Report linasema kwamba “huenda vijana wanaobalehe ambao hujinyima vyakula fulani ili kupunguza uzito wakauongeza, na kusababisha wanenepe kupita kiasi.” Uchunguzi uliofanywa kwa kipindi cha miaka mitatu, na ambao ulihusisha watoto 15,000 hivi walio na umri wa kati ya miaka 9 hadi 14, ulionyesha kwamba “wavulana na wasichana ambao hujinyima vyakula fulani ili kupunguza uzito waliongeza uzito kuliko wale ambao hawafanyi hivyo, na uwiano kati ya kimo na uzito, unaoonyesha ikiwa mtu ni mnene kupita kiasi, ukaongezeka.” Gazeti hilo linaripoti kwamba watafiti wanasema “kujinyima vyakula fulani ili kupunguza uzito kunaweza kumfanya mtu ale kupita kiasi.” Wasichana ambao walijinyima vyakula fulani “walikabili uwezekano wa kula kupita kiasi mara 12 zaidi ya wale ambao hawakufanya hivyo.”

Upungufu wa Makasisi

Gazeti ABC la Kihispania linasema kwamba “zaidi ya nusu ya idadi ya seminari nchini Hispania huenda zikafungwa” kwa sababu ya ukosefu wa watu wanaotaka kuwa makasisi Wakatoliki. Mwaka uliopita, “seminari 14 hazikuwaandikisha wanafunzi wapya, huku seminari nyingine 18 ziliandikisha mwanafunzi mmoja tu kila moja.” Ni nini kimesababisha hali hiyo? Andrés García de la Cuerda, kasisi anayesimamia seminari ya Madrid, anasema sababu moja ni kwamba watu huko Ulaya “wameacha pole kwa pole kupendezwa na mambo ya dini,” na hivyo wamepoteza imani, na kuacha kuwa Wakristo. Pia García de la Cuerda alisema kwamba “watu hawapendezwi na Kanisa [Katoliki].”